Tuesday, 10 February 2009

Kwanini maisha ni magumu 'Yu Kei'*

Msukosuko wa uchumi ulioanzia kule Marekani umeitikisha uingereza ktk msingi wake wa kiuchumi na matokeo yake yanaonekana dhahiri mitaani na ktk nyumba za watu. Kwa hili wala halihitaji mtaalamu aliyebobea kutoka Chuo Kikuu kulielezea.

Chanzo kikubwa kabisa ni mabenki kutoa mikopo kwa watu wasio na sifa au kampuni zisizo na sifa za kukopeshwa. Kundi hili la watu au makampuni ni kubwa sana na nadhani ndio maana mabenki yalimezea mate uwingi wao na kuona kuwa watapata faida kubwa kwa kukopesha hela. Si unajua biashara ni matangazo na matangazo ni watu/wateja!!! Kwa maana hii mabenki yaliikubali 'risk' ya kuwakopesha watu hawa hela kwa mategemeo kupata faida mbeleni.

Kilichofuata ni mabenki kuwatafuta watu na kuwashawishi kuchukua mikopo kadri wawezavyo kwa masharti nafuu. Watu na makampuni yakakubali na kuchangamkia hizo pesa. Kukopa harusi kulipa matanga. Tukumbuke hii mikopo ilitakiwa ilipwe kidogo kidogo na kwa riba. Wateja walikuwa wepesi kupokea mikopo lakini kulipa wakawa na kigugumizi. Wateja walipozoea utamu wa hela, wakawa wanabadili benki. Wakichota toka Benki A, wanatumia wakiishiwa wanaenda benki B, baadae C, E, D n.k. Lakini cha ajabu ni kwamba hawa wateja walikuwa wanasahau wajibu wao wa kurejesha kidogo kidogo kila mwezi! Baada ya miaka kadhaa (mitano au zaidi)mabenki yakawa yametoa hela nyingi ambazo ziko mikononi mwa wateja, kwa upande mwingine wateja wakawa hawarudishi.

Mabenki yakashtuka. Kazi ya kufuatilia wateja ikaanza. Wateja hawana hela - wameshakula au kutumia na wengi wao hawarudishi (wameishia mitini?). Mabenki nayo yanatakiwa kurudisha hela maana na wao walikopa kwingineko. Ndio ikaanza vuta nikuvute hadi siri ikafichuka na kubatizwa jina 'credit crunch'. Huo ndio mchezo ulioanzisha 'Credit Crunch', kwa maelezo mepesi. Ikumbukwe kuwa wengi wa waliokopeshwa hawakuwa na sifa za kukopeshwa ila mabenki yalilegeza masharti ili kupanua uigo wa soko. Matokeo yake wema (au uongozi mbaya) umeziponza benki. Na benki nazo sasa zinadaiwa na wadeni wao. Mabenki mara nyingi hukopeshana wenyewe kwa wenyewe au hukopa kutoka mifuko mbalimbali ya akiba mfano mifuko ya pensheni. Na bahati mbaya sasa hela za pensheni za wastaafu ndio zimefyekwa na mabenki na hivyo 'credit crunch' imewakumba hata ambao hawakuwemo (wastaafu)!

Sasa baada ya mabenki kushtuka na kusitisha mikopo kwa wateja wake nini kimefuata?

Waingereza huwa wanaishi kwa mikopo. Karibu kila kitu cha mwingereza amekopa na kulipa taratibu. Wanatumia kadi za benki (credit card au debit card). Kuanzia nyumba wanazoishi, samani (fanicha), magari, simu za mikononi, safari (holiday), nguo na chakula wao hulipa kwa kadi. Na huo ni mkopo. Benki zinapositisha kuingiza hela ktk kadi hizo ina maana mteja hawezi kutumia kadi kwa kuchanja popote. Hii ina maana atakosa hata kununua mkate na sukari.

Hicho ndicho kitu kinachowaumiza waingereza kwa sasa. Hela haikai maana ikipita benki tu inakatwa kulipia madeni ya nyuma. Kwa hiyo mwisho wa mwezi ukifika mshahara hawauoni na wala hawaugusi. Wanachoambulia ni 'bank statement' inayoontesha hela iliyoigia mwisho wa juma au mwezi na kukatwa na wadeni (mabenki).

Makampuni nayo hayapati mikopo maana hayaaminiki. Kwa hiyo makampuni yanaishia kupunguza wafanyakazi au kufunga biashara maana hakuna mikopo ya kuendesha shughuli zao na wala hakuna wateja. Tayari makampuni kadhaa yamefunga biashara zao hapa Reading, kwa mfano: adams, marksandspencer (simplyfood outlets -caversham), woolworths na baa (pubs) nyingi tu. Kusema kweli hali ni ngumu kwa waajiri na waajiriwa. Mwajiri akibanwa mbavu anapunguzia maumivu yake kwa wafanyakazi.

Nani alitegemea kuwa bidhaa za madukani zitadoda Uingereza. Maana hapa kila msimu una fasheni yake na kuna misimu minne kwa mwaka kwa hiyo wafanyabiashara hutegemea kubadili bidhaa kila msimu mpya unapoanza. Kilichotokea sasa ni kuwa watu wameanza kutumia vya zamani, hawanunui vipya! Kama ni nguo zinavaliwa za misimu iliyopita, kiasi kwamba huduma ya mitumba nayo imeathirika. Watu hawatoi nguo au viatu vyao vilivyotumika kwa mashirika ya misaada kwa nchi zinazoendelea kwa vile hawawezi kumudu gharama za kununua nguo mpya. Huko Tanzania tusijeshangaa bei za mitumba kupaa, chanzo chake kiko huku -watu hawatoi nguo zao zilizotumika tena. Hela inaelekezwa ktk kununua mahitaji muhimu tu mfano chakula, kulipia bili za umeme na gesi. Watu wanaanza kutembea kwa miguu badala ya kutumia gari au kuchangia magari kuepuka gharama za mafuta. Kila mtu anaangalia kitu ambacho anaweza kujinyima ili mradi kuokoa matumumizi yasiyo ya lazima. Karibu familia zote za Uingereza zimeathirika na hali ya uchumi kuyumba.

Kibaya zaidi ni pale wazawa wanapotumia uzawa wao kuishinikiza serikali yao itoe ajira kwa wazawa tu na sio wageni toka nje ya Uingereza. Bahati nzuri serikali imekataa wazo hilo. Imetangaza kuwa kazi zitatolewa kwa ushindani endapo mwingereza atakuwa na sifa basi atapewa kipaumbele, lakini sio kwamba mwingereza apewe kazi kwa vile amezaliwa Uingereza. Sifa kwanza, uzawa baadae. Hata hivyo dalili hizi za uzawa si njema hasa kwa raia watokao nje ya nchi za jumuia ya Ulaya. Tayari sheria kadhaa zimetungwa hapa Uingereza kuwatenga watokao nje ya eneo la EU, waafrika tukiwemo. Huo nao ni uzawa tu! Pia ninaelewa kuwa kwa sasa hivi nafasi nyingi za kazi na mafunzo ya kazi huwaendea wazawa na wa-EU.

Hali inaweza kurejea kawaida au machungu haya yanaweza kupungua pale mabenki yatakapochukua hatua madhubuti kama vile kufuta madeni ya wateja wao sugu na pia kurudisha imani (confidence) kwa wateja wao (watu, makampuni madogo -small/medium scale enterprises, makampuni makubwa n.k.). Zoezi hili si la usiku mmoj, litachukua muda mrefu. Tayari serikali mbalimbali duniani zimeamua kuyakwamua mabenki yao ili yarejeshe imani kwa wateja wao na kuanza kukopesha tena. Ndio maana siku hizi tunasikia maneno kama vile 'stimulus packages', 'responsible lending' n.k. yakitumiwa na wakubwa ktk serikali (wanasiasa) na taasisi za kimataifa. Haya ni maandalizi ya kusawazisha mambo na ni jukumu la serikali (zote) kusaidia mabenki ili yaondokane na matatizo yaliyoyakumba ili yawe huwe huru tena kufanya kazi zake za kibenki kama kawaida. Kama zoezi hilo litafaulu, ni dhahiri pia ajira zitashamiri tena, kazi mpya zitachomoza na waliojiajiri watapata ahueni kwa kupata huduma za kibenki ambazo kwa sasa zimesitishwa. Hatimaye watu wataendesha maisha yao kwa uhakika na furaha. Hayo ndiyo mategemeo na matumaini ya wengi.*nimeandika makala hii kwa uelewa wangu wa kawaida. mimi sio mchumi.

No comments: