Monday, 23 February 2009

Benki Kuu: Hivi ni kweli?

.
.
Hivi ni kweli na inawezekana .....

.... mtu mmoja (Amatus Liyumba) apitishe ujenzi wa mabilioni ya hela pale Benki Kuu na pakajengeka kwa miaka 6 bila wakubwa wa Benki Kuu na wa nchi kuhusishwa?

... ghorofa 2 zijengwe pale mahali nyeti vile bila idhini au baraka za ikulu?


Tusidanganyane!
.
.

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Ya Liyumba ni mkorogo


Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (Takukuru), imesema imefanya jitihada zote, lakini imeshindwa kumpata aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ambaye ameshitakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh. 221, 197,299,200.95 ya mradi wa maghorofa pacha ya benki hiyo.

Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, aliiambia Nipashe jana kwamba taasisi yake imetafuta, lakini bado haijaweza kumpata.

``Mpaka sasa hajapatikana na tunaendelea na jitihada za kumtafuta, tunaomba mtu yeyote mwenye taarifa za alipo atupatie, atapewa donge nono,`` alisema

Liyumba alipewa dhamana tata na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Jumanne wiki iliyopita, baada ya kuwasilisha hati ya nyumba yenye thamani ya Sh. 800,820,000 kati ya masharti ya dhamana ya kuwasilisha mali yenye thamani ya Sh bilioni 55.

Yeye na mwenzake, Deogratius Dawson Kweka, aliyekuwa meneja wa mradi wa ujenzi wa maghorofa pacha ya BoT, wanashitakiwa kwa makosa tofauti, yakiwemo matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara hiyo.

Katika masharti ya awali, kila mshitakiwa alitakiwa kutoa hati yenye thamani ya Sh. Bilioni 55, hivyo thamani ya hati aliyowasilisha na kupata dhamana wiki iliyopita, ilikuwa sawa na asilimia 1.4 ya kiasi kilichostahili.

Hata hivyo, siku moja baada ya kupewa dhamana, Jamhuri ilitoa notisi ya kukamatwa Liyumba na wadhamini wake, Benjamin Ngurugulu na Otto Agatuangelus, ili warejeshwe mahakamani hapo.

Wadhamini wake walishikwa na kuwekwa maabusu kwa saa tatu kisha kuachiwa.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza Nipashe kwamba tangu kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwa Liyumba, maofisa wa Takukuru wamefanya uchunguzi katika viwanja vingi vya ndege hapa nchini, lakini hakuna sehemu iliyoonyesha kwamba amesafiri nje ya nchi kupitia viwanja hivyo.

Habari zilisema kuwa hata kamera zilizoko Viwanja vya Ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro na Zanzibar zimeangaliwa, lakini hazionyeshi Liyumba akipita.

``Tumeangalia katika viwanja vyote vya ndege, kumbukumbu, na hata kamera, lakini hakuna sehemu ambayo Liyumba anaonekana,`` kilisema vyanzo kimojawapo kutoka Takukuru.

Habari zinadai maafisa wa Takukuru wanadai kama atakuwa ametoroka basi atakuwa ametumia usafiri wa barabara, hivyo nguvu sasa imeelekezwa sehemu za mipakani.

``Sasa tunafanya jitihada kuangalia maeneo ya mipakani ili kuweza kubaini kama alitumia njia hizo au la,`` alisema mtoa habari mmoja ndani ya Takukuru.

Wakati Takukuru wakidai hivyo, kumekuwa na tetesi kwamba huenda Liyumba yuko hapa nchini na amejichimbia mafichoni kwa ajili ya kukusanya ushahidi wa kwenda mahakamani kesho ambayo ni siku ya kesi yake.

Tetesi hizo ambazo jana zilikuwa zimezagaa nchini, zilidai kuwa kuna taarifa kwamba Liyumba ambaye sasa anatajwa kwamba ametoroka na hajulikani aliko, hajatoroka na kwamba alikuwa amejipumzikia akiangalia afya yake huku akijipanga kutimiza masharti ya dhamana.

Tetesi hizo zilidai huenda Liyumba akaibuka tena mahakamani kesho kuwasilisha hati za ziada za dhamana zenye thamani sawa ama zaidi ya Sh Bilioni 54 .

Hadi sasa si Takukuru wala Mahakama ambao wamekuwa tayari kueleza sababu za kutolewa kwa hati ya kukamatwa Liyumba.

Wiki iliyopita mwanasheria wa Takukuru, Tabu Mzee, alisema tangu kutolewa kwa hati ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo, Liyumba hayajaonekana na hakuna taarifa zinazohusu mahali alipo.

Baada ya jitihada za kumnasa Liyumba kugomba mwamba, wadhamini wa mshitakiwa huyo Ijumaa waliachiwa huru baada ya Hakimu Mkazi Khadija Msongo kuahirisha shauri hilo.

Akitoa uamuzi wa dhamana kwa Liyumba Jumatatu iliyopita, Hakimu Mkazi Msongo alieleza kuridhishwa na hati iliyowasilishwa, huku pasi yake (Liyumba) ya kusafiria yenye namba A0320091 ikishikiliwa.

Pasi hiyo iliyoonyesha kumalizika muda wake Februari 12, mwaka huu, ilibaki mahakamani hapo kwa uchunguzi zaidi.

Kwa upande mwingine, hati iliyowasilishwa mahakamani hapo na kusababisha Liyumba kupata dhamana, ilisajiliwa kwa kitalu namba 6233 kilichopo Mbezi Juu jijini hapa.

Aidha, hati nyingine zilizowasilishwa mahakamani hapo, zilikataliwa baada ya kubainika kwa na mapungufu kadhaa.

Shitaka la kwanza linalomkabili Liyumba ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma, kwamba kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa ghorofa pacha bila baraka za uongozi wa juu wa benki hiyo.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo anatuhumiwa kuidhinisha malipo ya ujenzi huo bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa BoT na shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa wote, ni kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 221.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya mwaka 2001 hadi 2006, wakiwa ni watumishi wa umma, kwa makusudi au kwa kushindwa kuwa makini na kazi yao.SOURCE: Nipashe 2009-02-23 10:05:32 Na Joseph Mwendapole