Tuesday 31 July 2007

ENERGY PERFORMANCE CERTIFICATES ANDHOME INFORMATION PACKS

Announcement : Home Information Packs
22 May
Communities Secretary Ruth Kelly this afternoon made a statement to the House of Commons on the implementation of Home Information Packs and Energy Performance Certificates. Read a copy of the press release, the full Ministerial statement, and updated Q&A below.
______________________________________________________________
Press statement: ENERGY PERFORMANCE CERTIFICATES ANDHOME INFORMATION PACKS
The Government is today announcing that we will be implementing Energy Performance Certificates (EPCs) and Home Information Packs (HIPs) from 1 August instead of 1 June. The Government has also reached an agreement with the Royal Institution of Chartered Surveyors (RICS) on their judicial review of Energy Performance Certificates.
The Judge, considering the application for Judicial Review by RICS, had issued an Order preventing EPC's from being included in HIPs from 1 June until a court had fully considered the RICs application.
We did not consider it to be acceptable or practical to delay the introduction of EPCs in this way.
We have always made clear greater transparency in the housing market and tackling climate change goes hand in hand. In addition, we have created a new energy assessor workforce - the majority of whom expect to start work in June.
We have therefore been in negotiation with RICS in order to avoid a lengthy delay as a result of the legal process. The Government can today announce an agreement has been reached.
The Government will revise regulations and implement the following changes -
- HIPs and EPCs to start on August 1, implemented on a phased basis. From August 1 packs - including energy performance certificates - will be required for the sale of four bedroom properties and larger. These are the properties which are the most energy inefficient. We will phase in packs for smaller properties as sufficient energy assessors become ready to start work.
- Until the end of the year, we will allow people to market their properties as soon as they have commissioned a pack - rather than making them wait until they have received them.
- As a temporary measure, we will allow EPCs to be up to twelve months old when the property is put up for sale and will consult further on the long-term arrangements for the age of EPCs.
- We will also be inviting councils and registered social landlords to work with us to introduce EPCs on a voluntary basis in social housing, for example at the time of stock transfers. The Government will therefore lead the way in efforts to tackle climate change, whilst providing work for energy assessors in advance of the full implementation of HIPs and EPCs.
Towards the end of the year we will assess the implementation of HIPs and consider what further steps might be needed to maximise the reduction in carbon emissions and drive forward the reform of home buying and selling.
This assessment will be informed by the operation of the market from 1 August; by the results of the area trials; and by a further consultation on the next steps in implementing HIPs and EPCs, which we will begin in the summer.
Communities Secretary Ruth Kelly said:
"We are pleased we have reached an agreement with RICs and potentially avoided a lengthy court case and months of delays.
"The approach we have set-out preserves the principles of HIPs and EPCs, while ensuring a transition period for the people buying and selling their property. Most importantly, it provides an opportunity to make real progress towards cutting carbon emissions from our homes."
Housing Minister Yvette Cooper said:
"Energy ratings for homes will help cut carbon emissions and family fuel bills. Given the serious threat from climate change, it would not have been acceptable for energy certificates to be subject to long legal delays and uncertainty."
Today we are also publishing the latest figures on energy assessor numbers, we now have 2,500 in training, a further 3,200 who have passed their exams, and 1,500 who have been accredited or have applied for accreditation but only 520 of these have been fully accredited. For implementation on 1 June, we would need more than 2,000 to be accredited.
Whilst more than enough are in the system, the current uncertainty caused by this legal challenge and the campaign of misinformation by opponents have had an impact on the numbers of energy assessors who are waiting before paying out for accreditation. The phasing in of the programme will ensure that the numbers of assessors matches the need in the market place.
______________________________________________________________
Home Information Packs: Ministerial Statement 22 May
With Permission, Mr Speaker, I would like to update the House on the Government's proposals for the implementation of Home Information Packs.
It had been the Government's intention to implement Home Information Packs, including Energy Performance Certificates, on 1 June.
In debate last week, reference was made to the Judicial Review requested by the Royal Institution of Chartered Surveyors. This Judicial Review focussed on Energy Performance Certificates - not Home Information Packs.
On Wednesday, the judge issued an interim order, which was received by my Department on Thursday. That Order would have effectively prevented the introduction of Energy Performance Certificates on 1 June, while the case was being considered.
The Government believes that introducing Home Information Packs without Energy Performance Certificates would be neither practical nor acceptable. It is important to introduce Energy Performance Certificates and Home Information Packs at the same time, because cutting carbon emissions should go hand in hand with market transformation.
We have been in detailed discussion with RICS to prevent lengthy legal delays. Both the Government and RICS are committed to the swift and smooth introduction of both Home Information Packs and Energy Performance Certificates. I am pleased we have today reached a pragmatic way forward that gives certainty and allows us to get on with implementation.
As a result, we are therefore proposing to withdraw the Home Information Pack regulations in order to clear the way for successful implementation of revised arrangements.
Although the issue of the judicial review is now resolved, long-running uncertainty has already had an impact on the numbers of energy assessors. For implementation on June 1, we would need at least 2,000 to be accredited, with over 2,500 by the end of the month. Today I am updating the House with the latest figures. There are over 2,500 people currently in training. A further 3,200 have already passed their home inspector or domestic energy assessor exams. Of those, 1,500 have been accredited or have applied for accreditation but only 520 of these have been fully accredited. These figures show that the number of assessors is unlikely to meet our needs for 1 June implementation. Equally, they show that in the long term, there will be enough assessors to meet demand.
The Government remains convinced of the importance of Home Information Packs and Energy Performance Certificates. Home Information Packs will cut costs and delays in buying homes. Energy Performance Certificates will help reduce energy bills and cut carbon emissions from our homes, which, as they make up 27% of our national carbon emissions, could make a big difference in our effort to tackle climate change. The measures in Energy Performance Certificates will cut carbon emissions by nearly a million tonnes every year.
I have always said that the right test of the legislation should be how it brings benefits for consumers and how it protects the environment. Today, therefore, I am setting out a practical way forward.
I propose to change the start date for Home Information Packs to August 1, and intend to phase its introduction.
From August 1 Home Information Packs - including energy performance certificates -will be required for the sale of four bedroom properties and larger. These are the properties where there is the greatest potential to make energy efficiency savings. This will ensure work for those energy assessors who have already been trained and accredited.
We will extend to smaller properties as rapidly as possible, as sufficient energy assessors become ready to work. As we see the number of accredited assessors rise, so more properties will be included in the system.
We are also introducing a number of transitional measures.
First, until the end of the year, we propose allowing people to market their properties as soon as they have commissioned a pack - rather than making them wait until they have received them, in order to avoid unnecessary delays when the systems come in.
Second, to allow energy performance certificates to be implemented at the earliest opportunity, we will make amendments to allow Energy Performance Certificates to be up to twelve months old when the property is put up for sale - extending the current three month age limit.
Third, we are inviting councils and registered social landlords to work with us to introduce Energy Performance Certificates on a voluntary basis in social housing, for example at the time of stock transfers. This will also provide work for energy assessors at an early opportunity.
I will shortly bring forward revised regulations to implement the changes I have outlined.
Towards the end of the year we will assess the implementation of Home Information Packs and consider what further steps might be needed to maximise the reduction in carbon emissions and drive forward the reform of homebuying and selling.
This assessment will be informed by the operation of the market from 1 August; by the results of the area trials; and by a further consultation on the next steps in implementing Home Information Packs and Energy Performance Certificates, which we will begin in the summer.
Mr Speaker, the approach I have set out gives clarity to everyone about the next steps.
It delivers Home Information Packs and Energy Performance Certificates, removes uncertainty for energy assessors and others, and ensures a smooth transition for the people buying and selling their property.
Most importantly, it provides an opportunity to make real progress towards cutting carbon emissions from our homes.
______________________________________________________________
Q&A for ENERGY PERFORMANCE CERTIFICATES ANDHOME INFORMATION PACKS
Q.The judgement was only about EPCs - why can't you do HIPS on their ownA.As the statement said, the HIP and EPBD regulations are tied together. They could not be separated quickly, and that would have made no sense given the package we have announced.
Q. Why don't you just scrap this failed policy?A. We believe that tackling carbon emissions from homes and getting a better deal for home buyers and sellers is the right thing to do. Key green groups - e.g. FoE and WWF - agree. That is why we have taken pragmatic steps to address concerns whilst preserving the principles of HIPs and EPCs and ensuring a smooth transition for the market.
Q. Why don't you just fight RICS in the courts if you are so confident of your case?A. We have reached an agreement with RICS which gives us a pragmatic way forward and will prevent lengthy legal delays. Both we and they are committed to the swift and smooth introduction of both HIPS and EPCs.
Q. Are you just doing this because there were not enough energy assessors?A. The recent uncertainty created by the court case and deliberate attempts to disrupt delivery of the programme have meant that some assessors have adopted a "wait and see" approach before signing the cheque to become accredited. The approach we have announced today should give them the reassurance they need. There are over 2,500 people currently in training. A further 3,200 have already passed their home inspector or domestic energy assessor exams. Of those, 1,500 have been accredited or have applied for accreditation but only 520 of these have been fully accredited. So there are more than enough in the system, and the phasing should allow us to build up numbers in a way which matches need in the market place.
Q. If you are consulting now, why didn't you consult in the first place?A. EPCs originally formed part of mandatory HCRs, and consultation was on that basis. When we separated the EPC from the HCR last summer we did not change the existing policy on the age of certificates. Consumers will take more notice of up-to-date information.
Q. There will not be any work for energy assessors until 1 August.A. 1 August phasing date is designed to ensure we have enough assessors in place to meet demand for EPCs. From August 1 packs - including energy performance certificates - will be required for the sale of four bedroom properties and larger. These properties - where there is the greatest potential to make energy efficiency savings - will ensure work for those energy assessors who have already been trained and accredited.We are also inviting councils and registered social landlords to work with us to introduce EPCs on a voluntary basis in social housing, for example at the time of stock transfers. This will also provide work for energy assessors at an early opportunity.


Home Info Pack? Whats That?
A Home Info Pack (also known as a Home Buyer Pack or Home Seller Pack) is part of the Governments supposed commitment to making UK property purchases easier. Due to Part 5 of the Housing Act 2004 home owners or their agents have a legal obligation to provide a Home Information Pack when marketing a property. Home Information Packs will provide important information to prospective purchasers at the very start of their interest in a new home, giving increased transparency on key issues and meaning any offer to purchase is based on an informed decision. Recent News No water risk details in home information packs Ministers faced renewed criticism over the flooding crisis after it emerged that controversial new home information packs (http://news.independent.co.uk/uk/this_britain/article2819587.ece) will not...
Tue, 31 Jul 2007 00:00:00 +0100 Status anxiety hits homeowners Two in three Brits in their 30s and 40s are now suffering from status anxiety about their homes, according to research from Standard Life Bank. Living in a house that looks good and is located in the best area a Thu, 17 May 2007 00:00:00 GMT Home Info Pack LinksHome Information Packs - Everyone involved in buying and selling a home will need to know about Home Information Packs (HIPs). Home Seller Packs - Home Information Packs have proved a permanent embarrassment for the Government ever since the idea was first conceived almost a decade ago. Seller's packs as they are also known are in fact no bad idea, and no big deal. HIPs - We cannot police new home seller packs. Home sellers who market their properties without a pack will be liable for a £200 fine. Interested in becoming a Home Inspector? - Do you want to become a Home Inspector? All the information you need is available from the web site.

{wikipedia}

MHE. BENJAMIN MKAPA:Ushupavu wa Uongozi (The Courage of Leadership)

HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CCM, DODOMA, 25 AGOSTI 2004


Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara),
Mhe. John Samwel Malecela, Mb.;
Rais na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Mzee Ali Hassan Mwinyi;
Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Dkt. Salmin Amour;
Katibu Mkuu wa CCM,
Mhe. Philip Mangula;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu;
Mabibi na Mabwana:

Karibuni nyote tena kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi.
Leo nimeamua kutoa hotuba, tena iliyoandikwa, maana jambo nitakalo kulizungumza ni zito na nimelitafakari kwa muda sasa. Napenda kuzungumza nanyi kuhusu Ushupavu wa Uongozi, kwa Kiingereza: “The Courage of Leadership.”
Nafanya hivyo kwa vile tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani, uchaguzi ambao tuna kila sababu ya kuamini kuwa utaendeleza Awamu ya Sita ya Uongozi Zanzibar, na utaanzisha Awamu ya Nne ya Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Chama Cha Mapinduzi. Na ningependa tujiandae vizuri kifikra, kimaadili, kiutawala, na kwa kujikumbusha kanuni na taratibu zetu zote.
Napenda leo tujiulize swali la msingi kabisa: Sisi Chama Cha Mapinduzi tunataka uongozi; vema, lakini je Chama chetu kinao ushupavu wa uongozi unaohitajika katika mazingira ya Karne ya 21? Wagombea wetu watarajiwa nao je?
Waheshimiwa Wajumbe:
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi imeorodhesha malengo na madhumuni ya CCM, na mwanzo kabisa kwenye orodha hiyo ni:

“Kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.”

Na zipo njia mbili kubwa za mtu kushinda uchaguzi. Moja ni kuhakikisha unakuwa mgombea wa chama chenye nguvu na mvuto, kama ilivyo CCM hivi sasa. Maana yake ni kuwa hata wewe mgombea ungekuwa hovyo kiasi gani, utabebwa na chama, na utachaguliwa kuwa diwani, mbunge au rais, kwa sababu tu ya chama. Njia nyingine na ya pili ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi wampigie kura, sio chini ya kivuli cha chama chake. Napenda leo tujikumbushe kuwa yote haya mawili ni muhimu: Chama imara, chenye ushupavu wa uongozi; na wagombea imara, wenye sifa, uwezo na ushupavu. Na kuhakikisha kabisa, yote mawili ni muhimu na ni vema yaambatane.
Napenda tujikumbushe maana upo uwezekano wa wana-CCM kubweteka. Kwa vile tunajua chama chetu kina nguvu na mvuto, hatuweki mkazo mkubwa kwenye kujinoa binafsi. Badala yake tunapigana vikumbo kutafuta kuteuliwa, kwa kuamini ukishateuliwa ndio “umeula”. Na tukishaelekea huko, hakutakuwa na kingine kinachotusukuma ila ubinafsi—ubinafsi wa kusema mimi lazima niendelee, na anayenisogelea ni adui; au ubinafsi wa kusema wewe sasa imetosha, sasa ni zamu yangu. Upo uwezekano pia kuwa tusipokuwa waangalifu, ajenda yetu kuhusu mwakani haitaandaliwa na sisi, katika CCM, bali na wapinzani wetu na vyombo vya habari. Wapinzani wanataka kutuvuruga na kutugonganisha, na wenye magazeti wanataka kuuza na kupata faida. Lakini wajibu wa hatma ya nchi yetu umo mikononi mwa CCM, si mikononi mwa wapinzani wala waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari. Lazima tuuchukulie wajibu huo kwa uzito unaostahili, na tujenge ushupavu wa uongozi wa kuutimiza.
Hivi sasa waandishi wa habari na vyama vya upinzani wanatuchokoza tujielekeze kwenye kuzungumzia wagombea wetu kwa uchaguzi wa mwakani. Tusikubali. Tukiwaendekeza, tutajikuta tunatafuta au kuunga mkono wagombea kabla ya wakati, na hivyo kuanza kugawanyika na kudhoofika, badala ya kushirikiana kubuni malengo na dira kwa miaka 5 ijayo. Vyama vya upinzani na vyombo vya habari wanataka tuzungumzie watu, badala ya kuzungumzia kazi muhimu ya chama iliyo mbele yetu. Kama ilivyo mtego wowote, huu pia unavutia, hasa kwa wanaokusudia kugombea uongozi. Tuwe shupavu kuukwepa mtego huu.
Waheshimiwa Wajumbe:
CCM ina nguvu. Lakini nguvu peke yake haitoshi. Nguvu hiyo inapasa kudhihirisha na kuainisha mwelekeo wake. Huu ni wakati wa kujenga ushupavu wa uongozi, ili CCM iandae ajenda na mwelekeo wa taifa, na iongoze taifa—kwa maana ya watu na raslimali—katika karne ya 21 ya utandawazi. Ushupavu huo ndio utasaidia kuhakikisha chipukizi wa CCM nao watakuja kuongoza nchi hii.
Mimi ni muwazi na mkweli: Naamini hivi sasa wananchi wana wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya uongozi wa taifa letu baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani. Wasiwasi huo ni wa kweli, na upo, ingawa wanajua CCM itashinda. Tujiulize kwa nini wana wasiwasi. Wanaona mapungufu gani ambayo sisi viongozi wao ama hatuyaoni, au hatuna ushupavu wa kuyashughulikia?
Nizungukapo mikoani wazee wa CCM hunijia, pamoja na viongozi wengine wa CCM, na hata wananchi wa kawaida, wakinisihi nihakikishe CCM inachagua vizuri wagombea wake katika ngazi zote za uongozi. Wanahofu kuwa pengine hatutakuwa makini vya kutosha, na kwamba pengine CCM italewa nguvu yake na kubweteka. Wangejua tutakuwa makini wasingehofu. Huo ndio ukweli. Na hofu yao inatokana na kujua, kama alivyobainisha Baba wa Taifa, kuwa: “Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba.”
Pamoja na kelele zote za wapinzani na magazeti, mwananchi wa kawaida anajua kuwa CCM ndiyo mhimili wa taifa hili, na ndiyo bima yake dhidi ya matatizo yanayozikumba nchi nyingine, ikiwemo baadhi ya nchi jirani. Ndio maana hata wapinzani wenyewe wanafuatilia sana afya ya Chama Cha Mapinduzi. Tukipiga chafya sisi, kila mtu anapata homa. Sisi tuna dhamana ya uongozi wa nchi hii, dhamana ya amani, usalama na utulivu wa nchi, na dhamana ya kuongoza vita dhidi ya umaskini. Tujikumbushe kila mara uzito wa dhamana hiyo. Na wale miongoni mwetu tulio Serikalini, tuliokula viapo vya utumishi wetu, tutafakari tena uzito wa viapo hivyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakula viapo vitatu:

· Kiapo cha kwanza ni cha utii, ambapo anaapa kuwa atakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wake wote, na kwamba ataihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

· Kiapo cha pili ni cha Rais, ambapo anaapa kwamba atatenda kazi zake za Urais kwa uaminifu na kutimiza wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba atawatendea haki watu wote kwa mujibu wa Sheria, mila na desturi za Tanzania bila woga, upendeleo, huba wala chuki; na,

· Kiapo cha tatu ni cha kudumisha Muungano, ambapo anaapa kwamba ataitetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wao, Mawaziri wanakula viapo viwili. Kiapo cha utii kinachofanana na kile cha Rais, na kiapo cha Waziri ambapo wanaapa kuwa wataitumikia vema na kwa moyo thabiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi za Uwaziri na kuwa kwa wakati wote watamshauri kwa hekima na uaminifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa kwa vyovyote vile hawatatoa siri za Baraza la Mawaziri.
Waheshimiwa Wajumbe:
Hivi ni viapo vizito. Tunaapa sisi tulio Serikalini, lakini tumetumwa na Chama. Hivyo viapo hivi vinakipa Chama wajibu kuhakikisha waliomo Serikalini wanaishi na kutumikia nchi yetu kwa utimilifu wa viapo hivyo. Wapinzani hawali viapo kama hivi, hivyo wanaweza kupayuka hovyo na kukosa umakini. Hawana wajibu tulionao sisi. Lakini sisi tunaokula viapo hatupaswi kwa vitendo vyetu na kauli zetu kuonekana na sisi ni wapayukaji hovyo na watu wasio makini. Tukionekana au kufikiriwa hivyo, hatutoshi kuongoza!!
Lazima, kwa ushupavu, tuwatoe wananchi hofu, waishi na kufanya kazi zao wakiwa na uhakika kuwa nchi yao imo, na itaendelea kuwa, mikononi mwa viongozi waadilifu, na Chama makini. Tupende tusipende, hofu miongoni mwa raia ni hisia, na hata kielelezo, cha mapungufu ya uongozi. Na hofu hiyo huzidi waonapo watu wanataka kuingia Serikalini kwa uhodari wa ujanja, hila au rushwa, badala ya kutaka kuingia kwa uhodari wa ushupavu wa kutumikia nchi.
Siku moja walikutana marafiki wawili waliokuwa wamepoteana kwa muda mrefu. Mmoja akamuuliza mwenziwe, “Hivi yule kaka yako aliyekuwa anatafuta kazi Serikalini anafanya nini siku hizi?
Rafiki yake akajibu, “Ah, yule hafanyi kitu siku hizi. Alipata ile kazi ya Serikali aliyokuwa anaitafuta!”
Waheshimiwa Wajumbe:
Iwapo wananchi watapata hisia hizi, au iwapo kwa vitendo vyetu tutawadhihirishia, kuwa tunatafuta uongozi Serikalini ili tusifanye kazi zao, lakini tushibe, watakuwa na hofu kila tunapoelekea kwenye uchaguzi.
Tunahitaji ushupavu wa uongozi. Nikiwaulizeni hapa mmojammoja, nina uhakika wengi watasema kuwa zimeanza kampeni za chinichini huko mikoani na wilayani. Wengine wameniambia wapo wenye mkakati wa kununua wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa. Kama ni kweli, ujasiri wa viongozi huko mliko wa kusimamia maadili uko wapi? Kwa nini sisikii viongozi wa CCM wanaokerwa na hali hiyo wakiikemea katika vikao vya ndani? Kwa nini taarifa za namna hiyo haziji rasmi, kwa taratibu zetu, lakini zinakuja kwa njia ya tuhuma, minong’ono na kupakana matope? Waasisi wetu wasingekuwa jasiri na shupavu tusingepata uhuru, wala kufanikisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Ujasiri na ushupavu wetu sisi, tunaodai haki ya urithi wa waasisi wetu, uko wapi?
Ninyi ndiyo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Na mojawapo ya kazi za Halmashauri hii ni “Kudumisha uangalizi juu ya vitendo vya Wanachama na Viongozi wa CCM na endapo itadhihirika kwamba tabia na mwenendo wa Mwanachama fulani vinamwondolea sifa za uanachama au uongozi itakuwa na uwezo wa kumwachisha au kumfukuza uanachama au uongozi alio nao…” (Katiba ya CCM, 77(8)). Haya ni madaraka makubwa, lakini sioni ushupavu wa kuyatumia katika ngazi zote za uongozi wa Chama. Badala yake ni malalamiko ya chini kwa chini. Hiyo ni hatari kubwa kwa Chama, na kwa Taifa.
Nasema ninyi ndio Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi. Hatma ya CCM na Taifa letu imo mikononi mwenu. Jiulizeni: Kama kweli hiyo minong’ono ni ya kweli, hivyo ndivyo mnavyotaka iwe? Ndio mustakabali wa Chama chetu mnaoutaka—kwamba maslahi binafsi yawe na nguvu kuliko maslahi ya CCM na Taifa? Kama sivyo, ujasiri wenu wa kusimamia maadili na haki uko wapi? Nitauliza maswali mengi leo.
Kwa asili yetu, huko tulikotoka, kulikuwa hakuna fedheha kama ile ya mwanachama kujulikana kuwa eti amenunuliwa. Tuliona kununuliwa ni sawa na utumwa, ni sawa na kuuza utu wako. Maana, huamui tena kwa akili aliyokupa Mwenyezi Mungu, bali kwa kutumwa na aliyekununua. Utakuta mtu na akili yake anatetea ambacho hakiwezekani kutetea. Tutastahilije kuongoza nchi katika mazingira hayo? Mtu mzima una macho, lakini unakuwa huoni kwa kupofushwa na fedha; una masikio lakini husikii kwa vile masikio yako yamezibwa na ahadi za vyeo. Kisha unapojiangalia kwenye kioo, unamwona nani: unaona kiongozi, au unaona kibaraka?
Nasema sisi katika Halmashauri Kuu ya Taifa, wenye jukumu la kusimamia maadili, lazima tuwe mfano wa kufuata maadili, mfano wa kuheshimu Katiba; mfano wa kuheshimu haki za kila mwanachama. Agombeaye nafasi si adui. Na tusisahau kuwa sifa moja ya kiongozi iliyo ndani ya Katiba ni kuwa, “Awe ni mtu aliyetosheka, na asiwe mtu aliyetawaliwa na tamaa.” (Katiba ya CCM, (17(1)). Aliyetawaliwa na tamaa yuko radhi kuhujumu haki za wengine kugombea, yuko radhi kuwazulia kashfa anaowaona ni washindani wake, na yuko radhi hata kuhujumu maslahi ya Chama, ili mradi tu apate anachokitamani. Hatujengi Chama namna hiyo!
Ipo hadithi ya mgombea mmoja kwenye uchaguzi aliyetaka ushauri wa kiongozi wake wa chama kabla ya kampeni kuanza.

Mgombea: “Nadhani jambo muhimu kwenye kampeni hii ni mimi kuelezea na kusimama kwenye rekodi yangu.”

Kiongozi wa chama: “Hapana. Jambo muhimu ni wewe kukanyaga na kupondaponda rekodi ya mpinzani wako.”

Sasa, pengine mbinu hiyo inafaa kwa wapinzani kutoka vyama tofauti. Lakini inawapa wananchi mashaka pale inapotumika miongoni mwa wagombea kutoka chama kimoja. Wana-CCM tuiepuke! Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tahadhari ni kwamba adui wa CCM anaweza kuwa yupo miongoni mwetu. Kikulacho kinguoni mwako. Hakuna wapinzani wenye nguvu ya kutudhoofisha. Tukidhoofu, tumejidhoofisha wenyewe, na hasa kwa kuendekeza ubinafsi.
Hivi Mbunge au Diwani ambaye haoni lolote jema lililofanywa na Serikali ya CCM anafanya nini ndani ya CCM? Na atajinadi vipi kwa rekodi ya utekelezaji wa sera za CCM? Nchi hii imepata sifa kubwa kwa kazi zilizofanywa na Serikali ya CCM, halafu Diwani au Mbunge wa CCM anasema hakuna kilichofanyika. Nauliza tena. Anafanya nini ndani ya CCM? Ana tofauti gani na wapinzani? Mwalimu Nyerere alituonya tuhakikishe CCM haiwi dodoki linalonyonya maji masafi na maji machafu sawia. Ushupavu wa NEC uko wapi?
Waheshimiwa Wajumbe:
Sitaki ieleweke kwamba Wabunge na Madiwani wa CCM hawana haki ya kuikosoa Serikali. Wanayo haki hiyo. Lakini, kuna tofauti ya kukosoa utekelezaji wa sera, ambao ni wajibu wa Wabunge na Madiwani wa Chama Tawala; na kukosoa sera yenyewe, ambao ni wajibu wa Wabunge na Madiwani wa Upinzani. Katiba na busara zinataka tupambanue wapi na lini tukosoe sera na utekelezaji wake. Mbunge na Diwani lazima aamue yuko upande gani.
Na hata ukosoaji wa utekelezaji sera lazima nao uwe wa staha, wa kujenga heshima na kuimarisha umoja, si ukosoaji wa kudhalilisha, kubomoa na kukomoa. Nitatoa mfano. Hivi Mbunge au Diwani anaposema madarasa ya MMEM hayafai kabisa, maana yake ni nini. Kwanza, kauli hiyo si ya kweli kwa ujumla wake. Maana mimi nimezunguka nchi hii kuliko wengi wenu. Nimeona madarasa ya MMEM vijijini ambayo ni mazuri kuliko baadhi ya yaliyopo mijini. Nimezungumza na wahisani wetu ambao wamekiri hivyo. Nimepokea barua za pongezi kutoka kwao.
Ni kweli kuna maeneo machache ambapo ujenzi wa madarasa hayo haukuwa mzuri. Lakini, tatizo si sera, wala MMEM yenyewe, wala Waziri mhusika. Tatizo ni uongozi wa eneo linalohusika; na Mbunge au Diwani ni sehemu ya uongozi huo. Kashfa ambayo Mbunge au Diwani anafikiri anaizua, anajizulia yeye mwenyewe kwanza. Iweje maeneo ya Wabunge au Madiwani wengine yawe na madarasa ya MMEM mazuri yanayosifiwa mpaka Washington, na ya kwake yeye ndiyo yawe mabaya? Kulalamika Bungeni au kwenye Halmashauri, badala ya kuongoza kusahihisha makosa, ni mapungufu ya ujasiri wa uongozi.
Nasema, tunahitaji ushupavu wa kuongoza. Ushupavu huo si hotuba nzuri Bungeni au kwenye Halmashauri; ni ushupavu wa kukaa na wananchi na kuwaongoza. Penye makosa ni kusaidia kusahihisha, si kugeuka mwangwi wa kuchafua rekodi ya Serikali ya CCM. Fedha za Serikali zinaliwa kwenye jimbo la Mbunge, lakini anakuja kupigia kelele Bungeni. Anaogopa kusemea kwenye jimbo lake kwa kukosa ujasiri. Hayo nayo ni mapungufu ya ushupavu wa uongozi. Halmashauri au Bunge la watu wenye haraka ya maendeleo ni mahali pa kubadilishana uzoefu wa uhamasishaji na uchangiaji maendeleo huko Wabunge na Madiwani wanakotoka, kila mmoja akieleza aliyoyafanya yeye kwenye jimbo lake, au kata yake, kusudi wengine wamuige. Tusigeuze Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri kuwa mahali pa kumlaumu kila mtu isipokuwa wewe mwenyewe. Narudia. Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ina wajibu kusimamia nidhamu ya Chama. Bila nidhamu, punde si punde hatutakuwa na Chama.
Waheshimiwa Wajumbe:
Nchi rafiki, wahisani na mashirika ya kimataifa nao wamenieleza hofu yao. Wawekezaji wamenieleza hofu yao. Wanataka uhakika wa kitakachotokea baada ya uchaguzi mwakani. Na kwa nchi maskini na tegemezi kama yetu, ambapo asilimia 42 ya bajeti yetu bado inawategemea wahisani, hatuwezi kupuuza hofu yao. Kwa nchi ambayo fursa za ajira na mapato ya Serikali hutegemea zaidi na zaidi uwekezaji wa sekta binafsi, hatuwezi kupuuza hofu ya wawekezaji.
Si kwamba wana husuda tu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu; wengi wao ni watu makini wanaotaka uhakika kuwa yale ambayo sisi na wao tumekubaliana kuwa ni mema na ya maslahi kwa nchi yetu yatadumishwa; na yale ambayo si mema na hayana maslahi kwetu, ambayo tumeanza kuyashughulikia, kuyafuta au kuyakomesha, yataendelea kushughulikiwa. Wao pia wanajua CCM itashinda mwakani, lakini bado wana wasiwasi. Kwa nini? Kwa kazi kubwa ya mageuzi na kukuza uchumi tuliyoshirikiana nao kuifanya, wangependa Tanzania ipige hatua mbele kwa kasi, si kuanza kubabaika, kusuasua, au kurudi nyuma. Kila mara ninarudia kuwaambia wahisani na wawekezaji kuwa mageuzi haya si yangu mimi binafsi, na kwamba ninaongoza utekelezaji tu wa Mwelekeo, Sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Lakini bado wana hofu. Najiuliza, kwa nini? Nanyi nataka mjiulize: Kwa nini, na kwamba mtazamo huo unaashiria nini?
Waheshimiwa Wajumbe:
Leo napenda, kwa unyenyekevu kabisa, nikupeni tathmini yangu kwa nini wananchi wanahofu, kwa nini wanachama wenzetu wanahofu, na kwa nini wahisani na wawekezaji wanahofu. Kwa tathmini yangu binafsi, hofu yao inatokana na mambo mawili ya msingi yanayoashiria mapungufu ya ushupavu wa CCM katika kuongoza nchi yetu kwa kuzingatia mahitaji, na mazingira halisi, ya dunia ya leo na ijayo.
Kwanza, wanashuhudia utekelezaji wa baadhi ya mambo yaliyo katika Ilani yetu, na Mwelekeo wa Sera za CCM, ukichelewa au kusuasua kwa upinzani wa baadhi ya wenzetu katika CCM, au kwa kukosa umakini miongoni mwa baadhi ya wenzetu tuliowakabidhi kazi ya kusimamia utekelezaji. Mara kadhaa wamesikia kuwa imebidi mimi mwenyewe kukutana na Wabunge wa CCM kuwakumbusha kwamba Serikali inachotaka kukifanya ni utekelezaji wa Sera za CCM. Mara kadhaa inabidi tufanye semina za Chama katika ngazi mbalimbali kuelimishana na kukumbushana sera hizo. Sera zetu zinapopingwa kidogo na wapinzani wetu au vyombo vya habari, au Asasi Zisizokuwa za Serikali, ambao wengi wao hawaitakii CCM mema, baadhi ya wenzetu wanaanza kuyumba. Hofu ya wahisani na wawekezaji inatokana na mapungufu ya ushupavu wa CCM kutetea sera zake yenyewe, hata pale ambapo mafanikio yake yanaonekana wazi. Wanasikia kauli tofauti kutoka ndani ya CCM. Njia pekee ya kuondoa hofu hiyo ni kurejesha umoja, mshikamano na ushupavu wa uongozi wa taifa letu ndani ya CCM.
Chanzo cha pili cha hofu yao, kwa tathmini yangu, ni kuwa kwa miezi kadhaa sasa wanaona sisi wenyewe kwenye Chama Cha Mapinduzi tukitaka kutoana roho kwa kujiweka vizuri kwa Uchaguzi Mkuu mwakani. Kama nilivyosema, baadhi ya madiwani waliopo wanafanya kila mbinu wasitokee wengine kuwania nafasi zao. Baadhi ya wabunge waliopo wanafanya kila mkakati kulinda wanachokiona kama vile ni himaya yao. Sisemi wanaotarajiwa au kushabikiwa kujipanga kuwania Urais!!
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kugombea au kutetea nafasi za uongozi ni haki ya kila mwanachama. Tatizo langu si hilo. Tatizo langu ni kuwa wakati bado. Kama nilivyosema awali, tatizo langu ni pale tunapogombea nafasi kabla ya kukubaliana hao tutakaowapendekeza kugombea watakwenda kufanya nini. Hivyo naomba tuache kwanza kuzungumzia, na pengine hata kuchukiana na kuhujumiana, juu ya majina ya wagombea.
Tusitangulize mkokoteni kabla ya farasi. Tusiwe kama wapinzani. Sisi tuzungumze kwanza kuhusu programu na Ilani ya CCM kwa miaka 5 ijayo. Tuzungumze mambo ya maslahi kwa wananchi na taifa badala ya yale ya maslahi ya wagombea na wapambe wao. Tuzungumze kukuza uchumi wa kisasa katika mazingira ya utandawazi. Tutafakari changamoto zilizopo na zijazo, na kisha ndipo tuone nani kati ya makada wetu wanaweza, na wanatosha, kuaminiwa kukabidhiwa usimamizi wa utekelezaji wake.
Mambo hayo yatatutofautisha na wapinzani na ndiyo yatatupa vigezo vya kisayansi vya kujua nani miongoni mwetu anafaa kwa uongozi, kwenye ngazi ipi, kwa malengo gani. Tutapata pia vigezo vya kupima utendaji wa tutakaowachagua. Kama tunataka kujenga ushupavu wa uongozi lazima tuanze hivi. Kazi ijulikane kwanza; majina ya watakaosimamia kazi hiyo yaje baadaye.
Maana CCM inayo hazina kubwa ya wanaofaa kuwa madiwani, wabunge, na marais. Chama kimoja cha siasa kiliitisha mkutano wa kura za maoni kupata mgombea wa chama hicho. Mmoja kati ya ambao hawakushinda akalalamika, “Mimi nilisikia kabisa sauti za wananchi wakinitaka nigombee!”
Rafiki yake akamfariji, “Usijali rafiki yangu. Pengine sauti hiyo ilikuwa yako mwenyewe ukiwaza kwa sauti.”
Waheshimiwa Wajumbe:
Ipo tofauti kubwa kati ya Chama kuwa na nguvu, na Chama kuwa shupavu. Nguvu ya CCM leo ni ya kihistoria; ni ya huko tulikotoka kwa waasisi wetu, na mazingira tofauti ya wakati huo. Na nguvu hiyo imeegemea sana kwenye heshima ya waasisi hao. Tuelekeako, nguvu ya CCM itategemea zaidi ushupavu wa uongozi wa leo na wa kesho, na hasa katika kusimamia maadili ya utendaji katika mazingira tofauti kabisa kitaifa, kikanda na kimataifa. Ushupavu wa uongozi una sifa nne kuu: Kwanza ni upeo mkubwa wa kubuni malengo na dira; Pili, ni uongozi madhubuti wa watu na raslimali kuelekea kwenye malengo hayo na kuzingatia dira hiyo; Tatu, baada ya kuridhia malengo, ni ung’ang’anizi na kukataa kuyumbishwa bila sababu za msingi; na Nne ni ujasiri wa kusimamia na kutetea maadili. Maana kwa hakika, asiye na maadili hawezi kuwa shupavu.
Kuongoza ni kupanga kwanza. Mipango mizuri huleta maamuzi mazuri kimkakati na kiutendaji. Chama Cha Mapinduzi kinapaswa kuongoza kwa kupanga; ili iwe rahisi kwa Serikali yake kutekeleza. Uzoefu wangu wa kuongoza Chama hiki na Serikali yake ni kuwa Chama kimeiachia Serikali madaraka ya kupanga, lakini wakati wa maamuzi ya mkakati na utendaji, kama nilivyosema, wanatokea viongozi wa Chama, wakiwamo Wabunge na Madiwani wanaochelewesha maamuzi, hata pale ambapo msingi wa maamuzi hayo ni sera za Chama.
Waheshimiwa Wajumbe:
Chama Cha Mapinduzi ndicho hasa kiongozi wa nchi hii. Au tuseme hivyo ndivyo inavyopasa kuwa. Chama kwanza, mtu baadaye. Ndiyo maana huko nyuma tukasema, “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Nami leo naongeza: Chama shupavu, huzaa viongozi shupavu.
Mtaalamu mmoja wa menejimenti alisema: “Wajibu wa kwanza wa kiongozi ni kuwafafanulia anaowaongoza hali halisi.” Kama Chama Cha Mapinduzi kinataka kuendeleza sifa zake za uongozi, na nguvu yake katika siku za usoni, lazima kiwe chama shupavu, chama kisichoogopa kusimamia maadili yake, chama kisichoogopa kusema ukweli, chama cha kuwafafanulia wananchi hali halisi ya tulipo, na mahitaji na masharti ya mafanikio ya huko tuendako.
Waheshimiwa Wajumbe:
Ninakusudia mwishoni mwa mkutano wetu huu kutangaza timu ya kuandaa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, na kuwataka kuikamilisha kabla hatujafikia kipindi cha kuteua wagombea. Kama nilivyosema, hii ina faida mbili. Kwanza Ilani hiyo ndiyo itamwezesha anayetaka kugombea aitafakari vizuri na kujishauri yeye mwenyewe iwapo anaona anazo sifa na nia thabiti ya kutekeleza Ilani hiyo, akijua sisi wengine tutamtarajia afanye hivyo kwa niaba ya Chama. Pili, Ilani hiyo, na majukumu itakayokuwa imeyaainisha, itatuwezesha sisi kwenye Chama kubaini ni kada gani miongoni mwetu anafaa kugombea wadhifa gani, kwa malengo na sababu gani, na kwa kipindi gani. Maana, hatimaye, katika kuamua nani awe mgombea wetu wa Udiwani, Ubunge na Urais, kigezo cha msingi ni uwezo wa kutekeleza sera na malengo ya Chama. Uhodari binafsi wa kampeni si sifa ya msingi, maana jukumu la kampeni kimsingi ni la Chama, si la mgombea binafsi.
Naomba sana tujifunze kwa marafiki zetu wa siku nyingi, Wachina. Hapana shaka kuwa kiongozi hasa wa China ni Chama cha Kikomunisti cha China. Chama hicho kina uwezo mkubwa na ushupavu wa kupanga na kusimamia mwelekeo, si wa Chama tu, bali wa nchi nzima. Kila awamu ya uongozi nchini China inapangiwa majukumu ya msingi (Central Tasks), tena yanapangwa mapema kabisa, na yanapangwa na Chama, hayapangwi na Serikali. Kisha kila awamu inapatiwa viongozi wanaolingana na kushabihiana na mahitaji ya majukumu hayo ya msingi. Hivi leo, tayari wanajua majukumu ya miaka 20 – 25 ijayo, na tayari wanaandaa viongozi wa kuyasimamia majukumu hayo. Huo ndio ushupavu wa uongozi ninaouzungumzia.
Uongozi shupavu hauogopi kubadili mkakati iwapo ni lazima kufanya hivyo. Leo China ina uchumi wa soko unaoshindana, na kwa kweli unaowatoa jasho, wakongwe wa uchumi wa soko kwenye nchi za Magharibi. Leo China, kwa uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, imeweka ndani ya Katiba yao haki ya kumiliki mali na raslimali binafsi. Nani angeamini, miaka 10 tu iliyopita, kuwa China ingefanya hivyo? Wameweza kwa vile hawaogopi kukubali ukweli kuwa dunia imebadilika; hawaogopi kuwaeleza wananchi wao hivyo; hawaogopi kubuni mipango na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo; hawaogopi kuwaonyesha wananchi wao njia sahihi ya kuinusuru nchi yao, na kuwaongoza katika njia hiyo; na hawaogopi kusimamia maadili ya Chama chao. Wakishakubaliana kwenye Chama wote wanazungumza lugha moja. Ukimsikiliza mmoja ni sawa na umewasikiliza wote.
Sisi hapa tunababaika kwa nini? Wakati mwingine, ungempeleka mgeni kutoka nje ya nchi kwenye Bunge letu, kwenye Baraza la Wawakilishi, au kwenye Mabaraza ya Madiwani, akisikiliza mijadala hawezi kujua anayezungumza ni wa Chama Tawala au anatoka kwenye vyama vya upinzani. Tunapimana uhodari wa ubishi, badala ya uhodari wa kuelezea sera na kuongoza utekelezaji wake kwa makini na ushupavu. Maneno hayajengi nchi. Nchi gani imejengwa kwa uhodari wa maneno? Nchi inajengwa kwa kazi. Tukishaamua sera tunahitaji ujasiri wa kutenda, si wa maneno. Ukiwepo ubishi uwe wa kasi na ubora wa utendaji, si wa sera tena.
Nchi pia haijengwi kwa madai. Maana tunazoea kila mara kuuliza: Serikali ina mpango gani? Serikali inafanya lini jambo hili au lile? Serikali italipa lini mshahara wa kutosha? Na hakuna anayekwambia fedha zitatoka wapi. Hakuna anayejenga hoja kuwa uwezo utoke wapi, au utokane na nani! Na sisi ndio viongozi, lakini hatuna ujasiri wa kulinganisha mapato na matumizi, wala matokeo yake. Uwazi na ukweli, ushupavu na ujasiri.
Haifai viongozi wa Chama hiki wakose ujasiri wa kueleza ukweli wa uwezo mdogo, kama alivyokosa ujasiri bwana mmoja aliyeambiwa na mkewe waende kununua vitu vya sherehe ya mwaka mpya. Alikuwa hana fedha za kutosha, na alikuwa hana ujasiri wa kutosha. Alipofika kazini akamwendea mkubwa wake wa kazi. Akamwambia, “Tafadhali bwana mkubwa, naomba ruhusa niende na mke wangu kununua vitu vya sherehe ya mwaka mpya.”
“Haiwezekani”, akajibu mkubwa wake wa kazi. “Tuna kazi nyingi sana.”
Bwana yule akashusha pumzi, “Nakushukuru sana, bwana mkubwa. Una huruma tele kwa kunikatalia.”
Waheshimiwa Wajumbe:
Wakati wa kuandaa Ilani mpya ni wakati pia wa kufanya tathmini yetu ya ndani ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2000. Mimi nadhani tumefanya vizuri, lakini kufanya vizuri kwa kipindi kilichopita si sifa pekee ya kuaminiwa kuendelea kuongoza nchi. Utekelezaji mzuri wa Ilani ya 2000 ni ushahidi wa usahihi wa sera kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine ni ushahidi kuwa sisi ni waungwana, na kwa kadri ya uwezo wa Serikali tunatekeleza tunayoyaahidi.
Uungwana huo ni sifa nzuri, lakini tutakachowaahidi wananchi kwa miaka 5 ijayo nacho ni muhimu, tena pengine ni muhimu zaidi. Yaliyopita yamepita; japo ni mema, wananchi watakuwa wanaangalia yajayo. Lazima tujiandae vizuri kuelezea tuliyoyafanya, na yale tunayoahidi kuwa tutayafanya. Hata kama awamu ya sasa italala salama, wananchi watatahayari: wataamka salama na awamu ya taswira gani?
Kwa heshima na unyenyekevu, nathubutu kusema kuwa mwaka 2000, CCM ilipata ushindi mkubwa kuliko mwaka 1995, si kwa sababu ya uhodari wetu wa maneno bali kwa vile wananchi walianza kuelewa usahihi wa sera zetu kutokana na matunda ya utekelezaji yaliyoanza kuonekana. Matunda hayo yameongezeka tangu mwaka 2000. Wananchi wanaona wazi matunda hayo kwenye elimu, afya, maji, miundombinu kama vile barabara, madaraja, vivuko, bandari na simu, kushuka kwa mfumuko wa bei, nyongeza ya mapato ya Serikali, mafao mazuri zaidi ya watendaji wa Serikali, heshima ya taifa na diplomasia yake, misamaha ya madeni, nyongeza ya misaada na uwekezaji. Wanachotaka wananchi ni uhakika kuwa hatutarudi nyuma.
Mambo mawili ni muhimu sana yazingatiwe kwa makini. La kwanza ni kuwa Ilani ijayo itahusu kipindi cha 2005-2010, ambacho ndicho kipindi cha mwisho cha kutekeleza Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000-2010. Kwa hiyo Ilani lazima iandaliwe kwa kuzingatia ukweli huo. Tupitie tena mwelekeo huo, na kuona yapi yametekelezwa, na yapi yanapaswa kuzingatiwa kwenye kipindi kijacho. Na kwa yale ambayo yametekelezwa tuone ni namna gani tutahakikisha kwamba haturudi nyuma, kwamba tunayaimarisha, na kwamba tunajenga juu ya msingi wa mafanikio ambayo tayari yamepatikana na kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii.
Tufanye hima kukubali pia kuwa dunia yetu inabadilika haraka sana, na kila mabadiliko yanahitaji nasi tujipime tulipo. Tuwe wepesi kutambua maslahi yetu katika mabadiliko hayo, na tuwe wepesi kubuni mikakati ya kutetea maslahi hayo. Tuwe shupavu kama Chama kuwaiga rafiki zetu Wachina. Uchumi wa dunia ya leo ni uchumi wa soko. Ni kujidanganya kufikiri tunaweza kuukwepa.
Ushupavu wa uongozi ni kuwaeleza wananchi ukweli huo, na kutekeleza kwa dhati na makini yale tunayoamua ili kujenga uwezo wetu wa ushindani kibiashara na kiuwekezaji. Leo tunasifiwa kuwa nchi yetu imedhibiti vizuri vigezo vya uchumi mkuu, kama vile mfumuko wa bei na mapato na matumizi ya Serikali. Tunasifiwa kwa kujenga uwezo wa ushindani kibiashara na kiuwekezaji. Tunao uwezo wa kuamua na kuhakikisha haturudi nyuma, na tunalinda sifa hizo.
Waheshimiwa Wajumbe:
Ni kweli Tanzania imepata mafanikio mengi baada ya Serikali kujiondoa kwenye uwekezaji, biashara na huduma za kiuchumi, na kwa kushirikisha zaidi sekta binafsi katika kukuza uchumi, kuongeza nafasi za ajira, kuingiza nchini teknolojia ya kisasa, kutoa huduma za kiuchumi na kijamii, na kuongeza mapato ya Serikali. Napenda niongeze jambo muhimu sana. Tunaondoa mikono ya Serikali kwenye uchumi wa soko, lakini hatuondoi macho ya Serikali. Uchumi wa soko unahitaji sana usimamizi wa Serikali, kwa maana ya mwelekeo wa sera za kiuchumi na kijamii, kuleta ushindani wa haki kwenye soko, na kulinda maslahi ya taifa na wananchi. Aidha, yapo baadhi ya mambo ambayo kwenye hatua yetu ya maendeleo hatuwezi kutegemea sekta binafsi iyafanye, ikiwemo ulinzi na usalama, utawala wa sheria na haki za binadamu, huduma za kijamii, na miundombinu.
Tumeanza katika Awamu ya Tatu, na inabidi tuendelee katika Awamu ya Nne, kuimarisha dola na asasi zake za uongozi na usimamizi wa uchumi wa soko. Usimamizi huo ni pamoja na kuendeleza na kudumisha mambo ya msingi kwa utaifa na umoja wetu, usawa wa fursa za kuishi na kujiendeleza, na mshikamano wa kitaifa na muungano wetu. Nchi hii pia, chini ya uongozi wa CCM, lazima iendeleze dhana ya maendeleo ambayo hayapishani sana. La msingi si kuwarudisha nyuma wanaotajirika kwa njia halali, bali kuwasaidia wanaofukarika kwa kuwahimiza na kuwawezesha kutumia fursa zinazoletwa na uchumi wa soko.
Uchumi wa soko hauwezi kushamiri iwapo wananchi walio wengi si washiriki. Kwa hiyo kazi kubwa iliyo mbele ya Chama chetu ni kubuni na kusimamia mikakati ya kuingiza wananchi wengi iwezekanavyo kwenye uchumi rasmi wa soko. Mkakati mmojawapo, ambao tayari tunaushughulikia, ni wa kutambua rasmi raslimali na biashara za wanyonge ambazo bado ziko kwenye sekta isiyo rasmi ili zitumike kuwafanya wawe washiriki kamili kwenye uchumi rasmi wa taifa.
Jambo la pili muhimu sana ni wajibu wa dola kujenga miundombinu ya kiuchumi na kijamii ambayo bila kuwapo uchumi wa soko hauwezi kushamiri. Tumeanza, na lazima tuendeleze, ujenzi na uimarishaji wa barabara, madaraja, vivuko, reli, bandari, simu na umeme. Lazima tuendeleze maandalizi ya Watanzania kuwa na elimu, ujuzi na afya ya kuwawezesha kushiriki uchumi wa soko. Hivyo miradi ya elimu, maji, afya na vita dhidi ya UKIMWI na Malaria itabidi iendelezwe kwa kasi. Mapato ambayo Serikali inapata kutokana na shughuli za sekta binafsi hayana budi kuelekezwa kwenye kuimarisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake huu usiokwepeka.
Waheshimiwa Wajumbe:
Napenda kumalizia kwa kuwakumbusha mambo matatu tuliyoyabainisha kama ndiyo mambo makuu ya kuzingatiwa katika kipindi cha 2000-2010:

· Kwanza, kwamba CCM iwe mhimili wa umoja wa taifa, na wa muungano wetu. Mwelekeo unasema “Ili CCM iendelee kuwa na nguvu ya mhimili wa umoja wa taifa, lazima ihakikishe kuwa sarakani ya udini, ukabila na ubaguzi wa aina nyingine yoyote haijipenyezi ndani ya CCM yenyewe...Wana-CCM wanaoendekeza au kupandikiza ubaguzi ndani ya Chama chetu lazima wafichuliwe au kuchukuliwa hatua”;

· Pili, kwamba CCM idumishe amani na kutoa uongozi kwa taifa. Mwelekeo unasema, “CCM lazima ionekane kuwa ndilo chimbuko la sera za kuwawezesha wananchi kiuchumi.” Mwelekeo unaendelea kusema, “Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ziendeleze msimamo thabiti wa kulinda na kutetea maslahi ya chama dhidi ya maslahi ya ubinafsi; na maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya vikundi vya kibinafsi. Hivi ndivyo CCM itajijengea uhalali wa kuwa chama kiongozi kwa taifa;” na

· Tatu, kwamba CCM iongoze ujenzi wa uchumi wa kisasa na kuutokomeza umaskini. Leo dunia nzima inakiri kuwa vita dhidi ya umaskini haiwezi kufanikiwa bila uchumi kukua. Kwa hiyo jukumu la msingi ni kwanza kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi, na pili kwamba uchumi ukuavyo maslahi ya wanyonge na ya taifa yanazingatiwa. Uwezeshaji wa wananchi, na usimamizi wa uchumi wa soko, ni mambo ambayo yatahitaji mkazo maalum. Mwelekeo unasema, “Kazi hii ni nzito na inahitaji uongozi thabiti wa vitendo wa Chama na Serikali zake. Serikali zitabidi ziyaelewe na kuyaainisha majukumu yake na kuyatafsiri katika programu mbalimbali.”

Waheshimiwa Wajumbe:
Mimi ninaamini kuwa iwapo tutaandaa programu yetu, na Ilani yetu, kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, tutaonekana wazi kustahili kuendelea kukabidhiwa uongozi wa nchi hii. Lakini narudia. Tukubaliane kwanza kuhusu programu na Ilani, kabla ya kutafuta wagombea. Pili, tuazimie kuwa na uongozi shupavu, uongozi usiosuasua, uongozi unaokiri hatua tuliyopiga, usioogopa kubuni, kuongoza na kusimamia mabadiliko. Chama kisicho tayari kubadili mikakati na mbinu kitapoteza uhalali wa uongozi katika dunia inayobadilika, na Chama ambacho si shupavu, hakiwezi kubadilika.
Unaweza kuwa nahodha hodari wa merikebu, lakini huwezi kuwa nahodha wa bahari. Watanzania, Chama Tawala cha CCM na viongozi wake, tusifikiri tunaweza kuwa nahodha wa bahari ya utandawazi inayotuzunguka kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Badala yake, tuboreshe unahodha wetu wa merikebu ya taifa katika bahari iliyotibuka. CCM tuna wajibu kuwa waaminifu, shupavu, kubadilika, na kuongoza na kusimamia mabadiliko, bila kuathiri hata chembe imani yetu ya kisiasa na itikadi inayoambatana nayo. Tunahitaji ushupavu wa uongozi. Tukiamua tulio ndani ya ukumbi huu, inawezekana kujenga ushupavu huo. Ombi langu ni kuwa kila mmoja wetu asikilize dhamira yake na kisha atimize wajibu wake.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

source: http://www.ccmtz.org/

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 12 FEBRUAR

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 12 FEBRUARI 2004


Mheshimiwa Spika,

Awali ya yote, napenda sote tuungane kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai tangu nilipohutubia Bunge hili Tukufu mara ya mwisho, tarehe 30 Januari 2002, hadi leo hii. Namshukuru pia kwa afya yangu inayoimarika siku hadi siku. Nanyi, Waheshimiwa Wabunge, nakushukuruni sana kwa salamu zenu za pole na dua kwa ajili ya afya yangu zilizowasilishwa kwangu na Mheshimiwa Spika wakati nikiwa nimelazwa hospitalini kule Uswisi.

Mheshimiwa Spika,
Nilipohutubia wananchi, tarehe 31 Desemba 2003, niliwaambia kuwa ningependa katika kipindi cha uongozi wangu kilichobaki nielekeze nguvu zangu kwenye kuimarisha uendelevu wa mageuzi na mafanikio yetu, na unyumbulifu wa taifa letu kisiasa, kiuchumi na kijamii, pamoja na kuweka mkazo mpya kwenye kujenga uwezo wa Watanzania kutumia fursa za kujiendeleza ambazo mafanikio ya mageuzi yetu yanaziweka mbele yao. Niliahidi pia kuwa, Inshallah, ningetafuta fursa ya kufafanua nini hasa nilichokuwa nazungumzia.

Hakuna fursa iliyo bora kwa lengo hilo kuliko hii ya kuzungumza na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge hili si tu mahali ambapo Watanzania wote wanawakilishwa, bali pia ni mshirika wangu mkuu katika kutekeleza yote ninayokusudia kuyafanya. Na kwa vile nchi hii ni yetu sote, kiasi kwamba hata viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani nao hufaidi matunda ya kazi za Chama Tawala, na huhasirika tusipopiga hatua mbele, nimeomba viongozi hao wawe hapa kunisikiliza. Kwa heshima naomba sasa niwatambulishe, na kuwaomba wasimame ili Waheshimiwa Wabunge nao wawatambue.

Mheshimiwa Spika,
Napenda nianze kwa kurejea kwenye muhtasari nilioutoa kuhusu sura kuu za mwelekeo wa miezi 20 ijayo:

· Kwanza, kuongeza kasi ya kubadili mtazamo wa watumishi wa umma—kwenye Serikali Kuu na Serikali za Mitaa—ili wajue kuwa kazi yao ya msingi sasa ni kuwasaidia na kuwawezesha wananchi kujiendeleza.
· Pili, kujenga na kuimarisha uwezo kitaifa wa udhibiti, uratibu na usimamizi wa uchumi wa soko.

· Tatu, kufikiria upya haki za wanyonge wakiwemo wananchi walio katika sekta isiyo rasmi; hasa zile haki za kumiliki raslimali na mitaji, ikiwemo nguvu zao, na ardhi, kama mbinu ya kuwawezesha kuingia katika mfumo rasmi wa uchumi wa kitaifa.

· Nne, kuweka kipaumbele kinachostahili kwenye mauzo nje ya nchi, ikiwemo kuongeza thamani yake kwa kuyasindika, na kukaribisha uwekezaji kwenye viwanda vitakavyotupatia haraka uwezo wa kufanya hivyo.

· Tano, kuendelea kubainisha kero za wananchi, na kuondosha vikwazo vilivyo katika njia ya Watanzania walio tayari kujiendeleza.

Mheshimiwa Spika,
Ningependa Waheshimiwa Wabunge waniunge mkono katika kuweka kipaumbele kwenye maeneo haya, na wawe wabia wa Serikali katika utekelezaji wake wa dhati. Nawaomba mambo mawili ya msingi kabisa:

· Kwanza, nawaomba wazingatie wakati wote ukweli kuwa nchi yetu ni maskini, na kama alivyotuasa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tunapaswa kukimbia wakati wengine wakitembea. Kwa kweli mimi nimechoka kila mara kusikia Tanzania inaitwa “moja ya nchi maskini kuliko zote”. Inawezekana kuachana na sifa hiyo ya umaskini, lakini si kwa kasi yetu ya sasa. Nchi nzima, ikiongozwa na Bunge hili, inapaswa kubadili gia, na tuonyeshe dunia kuwa baada ya kubuni sera na mwelekeo sahihi, sasa tunachochea mwendo kweli. Sijengi hoja ya kugeuza Bunge hili kuwa muhuri wa Serikali. Wala sithubutu. Lakini najenga hoja ya mazingira ya kibunge yanayoiwezesha Tanzania kukimbia badala ya kutembea. Najenga hoja ya “a sense of urgency”.

· Pili, naomba katika kuzungumza na wananchi, na pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao mwakani, sisi sote tusiwape matumaini kuwa ipo Serikali yenye majibu yote na uwezo wote. Serikali ya aina hiyo haipo popote duniani. Serikali haina muujiza wa peke yake. Lakini inawezekana kupata muujiza wa kitaifa, kwa kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa matatizo, kwa kujituma na kukubali wajibu wa kujiendeleza kama mtu binafsi, na kama jamii. Dhana ya kwamba wajibu wa Serikali ni kutoa, na wajibu wa wananchi ni kushukuru, ni sawa na mbio za sakafuni, mwisho wake ni ukingoni. Dhana hiyo inaweza kumpatia mgombea kura, lakini haitotufikisha mbali kama taifa.

Hali ya Siasa

Mheshimiwa Spika,
Baada ya miaka arobaini na mbili ya Uhuru wa Tanzania Bara, na miaka arobaini ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tanzania imeuzatiti uhuru wake wa kisiasa, na kujenga umoja wa kitaifa usio na shaka, ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya amani na utulivu.

Katika bara hili lenye historia ya vurugu za kisiasa na ghasia, Tanzania, iliyozaliwa mwaka 1964 kwa kuunganisha nchi mbili huru— Tanganyika na Zanzibar—hadi leo hii ndiyo Muungano pekee wa aina hiyo unaoendelea na kuweka hai matumaini ya umoja wa bara la Afrika.

Serikali zetu zinabadilishwa kupitia sanduku la kura, kwa kuheshimu Katiba ya Taifa. Hakuna Rais—Bara na Zanzibar—aliyeachia madaraka na kisha kulazimika kuikimbia nchi yake. Wote wanaishi nasi, na wanaheshimiwa.

Tanzania ni nchi ya kidemokrasia. Serikali ya Awamu ya Tatu Tanzania Bara, na Awamu ya Sita Tanzania Zanzibar, zimefanya kazi kubwa kuimarisha misingi ya uhuru wa raia, demokrasia, haki na usawa, kwa mujibu wa Katiba.

Siwezi kusema Tanzania sasa ni peponi. Kote duniani vyama vya upinzani vinakuwa na malalamiko ya aina fulani dhidi ya Chama Tawala na Serikali yake. Ni mambo ya kawaida kwenye ushindani wa kisiasa.

Matatizo ya kisiasa Zanzibar, kufuatia Uchaguzi Mkuu uliopita, yametatuliwa kwa amani na majadiliano. Matukio ya Januari 26 – 27, mwaka 2001, ambapo wenzetu walipoteza maisha yao, yamebaki kama kasoro na si hulka ya Watanzania. Na kasoro ni kasoro—haifai kutukuzwa. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Tunaandaa mfumo endelevu wa ushindani wa kisiasa ambao ni wa kistaarabu, huru na wa amani Zanzibar na Tanzania nzima. Kwetu sisi, majadiliano ndiyo njia muafaka zaidi na ya uhakika ya kuendesha siasa huko tuendako. Kama alivyosema mshairi maarufu, Kahlil Gibran, “Tunapogeukiana na kushauriana tunapunguza idadi ya maadui zetu.” Mimi binafsi na Chama Cha Mapinduzi hatutaki uadui kwenye siasa. Tuko tayari kushauriana na kuelewana na wote wenye nia njema.

Utayari wetu umedhihirika kwenye MWAFAKA baina ya vyama viwili vikuu, CCM na CUF, uliowekwa saini tarehe 10 Oktoba 2001 ambao umeendelea kuimarika, na umechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa kisiasa uliopo sasa Zanzibar, kielelezo kimojawapo kikiwa uchaguzi mdogo Mei 2003. Naipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutekeleza wajibu wake chini ya Mwafaka, na kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayoonekana wazi.

Katika miezi ijayo tutapendekeza mabadiliko ya Katiba ambayo kwa maoni yetu yatasaidia kuimarisha demokrasia katika nchi yetu. Tutatimiza pia ahadi yetu ya kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Na tutazidi kuongeza nafasi na uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi. Kwa upande wa Bunge, ninakusudia idadi yao isipungue asilimia 30 ya Wabunge kabla sijaondoka madarakani.

Lakini, Mheshimiwa Spika, yapo mambo mawili katika siasa nchini mwetu yasiyoniridhisha. La kwanza, ni udhaifu wa vyama vya upinzani. Miaka michache iliyopita nilielezea hofu hiyo kwa kofia yangu ya Urais. Lakini nikajibiwa kuwa si kazi yangu kufikiria udhaifu wa vyama vya upinzani. Mimi ninaamini wako Watanzania wengine walio na wasiwasi kama wangu, maana ama tunao ushindani wa kweli, wa timu zinazokaribiana kwa nguvu, au tunafanya mzaha. Ni nia yangu CCM iendelee kutawala daima, lakini naelewa pia faida kwa taifa ya vyama vya upinzani makini vinavyoweza kutuamsha tusilale usingizi. Na CCM ikiwa macho, ni kwa faida ya wananchi na taifa.

Mheshimiwa Spika,
Jambo la pili linalonifadhaisha ni kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanachama wao ambazo zinaonyesha kutojali thamani ya amani na utulivu nchini. Wapo hata wanaothubutu kuzungumzia damu kumwagika, japo sijasikia wakijitolea damu yao wenyewe, hata kwa jambo jema kama vile kutunisha akiba ya damu kwenye hospitali zetu!

Pengine hakuna sifa muhimu kwa nchi yoyote kama sifa ya amani na utulivu. Kiongozi, au mtu anayewania uongozi, lazima ajifunze kuheshimu thamani ya uhai wa raia. Inachukua muda mrefu kwa nchi kujijengea sifa ya amani na utulivu, lakini ni rahisi sana kuibomoa, hasa ukipata viongozi wasiothamini uhai wa raia, walio tayari kuutumia kama ngazi ya kuingia madarakani. Katika nchi huru ya kidemokrasia hakuna uhalali wowote wa kutumia fujo na vurugu kutafuta madaraka.

Naomba sana kuwa tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu mwakani, tusithubutu hata kuwazia matumizi ya fujo na vurugu. Na sisi Serikalini, wenye dhamana ya utulivu na usalama nchini, hatuwezi kuruhusu siasa za fujo na vurugu. Ni wajibu wetu kikatiba kudumisha amani na usalama nchini kote.

Serikali za Mitaa

Mheshimiwa Spika,
Tunataka kuhakikisha kuwa vikwazo dhidi ya ushiriki wa wananchi kwenye utawala na maendeleo ya nchi yao vinaondolewa. Maana demokrasia si siasa tu, demokrasia ni uchumi vile vile. Kwa asiye na chakula, demokrasia ni anasa. Kwa wananchi walio wengi demokrasia inayowagusa moja kwa moja, na inayohusu maisha yao ya kila siku na mustakabali wao, ni Serikali za Mitaa. Demokrasia ni madaraka kwa wananchi. Na ibara ya 146(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.” Kwa sababu hiyo, Serikali ilibuni na inaendelea kutekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kuwa Halmashauri za Wilaya na Miji zinawajibika kwa wananchi, pamoja na kutoa huduma bora zaidi kwao na kurahisisha jitihada zao za kujiendeleza.

Mheshimiwa Spika,
Kielelezo cha utashi wa kisiasa kuimarisha Serikali za Mitaa ni kiasi cha fedha kinachokabidhiwa kwa Halmashauri. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana—mara 24—la ruzuku ya Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa kutoka Sh.12.3 bilioni mwaka 1995/96 hadi Sh. 292 bilioni mwaka huu wa fedha. Huu ni uwezeshaji kimapato, utokanao na mafanikio ya mageuzi yetu ya uchumi.

Upo pia uwezeshaji kielimu. Mafunzo ya kuimarisha utendaji yametolewa kwa Wakuu wa Mikoa wote, na baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa. Mpango wa mafunzo ya Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Maafisa Watendaji wa Vijiji umeandaliwa. Hadi sasa viongozi 72,000 wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji wamepatiwa mafunzo ya kuimarisha utawala bora. Madiwani 3,447 na Maafisa Watendaji wa Kata 2,303 nao wamepatiwa mafunzo. Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri zote wamepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa mabadiliko. Na yote hayo yanawezekana kutokana na mafanikio ya mageuzi yetu ya kiuchumi.

Mafanikio hayo pia yamesaidia uwezeshaji kiutendaji. Kwa mfano, Makatibu Tarafa wote wamepewa pikipiki ili kuwawezesha kusimamia vizuri shughuli za maendeleo. Pikipiki hizo zisingepatikana kama si mageuzi ya uchumi tuliyoyafanya.

Sera zetu na mageuzi yetu vimetujengea mahusiano mazuri na wahisani wanaotusaidia kutekeleza Mpango huu wa Uboreshaji Serikali za Mitaa. Aidha, mapato ya Serikali ambayo yameongezeka sana baada ya mageuzi hayo ndiyo yamewezesha Serikali Kuu kugharamia uwezeshaji wa Halmashauri nilioutaja hapa. Ni mafanikio ya mageuzi hayo ndiyo vile vile yaliyoipa Serikali uwezo wa kufuta kodi mbalimbali zilizokuwa kero kwa wananchi kwa miaka mingi. Wanaokebehi mageuzi waulizwe, ingewezekanaje?

Mabadiliko ya Fikra na Usimamizi wa Uchumi wa Soko

Mheshimiwa Spika,
Jambo jingine ambalo nitalitilia mkazo katika kipindi changu kilichobaki ni mabadiliko ya fikra ya viongozi na watendaji wa Serikali, pamoja na Serikali za Mitaa, kuhusu nafasi ya sekta binafsi. Kila kiongozi na mtumishi wa Halmashauri anapaswa kujua kuwa maslahi yake binafsi, na maendeleo ya wilaya au mji unaohusika, vinategemea sana mafanikio ya uwekezaji, uzalishaji, huduma na biashara. Wakati umefika sasa kwa Halmashauri kushindana kwa dhati miongoni mwao katika kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara. Watumishi wa umma waelewe kuwa nyakati zimebadilika, na tunahitaji mbinu mpya kukabiliana na changamoto za leo na zijazo.

Ipo hadithi ya bwana mmoja aliyekuwa anatembea barabarani. Akamsimamisha mtu mmoja na kumuuliza wakati. Mtu yule akaangalia saa yake na kumjibu, “Hivi sasa ni saa 10:00.” Yule bwana aliyeuliza akakuna kichwa na kusema, “Unajua, ninyi wenye saa mnanichanganya kweli. Siku nzima ya leo nimekuwa nauliza watu wakati, na kila mara ninapewa jibu tofauti!”

Na mimi nawaambia watumishi wa umma kuwa wasiwalaumu wenye saa, wala wasichanganyikiwe. Ukweli ni kuwa nyakati zinabadilika haraka, na majibu lazima yabadilike.

Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa ni kama vile kila mmoja anakubali kwa wepesi kuwa uwekezaji mkubwa na biashara mahali pake ni Dar es Salaam. Hivi leo Mkoa wa Dar es Salaam, na hususan Jiji la Dar es Salaam, huchangia karibu asilimia 82 ya mapato yote ya Serikali. Hali hii si nzuri hata kidogo. Chanzo cha maendeleo ni uwekezaji, uzalishaji, huduma na biashara. Kwa kadri mambo hayo yanavyofanyika Dar es Salaam, ndivyo maendeleo yatakavyoelekea Dar es Salaam, na kuzidi kuwavuta vijana toka pande zote za nchi kuja Dar es Salaam kwa matumaini kuwa huko ndiko kwenye uwekezaji, na hivyo kwenye ajira; na kwamba huko ndiko kwenye maendeleo na hivyo maisha bora. Bila Halmashauri kwenye mikoa mingine kufanya bidii kuvutia uwekezaji huko waliko, tatizo hili haliwezi kwisha na hakutakuwa na usawa wa kijiografia kwenye maendeleo ya taifa.

Ndio maana nachukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa mstari wa mbele kujiandaa kuvutia wawekezaji, na kuitisha Kongamano la Uwekezaji Kilimanjaro lililofanyika tarehe 14-15 Agosti 2003.

Lakini, Mheshimiwa Spika, uchumi wa soko lazima udhibitiwe kwa maslahi ya taifa na walaji. Ili kuwalinda wateja na kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki kwenye biashara, Serikali imeanzisha mashirika manne ya usimamizi ambayo ni: Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Maji na Nishati (Energy and Water Utilities Regulatory Authority -EWURA), Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Surface and Marine Transport Regulatory Authority- SUMATRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Mawasiliano (Tanzania Communication Regulatory Authority-TCRA), na Mamlaka ya Serikali ya Tanzania ya Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga (Tanzania Government Aviation Regulatory Authority-TGARA). Mamlaka hizi na nyingine zote zitahitaji kuimarishwa sana katika siku zijazo.

Hali ya Uchumi

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla, uchumi wa Tanzania umeendelea kuboreka katika miaka ya hivi karibuni, kufuatia utekelezaji wa kina uliofikiwa katika marekebisho mbalimbali ya uchumi na sekta ya fedha. Viashiria vya mafanikio ya hivi karibuni, yaliyoleta kutengamaa kwa uchumi mpana, ni pamoja na kuongezeka kwa mitaji katika sekta za umma na sekta binafsi, na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kujenga uwezo wa kutosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 7 – 8 hivi sasa ukilinganisha na miezi 6.3 katika mwaka 2001.

Kuanzia mwaka 1990 hadi Desemba 2003, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimeidhinisha jumla ya miradi 2,527, inayokadiriwa kutoa nafasi za ajira 497,539. Kati ya miradi hiyo, miradi 1,809 ilikuwa mipya, na miradi 718 ni ya upanuzi na ukarabati. Miradi 1,113 (asilimia 44) inamilikiwa na wawekezaji wa ndani ya nchi, miradi 609 (asilimia 24) ni ya wawekezaji wa nje, na miradi 805 (asilimia 32) ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa imeendelea kuongezeka, kutoka asilimia 3.3 katika mwaka 1997 hadi kufikia asilimia 6.2 mwaka 2002. Wastani wa ukuaji huu wa kiuchumi wa asilimia 5.6 kwa mwaka kwa miaka mitatu mfululizo unatia moyo, hasa ukilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi barani Afrika wa asilimia 3.4 katika kipindi hicho.

Kwa sababu ya ukame uliotupata, inakadiriwa kuwa mwaka 2003 uchumi umekua kwa asilimia 5.7, na mfumuko wa bei umeongezeka kidogo kutoka wastani wa asilimia 4.5 mwaka 2002 hadi asilimia 4.6 mwezi Desemba 2003. Kwamba ukame huu haukuathiri sana utulivu wa uchumi mkuu ni ishara ya mafanikio makubwa ya mageuzi yetu ya uchumi. Tutaendeleza mageuzi hayo, na tutayaimarisha ili kamwe tusirudi nyuma tulikotoka.

Mheshimiwa Spika,
Sababu kubwa ya Azimio la Arusha kusema “Fedha si msingi wa maendeleo”, ni kwa vile tulikuwa hatuna fedha. Likasisitiza kuwa huwezi kupanga maendeleo kwa kutegemea kitu ambacho huna. Ni hoja nzito, na ya haki kabisa.

Lakini dunia inabadilika, na mahitaji ya maendeleo nayo hubadilika. Kwenye orodha ya mambo ambayo Azimio lilituambia ni muhimu kwa maendeleo—yaani ardhi, watu, siasa safi, na uongozi bora—napenda niongeze jingine, nalo ni mitaji. Ipo mitaji ya aina nyingi. Mtaji wa maskini ni nguvu zake. Lakini wakati umefika pia kutumia siasa safi na uongozi bora kuongeza upatikanaji wa mitaji ya fedha.

Sote tutakumbuka hali ya uchumi ilivyokuwa mwaka 1995. Na wala sisemi hivyo kwa kulaumu. Nimlaumu nani wakati mimi pia nilikuwa sehemu kamili ya Serikali zilizopita nikiwa Waziri kwa miaka mingi?

Lakini ukweli ni kuwa wakati ule ukuaji wa Pato la Taifa ulikuwa chini ya asilimia 3 kwa mwaka, mfumuko wa bei ulikuwa karibu asilimia 30, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa ndogo isiyotosha hata miezi minne ya thamani ya bidhaa na huduma kutoka nje, Serikali ilikuwa inakusanya mapato yasiyozidi wastani wa Sh. 25 bilioni kwa mwezi, nidhamu ya matumizi ya Serikali na usimamizi wa fedha za umma ilikuwa ndogo sana, uwajibikaji Serikalini na katika Sekta ya Umma kwa ujumla ulikuwa mdogo, na Serikali ilikuwa inadaiwa kulia na kushoto, nje na ndani ya nchi. Aidha, ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi ulikuwa wa kiwango cha chini, na uwekezaji ulikuwa unasuasua. Misaada ya nje ilikuwa michache na ilipatikana kwa masharti magumu. Kweli yupo anayetaka turudi huko? Kiongozi, msomi au mwandishi habari aliye makini atakosaje kulinganisha tulikotoka na tulipo leo? Ni kweli bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Lakini hiyo si sababu ya kupuuza yaliyofanyika.

Mheshimiwa Spika,
Mojawapo ya mambo ya mwanzo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ilikuwa kubuni sera na mikakati itakayoongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili Serikali iweze kuboresha huduma za uchumi na za jamii na hivyo kusaidia jitihada za kupunguza umaskini. Tuliimarisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuipa madaraka kamili ya kukusanya mapato bila kuingiliwa na Serikali. Aidha, Serikali ilianzisha utaratibu thabiti wa majadiliano na wadau, hasa walipa kodi wakubwa, kuhusu sera za kodi na utawala wa ukusanyaji wa kodi. Matokeo yake leo TRA inakusanya wastani wa Sh. 108 bilioni kwa mwezi, ikilinganishwa na Sh. 25 bilioni mwaka 1995. Hadi mwisho wa mwezi uliopita, pamoja na matatizo ya ukame, TRA ilikuwa imeshavuka lengo lake la miezi 7 ya kwanza ya mwaka huu wa fedha kwa kukusanya Sh. 788.3 bilioni ikilinganishwa na lengo la Sh. 757.4 bilioni. Yaani wamevuka lengo kwa karibu Sh. 30.9 bilioni. Naomba Bunge hili liungane nami kuwapongeza kwa dhati kabisa viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kazi nzuri, na kuwataka waendelee mbele. Tuna kazi ya kupiga vita umaskini.

Jambo la pili lilikuwa kurejesha mahusiano mazuri na nchi wafadhili na mashirika ya fedha ya kimataifa. Leo tunapata misaada yenye thamani zaidi ya mara nne ya ile tuliyokuwa tunapata kabla ya 1996. Aidha, Tanzania ilikuwa moja ya nchi nne za kwanza kufuzu mtihani wa kufutiwa madeni chini ya mpango wa HIPC, jambo ambalo limetuongezea uwezo wa kutoa huduma za uchumi na za jamii. Fedha zinazotolewa kwa sekta za kipaumbele kwenye vita dhidi ya umaskini, ikiwemo elimu, afya, barabara, maji, vita dhidi ya UKIMWI na kilimo, sasa ni mara nne zaidi ya kiwango cha mwaka 1996.

Tumeimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali, kwa kuamua kutumia kile tu tulichonacho. Nalishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha sheria mbili muhimu kwa nidhamu na usimamizi bora wa fedha za Serikali: Sheria ya Fedha za Umma (Public Finance Act 2001), na ile ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Act 2001). Sheria hizi mbili zimeimarisha nidhamu na utawala bora kiasi kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini zinazosifiwa sana kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika,
Uchumi mpana tulivu ni nyenzo muhimu sana ya kuvutia uwekezaji, kuchochea ukuaji wa uchumi, kupanua nafasi za ajira, kuongeza mauzo ya nje, kuongeza mapato ya Serikali na kuongeza misaada ya nje pamoja na mikopo yenye masharti nafuu. Uwezeshaji wananchi kimitaji nao unahitaji ushindani kwenye sekta ya fedha. Tumepiga hatua kubwa ukizingatia tulikotoka. Benki za biashara sasa ziko 26, taasisi nyingine za fedha ziko 6, kuna kampuni za bima zaidi ya 10, tumeanzisha Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) unaoongezea kwenye huduma inayotolewa na mifuko iliyopo ya PPF, NSSF na LAPF, soko la mitaji limeanzishwa na linakua, ipo sera mpya ya mikopo midogo midogo, umeanzishwa mfuko wa kudhamini mikopo kwa sekta za kipaumbele ambazo ni pamoja na vyama vya ushirika na kampuni zinazozalisha bidhaa maalum kwa ajili ya kuuza nje, na umebuniwa mfuko wa hisa za pamoja (Unit Trust of Tanzania). Maeneo haya yote yana mchango mkubwa katika kukua kwa uchumi, na kuwawezesha Watanzania kimitaji. Nitakazania sana eneo hili katika siku zijazo.

Mheshimiwa Spika,
Tusisahau tulikotoka, na wala tusione haya kujivunia mafanikio yetu. Lakini kamwe tusiridhike, maana ukweli ni kuwa bado ipo kazi kubwa mbele yetu, na matatizo bado ni mengi. Lakini tumeweka msingi mzuri, na hakuna sababu ya kukosa ujasiri na kuanza kuangalia nyuma. Katika miaka michache ijayo, tutaweka mkazo katika maeneo yafuatayo:-

1. Kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa zaidi. Asilimia 6 haitoshi. Tunataka kufika asilimia 8 na kuzidi. Huduma za benki na vyombo vya fedha zitatakiwa kurahisisha upatikanaji mitaji na kushiriki kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Marekebisho ya Sheria ya Ardhi yatasaidia. Bajeti ya Serikali nayo itatumika kuboresha miundombinu na kuondosha vikwazo vingine vya uwekezaji na biashara.

2. Tutatumia bajeti ya Serikali kuchochea upatikanaji wa ajira kwa kutumia sera za mapato na matumizi, hasa kupitia mifuko ya udhamini wa mikopo kwa wawekezaji wadogo na wa kati.

3. Bajeti ya Serikali pia itatumika kama kichocheo cha kuinua uzalishaji wa kilimo kwa njia za udhamini na uwezeshaji, hasa kuhusu upatikanaji wa pembejeo na mbegu.

4. Tutaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za Serikali ili mapato yanayoongezeka kutokana na mafanikio ya mageuzi yetu yatumike kwa ufanisi katika vita dhidi ya umaskini na kuwezesha wananchi kujiendeleza.

5. Kwa kadri uchumi unavyokua, na ukusanyaji kodi unavyoboreshwa, tuna lengo la kuongeza mapato ya Serikali kutoka asilimia 12 ya Pato la Taifa hivi sasa hadi asilimia 15 ifikapo mwaka 2006, na asilimia 18 ifikapo 2008.

6. Tutaanzisha mpango wa kubainisha na kutambua kisheria mitaji na raslimali za watu walio katika sekta isiyo rasmi, pamoja na kubaini na kuondoa vikwazo vinavyofanya iwe vigumu kwao kuingia kwenye sekta rasmi, inayotambuliwa kisheria.

Vita Dhidi ya Umaskini

Mheshimiwa Spika,
Umaskini una sura nyingi—upo umaskini wa kukosa kauli katika masuala yanayomhusu mtu; na upo umaskini wa kipato, miongoni mwa sura nyingine za umaskini.

Nimekuwa Rais kwa zaidi ya miaka 8 sasa. Na mambo mawili kuhusu umaskini yananitatiza sana kinadharia.

La kwanza, ni namna ya kupima umaskini. Wengi wanapenda kutumia kigezo cha mapato, tena kwa dola za marekani, kwa siku. Lakini hicho ni kigezo finyu sana, na kisicho sahihi hata kidogo. Ni kipimo kinachokazania umaskini wa kipato tu, wakati umaskini hauna sura ya mapato peke yake. Isitoshe, kwa uchumi uliojikita kwenye sekta isiyo rasmi, kuna uhakika gani kuwa takwimu zetu zinabeba ujumla wa mali na raslimali za jamii zetu? Mfugaji wa Kitanzania anaweza kuwa anahama kila baada ya miezi michache, nyumba yake wala haistahili kuitwa nyumba, na mfukoni hana pesa. Lakini anao ng’ombe 500. Halafu anaambiwa anaishi kwa chini ya dola moja kwa siku!

Mimi nafikiri wakati umefika tuwe na tafsiri ya umaskini inayozingatia mazingira yetu.

Jambo la pili linalonitatiza linahusu swali la msingi kabisa. Hivi hasa vita dhidi ya umaskini inapiganwaje? Na, ni nani hasa mwenye wajibu wa msingi kupigana na umaskini? Maana huishi kusikia au kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa Serikali haipigi vita umaskini, au mageuzi hayasaidii kupiga vita umaskini.

Ninyi, Waheshimiwa Wabunge, ni wawakilishi halali wa wananchi. Naomba mnisikilize vizuri. Umaskini wa kauli unapigwa vita kwa kuwapa watu kauli. Lakini umaskini wa kipato haupigwi vita kwa kuwagawia watu pesa!

Mtaniwia radhi, lakini lazima niweke jambo hili wazi, maana utakuta mtu mzima, mwenye akili timamu, anauliza: “Kama mageuzi yamefanikiwa mbona sina pesa mfukoni? Serikali ina mpango gani? Serikali hii haipigi vita umaskini.”

Ukweli ni kuwa anayekuahidi kuwa Serikali inaweza kukuondolea umaskini wa kipato anakudanganya. Nchi hii haiwezi kushinda umaskini wa kipato kwa hadaa kama hizo, hadaa zinazowafanya wananchi wabweteke, wasijitume vya kutosha wakingojea msaada. Serikali makini haifanyi hivyo.

Yapo mambo makuu manne niliyoyaahidi kwa nyakati mbalimbali kama mkakati wa vita dhidi ya umaskini:

· Kwanza, ni kuwapa watu kauli juu ya mambo yanayowagusa, ikiwemo ushirikishwaji wa kidemokrasia katika kupanga, kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan ile ya kuondoa kero zao. Miradi mikubwa kama TASAF na MMEM imejengwa imara juu ya dhana hii, kama ulivyo mpango wa kuboresha Serikali za Mitaa.

· Pili, ni kuweka mazingira bora ya uchumi kukua na ajira kupatikana, ikiwemo mazingira yanayovutia uwekezaji na kurahisisha biashara.

· Tatu, ni kupeleka kiasi kikubwa zaidi cha bajeti ya Serikali kwenye maeneo muhimu kwa vita dhidi ya umaskini, ambayo tumekubaliana kitaifa kuwa ni elimu, afya, maji, barabara za vijijini, na UKIMWI.

· Nne, ni kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kujiendeleza, ikiwemo kwa kubaini na kisha kuondosha vikwazo vyote kwa wananchi wanaotaka, na walio tayari, kujiendeleza.


Mheshimiwa Spika,
Nafurahi wanapojitokeza wananchi kutathmini vita dhidi ya umaskini niliyoahidi kuiongoza. Lakini wafanye tathmini ya haki, kwa yale niliyoahidi. Niliyoyataja hapa niliyaahidi, na niko tayari kupimwa nayo. Lakini sikuahidi, wala Chama changu hakikuahidi, kuweka fedha mifukoni mwa watu. Tuliahidi fursa, na fursa zinawafaa wanaozitumia. Haziwezi kuwafaa wasiozitumia.

Ushirika

Mheshimiwa Spika,
Idadi kubwa ya Watanzania ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa hawa, na kwa hali halisi ya nchi yetu, ipo njia moja tu ya uhakika ya kuwawezesha kutumia fursa za kujiendeleza katika mazingira ya uchumi wa soko. Njia hiyo ni ushirika. Pamoja na matatizo yote yaliyovisibu vyama vya ushirika bado ukombozi wa uhakika wa wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara ndogondogo ni umoja kupitia ushirika. Nguvu ya mnyonge ni umoja.

Mwaka 2000 niliitisha kongamano kuhusu ushirika kule Mwanza kuchambua matatizo ya ushirika, na kuyatafutia ufumbuzi ili ushirika ukidhi matarajio yetu ya kuimarisha umoja wa wanyonge, umoja ambao ndio uwezeshaji wao.

Ninalishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha Sheria mpya ya Ushirika mwezi Novemba 2003 ambayo inaweka mazingira mazuri ya kuimarisha ushirika, na kuwapa wanachama kauli kubwa zaidi ya kidemokrasia katika uendeshaji wa vyama vyao. Sheria hii pia itasaidia kudhibiti wizi na ubadhirifu, mambo ambayo huko nyuma yalihujumu ushirika kwa kuwavunja moyo wanachama.

Lakini, sera na sheria zitakuwa na maana tu iwapo wanachama wenyewe watakuwa jasiri kudhibiti viongozi wao na mwenendo wa ushirika wao. Hivyo, tumeanzisha Mpango wa Elimu ya Ushirika Shirikishi ili kuwajasirisha wanachama, kuwapa mbinu za ujasiriamali, na mbinu za kusimamia vizuri zaidi vyama vyao.

Mheshimiwa Spika,
Sera ni muhimu. Sheria ni muhimu. Na uwezeshaji kielimu ni muhimu. Lakini mitaji nayo ni muhimu. Hali ya mitaji ya vyama vingi vya ushirika, hasa vya mazao ya kilimo, ni mbaya sana. Hivyo, Serikali imeamua kuvisaidia na kuviwezesha vyama hivyo kimitaji kupitia utaratibu wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje (Export Credit Guarantee Scheme) unaoviwezesha kukopa fedha za kununulia mazao ya wakulima, na kuyauza nje ya nchi. Kwa utaratibu huu, vyama vya ushirika vilikopeshwa Sh.10.1 bilioni na CRDB mwaka 2002/03. Mwaka huu, 2003/04, vyama vimekopeshwa Sh.16.3 bilioni na CRDB na Benki ya Ushirika Kilimanjaro (Kilimanjaro Cooperative Bank). Nazishukuru Benki hizi kwa kushirikiana nasi, na navionya vyama vya ushirika visithubutu tena kutumia mikopo hii nje ya makusudio yake, na wahakikishe wanailipa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika,
Huu ni ufumbuzi wa muda mfupi wa matatizo ya mitaji. Ufumbuzi wa kudumu ni kujenga uwezo wa mitaji ndani ya vyama vyenyewe. Huo ndio utakuwa uwezeshaji wa kudumu. Vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa ni jibu la uhakika la tatizo la mitaji. Tumeweka mkazo mkubwa sana kwenye jambo hili, na mafanikio yameanza kuonekana. Vyama vya Akiba na Mikopo vimeongezeka kutoka 803 mwezi Juni 2000 hadi 1,264 mwishoni mwa 2003, sawa na ongezeko la asilimia 57 katika kipindi cha miaka 2½ tu. Hisa na akiba kwenye vyama hivyo nazo zimeongezeka kutoka Sh.14.0 bilioni hadi Sh.25.7 bilioni, ongezeko la asilimia 83. Mikopo nayo ikaongezeka kutoka Sh.11.5 bilioni hadi Sh.28.5 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 117. Huu ndio uwezeshaji wanyonge kimitaji, na utawanufaisha walio tayari kushirikiana na wenzao. Wasiotaka kushirikiana watabaki kulalamika.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kuviwezesha vyama vya ushirika kwa kuviwekea mazingira bora ya kisera na kisheria, na pamoja na kuviwezesha kielimu na kimitaji, tutaweka mkazo pia kwenye ukaguzi ili kuhakikisha kuwa mali na fedha za vyama zinatumika vizuri, kwa ufanisi, kwa manufaa ya wanachama badala ya manufaa binafsi ya viongozi.

Mheshimiwa Spika,
Wapo wanaouliza faida ya mageuzi yetu ya kiuchumi ni nini kwa wananchi wa kawaida. Nasema, utashi wa wazi wa kisiasa wa kuwasaidia wanyonge kupitia ushirika, mapato ya Serikali yalioongezeka na kutuwezesha kugharamia uwezeshaji kwenye ushirika kama nilivyoelezea hapa, na mageuzi kwenye sekta ya fedha yaliyowezesha vyama vya ushirika kukopeshwa, ni faida za wazi kwa wanyonge na ni uwezeshaji wao katika uchumi wa soko, na utandawazi. Lakini ili wafaidike, wanyonge lazima wajiunge kwenye ushirika, lazima wausimamie vizuri ushirika wao, lazima wawe wajasiriamali, wabunifu na wenye kuthubutu na kujiamini. Sifa hizo zinatokana na wananchi wenyewe. Serikali haiwezi kuzishurutisha kwao. Waheshimiwa Wabunge mnayo nafasi nzuri, na ni wajibu wenu, kujenga sifa hizo miongoni mwa wananchi kwenye kila jimbo la uchaguzi, na ni vema muwaambie wananchi ukweli huu.

Unajua, Mheshimiwa Spika, wasiotupenda wanadai kuwa sisi wanasiasa ni walaghai, wasiosema ukweli wote. Si sifa nzuri hata kidogo na inaweza kuwa na madhara baadaye. Siku moja basi lililojaa wanasiasa liliacha njia na kugonga mti kwenye shamba la mkulima mmoja mzee. Mzee yule akaenda kuchunguza. Kisha akachimba kaburi na kuwazika wanasiasa wote. Siku chache baadaye akaja askari polisi. Akamuuliza yule mzee, “Je, wote walikufa?” Mzee akajibu, “Ah!, wengine walisema hawajafa, lakini unajua tena jinsi wanasiasa walivyo hodari wa kudanganya!”
Mungu apishie mbali!

Elimu ya Msingi

Mheshimiwa Spika,
Ulimwengu, kupitia Umoja wa Mataifa, ulijiwekea malengo 8 ya kufikiwa ifikapo 2015 ili kupunguza umaskini kwa nusu duniani. Yanaitwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Lengo la 2 kwenye orodha hiyo linahusu elimu, kwamba ifikapo mwaka 2015 kila mtoto, wa kike na wa kiume, apate elimu kamili ya msingi. Benki ya Dunia inasema ifuatavyo kuhusu lengo hilo:

“Elimu ni maendeleo. Inawapa watu uwezo wa kuchagua na inawapa fursa, inawapunguzia mizigo miwili ya umaskini na maradhi, na inampa mwenye nayo kauli nzito zaidi kwenye jamii. Inafanya nchi ziwe na nguvukazi yenye elimumwendo (dynamic) na raia waelewa wanaoweza kushindana na kushirikiana na wengine duniani—ikifungua milango ya mafanikio ya kiuchumi na kisiasa.”

Mheshimiwa Spika,
Serikali inakubaliana kabisa na kauli hiyo. Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tatu imeweka mkazo mkubwa sana kwenye elimu ya msingi; na tukaona kuwa mwaka 2015 ni mbali mno kufikia lengo muhimu kama hili.

Tukabuni Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi, (MMEM), 2002-2006, kuhakikisha lengo hili linafikiwa ifikapo mwaka 2006. Yapo mafanikio mengi ya mpango huu katika miaka yake miwili ya kwanza. Nitataja machache tu.

1. Tumefikia usawa wa kijinsia kwenye shule za msingi;

2. Idadi ya wanafunzi kwenye shule za msingi imeongezeka kwa asilimia 50;

3. Tumeongeza uwiano wa watoto wanaoandikishwa shule kwa rika ya wanaopaswa kuwepo shuleni (GER) kutoka 77.6% mpango ulipoanza hadi 105.2% hivi sasa;

4. Tumeongeza kiasi cha wanafunzi wanaobakia shuleni mpaka mwisho (NER) kutoka 58.8% tulipoanza hadi 88.5% hivi sasa.

5. Tumejenga madarasa 31,825, na nyumba za walimu 7,530 kwa kushirikiana na wananchi;

6. Tumejenga shule mpya za msingi 1,081;

7. Walimu wapya 17,851 wameajiriwa, na 14,852 kupatiwa mafunzo ya kujenga uwezo wao na kujiendeleza;

8. Upatikanaji wa vitabu umeongezeka kutoka uwiano wa kitabu 1 kwa wanafunzi 8 (1:8) katika madarasa ya I-IV hadi kufikia 1:3, na kutoka 1:10 hadi 1:6 kwa madarasa ya V-VII;

9. Kiwango cha kufaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka 22% mwaka 2000 hadi 40.1% mwaka 2003;

10.Kamati za shule 12,689 zimepatiwa mafunzo ya kujenga uwezo wa kusimamia miradi ya shule na shule zenyewe.


Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya MMEM yameonyesha usahihi wa mwelekeo ambao tunaamini ndiyo njia pekee ya kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Mimi ninaamini kuwa malengo hayo yatafikiwa iwapo tu kuna ushirikiano wa kimataifa unaozingatia mambo matatu yafuatayo:

· Kwanza, utashi wa kisiasa na utawala bora katika nchi maskini.

· Pili, mipango-shirikishi kwenye kila jamii.
· Tatu, mazingira nje ya nchi yanayosaidia jitihada za nchi maskini kama vile kusamehe madeni, kuongeza misaada badala ya mikopo, na kutoa fursa za uwekezaji na biashara.

Haya mambo matatu ndiyo yametuwezesha kupata mafanikio yetu, na kutupa matumaini kuwa malengo ya elimu ambayo dunia ilifikiri yatafikiwa mwaka 2015, sisi tutayafikia mwaka 2006, yaani miaka 9 kabla ya tarehe iliyowekwa na Umoja wa Mataifa!!

Lakini narudia kibwagizo changu. Ni mageuzi yetu ya uchumi ndiyo yaliyosaidia kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa mapato ya Serikali, na hivyo kutuwezesha kufuta ada kwenye shule za msingi. Ni mageuzi yetu ndiyo yalitufanya tuwe na mahusiano mazuri na wahisani, na kusamehewa kiasi fulani cha madeni ya nje na kuelekeza unafuu tulioupata kwenye sekta muhimu kwenye vita dhidi ya umaskini kama ilivyo elimu. Ni mageuzi yetu ndiyo yametufanya tuaminiwe na wahisani na kupewa misaada zaidi na mikopo ya masharti nafuu. Na ni utashi wa kisiasa uliotuwezesha kuongeza sehemu ya bajeti ya Serikali iendayo kwenye sekta za kipaumbele kwenye vita dhidi ya umaskini.

Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi yametupa uzoefu na dhamira ya kuwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari utakaoongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kutoka asilimia 22 ya waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2003 hadi asilimia 50 ya watakaomaliza elimu hiyo mwaka 2009, tena kwa kuzingatia jinsia na mtawanyiko kijiografia ndani ya nchi. Lengo pia ni kuongeza kiwango cha kufaulu mtihani wa kidato cha IV ili wanaopata Daraja la I – III wafikie asilimia 70 ya wanafunzi wafanyao mtihani ifikapo 2009.

Mheshimiwa Spika,
Yote haya yamewezekana, na yataendelea kuwezekana kutokana na mafanikio ya mageuzi yetu, ili mradi tusirudi nyuma wala kupunguza kasi. Mageuzi yanafungua milango na fursa kwa wengi, ukianzia na hawa wapatao elimu. Baadhi yao wamefanya vizuri sana katika shule zetu za Serikali na za binafsi, na kututia moyo.

Leo, mbele yenu, Waheshimiwa Wabunge, napenda niwatambulishe vijana wetu wanafunzi, mmoja wa kike na mwingine wa kiume, waliofanya vizuri kuliko wenzao wote Tanzania kwenye mitihani iliyopita ya Darasa la VII, Kidato cha IV, na Kidato cha VI.

Katika mtihani uliofanyika Septemba 2003 wa kumaliza elimu ya msingi, binti wa Kitanzania, Mbuke Solomoka, aliyekuwa anasoma Shule ya Kanawa, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, alikuwa msichana wa kwanza; na kijana wa Kitanzania, Kesy Fulano, kutoka Shule ya Bumanji, Wilaya ya Geita, naye alikuwa wa kwanza kwa upande wa wavulana.

Katika mtihani wa Kidato cha IV uliofanyika Oktoba 2003, binti mwingine wa Kitanzania, Sara A. Cheche, aliibuka cheche kweli kweli na kuwa wa kwanza kwa upande wa wasichana Tanzania nzima. Yeye alikuwa anasoma St. Mary, Mazinde Juu. Kwa upande wa wavulana, kijana wa Kitanzania, Mosses Mwizarubi aliyekuwa anasoma Ilboru alikuwa wa kwanza.

Katika mtihani wa kumaliza Kidato cha VI uliofanyika mwezi Mei 2003, binti wa Kitanzania, Alice Edward, kutoka St. Mary, Mazinde Juu alikuwa msichana wa kwanza, na kijana Emil Patrick aliyekuwa anasoma Mzumbe alikuwa wa kwanza.

Vijana wetu hawa wako katika ukumbi huu, na naomba wasimame Bunge hili liwatambue ipasavyo. Naomba tuwapigie makofi wanayostahili.

Mheshimiwa Spika,
Nataka Bunge liwatambue maana hawa na wenzao wengi ndilo tumaini la Tanzania ya kesho. Uendelevu na ustawi wa Tanzania unawategemea hawa. Lazima kama wazazi na kama taifa tuwekeze sana kwenye vijana wetu kama hawa. Dunia ijayo ni ya ushindani mkubwa sana. Walioelimika vizuri ndio wenye uhakika wa kuhimili ushindani huo, iwe kwenye ajira au kwenye biashara.

Kupitia kwa vijana hawa napeleka ujumbe kwa wenzao wote wa Kitanzania. Ujumbe wangu ni mfupi sana. Tutafanya kila tuwezalo kuwapeni elimu. Lakini uamuzi wa kutumia elimu hiyo ni wenu. Tambueni kuwa upo mzigo mkubwa wa kuendesha nchi hii ambao unawasubiri. Jiandaeni vizuri. Someni kwa makini. Msituangushe. Na zaidi sana msipate UKIMWI. Thamani yenu ni kubwa sana na ni ya kudumu. Msiipoteze kwa tamaa za mwili zipitazo.

Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika,
Mafanikio ya mageuzi ya uchumi yametuwezesha pia kupanua elimu ya juu, kwa kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya dini. Matokeo yake katika miaka 4 iliyopita (1998/99 – 2002/03) idadi ya wanafunzi katika vyuo vya ufundi, vyuo vikuu binafsi na vyuo vikuu vya umma iliongezeka kutoka 18,829 hadi 30,602, sawa na ongezeko la asilimia 62.5. Cha kutia moyo zaidi ni kuwa ongezeko kubwa lilikuwa la wanafunzi wa kike ambao wameongezeka kutoka 3,889 hadi 10,137, sawa na ongezeko la asilimia 160.7. Miaka 4 tu iliyopita wanawake walikuwa asilimia 20.7 ya wanafunzi wote kwenye vyuo hivi. Leo wapo asilimia 33.1. Nawapongeza sana wanawake waliojitokeza kutafuta elimu ya juu. Maana Serikali inaweza kutoa fursa, lakini uamuzi wa kutumia fursa hizo ni wa mtu binafsi.

Mheshimiwa Spika,
Uwezeshaji kwa njia ya elimu ni sehemu muhimu ya mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto za utandawazi. Bado tunayo kazi kubwa ya kufanya. Lengo la Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2008 wawepo wanafunzi 55,000 katika vyuo vya ufundi, vyuo vingine vya elimu ya juu, na vyuo vikuu. Mambo matatu ni muhimu sana ili tufike hapo. Kwanza, Bunge hili liendeleze utashi wa kisiasa wa mkakati huu. Pili, uchumi ukue kwa kasi zaidi na kuipa Serikali mapato ya kutekeleza mipango yetu, na Bunge hili lichochee ukuaji huo. Tatu, elimu ya sekondari ipanuke na iboreke, kupitia mpango ambao nimeuzungumzia, ili tupate wahitimu bora wa kutosha kudahiliwa kwenye vyuo vyetu.

Napenda nilishukuru Bunge hili Tukufu kwa kukubali kupitisha Sheria Na. 8 ya 2001 iliyoanzisha Mfuko wa Elimu, ambao kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge watakumbuka una malengo matatu makuu:

· Kwanza, kuhakikisha elimu yetu katika ngazi zote ni bora zaidi;
· Pili, kuhakikisha upo mfumo endelevu wa kugharamia elimu nchini; na
· Tatu kuhakikisha mfumo wa elimu unatoa fursa sawa kwa wote, bila ubaguzi wowote.

Mfuko umeanza kazi, na tayari Mamlaka ya Elimu Tanzania inayousimamia imetoa Sh.3.4 bilioni kwa vyuo vya ufundi na vyuo vikuu vya umma Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na vyuo vikuu binafsi na vya mashirika ya dini. Narudia. Mfuko huu ni wa kuwezesha elimu kwa Watanzania wote, bila ubaguzi. Popote Mtanzania anapopata elimu, ujumla wake ni ongezeko la wasomi nchini ambayo ni hazina ya taifa. Tutaendeleza ushirikiano huu kati ya Serikali zetu mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, na taasisi binafsi za elimu nchini kwa lengo moja la kuongeza idadi na ubora wa nguvukazi ya taifa.


Afya

Mheshimiwa Spika,
Sekta ya afya ni muhimu sana katika vita dhidi ya umaskini. Lakini ni wazi pia kuwa mafanikio yake hayategemei utashi na maamuzi ya Serikali peke yake. Hatimaye afya ya mtu ina gharama, ambayo mwenyewe lazima awe tayari kuibeba. Ipo gharama ya kuzuia usiumwe – kwa kula chakula bora, kwa kuweka mazingira ya pale unapoishi na kufanya kazi kuwa safi, kwa kufanya mazoezi, kwa kuzuia magonjwa kwa chanjo pale palipo na chanjo, au kwa kuepuka kuambukizwa kwa magonjwa kama UKIMWI yasiyo na chanjo, na kwa kuchangia gharama za matibabu.

Mafanikio ya mageuzi yetu, na mahusiano mazuri na wahisani na sekta binafsi, yote yametusaidia kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo wa huduma za afya, ukarabati wa taasisi za afya na upatikanaji wa chanjo. Bajeti ya afya imekuwa ikiongezeka kwa miaka 3 mfululizo. Hili nalo limewezekana kwa sababu ya mafanikio ya mageuzi yetu ya kiuchumi.

Hali ya chanjo imeboreka na kufikia asilimia 83, kuzidi kiwango cha asilimia 80 ambacho kimataifa kimekubalika kuwa ni kiwango kizuri. Hivi sasa tumeanza kutoa chanjo ya Hepatitis ambayo imechanganywa na chanjo iliyopo ya DPTT bila malipo ya ziada. Hii itasaidia kuokoa maisha kati ya 20,000 – 25,000 yanayopotea kwa mwaka hivi sasa.

Tanzania ipo mstari wa mbele duniani katika vita dhidi ya malaria. Lakini tunaomba uelewa na ushirikiano wa wananchi. Tumefuta kodi kwenye vyandarua na bidhaa zinazosaidia vita dhidi ya malaria. Tumepata msaada wa Mfuko wa Kimataifa wa Kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. Hivyo tumeweza kufidia baadhi ya gharama za vyandarua vilivyotiwa dawa ambavyo imedhihirika vinasaidia sana kupunguza maambukizo ya malaria hasa kwa kina mama waja wazito na watoto wachanga. Lakini jitihada zetu hizo ni bure iwapo wananchi hawatatumia utaratibu uliowekwa.

Mheshimiwa Spika,
Duniani kote bima ya afya ndiyo kinga thabiti, hasa kwa wanyonge, ya kukabiliana na gharama za tiba. Kwa wananchi wa kawaida tumeanzisha Mifuko ya Afya ya Jamii. Pale ambapo mifuko hii inafanya kazi yapo mafanikio makubwa ambayo siri yake ni ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wananchi. Mifuko hiyo imewapunguzia mzigo na hofu wananchi, na kuzipatia hospitali uwezo wa kujiendesha. Tunataka mifuko hii ianzishwe katika wilaya zote zilizobaki katika miaka michache ijayo.

Kwa wafanyakazi wa sekta ya umma, tumeanzisha bima ya afya ambayo huchangiwa kati ya mfanyakazi na mwajiri. Matatizo mengi ya awali kutokana na uchanga wa mfuko yamepatiwa ufumbuzi, na kazi iliyo mbele yetu ni kuimarisha mfuko huo, na kuboresha taratibu zake.

Tumeendelea pia na ukarabati mkubwa wa vituo vya huduma za afya, kuanzia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo kazi inaendelea, mpaka hospitali za wilaya. Kwa mfano, kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi, tayari tumefunga mashine za eksirei na mashine nyingine katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa. Kazi iliyo mbele yetu ni kuvitumia vifaa hivyo vizuri, na kuvitunza, ili viendelee kutumika kwa miaka mingi ijayo na kuboresha uwezo wa madaktari kutibu wagonjwa kwa usahihi na uhakika zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Tumeendelea pia na mageuzi ya sekta ya afya (Health Sector Reform). Wilaya zote sasa zinatekeleza mageuzi hayo, yanayohusu, pamoja na mambo mengine, kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi katika kuamua kinachofanyika katika vituo vyetu. Hiki ni kielelezo kingine cha kuimarika kwa demokrasia kwenye eneo muhimu kama hili la vita dhidi ya umaskini. Nawasihi wananchi wachukue nafasi hii kuboresha huduma zinazotolewa kwenye vituo vya huduma ya afya, kupitia Bodi na Kamati za Huduma za Afya. Ningependa katika muda mfupi iwezekanavyo, Bodi na Kamati hizo ziwe zimeanzishwa nchini kote.

UKIMWI

Mheshimiwa Spika,
Tarehe 31 Disemba 1999, nilitangaza kuwa UKIMWI ni janga la Taifa. Niliwasihi wananchi wote, viongozi wa serikali, siasa, dini na wa kiraia, na asasi zisizo za serikali, kuchukua hatua mpya na za ziada ili kuliandaa Taifa kupambana na UKIMWI.

Zipo dalili za ongezeko la mwamko katika jamii kuhusu UKIMWI. Kila siku kuna taarifa kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu kuhusu jitihada za kudhibiti UKIMWI. Leo, UKIMWI unazungumzwa kwa uwazi zaidi kuliko miaka iliyopita.

Taarifa za awali zinaonyesha dalili ya kupungua kwa maambukizo ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa wanawake waja wazito katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu. Ili kupata taarifa sahihi za mwelekeo wa janga hili utafiti unafanywa kujua kiwango halisi cha maambukizo ya virusi vya UKIMWI.

Pamoja na ufinyu wa bajeti, Serikali imeamua kutoa dawa za kurefusha maisha bure kwa waishio na virusi vya UKIMWI kwa kadri ya uwezo wetu na msaada wa wahisani mbalimbali. Tunawashukuru wote wanaotusaidia na kushirikiana nasi.

Mheshimiwa Spika,
Vita dhidi ya UKIMWI ni ngumu na ya muda mrefu. Inahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu na hususan viongozi, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hatua inayofuata sasa ni kuhakikisha kila Mtanzania anaongozwa na kanuni tatu kuu za maisha zifuatazo:

· Kama hujaambukizwa, hakikisha huambukizwi;
· Kama umeambukizwa, hakikisha humwambukizi mwingine, na ujitunze ili uishi muda mrefu iwezekanavyo; na
· Unyanyapaa uwe mwiko.

Maji

Mheshimiwa Spika,
Mojawapo ya kero za wananchi, na kikwazo katika njia yao ya kujiendeleza, ni maji safi na salama. Ndiyo maana maji ni miongoni mwa vipaumbele katika Mkakati wa Taifa wa Kupiga Vita Umaskini. Mageuzi yetu ya uchumi, na usahihi wa sera zetu, kwa pamoja vimesaidia kuleta mafanikio ya kutia moyo. Kwa mfano:

· Idadi ya wakazi wa mijini wanaopata huduma ya maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 1998 hadi asilimia 73 hivi sasa.

· Idadi ya wananchi vijijini wanaopata maji safi imeongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 1995 hadi asilimia 53 hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,
Mafanikio haya yana maelezo yake. Kwanza, ni utashi mkubwa kisiasa kupambana na umaskini, kiashiria kimojawapo cha umaskini kikiwa kero ya maji. Pili, ni usahihi na Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 1991, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, ambayo inasisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga, kujenga, kuendesha na kumiliki miradi ya maji vijijini. Katika utaratibu huu miradi ya maji inamilikiwa na wananchi wenyewe, na Serikali na Wafadhili wanachangia nguvu zao katika utekelezaji. Kwa utaratibu huu wananchi wengi wameanzisha Kamati za Maji, na Mifuko ya Maji. Hadi kufikia Desemba 2003 Kamati za Maji 8,363 zilikuwa zimeshaanzishwa na kati ya hizo 7,226 zilikuwa na mifuko ya maji yenye thamani ya sh. 1.3 bilioni.

Kwa maneno mengine, sera hii inasema kuwa kero ya maji itamalizwa kwa ubia kati ya Serikali na wananchi. Hakuna tena wananchi kukunja mikono wakingoja Serikali au wahisani walete maji na wananchi watoe shukrani. Sasa ni ubia. Asiyetaka ubia, anayetaka kusubiri Serikali, atabakia kwenye lindi la umaskini. Na kwa mijini ubia huo ni wajibu wa kulipia huduma ya maji ili Mamlaka za Maji zijiendeshe bila kutegemea ruzuku ya Serikali, na zimudu gharama za utunzaji na ukarabati wa miundombinu ya maji. Lakini pia tuna utaratibu wa bei nafuu kwa wenye kipato cha chini.


Mheshimiwa Spika,
Nafurahi kuwa matunda ya sera hii yameanza kuonekana. Makusanyo ya maduhuli ya matumizi ya maji yameongezeka kutoka Sh. 400 milioni mwaka 1995 hadi Sh. 13.4 bilioni mwaka 2003. Kutokana na ongezeko hili la mapato, Mamlaka nane za Arusha, Tanga, Moshi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Tabora na Dodoma hivi sasa zinajitegemea katika gharama zote za uendeshaji, zikiwemo za umeme, mishahara na madawa ya kusafishia maji. Aidha, Mamlaka hizo zimeweza kuchangia katika ukarabati na upanuzi wa miundombinu yake. Lengo sasa ni kuhakikisha Mamlaka zote zinajitegemea kikamilifu ifikapo mwaka 2006.

Mheshimiwa Spika,
Maelezo ya tatu kwa nini tumefanikiwa ni usahihi wa, na matunda ya, mageuzi yetu ya kiuchumi. Kukua kwa uchumi, na ongezeko la mapato ya Serikali vimechangia kuipa Serikali uwezo wa kuongeza bajeti ya sekta hii muhimu kwa vita dhidi ya maskini. Na baada ya wahisani kuridhika kuwa tuko makini wametupunguzia deni la nje na kutuongezea misaada na mikopo ya masharti nafuu, na kutupa ushauri wa kiufundi.

Matokeo yake tumeweza kuongeza sana uwekezaji kwenye miradi ya maji mijini na vijijini. Hadi sasa miradi ya maji safi yenye thamani ya Sh. 20.4 bilioni katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Arusha, Moshi na Tanga, na miradi yenye thamani ya Sh. 11.4 bilioni ya uondoaji maji-taka katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Mwanza, Iringa, Arusha, Moshi na Mwanza imekamilika. Tunawashukuru sana wahisani kwenye sekta ya maji ambao ni pamoja na KfW, Benki ya Dunia, EU, ADB, BADEA na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Spika,
Ipo hadithi ya mlevi mmoja aliyepiga simu polisi akidai wezi wameingia kwenye gari lake na kuiba kila kitu. “Wameniibia dashibodi, usukani, breki, radio na hata kichapuzi,” akasema kwa uchungu. Lakini, kabla polisi hawajaanza uchunguzi, wakapokea simu nyingine kutoka kwa mlevi yule yule. “Oh!, msijali sana!” akasema huku akikatishwa na kwikwi. “Kumbe niliingia kwenye kiti cha nyuma kwa bahati mbaya.”

Mimi naamini kuwa wanaolalamikia mageuzi yetu ni wale ambao kwa bahati mbaya wanatafuta mafanikio yake mahali ambapo sipo. Naomba niwarejeshe kwenye kiti cha mbele, ili leo tumalize ubishi wa iwapo mageuzi yetu ya uchumi yana faida kwa mwananchi wa kawaida au la. Mimi nasema kama yupo anayengoja Serikali iweke fedha mfukoni mwake, huyo atasubiri sana na siku zote ataona mageuzi haya hayana faida kwake yeye binafsi, na pengine atahisi anaibiwa. Lakini hili ni Bunge, Bunge la nchi maskini. Bunge hili linapaswa kuwa na upeo mpana zaidi ya yule anayengoja Serikali iweke fedha mkononi mwake.

Kwa miaka mingi tumetamani kuwaletea wananchi wa mkoa wa Shinyanga maji kutoka Ziwa Victoria. Haikuwezekana kwa vile tulipanga kwa kutegemea fedha za wengine. Tulikazania kutafuta wahisani. Ufumbuzi umepatikana baada tu ya mageuzi yetu ya kiuchumi, yaliyoongeza uwekezaji nchini, yaliyofufua uzalishaji na huduma, na yaliyoongeza mapato ya Serikali.

Matokeo yake juzi hapa hapa Dodoma umetiwa saini mkataba wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya miji ya Kahama na Shinyanga kupitia vijiji kadhaa vya mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Ujenzi utaanza mwezi Mei 2004, na awamu ya kwanza imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2005. Gharama kwa awamu zote za mradi ni Sh.85.1 bilioni ambazo zitakuwa fedha zetu wenyewe.

Sasa mimi nauliza. Ninaposema anayedai mageuzi ya uchumi hayana faida kwa wananchi kafumba macho, ninakosea?

Mheshimiwa Spika,
Naomba nigusie kidogo tatizo la maji Jijini Dar es Salaam na ufumbuzi wake kama kielelezo kingine cha usahihi wa sera zetu, na mafanikio ya mageuzi yetu ya kiuchumi.

Sisi wote hapa ni viongozi. Zipo sifa za kiongozi bora: upeo mpana, uwezo wa kupima na kuamua, ujasiri wa kutenda. Na zipo sifa za kiongozi asiye bora: upeo finyu, uwezo mdogo wa kupima na kuamua, na woga na mashaka katika kutenda. Mimi ni muwazi na mkweli. Naomba Bunge hili Tukufu, Bunge ambalo ni tumaini la Watanzania, liniunge mkono ili kwa pamoja tuwe na upeo mpana zaidi, tuimarishe zaidi uwezo wetu wa kupima na kuamua, na hasa hasa tuwe jasiri zaidi kwa vitendo. Kubabaika, hata pale ambapo sera ni nzuri, ati kwa vile tu kuna kikwazo au mapungufu madogo hapa na pale, huleta picha ya watu, na viongozi, ambao hawajaamua kwa dhati, wanababaika, wanakwenda hatua mbele na hatua nyuma.

Nasema sisi ni viongozi. Tuonyeshe ujasiri wa kupeleka taifa mbele, si ujasiri wa kuwekea taifa breki. Nchi yetu ni maskini. Kila uamuzi una wema na ubaya wake. Inahitaji viongozi jasiri, wasioogopa, kuamua na kutenda.

Uamuzi wa kubinafsisha huduma za maji safi na maji-taka Jijini Dar es Salaam haukuwa rahisi hata kidogo. Lakini ilibidi tuamue baada ya kupima faida na hasara zake. Hatimaye tuliamua, tukakodisha miundombinu ya huduma hizo kwa kampuni ya City Water kuanzia tarehe 1 Agosti 2003. Cha kushangaza ni kuwa hata kabla miezi 6 ya ukodishaji huo haijaisha wapo wanaoanza kukosa subira, wakitaka matatizo yaishe mara moja. Haiwezekani. Matatizo haya tumekaa nayo, tumeyalea, kwa miaka chungu nzima. Tunathubutuje kutaka City Water iyamalize katika miezi 6 tu?

Ukodishaji huo umeiwezesha Serikali kupata mkopo wa Sh.164.6 bilioni kutoka Benki ya Dunia (IDA), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Rasilimali ya Ulaya (EIB). Utakaotumika kuboresha huduma ya maji Jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Kibaha na Bagamoyo.

Kazi ya kukarabati mifumo ya maji safi na uondoaji maji-taka inatarajiwa kuanza hivi karibuni. Ukarabati muhimu na wa haraka wa mitambo ya maji na mabomba ya maji yaletayo maji Jijini umeanza, na ukarabati mkubwa wa mitambo ya kusafisha maji ya Mtoni, Ruvu Juu na Ruvu Chini inatarajiwa kuanza mwezi Aprili 2004. Na kazi nyingine nyingi zitaanza mwaka huu.

Baada ya kazi hizi kukamilika huduma ya maji safi na uondoaji maji-taka katika Jiji la Dar es Salaam itaboreshwa kwa kiasi kikubwa. Uvujaji wa maji utapungua kutoka asilimia 55 za sasa hadi asilimia 28, na ukusanyaji wa mapato utaongezeka kutoka asilimia 45 hadi 90. Wateja walioungiwa maji wataongezeka kutoka 97,000 hadi 140,000, na wanaopata maji kwa uhakika kwa saa 24 watafikia asilimia 70. Vile vile idadi ya wateja waliofungiwa mita itaongezeka kutoka asilimia 3 hadi 95, na hivyo kuwafanya wateja wengi zaidi walipie maji kulingana na matumizi yao halisi. Na muhimu zaidi, uwekezaji katika kuboresha huduma ya maji hautategemea tena fedha kutoka Serikalini, bali itakuwa ni mapato yanayotokana na huduma yenyewe. Maana kila huduma ina gharama yake, inayopaswa kubebwa na anayeitumia, isipokuwa kwa wasiojiweza.

Kilimo

Mheshimiwa Spika,
Katika miaka kumi iliyopita, kilimo kimekuwa kikikua kwa wastani wa asilimia 3.1 kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa idadi ya watu unaokisiwa kuwa asilimia 2.9 kwa mwaka katika kipindi hicho. Ukuaji huu wa kilimo bado ni mdogo sana na hautawezesha kuondoa umaskini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Ndio maana tumeweka mkazo mpya kwenye kilimo. Mwaka 2002 kilimo kilikua kwa asilimia 5.0. Mwaka huu tulitarajia tufike asilimia 6, lakini kutokana na ukame unaoendelea kuikumba nchi yetu lengo hilo halitafikiwa.

Kati ya mwaka 2000/2001 na 2002/2003 uzalishaji wa mazao makuu ya biashara uliongezeka kama ifuatavyo: pamba tani 123,558 hadi 188,690; tumbaku tani 28,000 hadi 32,693.62, sukari tani 135,534 hadi 190,120, Mkonge tani 20,500 hadi 23,641, chai tani 26,385.5 hadi 28,028.13 na pareto tani 1,850 hadi 3,000. Uzalishaji wa mazao ya korosho ulishuka kutoka tani 122,283 hadi 90,000 na kahawa kutoka tani 58,134 hadi 52,439. Kushuka kwa uzalishaji wa korosho na kahawa kulitokana na wakulima kukosa fedha za kununulia pembejeo baada ya bei ya mazao hayo kushuka.

Eneo lililolimwa maua liliongezeka kutoka hekta 30 mwaka wa 1995 hadi hekta 100 katika mwaka wa 2002. Kiasi cha maua yaliyokatwa kilichouzwa nje kiliongezeka kutoka vikonyo milioni 98 hadi milioni 420 katika kipindi hicho. Aidha, Serikali imehamasisha sekta binafsi ambayo imeanza kuuza matunda na mbogamboga mbalimbali nje ya nchi.

Ubinafsishaji na uwekezaji katika viwanda vya kusindika mazao ya biashara hususan chai na sukari, umeonyesha mafanikio. Kwa mfano, ubinafsishaji na uwekezaji katika viwanda vya sukari vya Kilombero, Mtibwa, na Tanganyika Planting Company (TPC) umeongeza uzalishaji wa sukari nchini kutoka tani 113,622 za sukari mwaka wa 1998 hadi tani 228,743 katika msimu wa 2003/2004. Kiwanda cha Sukari cha Kagera kitaanza tena uzalishaji msimu wa 2003/2004 na kinatarajia kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka wa kwanza. Aidha, kufufuliwa kwa viwanda hivi kumeongeza ajira na mapato ya Watanzania na kuwezesha wakulima wengi kuingia katika kilimo cha mkataba (outgrowers). Kama yupo asiyekuwa na uhakika wa faida za ubinafsishaji akawaulize wakulima wadogo wa mkataba jirani na viwanda vya sukari vya Mtibwa na Kilombero, na baadaye mwaka huu, Kagera. Wabunge mnaotoka maeneo hayo mnajua.

Serikali katika awamu ya tatu imeongeza uwekezaji katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji maji mashambani, hususan katika ujenzi na ukarabati wa skimu ndogo za umwagiliaji maji mashambani. Narudia. Wanaodhani Serikali haikazanii kilimo cha umwagiliaji wanisikilize vizuri. Tangu mwaka wa 2002/2003 jumla ya Sh. 3.16 bilioni zimetumika katika kutekeleza shughuli za kilimo cha umwagiliaji maji mashambani. Mwaka wa 2002/2003 hekta 8,995 ziliendelezwa kwa ajili hiyo na kufanya eneo lote linalolimwa kuwa hekta 200,895. Aidha, ni matarajio ya serikali kwamba ifikapo Juni, 2004 eneo litakalokuwa limeendelezwa kwa umwagiliaji litafikia hekta 230,292.

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA), imekamilisha maandalizi ya sehemu ya kwanza ya Mpango Kabambe wa Kilimo cha Umwagiliaji Maji Mashambani. Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kwamba kuna hekta milioni 2.3 zenye uwezekano mkubwa wa kuendelezwa. Kwa jumla, Taifa lina hekta milioni 29.4 zinazofaa kuendelezwa kwa umwagiliaji maji mashambani.

Wakulima wanaoshiriki katika skimu ndogo za umwagiliaji sasa wanaweza kulima eneo moja hadi mara tatu kwa mwaka na kwa tija kubwa zaidi. Kwa mfano, uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka wastani wa tani 1.8/ha. hadi tani 5.0/ha., na unatarajiwa kuongezeka hadi tani 6-8/ha. Kipaumbele kimewekwa katika kufufua miundo mbinu ya umwagiliaji iliyojengwa miaka iliyopita, kuimarisha skimu ndogo za umwagiliaji maji mashambani, kuongeza uvunaji maji ya mvua kwa kujenga mabwawa na kueneza teknolojia ya uchimbaji visima na matumizi ya pampu ndogo zinazotumia dizeli na nishati mbadala ya jua na upepo.

Katika jitihada za kuwakaribisha na kuwashirikisha wakulima wa kati na wakubwa wakiwemo wataalam wa kilimo, Serikali imeendelea kuhamasisha sekta binafsi kuingiza nchini zana bora kwa ajili ya kuendeleza kilimo. Hatua hii ilichangia kuingiza matrekta 1,080 kati ya mwaka 2001 na 2003. Idadi hii ya matrekta ni kubwa ikilinganishwa na matrekta makubwa 50 yaliyoingizwa nchini mwaka wa 1999/2000. Aidha, mwaka wa 1999/2000 yaliingizwa matrekta madogo ya mkono 60 yaliyouzwa kwa bei nafuu na kwa mkopo. Aidha, Serikali iligharamia usafirishaji wa matrekta hayo hadi mikoani ili kumpunguzia mkulima gharama za usafirishaji.

Katika azma ya kumsaidia mkulima mdogo kuboresha kilimo, Serikali inaendelea kutoa mikopo ya kukarabati matrekta machakavu na ununuzi wa matrekta mapya. Mpaka sasa waombaji 272 wamepitishiwa maombi yao.

Katika kuzidi kuboresha huduma za utafiti, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa Vituo vyake 17 kati ya 22. Ukarabati huu umehusisha maabara, ofisi, nyumba za watumishi na miundombinu ya mashamba ya majaribio. Aidha, Vituo vyote 22 vimepatiwa vitendea kazi kama vile magari, matrekta, pikipiki na kompyuta. Jumla ya wataalam 97 kati ya wataalam 350 wamepatiwa mafunzo ya shahada za juu (MSc na Ph.D) katika kipindi hiki, na hivyo kuwaimarisha kitaaluma.

Katika kuimarisha utafiti wa mazao ya biashara, Serikali imeamua kuwashirikisha wadau wa mazao ya chai, kahawa na tumbaku katika uendeshaji na usimamizi wa utafiti wa mazao hayo kwa kuanzisha Taasisi za Utafiti zilizo nje ya mfumo wa kiserikali. Taasisi hizo ni ‘Tea Research Institute of Tanzania’ (TRIT), ‘Tanzania Coffee Research Institute’ (TACRI) na Tobacco Research Institute of Tanzania’ (TORITA). Vyombo hivi vinawajibika moja kwa moja kwa wadau wa mazao hayo, hususan wakulima. Ufanisi mkubwa tayari umeshaonekana kutokana na mfumo huu.

Narudia, Mheshimiwa Spika, utashi wa kisiasa wa Serikali hii kukuza kilimo ni mkubwa, na yote yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika yanawezekana kutokana na mafanikio ya mageuzi ya uchumi nchini. Hatuna muujiza wa kumaliza matatizo yote siku moja; lakini usahihi wa sera na mwelekeo wetu upo dhahiri, sambamba na utashi wa kisiasa.

Mifugo:

Mheshimiwa Spika,
Ubinafsishaji ni sehemu ya mageuzi ya uchumi tunayoyafanya, na ambayo yanatoa fursa kwa Watanzania kujiendeleza na kumiliki uchumi wa taifa lao. Ningependa nitumie mfano wa ubinafsishaji wa mashamba makubwa ya mifugo na ranchi za taifa kuelezea dhana hii na jitihada za Serikali kuwawezesha wananchi kutumia fursa hii.

Mwezi Februari 2002, Serikali, kwa makusudi, iliamua kuwa ubinafsishaji wa mashamba makubwa ya mifugo na ranchi za taifa utumike kuwezesha Watanzania kuingia kwenye ufugaji wa kisasa, ufugaji wa kibiashara.

Katika mkakati huo, ranchi saba za NARCO, ambazo ni Kikulula Complex, Kitengule, Mkata, Missenyi, Kalambo, West Kilimanjaro na Mzeri, kila moja itatenga eneo la hekta 20,000 ambalo litaendelezwa kama ranchi ya mfano chini ya NARCO. Maeneo ya ranchi hizi yanayobaki, pamoja na maeneo yote ya ranchi za Usangu na Uvinza, yatagawanywa katika maeneo ya ranchi ndogo za ukubwa wa hekta 4,000 kila moja ambazo zitamilikishwa Watanzania wenye nia na uwezo wa kufuga kibiashara.

Aidha, ranchi za Kongwa na Ruvu zitabaki kuwa maeneo yasiyo na magonjwa ili kuiwezesha nchi yetu kuwa na mifugo inayokubalika kwenye soko la nje. Utaratibu wa kugawa ranchi, ambao utakamilika mwezi Juni, 2004, utahusisha jumla ya hekta 400,000 ambazo zitagawanywa ili kupata ranchi ndogo zipatazo 100 zitakazoendelezwa na wawekezaji binafsi wa Kitanzania.

Mashamba ya ng’ombe wa maziwa ya Serikali yaliyokuwa chini ya DAFCO nayo yaliingizwa kwenye utaratibu huu wa kubinafsishwa kwa wananchi. Hadi sasa mashamba yaliyobinafsishwa kwa wawekezaji wananchi ni Utegi (Tarime), Ruvu (Pwani), Ihimbu (Iringa) na kwa shamba la maziwa la Rongai ubinafsishaji kwa mwekezaji Mtanzania upo katika hatua za mwisho. Shamba la ng’ombe wa maziwa la Malonje litagawanywa katika maeneo madogo ya hekta hamsini kila moja na kumilikishwa Watanzania wenye nia na uwezo wa kufuga kibiashara. Matumaini yangu ni kuwa ubinafsishaji huu wa makusudi ya kusaidia na kuwawezesha wananchi utakuwa na mafanikio makubwa kuliko ule tulioufanya kwenye mashirika ya biashara, huduma na viwanda. Naomba wajitokeze Watanzania wenye nia, mipango mizuri, na uwezo, na sisi Serikali tutawaunga mkono na kuwasaidia.

Miundombinu

Mheshimiwa Spika,
Miundombinu bora ya kiuchumi ni ya lazima ikiwa tunataka kuvutia wawekezaji, na kuwawezesha wananchi kushiriki uchumi wa soko. Kazi kubwa imefanyika kwenye eneo hili, lakini nitatoa mifano mitatu tu—barabara, simu na bandari.

Mojawapo ya miundombinu muhimu kwa uwezeshaji wananchi kiuchumi na kijamii, pamoja na kuchochea uzalishaji na biashara, ni barabara. Uchumi wa soko ndani na nje ya nchi hauwezi kutengemaa bila barabara nzuri zinazowezesha watu, mazao, bidhaa na huduma kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tatu iliamua tangu mwanzo kuendeleza kazi ya ujenzi wa barabara iliyoanza kwenye Serikali zilizotangulia. Kwa ushirikiano na Bunge hili, tumefanya kazi kubwa ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, madaraja na vivuko.

Katika miaka 8 iliyopita (1995 – 2003) tumekamilisha miradi ifuatayo: Tumekarabati na kupanua barabara zenye urefu wa km 68; tumejenga barabara za lami kiasi cha km 194; tumejenga Daraja la Mto Rufiji na madaraja mengine 22; tumekamilisha upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Songea-Mbamba Bay; na tumenunua vivuko vya Kilombero na Ukara.

Hiyo ni miradi iliyokamilika. Lakini ipo mingine mingi iliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo: Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa km 961; ukarabati wa km 197 za barabara za lami; upembuzi yakinifu wa barabara zenye urefu wa km 943; na usanifu wa kina wa km 367 za barabara.

Ipo pia miradi ambayo maandalizi yake ya ujenzi na ukarabati wa km 587 yanaendelea. Miradi ya barabara na madaraja ni mingi. Siwezi kuiorodhesha yote hapa. Napenda nikushukuruni, Waheshimiwa Wabunge, kwa kuunga mkono Serikali katika mkazo huu tuliouweka kwenye mundombinu na hususan barabara.

Mheshimiwa Spika,
Naomba nielezee mradi wa ujenzi wa barabara kwa fedha zetu wenyewe kama kielelezo kingine cha mafanikio ya mageuzi yetu ya kiuchumi, na dhamira ya Serikali kuwawezesha wananchi kujiendeleza.

Kwa miaka mingi miradi muhimu ya barabara ilichelewa kwa vile tulikuwa tunawategemea mno wahisani. Wakati mwingine walisema hawana fedha, wakati mwingine fedha zilichelewa na kusababisha gharama za ujenzi kupanda, wakati mwingine masharti ya kupewa msaada au mkopo yaligeuka kuwa kero.

Kwa kadri mapato ya Serikali yalivyoongezeka, tulipata ujasiri wa kujenga barabara kwa haraka zaidi, kwa kutumia fedha zetu wenyewe. Tukaamua kila mwezi kutenga Sh.1.84 bilioni kwa lengo hilo. Katika kipindi cha miaka mitano, 2001/02 – 2005/06, barabara zifuatazo zitajengwa kwa kiwango cha lami kwa utaratibu huu:

1. Barabara ya Somanga-Masaninga na daraja la Matandu (km 33).

2. Barabara ya Nangurukuru-Mbwemkulu (km 95).

3. Barabara ya Mbwemkulu-Mingoyo (km 95).

4. Barabara ya Dodoma-Manyoni (km 124).

5. Barabara ya Manyoni-Singida (km 122).

Mheshimiwa Spika,
Narudia. Asemaye mageuzi yetu hayamsaidii mwananchi amefumba macho kwa hiari yake. Bila mageuzi tusingepata mapato ya kutupa ujasiri huu wa kujitegemea, ambao ni uwezeshaji wa kweli wa wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Haiwezekani kushiriki fursa za utandawazi bila ya matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, kuanzia simu za kawaida, simu za mkononi, kompyuta, tovuti, intaneti, satelaiti, na kadhalika.

Uwezo wa mitambo ya simu umeongezeka kutoka njia 125,703 mwaka 1993 hadi njia 242,175 mwaka 2002. Hivi sasa zipo njia za simu za mkononi zaidi ya milioni moja. Huduma hii si tu imechangia kurahisisha mawasiliano ya kibiashara, kijamii na kifamilia, bali pia kwa ujumla wao makampuni ya simu sasa huchangia sana mapato ya Serikali.

Yapo maendeleo ya kutia moyo pia kwenye mifumo na matumizi ya intaneti, inayoweza kurahisisha sana upatikanaji wa elimu, habari na ufanyaji biashara, kwa gharama nafuu. Hivi sasa mikoa karibu yote ina vituo vinavyotoa huduma ya intaneti, kasoro Lindi, Rukwa na Ruvuma. Matarajio yetu ni kuwa mikoa hii nayo itapata vituo hivi kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mheshimiwa Spika,
Eneo moja lenye uwezo wa kuongeza mapato ya taifa kwa haraka ni bandari. Nchi yetu imebahatika kuwa katika eneo zuri sana kijiografia. Bandari zetu zinahudumia nchi jirani 6. Ni wajibu wetu kutoa huduma bora bandarini na hivyo kuhimili ushindani wa bandari nyingine kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi.

Ili kufikia lengo hili tumepanua na kuboresha Lango la Bandari kule Dar es Salaam, tumejenga eneo la kuhudumia makontena, tumenunua vifaa vya kuhudumia mizigo kwa bandari zote, tumepanua eneo la bandari ya Mtwara, tumejenga kituo cha kuongozea meli Dar es Salaam, na kuboresha eneo la matishari kwenye bandari ya Tanga.

Baada ya kubinafsisha huduma za Kitengo cha Makontena, ufanisi wake umeboreka sana na leo kimekuwa cha kwanza kwa ufanisi Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam imeongeza idadi ya mizigo iliyoshughulikiwa hapo kutoka tani 3.5 milioni mwaka 1998 hadi tani 4.5 milioni mwaka 2002.

Biashara ya Nje

Mheshimiwa Spika,
Yapo mambo ambayo Watanzania lazima tuelezane ukweli. Haiwezekani kwa nchi yetu kuendelea kwa heshima, kwa kujitegemea, bila kuongeza ukubwa na thamani ya mauzo yetu nchi za nje. Ni kweli kumekuwapo na ongezeko kubwa la mauzo ya nje katika miaka michache iliyopita, kutoka USD 682.9 milioni mwaka 1995 hadi USD 877.1 milioni mwaka 2002. Lakini ukweli ni kuwa ongezeko hilo limechangiwa zaidi na mauzo ya madini, hususan dhahabu. Sasa, si jambo zuri hata kidogo kutegemea mno mauzo ya madini. Maana, kwanza bei yake ina hulka ya kubadilika badilika kila mara. Na pili, madini yanakwisha. Tunahitaji kujenga uchumi wetu kwa mauzo nje ya nchi ambayo yanatokana na uzalishaji viwandani.

Tunajivunia pia akiba kubwa ya fedha za kigeni. Lakini ningefurahi zaidi iwapo fedha hizo zingekuwa za Watanzania waliouza nje bidhaa na huduma. Hivi sasa kiasi fulani cha akiba hiyo kinatokana na fedha za mikopo na wahisani. Si jambo zuri hata kidogo. Kwa nini Watanzania hawauzi nje ya nchi? Kinachotushinda ni nini? Hayo ndiyo maswali ya msingi kujiuliza. Kwa nini tunasita kuvutia wawekezaji kwenye viwanda ili kuongeza uwezo wetu wa kuuza nje bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, huku wananchi wakipata ajira? Lakini, nikihimiza uwekezaji huo, naambiwa Mkapa anauza nchi. Tutaamka lini Watanzania na kuelewa hali halisi ya dunia na mwelekeo wake ndani ya utandawazi?

Ngoja niwape mifano. Jamhuri ya Dominika ina ukubwa wa kilometa 48,072 za mraba (asilimia 5 ya Tanzania) na watu 8.7 milioni (asilimia 25 ya Watanzania) tu. Hawana kitu cha zaidi kuliko sisi. Uchumi wao unategemea sukari, kahawa, tumbaku, saruji na madini kidogo. Katika miaka ya karibuni sekta ya huduma, hususan utalii na maeneo huru ya biashara, imezidi kilimo kama mchangiaji mkubwa wa uchumi. Mwaka 2000 waliuza nje bidhaa za USD 5.7 bilioni (mara 8 ya kwetu kwa mwaka huo) na huduma za USD 3.2 bilioni (mara 5 ya kwetu kwa mwaka huo).

Mheshimiwa Spika,
Haya ndiyo maswali ya msingi ya Watanzania kujiuliza. Tunashindwaje na nchi ndogo kama Jamhuri ya Dominika kuuza nje ya nchi?

Mwaka jana, mwezi Agosti, tulizindua Sera ya Taifa ya Biashara, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuiwezesha Tanzania kupiga vita umaskini kwa kufanya biashara, ndani na nje ya nchi.

Nalishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha Sheria ya Maeneo Maalum kwa Mauzo Nje (EPZ) ili kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha bidhaa kwa soko la nje. Tayari viwanda viwili vimeanzishwa na vinauza nje kwa utaratibu huu. Lakini kasi hii bado ni ndogo sana. Ni aibu kubwa kwamba mimi niko mstari wa mbele kudai nchi tajiri zifungue milango kwa bidhaa zetu, wakati ambapo bado Tanzania haina bidhaa za kutosha za kuuza!!

Nikiulizwa kipi hasa ninashindwa kuuza nitasemaje? Nikiulizwa wauzaji nje makini wako wangapi nitajibu nini? “Hodari wa kelele, dhaifu wa vitendo.” Ndio sisi Watanzania, nitaambiwa! Haki yetu ya kuuza Marekani kwa masharti nafuu chini ya utaratibu wa AGOA bado hatuitumii kikamilifu. Jirani zetu Kenya wako mbali. Haki yetu ya kuuza katika nchi za Umoja wa Ulaya zinazoturuhusu kuuza karibu kila kitu isipokuwa silaha, nayo hatuitumii kikamilifu. Lakini ninapokaribisha wawekezaji kuharakisha kujenga uwezo wetu kuuza nje, na wakati huo huo kuleta ajira, wanaibuka wale wanaosema Mkapa anauza nchi. Watu wa ajabu sana hawa!

Mimi bado naamini kuwa tukijituma zaidi tunaweza kufanya mambo mengi makubwa. Mwaka jana, kwa mfano, Wizara ya Ushirika na Masoko ilihamasisha na kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wa mboga mboga, maua, matunda na viungo vya vyakula kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya bidhaa hizo kule Rostock, Ujerumani. Walipata mafanikio makubwa, ambapo Tanzania ilipata Nishani ya Heshima, na washiriki kutoka Tanzania walipata jumla ya medali 33, ikiwemo 12 za dhahabu, 14 za fedha na 7 za shaba. Medali hizo hata hivyo hazitakuwa na maana kama hatutauza.

Nasema inawezekana iwapo tutajituma zaidi na kutumia vizuri fursa na uwezeshaji unaofanywa na Serikali. Kwa taarifa tu, Jamhuri ya Dominika inauza nje bidhaa hizo za matunda na mbogamboga zenye thamani ya USD 104.2 kwa mwaka. Sisi, pamoja na nchi kubwa kama hii aliyotupa Mwenyezi Mungu tunashindwaje, hasa baada ya mafanikio ya Maonyesho ya Rostock?

Cancún

Mheshimiwa Spika,
Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Biashara Duniani ulivunjika kule Cancún mwezi Septemba 2003 bila makubaliano kufikiwa kuhusu mwenendo wa biashara duniani. Ulivunjika pia bila kuendeleza mbele ajenda ilioanza kule Doha, ya kuhusisha biashara na maendeleo ya nchi maskini. Kuvunjika kwa mkutano huo ilikuwa pigo kubwa kwa maendeleo ya nchi kama zetu, na kwa utaratibu bora wa utawala duniani kwa mashauriano badala ya kila nchi moja, au kundi la nchi, kujiamulia wenyewe, bila kuzingatia athari za maamuzi yao kwa wengine.

Chanzo hasa cha mkutano kuvunjika ni kuwa ahadi nyingi zilizowekwa kule Doha hazikutekelezwa, na nchi maskini zilionyesha wazi kukataa kuendelea na hadaa za mataifa makubwa. Karibu kila nchi, hata zile tajiri, inakiri kuwa ruzuku zinazotolewa kwa wakulima na wafugaji katika nchi tajiri – zikiwemo ruzuku za uzalishaji, na za kuuza nje ya nchi zao – zimeathiri sana uwezo wa wakulima na wafugaji katika nchi maskini, ambao wao hawapati ruzuku, wa kushindana na bidhaa za wenzao wanaopata ruzuku katika nchi tajiri.

Isitoshe nchi hizo zina vikwazo vya aina mbalimbali vinavyozuia wakulima na wafugaji katika nchi maskini kuuza kwao, hasa kwa kadri bidhaa hizo zinavyoongezewa thamani kwa kusindikwa.

Jambo la kujivunia kwa nchi maskini na zinazoendelea ni kuwa kule Cancún tuliungana na kuwa kitu kimoja, tukakataa kuendelea kuburuzwa kwenye suala la ruzuku kwa wakulima na wafugaji katika nchi tajiri, na pia suala la wakubwa kutuharakisha mno kuzungumzia mambo yaitwayo “Masuala ya Singapore”, masuala ambayo dhahiri yanawaongezea wao, na kutupunguzia sisi, fursa na tija katika biashara na uwekezaji. Umoja na uimara wa nchi maskini na zinazoendelea kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kushindwa kwa nchi tajiri kutoa majibu muafaka kwa madai ya nchi zinazoendelea, ndiyo mambo yaliyosababisha mkutano uvunjike.

Hivi sasa juhudi zinaendelea kujaribu kufufua duru ya mazungumzo ya biashara duniani, duru ambayo kule Doha tulikubaliana iitwe Duru ya Maendeleo. Lakini ni wazi duru hiyo haiwezi kuwa ya maendeleo bila makubaliano juu ya kupunguza na hatimaye kufuta zile ruzuku kwenye kilimo na ufugaji zinazofanya kusiwe na usawa wala haki kwenye biashara. Tunaziomba sana nchi tajiri wasiishie kwenye kukiri kwamba ruzuku zao zinatuumiza, bali wachukue hatua mapema ya kuzirekebisha na hatimaye kuzifuta.

Tunatoa wito kwa nchi zote duniani tuanze tena mazungumzo, lakini kwa kuelewana kuwa Cancún ilikuwa mwanzo wa mfumo mpya wa majadiliano, mfumo unaozingatia kwa dhati kuwa maskini nao wana haki, wanastahili kusikilizwa, na wanastahili kusaidiwa ili kutumia biashara kujiendeleza, badala ya kuzidi kutegemea misaada ya wahisani.

Utandawazi

Mheshimiwa Spika,
Wakati nahutubia Bunge lako Tukufu, 30 Januari 2002, ndiyo nilitoka tu kupewa heshima na Shirika la Kazi Duniani kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Kimataifa Kuhusu Masuala ya Kijamii katika Utandawazi. Tume hiyo niliyoiongoza na Mwenyekiti-Mwenza, Mheshimiwa Tarja Halonen, Rais wa Finland, imemaliza kazi zake na tunatarajia kuzindua Ripoti yake mjini Geneva na London tarehe 23 na 24 Februari 2004. Aidha, natarajiwa kuikabidhi Ripoti hiyo rasmi kwenye Baraza la Utendaji la Shirika la Kazi Duniani baadaye mwezi ujao.

Madhumuni ya msingi ya Tume ilikuwa kujaribu kuanzisha mjadala wa kiungwana kuhusu utandawazi, hususan athari zake katika masuala ya kijamii. Tume imezibainisha athari hizo, ikiwemo kwenye maeneo ya kiuchumi na kimaendeleo. Aidha, imesisitiza nafasi kubwa ya utandawazi, ukiongozwa vizuri, kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya jamii zote duniani. Tume inaonya kwamba pamoja na kwamba utandawazi waweza kuwa wa manufaa makubwa kwa jamii zote duniani, sasa hivi kuna hofu na hasira kubwa kutokana na jinsi utandawazi unavyoendelea. Hii ni hatari, si tu kwa jamii inayoathirika, bali kwa jamii nzima ya kimataifa. Ipo methali ya Kichina isemayo: “Moto hauwezi kufunikwa kwa karatasi.” Ujumbe wa Tume ni kuwa moto wa chuki inayojengeka dhidi ya utandawazi haiwezi tena kufunikwa kwa karatasi.

Ili kuzikabili athari za utandawazi tutahitaji kuungwa mkono na viongozi wa kisiasa na kibiashara katika ngazi zote, kimataifa, kikanda na kitaifa. Lakini hatuwezi kuulaumu utandawazi kwa kila shida yetu, na umaskini wetu. Ufumbuzi wa matatizo ya utandawazi unaanzia nyumbani. Kama taifa, tunayo mengi ambayo hatuna budi kuyafanya ili kunufaika na utandawazi. Mojawapo, kama nilivyosema, ni elimu. Vijana tunaowatayarisha kuongoza maendeleo ya taifa letu hawana budi kuwa vijana wanaoyakidhi mahitaji ya maendeleo ya kisasa, hasa katika uzalishaji na ajira. Wakati tunajitahidi kujenga mazingira yatakayowezesha utandawazi kuwa wa manufaa kwa nchi zote, sharti tuelewe kwanza kwamba hatma ya nchi yetu ipo mikononi mwetu. Dunia iliyopo nje yetu inaweza kuendelea bila sisi. Lakini siamini kwamba sisi tunaweza kuendelea bila dunia hiyo.

Tukishajiandaa vya kutosha ndani ya nchi yetu ndipo tutapata nguvu na uhalali kudai ziwepo sheria na taratibu zinazotabirika na zinazolinda maslahi ya wanyonge katika biashara na maendeleo duniani.
Mambo ya Nje

Mheshimiwa Spika,
Yote niliyoyasema yanatoa changamoto kubwa sana kwa sera yetu ya mambo ya nje. Lazima tujenge uwezo wa kutambua misukumo ya mabadiliko yanayokabili dunia, na kubuni sera na mbinu zitakazotuwezesha kuyakabili na wakati huo huo kuendeleza amani, utulivu na maendeleo hapa nchini, kwa majirani zetu, bara letu na duniani kote.

Kwa muda mrefu ukosefu wa amani katika nchi za jirani umekuwa ni mzigo mkubwa kwa taifa letu, hasa kwa maana ya wakimbizi na uharibifu wa mazingira. Hatuwezi kupata suluhu ya kudumu ya matatizo kama haya kwa juhudi zetu peke yetu. Matatizo haya yanahitaji mtazamo mpana, wa pamoja, kikanda, na kimataifa.

Nchini Burundi, serikali ya mpito inaendelea vizuri, hivi sasa ikiongozwa na Rais Domitien Ndayizeye. Tunamshukuru yeye na Warundi wote kwa jitihada wanazozifanya ili amani ya kudumu ipatikane nchini kwao. Hivi karibuni vikundi vya waasi vimekubali kuweka chini silaha zao na kushiriki kutafuta suluhu ya matatizo yao. Tunaendelea kukihimiza kikundi kilichobakia cha FNL ili nao wajiunge na Warundi wenzao katika kujenga mustakabali wa nchi yao kwa amani. Kama kawaida tuko tayari kusaidia jitihada hizo.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jitihada za Wakongo chini ya Rais Joseph Kabila zinaendelea kuleta matumaini kwa amani ya nchi hiyo iliyoteseka sana, na hata katika eneo lote la Maziwa Makuu. Tunawashukuru sana Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Makamu wake Bwana Jacob Zuma kwa jitihada zao. Tunawashukuru viongozi wengine wa ukanda wa Maziwa Makuu ambao wametoa mchango mkubwa katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya eneo letu.

Aidha, kwa kuelewa umuhimu huu, jumuiya ya kimataifa, ikiongozwa na Umoja wa Mataifa, ipo mbioni kutayarisha Mkutano wa Kimataifa Kuhusu eneo ya Maziwa Makuu. Nchi yetu imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

Kusudi kubwa la mkutano huo ni kutafuta mkakati wa kimataifa utakaoziunga mkono juhudi za nchi zetu kukabili vyanzo vya vita, kuainisha misaada ya maendeleo na kujenga uwezo wetu wa kuzuia vita na kulinda amani.

Kwa muda mrefu eneo letu limefahamika kama eneo la vita. Hali hii imetunyima nafasi ya kutumia umoja wetu na maliasili zetu kwa manufaa ya nchi zetu na watu wake. Sura hii haitoi mtazamo wa maendeleo, na sio kivutio cha mitaji wala wawekezaji katika eneo letu. Tanzania itashiriki kikamilifu jitihada zote za kufanya eneo la Maziwa Makuu liwe na amani ya kudumu, na maendeleo endelevu, na ligeuke kuwa ukanda wa amani.

Ulinzi na Usalama

Mheshimiwa Spika,
Sababu mojawapo ya kuhamishia majukumu ya uzalishaji na biashara kutoka Serikalini kwenda sekta binafsi, ni kuipa Serikali fursa kushughulikia vizuri zaidi majukumu asilia ya dola ikiwemo ulinzi na usalama.

Na majukumu hayo yanatekelezeka tu iwapo Serikali ina uwezo wa mapato, uwezo ambao kwetu sisi umechangiwa sana na mafanikio ya mageuzi yetu ya uchumi. Ninafurahi kulijulisha Bunge hili Tukufu kuwa ongezeko kubwa la mapato ya Serikali limetuwezesha kuhudumia majeshi yetu vizuri zaidi, na kuyawezesha kutekeleza majukumu yake vizuri zaidi. Nitataja machache tu tuliyoweza kuyafanya.

La kwanza, kwa umuhimu, ni kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeweza kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha upo ulinzi imara kwa nchi nzima, ili wananchi wafanye kazi zao na kuishi bila hofu. Sera yetu ya ulinzi inaweka mkazo mkubwa kwenye ulinzi wa mgambo. Hali nzuri ya kifedha imetuwezesha kuendeleza mafunzo ya mgambo, na matunda ya kuimarika kwa ulinzi wa mgambo yameanza kuonekana hasa sehemu za mipakani.

Sera yetu pia ni ya kuwa na jeshi dogo, la kitaalam, lililoiva kwa ujuzi, uwezo, uhodari, nidhamu na utii. Mafunzo ya jeshi la aina hiyo ni ghali, lakini ni muhimu sana. Na kwa sasa hivi tumeweza kufanya mazoezi ya kijeshi sisi wenyewe, na pia kwa kushirikiana na nchi jirani.

Mafanikio ya mageuzi yetu ya uchumi yametuwezesha pia kukidhi baadhi ya huduma muhimu kwa Maafisa na Askari wa JWTZ na JKT. Kwa mfano:

· Hospitali za Jeshi, ikiwemo Hospitali Kuu ya Lugalo, na hospitali za kanda za Mbeya na Mwanza zimekarabatiwa na kupatiwa vifaa ili kuhudumia maafisa na askari, na wananchi.





· Upatikanaji na ubora wa chakula kwa wanajeshi umeboreka sana.

· Mabwalo vikosini yameimarishwa.

· Maduka ya Bei Nafuu yamefunguliwa kwenye vikosi vingi.

· Zimenunuliwa ndege mbili kubwa za usafirishaji ambazo pia zinaweza kutumika wakati wa maafa.

· Jeshi limenunua sare mpya za kutosha Maafisa na Askari wote.

· Tatizo la malazi kwa askari wapya na kwenye vyuo limeondolewa, na wanapata vifaa vya kutosheleza.

· Tumeweza pia kukamilisha ujenzi wa nyumba ambazo kwa miaka mingi zilikuwa hazijakamilika kule Monduli, Arusha, na Ihumwa, Dodoma.

· Tumeweza kuanza mradi wa kuboresha utawala na utoaji maamuzi kwa kuweka kompyuta kwa awamu.

· Uwajibikaji na usimamizi kuhusu matumizi ya fedha za Serikali umeboreka sana. Hakuna tena malimbikizo makubwa ya madeni, na hoja za ukaguzi zimepungua.

· Mishahara na posho za chakula vimeboreshwa kiasi, na ucheleweshaji malipo haupo tena.

· Tumefufua utaratibu wa kupeleka vijana Jeshi la Kujenga Taifa.

· Tumekarabati makambi ya JKT Ruvu, Makutupora, Oljoro na Mafinga. Mengine yanaendelea kukarabatiwa.

· Tumeweza kujenga ofisi mpya za Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye hadhi inayostahili.

· Tumeweza pia kuboresha hali kwenye majeshi yetu ya Polisi na Magereza.

Mheshimiwa Spika,
Ningeweza kuendelea na kuendelea. Niliyosema yanatosha kuonyesha kuwa anayesema haoni faida ya mageuzi yetu ya uchumi, basi ama amekaa kiti cha nyuma au amefumba macho! Nasema, tukumbuke tulikotoka. Na kwa kweli natoa shukrani zangu kwa uvumilivu wa Wakuu, Maafisa na Askari wa majeshi yetu yote ya ulinzi na usalama tulipokuwa tunakusanya nguvu na kurekebisha uchumi, kulikoambatana na kufunga mikanda. Nawapongeza wote pia kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwa niaba ya taifa lao. Najua matatizo hayajaisha, lakini tumeanza vizuri na tutaendelea kwa kadri uchumi unavyokua.

Kwa mfano, Jeshi la Polisi limepewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali ili kuliwezesha kutimiza kwa ukamilifu majukumu yake ya kuhakikisha panakuwepo amani nchini na kulinda watu na mali zao.

Bajeti ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) na maendeleo imeongezeka kutoka Sh.15.5 bilioni mwaka 2001/02 hadi kufikia Sh. 42.8 bilioni mwaka huu wa fedha wa 2003/04. Hii ni nyongeza ya asilimia 176.1 kwa miaka 2 tu!

Jeshi la Magereza nalo limepewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali. Bajeti ya Jeshi la Magereza kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) na maendeleo imepanda kutoka Sh.12.1 bilioni mwaka 2001/02 hadi Sh. 28.5 bilioni mwaka huu wa 2003/04. Hili ni ongezeko la asilimia 135.5. Kutokana na nyongeza hii hali katika magereza yetu imeanza kuwa nzuri. Kilichobaki sasa ni kushughulikia tatizo la msongamano wa wafungwa.

Serikali imeanza kuviimarisha vikosi vya Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri. Kwa kuanzia tayari Serikali Kuu imetoa Sh. 1.5 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari mapya kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na sh. 600 milioni kwa ajili ya Jiji la Mwanza. Halmashauri za Mikoa mingine saba zitafaidika na mpango huu katika mwaka ujao wa fedha. Na hapa napenda niwapongeze wote walioshiriki kwa namna, na kwa viwango, tofauti katika kuzima moto uliotokea tarehe 22 Januari 2004 kwenye matangi ya mafuta kwenye kituo cha TANESCO Ubungo, kule Dar es Salaam. Kwa namna ya pekee kabisa nawapongeza sana na kuwashukuru mno askari zimamoto wa Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam, Mrakibu Mpemba Mputa Magogo na Sajini Fadhili Matola, ambao ujasiri wao wa kupigiwa mfano uliepusha hasara kubwa na maisha ya raia wenzao wengi waliokuwa hatarini.


Tujivunie Mafanikio na Kujitangaza

Mheshimiwa Spika,
Leo nimekumbuka sana hadithi za walevi. Wawili walikuwa wanatembea usiku. Mmoja akaangalia juu, akamwambia mwenziwe, “ Usiku wa leo ni mzuri kweli. Hebu ona mwezi ulivyopendeza!” Mwenziwe akasimama, akapepesuka kidogo, kisha akajibu, “Wewe vipi, umelewa nini? Huo sio mwezi, hilo ni jua.” Wakabishana kwa muda mpaka walipomwona mtu wa tatu akipita karibu yao. Kumbe naye mlevi. Wakamwuliza, “Samahani bwana. Hebu tusaidie. Lile ni jua au mwezi?” Mlevi wa tatu akasimama, akafinya macho, kisha akajibu, “Sijui bwana, mimi ni mgeni hapa!”

Mheshimiwa Spika,
Sitarajii Mtanzania akiulizwa kuhusu uzuri wa wazi wa kazi iliyofanyika katika nchi yetu ajibu kuwa yeye hajui kwa vile haishi hapa. Sote tunaishi hapa, na tunajua tulikotoka. Nawaomba Watanzania wakumbuke tulikotoka, na wasione haya kukiri kuwa tumepiga hatua kubwa. Najua si hulka yetu kujisifu, lakini dunia ya leo inahitaji kujisifu. Tusiwaachie wageni tu ndio kila mara wanaimba sifa zetu, wakati wenyewe tunakuwa kama hatuhusiki na hatuoni.

Na wote hao wanaotusifu, pamoja na wawekezaji wakubwa wa kimataifa, wanauliza kwa nini Watanzania wenyewe hawajitangazi na kueneza habari njema ya mafanikio yao zaidi. Jibu langu siku zote limekuwa kwamba kwa asili na hulka yetu Watanzania, hatupendi kujisifu. Na wao hunikumbusha kuwa dunia imebadilika, na itabadilika zaidi. Haitoshi tena kufanya jambo jema tu. Lazima pia watu na dunia wajue jema ulilolifanya. Ushindani uliopo na ujao unahitaji nchi kujitangaza na kutambulika zaidi. Dunia sasa imekuwa ya wawamba ngozi, ambapo kila mtu anavutia kwake. Siku hizi hata nchi zinajitangaza kama bidhaa, na hivyo hujipachika rajamu (brand), yaani alama ya biashara. Nasi Watanzania, muda umefika tutambulike kwa sababu au sifa fulani.

Ndugu Wananchi:
Tusifiche kasoro na mapungufu yetu, hasa miongoni mwetu wenyewe. Lakini tusionee haya, wala kupuuza mafanikio tuliyoyapata. Mwanga wa kitaifa umulike zaidi mafanikio, na tuyainue juu ili kila mwananchi ayaone, na watu wa nje nao wajue kuwa hii ni nchi ya watu makini walioamua kwa dhati kulinda heshima na utu wao kwa kutafuta maendeleo. Si heshima kujidharau mwenyewe, kujipuuza mwenyewe. Sifa ya nchi si sifa ya mtu, au sifa ya chama, au sifa ya Serikali. Ni sifa ya nchi. Vivyo hivyo aibu ya nchi si ya mtu, au chama, au Serikali. Ni aibu ya nchi na Watanzania wote. Kosoa kwa uadilifu panapostahili kukosolewa; na sifu kwa bidii zote panapostahili sifa. Nitatoa mifano michache.

Kwa kutumia misingi imara waliyotuachia waasisi wetu, tumeweza kujenga taasisi za kisiasa ambazo ni nyumbulifu na endelevu zinazoweza kuhimili matatizo ya aina mbalimbali. Kielelezo kimojawapo ni Mwafaka. Kasi ya kupatikana kwa ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa Zanzibar, hasa baada ya kuushughulikia sisi wenyewe, peke yetu, iliwashangaza wengi. Maana, barani Afrika, lakini pia hata katika baadhi ya nchi za wakubwa, ipo migogoro ya kisiasa ambayo imechukua miongo na miongo bila kupata muafaka ulio murua na endelevu kama wa kwetu. Sisi tumeweza, na pande zote mbili zinaonyesha ukomavu wa kisiasa wa kuheshimu Mwafaka na utekelezaji wake. Mwafaka wetu sasa ni mfano kwa wengine; na sitashangaa wakija wasomi kutoka mbali wakautafiti na kujipatia shahada za udaktari wa falsafa. Lakini ni kama vile sisi wenyewe hatuoni kuwa hilo ni jambo kubwa sana la kujivunia, na kuwa Mwafaka wetu ni kielelezo cha ukomavu, unyumbulifu, na uendelevu wa taasisi zetu za kisiasa.

Mfano wa pili wa kisiasa, ni kipindi cha mwezi mzima ambao nilikuwa nje ya nchi kwa matibabu. Mimi sijui ni nchi ngapi barani Afrika zingeweza kutulia kisiasa kama Watanzania walivyotulia katika kipindi chote hicho ambacho sikuwepo nchini. Ni sifa kwaWatanzania, lakini pia ni kielelezo cha ukomavu, unyumbulifu na uendelevu wa taasisi zetu za kisiasa na za dola. Tusione aibu kujisifu.

Kiuchumi hali kadhalika. Kwa vigezo vyovyote vile, Tanzania sasa imejijengea misingi imara ya uchumi, na hivyo kuufanya uchumi wetu uanze kuwa nyumbulifu na endelevu. Kama nilivyosema, tunao ukame msimu huu kwenye sehemu kubwa ya nchi yetu. Ingekuwa zamani tungekuwa tunahaha kweli kweli. Lakini leo ninaposema wananchi wasiwe na wasiwasi, nasema hivyo kwa kujiamini, maana tunayo akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, na tunayo mahusiano mazuri na nchi wahisani ambao tunashukuru wanaunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kinakuwepo chakula cha kutosha kwenye pembe zote za nchi yetu. Tusione aibu kujisifu.

Kwa upande wa kijamii nako tunayo mengi ya kujivunia na kutangaza. Umoja wa kitaifa, heshima kwa watu wote, mafanikio katika vita dhidi ya ubaguzi wa dini, madhehebu ya dini, rangi, na kabila, yote yanasifiwa duniani kote. Sisi tumeyazoea, tunayaona ni ya kawaida. Lakini si mambo ya kawaida barani Afrika. Tumefika mahali ambapo hakuna mwanasiasa makini atakayethubutu hadharani kueneza mambo ya udini au ukabila. Akifanya, ni kwa kujificha.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, tunayo mengi ya kujisifu na kujitangaza nayo. Tusidhani ni sifa kujidharau au kujibeza wenyewe. Busara ni kujijengea heshima kwa kuhakikisha mafanikio yako yanajulikana.

Hitimisho

Mheshimiwa Spika,
Hotuba imekuwa ndefu mno, lazima sasa niihitimishe. Tumepiga hatua kubwa. Katika Bunge hili wapo waliotoa mchango wao mkubwa sana katika mafanikio haya. Kwa niaba ya Watanzania wote nawashukuru na kuwapongeza sana. Ombi langu Tusirudi nyuma, wala kupunguza kasi. Tanzania hapa ilipo ni kama ndege iliyo kwenye njia ya kurukia. Inakwenda mbele, inaelekea mahali panapostahili, lakini bado ipo ardhini, haijanyanyuka na kupaa. Kwa ajili ya watoto wetu, na hatma ya taifa letu katika utandawazi, lazima sasa tupae. Uchumi wetu unahitaji nguvu mpya, msukumo mpya ili upae. Na nguvu hiyo na msukumo huo si mwingine ila uwekezaji mkubwa zaidi, utakaotoa nafasi nyingi zaidi za ajira, utakaotuwezesha kuuza nje kwa wingi zaidi, na utakaoimarisha uchumi wetu na kutoa fursa nyingi zaidi za kila raia aliye tayari ajiendeleze. Tuwe jasiri, na tuwe makini.

Ninayo miezi 20 ya kuongoza nchi yetu, Mwenyezi Mungu akipenda. Tusaidianeni ili niache uongozi Tanzania ikiwa inapaa, si ikiwa bado kwenye njia ya kurukia. Inawezekana.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

source: www.ccmtz.org