Friday 27 February 2009

Swali

Nimekuwa najiuliza mara kwa mara swali hili.

Ktk miaka ya 1950 hadi 1960 wanafunzi kutoka barani Afrika walioenda ng'ambo kusoma walipokutana nje ya masomo walikuwa wanajadili mambo ya ukombozi wa bara letu la Afrika. Viongozi kama Mwalimu JK Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Robert Mugabe n.k. walidhamiria kupigania uhuru mara waliporudi nyumbani kwao. Na kweli miaka ya 1960 ilikuwa ni ya vuguvugu la ukombozi wa Afrika.

Miaka mingi imepita baada ya nchi za kiafrika kujipatia uhuru wao na bado kuna wanafunzi kutoka Afrika wanaendelea kwenda ng'ambo tena kwa kiwango kikubwa kuliko enzi zile za Mwalimu.

Je wanafunzi walioko ng'ambo kwa sasa wana ajenda angalao moja inayowaunganisha kuhusu bara la Afrika? Suala kubwa sasa Afrika linalotawala anga ni umaskini (uchumi), mazingira, magonjwa na utandawazi. Je kwa staili ya kina Mwalimu waafrika waliopata nafasi kufika nje ya nchi na kujionea maendeleo kwingineko duniani wanalo jukwaa la kuratibu uzoefu wao na kujipanga namna ya kusaidia nyumbani Afrika.

Kina Mwalimu, Lumumba, Kenyatta, Sekou Toure kama wangekuwepo tungewaonyesha nini kulinganisha na juhudi zao?

Wito wangu ni kuwa walioko nje waungane na kuwa kitu kimoja, kuwa na sauti moja, kuandaa ajenda ya pamoja ili kuibadilisha Afrika. Vizazi vijavyo vitashukuru endapo uzoefu uliopatikana ng'ambo utairudishwa nyumbani ili kusaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Wale wenye taaluma zao (mfano waliosoma uchumi, biashara, sayansi, uhandisi, udaktari n.k.) onyesheni cheche zenu kwa maendeleo ya Taifa mojamoja na bara zima kwa ujumla! Wimbi la mchango wenu litaonekana ikiwa kutakuwa na jukwaa la pamoja ktk kutoa sauti au nasaha zenu kwa manufaa ya nchi zenu na Afrika. Au mnasemaje?

No comments: