Wednesday, 25 February 2009

EWW

Miaka ya 1970-80 nchi yetu ilifanikiwa sana ktk kampeni ya kupambana na adui ujinga (kutojua kusoma na kuandika). Kutokana na mafanikio hayo Tanzania ilikuwa ya kwanza ktk bara la Afrika kwa kuwa na asilimia 90 ya watu wanaojua kusoma na kuandika.

Miaka ya 1990 rekodi yetu imeshuka sana hadi kufikia kwenye asilimia 60. Sina uhakika kipindi hiki tunachoanza karne mpya ya 21 kiwango hicho kiko ktk hali gani.

Mwalimu J.K. Nyerere alisema 'jifunze kusoma, wakati ni huu!'

Wakati ambapo serikali inatilia mkazo uanzishwaji na uimarishwaji wa elimu ya shule za msingi, sekondari na vyuo, Elimu ya Watu Wazima (EWW) nayo ipewe kipaumbele stahili ili isizimike kienyeji kwani wapo wanaoihitaji na serikali isiwanyime haki yao!

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Serikali yatakiwa kuongeza jitihada za kufuta ujinga

2009-04-27 19:40:48
Na Abdul Mitumba, Karimjee


Serikali imeombwa kuongeza bajeti ya fedha zinazotumika kufanikisha mpango wa utoaji elimu kwa watu wazima ili kuliokoa taifa na tishio la kutumbukia katika lindi la ujinga unaotokana na ongezo la wasiojua kusoma na kuandika.

Ombi hilo linatolewa wakati kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kikiongezeka kutoka asilimia 9.6 mwaka 1986 hadi kufikia asilimia 31 mwaka jana.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu nchini, TEN/MET, Bw. Joseph Kisanji, amesema hayo katika taarifa yake wakati wa maadhimisho ya kampeni ya wiki ya kimataifa ya elimu kwa wote iliyoadhimishwa mwishoni mwa wiki.

Amesema wakati Tanzania ikiungana na nchi wanachama kote duniani kuadhimisha wiki hii, changamoto iliyopo ni kwa Serikali kutenga fedha za kutosha zitakazosaidia kupunguza idadi ya wasiojua kusoma na kuandika.

``Kwa mfano, tunapoadhimisha wiki hii, Tanzania ina watoto wmilioni 1.5 ambao hawapati elimu ya msingi, huku kukiwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi uliolenga kuandikisha wanafunzi wengi zaidi,`` amesema.

Amesema hali hiyo imesababisha sekta ya elimu kuwa mojawapo ya sekta zilizo nyuma katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesema anguko hilo la elimu limechangiwa na bajeti finyu inayotengwa kwa ajili ya elimu ya watu wazima, hasa baada ya nchi za Scandinavia zilizokuwa zikifadhili mpango huo kujiondoa katika ufadhili tangu mwaka 1990.

Ameongeza kuwa tatizo limeongezeka zaidi baada ya kubainika kuwa karibu asilimia 40 ya wanafunzi ambao wanafaulu mtihani wa kitaifa kwa wastani hawaendelei na elimu ya sekondari.

Aidha, Mkurugenzi Msaidizi Msajili wa Shule, Bw. Aminiel Mfuru, amethibitisha kuwepo kwa ongezeko la wasiojua kusoma na kuandika na kusema kuwa jitihada zaidi zinaendelea kufanywa ili kuzuia ongezeko hilo.

SOURCE: Alasiri