Tuesday 5 May 2009

Tume ya Mabomu: ongezeeni hadidu yangu!

Tuesday May 05, 2009
Serikali imeunda tume ya wataalamu kuchunguza na kubaini yaliyotokea ktk ile ajali ya mabomu ktk kambi ya jeshi kule Mbagala Kizuiani.

Hadidu rejea kwa baraza hilo ni:
1. kuchunguza na kubaini chanzo, madhara, hasara
2. kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuzuia tukio kama hilo lisitokee tena.
3. kupendekeza hatua za ziada zitakazochukuliwa ili kuepusha tukio kama hilo lisitokee katika maghala mengine.

Kwa maoni yangu naona serikali ingeongeza hadidu moja nyeti. Tukio kama hili linapotokea ni nini kifanyike - kwa vile ajali haina kinga!

Nimesikitika kusoma ktk vyombo vya habari kuwa wananchi walikimbia huku na kule wasijue nini cha kufanya na hatima yake wakajitosa majini (mtoni) ambapo baadhi yao walipoteza maisha yao. Wanafunzi wa shule za msingi na watoto wadogo walitawaniyika na kutokomea kusikojulikana! Watu wazima wengine walikimbia kutafuta hifadhi maeneo ya mbali kama vile Buza!

Kwa hiyo kinachotakiwa ni kuweka utaratibu au mpango (kwa lugha ya kigeni wanaita plan) inapotokea hatari au dharura ya namna hii watu wafanye nini. Serikali kupitia taasisi au chombo husika kitoe elimu na mafunzo kwa wananchi ili kuondoa uwezekano wa raia kupoteza maisha kwa hofu tu (mfano kujitosa mtoni). Kwa hiyo nashauri mafunzo yatolewe kwa wananchi namna ya kujiweka ktk hali ya usalama (health and safety) pindi ajali za namna hii zinapotoea au hata ajali ya moto. Wakishapewa elimu na mafunzo, ni vizuri pia kuwa kila baada ya kipindi fulani, mathalani miaka 3, wawe wanapigwa msasa na kufanya majaribio (drills) ili kujiweka ktk utayari kukabiliana na maafa. Hii ni muhimu sana hasa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kambi za majeshi yetu ya ulinzi na usalama.

Wananchi waelemishwe pia jinsi ya kutoroka (how to escape) moto unapotokea majumbani au maeneo ya kazini na maeneo ya kukusanyika yaeleweke (assembly point) ili watu waweze kujuana ni nani ametoka ndani na ni nani amebakia ndani ya nyumba au jengo. Hii staili ya kuondoka baruti kila mtu kivyake sio nzuri, kwa sababu ni vigumu (hasa kwa zimamoto) kujua kama wanaokoa maisha ya watu (rescue) ktk jengo ama ni jengo tupu linawaka! Hii ni muhimu sana -hasa kwa usalama wa wazima moto. Kama hakuna mtu ndani ya jengo wana-zimamoto hawatakuwa na haja ya kuhatarisha maisha yao kuingia ndani ya jengo kutafuta watu 'walionaswa' ndani ya moto. Lakini huyu zimamoto atajuaje kama ndani ya jengo au nyumba inayoungua kuna mtu au watu kama kila mtu alitoka na kutokomea kusikojulikana? Hii ilitokea katikati ya jiji baada ya mlipuko wa mabomu, wafanyakazi walijitokea kiennyeji na kwenda wanakotaka wenyewe (nadhani hakuna walioitisha majina ya wafanyakazi waliotoka ndani ya jengo (roll-call)). Kwa hiyo kama maofisi yangeporomoka ingekuwaje, wakati wengine wako wanakojua wenyewe?

Ndio maana nasema hii tume itoe mapendekezo ya ni nini cha kufanya kwa wahanga endapo tukio kama hili au la moto mkubwa litatokea tena? Hatuwezi kusema kwa uhakika kuwa tukio kama hili au la aina hiyo haliwezi kutokea tena kwa sababu hii ni ajali (ni nani ajuaye ajali itatokea lini!). Kwa hiyo tujiandae na kisichotarajiwa. Na je kitakapotokea kisichotarajiwa wananchi tufanyeje?

Mimi naamini jibu sio kutokomea mitini!

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Ni vilio tu!

Wakati hadi sasa taarifa rasmi juu ya idadi kamili ya watu waliopoteza maisha katika mlipuko wa mabomu uliotokea wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam ni 23, baadhi ya wananchi wa maeneo ya Mbagala, wanadai kuwa idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi na kwamba miili yao huenda imekwama kwenye tope la mto Kizinga.

Kadhalika madiwani wa kata za Mbagala na Mbagala Kuu wameonyesha wasiwasi wao wakidai kuwa, wana hofu kwamba watu kadhaa wakiwemo watoto ambao walitoweka tangu siku ya tukio hilo la mlipuko, wakawa wamefia kwenye mto huo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleimani Kova amesema hadi sasa jumla ya watoto 19 wakazi wa Mbagala, tangu siku ulipotokea mlipuko huo, hawajulikani waliko.

Kufuatia hofu hiyo, jana Baraza la Madiwani la Manispaa ya Temeke liliitisha kikao cha dharura kujadili hali hiyo.

Katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, ambapo ndipo lilipotokea tukio hilo, Bw. Anderson Charles alisema kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo watoto wengi waliozama ndani ya mto Kizinga na kuwa miili yao imekwama kwenye tope la mto huo.

Akasema kasi ya uokoaji inayoendelea kufanywa na wananchi kwa kushirikiana na Polisi ni ndogo, hivyo akaomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, kufanya operesheni maalum kusaka miili ya watoto hao na kuiopoa mtoni.

Hoja ya Bw. Charles iliungwa mkono na Diwani wa Kata ya Mbagala, Bw. Peter Osoro aliyesema kuwa baada ya milipuko, watoto wengi walikimbia na kuingia mtoni, wakiwa na nia ya kuvuka mto Kizinga kwenda ng\'ambo maeneo ya Yombo.

Kwa mujibu wa diwani huyo, watoto wengi walizama mtoni katika maeneo ya Kingugi na Bugudadi mahali ambapo wengi wao walitaka kuvuka wakidhani maji ya mto ni machache, lakini wakajikuta wakizama kwenye tope na kupoteza maisha.

Aidha Bw. Osoro akasema kuwa hadi sasa kuna familia nyingi zinahaha kutafuta ndugu, jamaa pamoja na watoto wao, na hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kupeleka kikosi cha JWTZ kufanya operesheni maalum.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Bw. Steven Kongwa aliwahakikishia madiwani hao ambao wengi wao walikuwa wakibubujikwa machozi kuwa, juhudi kubwa za kuwasaidia wahanga wa tukio hilo zinaendelea na hivyo akawataka waheshimiwa madiwani wasiwe na huzuni sana.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Jerome Bwanausi, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maafa hayo, alisema kamati yake iko imara na wahanga wote wanapewa misaada.

Akasema mazishi ya maiti zote za ajali hiyo yamegharimiwa na kamati ya maafa ya mkoa wa Dares Salaam ambayo iko chini ya Mkuu wa Mkoa, Bw. William Lukuvi.

Madiwani hao walimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutembelea majeruhi na wahanga wa tukio hilo.

Aidha waliwashukuru watu wote waliotoa misaada ya hali na mali kusaidia wahanga wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema kuwa watoto 19 ambao hawajulikani waliko wanahisiwa kuwa wamekimbilia maeneo mbalimbali na wengine wamehifadhiwa majumbani na wasamaria wema.

Ametoa wito kwa watu wanaowahifadhi watoto wasio wao majumbani au wale wanaojua walipo, watoe taarifa ili juhudi za kuwakutanisha na wazazi wao ziweze kufanyika.

``Kuna watoto wamekimbilia maeneo ya mbali, wapo waliofika hadi Arusha, lakini pia kuna wengine wamehifadhiwa na wasamaria wema, nawaomba wote wajitokeze kutoa taarifa zao ili tuwakutanishe na wazazi wao,`` akasema Kamanda Kova.

Ameonya kuwa miongoni mwa watoto hao wamo watoto wa kike na wanafunzi, hivyo kutotoa taarifa zao inaweza kuleta hisia mbaya baadaye na ikawa shida.


SOURCE: Alasiri, 2009-05-05 20:55:02
Na Emmanuel Lengwa na Moshi Lusonzo