Friday, 27 February 2009

Mzee mzima kwenda na maji?

Siasa za Uingereza zinazidi kuingia ktk hatua nyingine. Kuna dalili kubwa kuwa Waziri Mkuu Gordon Brown anaelekea kupigwa mweleka na David Cameron wa chama cha Conservatives ktk uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani katikati.

Kwa kweli mambo hayakumwendea vema bwana Brown wa Labour tangu achukue madaraka. Hii inaonekana kuwa ni laana inamrudia kwa vile alihusika kwa namna moja au nyingine kumwondoa Tony Blair ktk 'mapinduzi baridi' ndani ya chama cha Labour.

Tayari kuna tetesi kuwa wabunge wa Labour wanajiandaa kuondoka 'benchi' upande wa serikali bungeni na kuhamia benchi la upinzani kwa vile chama chao kinaelekea kung'olewa madarakani. Wabunge wa chama tawala hukaa upande wa kushoto na wa upizani hugawana jukwaa la upande wa kulia (kuna vyama vingi vya upinzani mfano Consevertives, Lib.Dem, DUP, SNP-Scotland, PC-Wales, Respect n.k.).

Tetesi nyingine ni kuwa wabunge wale wakubwa (seniors) wanajiandaa kuwania kinyang'anyiro cha uongozi wa chama mara baada ya bwana Brown kung'oka (hii ni baada ya uchaguzi mkuu ambao Labour hawana matumaini ya kushinda na kurudi madarakani tena kama chama tawala bali wanatengemea kurudi kama chama cha upinzani ktk uchaguzi huo wa mwakani).

Ktk wingu hilo hilo kuna wabunge wa Labour ambao wameshaotea kuwa watapoteza ubunge wao na baadhi yao wameshatangaza kutowania tena ubunge. Mbunge aliyetajwa kukimbia 'aibu' hiyo ni Bwana Salter wa Reading Magharibi aliyetangaza kung'atuka kutoka siasa za Westminster mwakani. Mwenzake kutoka Labour -Reading Mashariki alidondoka ktk uchaguzi uliopita!

Dalili kubwa za Labour kubwagwa zilianzia ktk chaguzi za Udiwani mwaka jana ambapo mabaraza mengi ya udiwani yaliyokuwa chini ya Labour yalienda mikononi mwa Connservatives au Lib. Dems. Hiyo ilikuwa 'trela', picha kamili ni mwakani ambapo mzee mzima Brown na chama chake cha Labour wanatarajiwa kunyolewa bila maji!

Siwaombei Labour mabaya, bali hali halisi inaonyesha kuwa wataadhibiwa na wananchi ktk uchaguzi mkuu mwakani.

No comments: