Thursday 21 May 2009

Ushauri mnyenyekevu

Alhamis, 21/05/2009
Juma hili nilitembelea ubalozi wetu pale Stratford Place, jijini London. Nilifurahi kuona nyumbani kwetu 'mbali na nyumbani', maana pale ndio kimbilio; kwa mema au mabaya! Pale ndio baba, ndio mama, ndio mjomba na ndio kila kitu.

Nilifurahi pia kuona wafanyakazi wakarimu na wachapakazi.

Kwa vile pale ni nyumbani, sio vibaya kutoa maoni au ushauri wa kinyenyekevu (polite advice).

1. Nje: Ngazi za kuingia kwenye basement (eneo la hati za kusafiria) pamoja na eneo chini ya ngazi hizo za chuma panahitaji matengenezo au matunzo mazuri zaidi (TLC). Pale chini ya ngazi sio pasafi na panaonekana kama ni 'ka-stoo' ka kienyeji. Nashauri makorokoro yote pale chini yaondolewe na ukarabati mdogo ufanike na pia kupiga rangi kidogo ili papendeze. Marumaru sakafuni nazo zitupiwe macho ili ikiwezekana zishughulikiwe. Lile eneo la ngazi na 'landing yake' ni muhimu sana kwa kutangaza sura (image) ya nchi yetu. Ndio maana nashauri lifanyiwe kazi ili kuliinua kimuonekano. Zile railings za nje nazo zipigwe 'soap-soap' kidogo!
Pale mahala (ubalozini) pako karibu kabisa na mtaa ulio-bize wa Oxford na pia kituo cha treni za ardhini (Bond Street) kiko pale mlangoni kabisa!

2. Mlangoni: Mlango wetu pale 'basement' sio wa kiwango kinachostahili (hadhi ya ubalozi). Nilipokuwa nabisha hodi na kuingia ndani, vipeperushi vilidondoka kwa ndani. Kumbe vilikuwa vinaning'inia kati ya upenyo wa mlango na fremu yake. Hii inaonyesha kuwa kuna watu ambao hutembeza na kudondosha vipeperushi vya biashara ktk milango ya nyumba (note: ni kawaida kwa Uingereza kitu kama hicho)! Ila mimi nadhani ubalozi wetu hauwezi kuwaruhusu wachuuzi wa mitaani kudondosha 'vikaratasi' au vipeperushi vya kibiashara/matangazo ndani ya ofisi ya ubalozi wa nchi. Wote tunaelewa mahala pale ni nyeti. Kwa hiyo tuwe makini na hilo.

3. Ndani: Nitaongelea 'interior design'. Kuna kuta nyingi mno zisizo na sababu. Mfano ukuta kati ya meza za maulizo na pale wateja husimama. Nashauri ule ukuta na kidirisha chake viondolewe kabisa, na badala yake iwekwe meza iliyonyanyuka kama mita 1.2 kutoka usawa wa sakafu na wafanyakazi watumie viti virefu au wasimame. Pia ukuta kati ya kile chumba cha mapumziko na meza ya maulizo uondolewe. Kwa kuafanya hivyo eneo litaonekana kubwa na kutakuwa na mwanga wa kutosha pale ndani. Kwa sasa mtu akiingia panaonekana pafinyu sana na mwanga sio mzuri kwa standard ya ofisi. Na panaonekana pamejengwa kwa 'scale' ya nyumba ya kuishi (residential) na sio public space!

4. Ndani. Matangazo na 'Info': Pale maulizo pawekewe tray ya vipeperushi vya huduma mbalimbali zinazopatikana hapo ofisini. Hii itasaidia kuondoa utata wa maelezo ya wafanyakazi. Mfano mfanyakazi mmoja anaweza kukupa maelezo fulani (Facts) na mwingine akakupa ukweli mwingine! Naelewa hii inaweza kutokea kwa bahati mbaya, lakini kama kuna vipeperushi, ni rahisi kwa mfanyakazi kumpa mtu kipeperushi kwa ajili ya rejea anapokuwa na shida wakati wowote. Na pia tukumbuke kuwa sio kila mteja wenu anaewatembelea anapata huduma ya mtandao (internet). Kwa hiyo tusiwalazimeishe wateja wetu kwenda kusoma website kwani hiyo sio njia pekee ya kupata habari za ubalozi wetu.

Mwisho ninawapongeza wafanyakazi wote pale ubalozini kwa kazi nzuri wanayoifanya. Wanao ushirikiano wa hali ya juu na watanzania walioko nje ya nchi, na hiki ndicho kitu muhimu zaidi. Pia wanajitahidi kwa uwezo wao wote kuitangaza nchi yetu kwa nafasi walioyo nayo. Inawezekana kuwa moja ya matatizo makubwa yanayowakabili ni ufinyu wa bajeti, kwa hiyo tusiwe wepesi kuwarushia makombora ya lawama. Na wanaweza kuwa wanafanya kazi ktk mazingira magumu. Kwa ujumla kazi yao inaridhisha kwa kiwango kizuri. Hongera pia balozi wetu Mama Maajar, wewe ni shujaa na tunakupenda!

No comments: