Tuesday, 17 February 2009

TZ: Upinzani wa kisiasa uwe 24/7

Huwa naona viongozi wetu wa upinzani nchini wakati mwingine wanajisahau na kuwa wananchi wa kawaida tu. Ninamaanisha kuwa hawana kitu au sera mbadala ili kupambanisha na serikali ya CCM ktk maisha ya kila siku.

Mfano kila mwisho wa mwezi Rais wa Jamhuri ya Muungano hutoa hotuba kwa wananchi. Viongozi wa vyama vya upinzani hugeuka wananchi vijiweni kuijadili na wakati mwingine kuipiga 'madongo', wakati hawana kitu mbadala kuonyesha kuwa wao wangefanyaje au wangetoa ujumbe gani tofauti kwa wananchi ktk hali kama ile. Kwa uelewa wangu ningetegemea viongozi wakuu wa vyama vikubwa vya upinzani nao wangetoa salaam zao za kila mwezi na za kufunga mwaka ili wananchi, ambao ni wapiga kura, waone kitu ambacho wanaweza kukipata ikiwa watachagua upinzani.

Viongozi wa upinzani kuweni macho kila wakati kuwapa wananchi kitu ambacho wangekipata endapo wangewachagueni mwaka 2005 au kuwaonyesha wananchi uwezo wenu ikiwa watawachagua mwaka 2010.

Kila hatua ambayo CCM inaipiga navyi pigeni sambamba au zaidi. Pekueni ahadi zote za muda mrefu ambazo CCM imezitoa lakini haijatekeleza au imetekeleza kwa rasha rasha. Mfano wananchi tuliahidiwa maji safi na salama yatapatikana umbali wa mita 400 kwa kila mtanzania ifikapo 1992. Lakini leo hii hata wale waishio mjini maji ni ya shida achilia mbali wa vijijini.

Je wapinzani mna cha kuwahakikishia wananchi endapo watakupigieni kura? Mnasemanje kuhusu hilo la maji. Vipi kuhusu umeme, barabara, uchangiaji elimu toka shule ya msingi hadi elimu ya juu, makazi bora kwa wananchi, matibabu n.k. Wekeni pamoja sera zenu na zijulikane kwa wananchi wakati wote, hakuna haja kusubiri wakati wa uchaguzi. Ziwekeni wazi sera wa kupitia vipeperushi (kwa ajili ya kuwasambazia wananchi), wekeni matangazo ktk vyombo vya habari, internet (mambo ya utandawazi) n.k.

Ni muhimu wapiga kura waelewe ni kitu gani CUF, CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi n.k. wanaamini na wanasimamia (what is your selling point). Je mnauzika? Wateja watapenda bidhaa zenu (sera)? Mfano mteja akitaka kununua kitu au bidhaa fulani anajua duka au mahala pa kununua. Kwa maana hiyo hiyo ninaamini kuwa wapiga kura wangependa kujua kuwa endapo watahitaji mabadiliko kwa namna moja au nyingine ni chama kipi kiko tayari kuleta tofauti au mabadiliko wanayoyategemea. Kila siku kwenu iwe ni ya mapambano dhidi ya CCM. Wakati mwingine mnajisahau na mnakuwa wana-CCM bila kujijua!!

Pia nawashauri muandae orodha ya wagombea udiwani na ubunge ktk kata na majimbo ambayo yako mikononi mwa CCM ili wanolewe mapema na kuwa tayari kwa wakati wowote (kwa maana chaguzi ndogo huwa hazujulikani ziko lini). Orodha hii iwe kwa ajili ya matumizi ndani ya Chama sio kwa ajili ya Tume ya Uchaguzi. Chadema watakumbuka kilichowapata ktk uchaguzi mdogo kule Mbeya Vijijini hivi karibuni. Sababu yake ni ndogo tu, maandalizi ya zimamoto. Ndio maana nasema vyama vya upinzani jiandaeni sasa kwa kuteua orodha 'ghafi' ya wanaoweza kugombea endapo itatokea uchaguzi mdogo. Hili linawezekana endapo mtawashirikisha wanachama wenu. Mnaelewa ni majimbo gani yako kwa CCM kwa hiyo andaeni orodha ya wagombea (ndani ya chama) ktk majimbo hayo na kata zote kisha muyapitie na kuchuja halafu mnatunza hiyo orodha. Pia mtawapa mafunzo wahusika (candidates) mapema ili nao wawe tayari.

Anzeni sasa, msingoje 2010 MTACHELEWA!

NB: Sikumaanisha muanze kampeni za uchaguzi.

No comments: