Tuesday 26 May 2009

Maisha Uingereza -1

May 26, 2009
Nimeishi ugenini UK kwa muda mfupi kidogo. Kwa maana hiyo siwezi kujiita mwenyeji au 'al-watan'! Hata hivyo, ktk muda huo mfupi ni mengi nimeyaona; mazuri, ya kawaida na mengine yasiyo ya kuvutia! Leo, nimeamua kujipa zoezi (au 'assignment' kwa lugha ya kigeni) - kutoa tathimini ya maisha ya UK kutokana na uzoefu wangu wa muda mfupi wa kuishi hapa.

Hawa wenzetu huku Uingereza wanajali sana muda. Ndio maana huko nyumbani tumezoea kusikia msemo maarufu 'time is money'. Lakini maana halisi ya msemo huo utaiona huku. Mambo yao yote yako kwa ratiba ya muda (siku, saa hata dakika). Kazini wanaingia kwa kuweka sahihi (signing in) na mtu akitoka nje mapumziko au kwa shughuli zisizo za kikati anasaini kutoka ktk mtambo mdogo wa kunakili muda wa kila mfanyakazi (wao wanaita clocking in and out). Kwa hiyo mwisho wa wiki au mwezi masaa yako huhesabiwa na kompyuta na kulipwa masaa ambayo umefanya kazi 'kikweli kweli'. ule utaratibu wetu Afrika wa kuripoti kazini kisha kutoweka hapa haupo. Na ukiwa mtorokaji au mkwepaji kibarua chako kitaota majani haraka sana maana uthibitisho upo kitaalamu kuwa tija yako ni ndogo na ni hasara kwa kampuni au mwajiri wako.
Karibu kila mtu ana kitabu cha mambo yake (diary) ambapo hurekodi kumbukumbu zake zote ikiwa ni pamoja na masaa na siku za shifti zake. Muda wa kuanza kazi sharti uwepo kazini na muda wa kutoka tu ukifika mtu unafunga vilivyo vyako na kuondoka, na kila mmoja na njia yake! Sio kawaida mtu kudandia lifti huku, kama hauna usafiri wako itabidi upitie kituo cha basi au treni kwa ajili ya kurejea kwako. Ama kama ni karibu utaswaga mguu (sio aibu ni jambo la kawaida huku).

Zipo kazi mbalimbali huku. Lakini watu wengi kule nyumbani TZ wanaelewa moja tu -ya 'kubeba box'. Hii moja ya kazi ambazo kwa UK hujulikana kama Industrial (Pick&Packing). Pamoja na watu huko nyumbani kuiona kama kazi rahisi lakini inahitaji mafunzo ya awali ktk kuifanya, na inabidi mtu apitie kozi ndogondogo ili aweze kuruhusiwa kuifanya. Baadhi ya kozi ni za 'first aid', 'manual handling', 'Control of substances hazardous to health (COSHH)', 'fire fighting' n.k. Nguvu na akili yako huhitajika pia.
Kazi zingine ambazo watu hujihusisha ni za kijamii, kwa mfano kulea watoto au watu wazima (wazee au wale wenye matatizo ya kitabia yaani challenging behaviour). Hizi za wazee sana kiumri hujulikana kama Nursing. Ktk 'Nursing' mtu huajiriwa kufanya kazi kwenye 'nursing homes' ambapo wazee (vikongwe) husaidiwa ktk mahitaji yao ya kila siku (mfano kupikiwa na kulishwa chakula, kuogeshwa, kuvalishwa, kunyanyuliwa kitandani au kitini n.k.). Inabidi upate mafunzo kama yale ya industrial na ya nyongeza kama food hygiene.
Ktk kulea watoto, watu huajiriwa ktk shule za watoto watukutu ili kusaidia kuwaangalia na kuwatuliza. Zipo kazi zingine za kijamii za kuwaangalia watu wenye akili taahira na mtindio wa ubongo ktk 'Residential Care homes'. Utasikia watu wanaziita kazi za 'care'. Kundi hili ni la watu wa rika zote. Zipo kozi zake pia (hizo nilizotaja hapo juu nazo ni lazima uzifanye. Kozi za care ni pamoja na NVQ level 1-3 kwa kutegemea majukumu mtu aliyoajiriwa nayo au atakayopewa kama 'promotion' kazini). Kazi za care huhusiana na kuwaangalia, kusaidia kuwapatia huduma mbalimbali za kimahitaji ya kila siku na pia kuwapatia dawa za matibabu walizoandikiwa na daktari. Kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi zozote za kijamii ni lazima ufanyiwe uchunguzi wa kipolisi kuona kama una kosa lolote la jinai. Watu waliohukumiwa kwa makosa fulani ya jinai hawaruhusiwi kuchanganyikana na makundi ya watu wanaohitaji kusaidiwa kwa mfano wazee vikongwe, watoto wadogo na wenye ulemavu wa taahira ya akili na mtindio wa ubongo (vulnerable people).

Zipo pia kazi za kufanya usafi ktk mahoteli na maofisi (cleaning). Hizi hufanyika zaidi nyakati za jioni au alfajiri sana ama siku za mwisho wa juma (pale ofisi zinapokuwa wazi). Pia watu hupelekwa kufanya usafi maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu mfano kwenye viwanja vya michezo (mpira wa miguu, ragbi, mbio za farasi, kumbi za starehe n.k.).

Kazi zingine zinahusu usimamizi wa watazamaji (crowd safety/control) ktk matukio mbalimbali (events organizing). Kwa mfano siku za mashindano ya farasi, siku za mechi za mpira wa miguu (premier league, championship au mechi Euro uwanja wa Wembley). Hii ni mifano michache ya matukio ambayo watu huchukuliwa kusaidia -watu hawa wanaitwa 'stewards'. Polisi hukaa pembeni, wakisubiri kama kuna matukio yanayoweza kuwahitaji wao kuingilia.

Kwa ufupi, hizi ndizo baadhi ya kazi ambazo watu waendao UK hufanya ili kuweza kujikimu mahitaji yao mbalimbali. Kusema kweli kazi hizi hufanywa zaidi na wale tunaotoka nje ya UK; kama vile Afrika, Asia, Amerika ya Kusini, visiwa vya karibean n.k. Kwa wazawa wa UK wengi wao hawapendi kuzifanya kazi hizi na kama wapo wanaozifanya ni wale ambao hawakwenda shule au hawana elimu ya sekondari; kwani kwa wazawa wa hapa UK elimu ya sekondari inatosha kabisa kumpa mtu kazi nzuri.

Chai na sukari. Usije kushangaa mtu anakukaribisha chai na kukuliza 'how many sugar?'. Watu hunywa chai kwa kutumia sukari zilizo katika vipakiti vidogovidogo sawa na kijiko kimoja cha cha chai. Na wengi hutumia kipakiti kimoja au kijiko kimoja cha chai. Wengine hutumia viwili au hawatumii kabisa sukari. Wanakunywa chai kavu (bila sukari na maziwa kidogo sana!). Sisi tuliotoka Afrika mara nyingi hutumia vitatu au vinne! wazungu hushangaa sana wanaposikia tunasema 3 au 4 sugars!!! Kwa hiyo ukisikia unaulizwa 'how many sugars' ujue wanakuuliza unatumia vijiko (au vipakiti)vingapi vya sukari.

Hawa jamaa (wazungu) hawana cha siri. Uki'muuma mtu sikio' uelewe kabisa hiyo sio siri - itaanikwa hadharani muda wowote! Ndivyo walivyo, hawana kitu cha siri! Wanapenda sana kufuga wanyama wadogo (mbwa, paka, ndege n.k.) kama mapambo. Na wengine huwaita hao wanyama kama wenzi wao (companion).

Kwa tuliotoka Afrika kwenye maeneo ya joto, mbu na nzi ni wadudu wa kawaida. Pia magonjwa yatokanayo na wadudu hao ni ya kawaida - malaria, kipindupindu kuhara n.k. Kwa kweli hali ya hewa ya ubaridi huku UK hairuhusu wadudu hao kuishi ama kuzaliana. Kuna wakati huwa naona nzi wale wa kijani mara moja moja, na mbu husikika pia kwa mbali lakini sio mara kwa mara. Cha muhimu ni kuwa hakuna madhara yoyote yanayoletwa na kelele zao. Sijawahi kuona neti madukani wala ktk miji ya watu, hiki ni kiashirio kuwa hakuna tishio la malaria. Pia watu wa huku huwa hawazingatii sana usafi wa kunawa mikono (achilia mbali kunawa kwa sabuni!). Watu wanaweza kuwa wako kazini bize lakini wakati wa mapumziko wananunua mkate (sandwich) na kushika na mikono michafu na wakati mawingine mtu anaweka chini kipande cha mkate halafu anaendelea kula baadae! Kipindupindu na magonjwa mengine ya tumbo hayapo huku.

Baadhi ya vijana wadogo wa huku (miaka kati ta 16 hadi 30 hivi) wana tabia mbaya ya kugombana na kuchomana visu. Wengi wao wako ktk magenge na kila genge huwa na uongozi wao na eneo wanalotawala. ikitokea kundi moja (genge) likaingia himaya ya wengine fujo hutokea na aghalabu matokeo ya fujo hizo ni kuuana. miji mikubwa kama London na Manchester hali ni mbaya mno!

Kwa upande mwingine UK kuna hali ya ustaarabu au maendeleo ya namna fulani tofauti na nyumbani. Kwetu Afrika, nyumba au ofisi huwa hazijakamilika bila kuwa na mageti ya chuma milangoni na madirisha ya nondo. Kwa UK mambo sio hivyo. Milango ya nyumba, ofisi hata mabenki huwa ni ya vioo na hata madirisha ni ya vioo - hakuna vibaka wa kuvunja na kuingia kuiba,na kama matukio hayo yapo ni kwa asilimi ndogo sana. Hata magari hulazwa nje, tena barabarani kila siku - hakuna tatizo.

Shrika la Posta chini ya 'Royal Mail' wana utaratibu wa kusambaza barua au vifurushi vya wateja kwa kuwapeleakea ktk makazi yao. Ndio maana anuani za UK huwa zina jina la mpokeaji barua/kifurushi, namba ya nyumba anayoishi, mtaa na post code (mfano RG2 7HT, SL5 0TP, W7 3CX n.k.). Lakini ni lazima niseme kuwa kuna baadhi ya matatizo yanayojitokeza ktk nyumba za kuchangia. Barua zikishaletwa na watumishi wa Royal Mail, hupitishwa ktk kitundu kidogo kilichoko ktk mlango wa mbele. Mara nyingi ktk nyumba za kuchangia sio wakazi wote wa nyumba huwa wapo nyumbani wakati wote, na kwa hiyo barua hukusanywa toka pale chini ya mlango na yeyote aliyepo nyumbani kwa wakati huo. Baadhi yetu uaminifu wetu ni mdogo na inatokea mara kwa mara barua hupotea kwa mazingira ya kutatanisha! Hapa tatizo linakuwa ni mtu kufungua na kusoma barua isiyomhusu na kuitupa. Hii hutokea kwa barua zenye statement ya akaunti za benki au bank/credit cards, risiti ya malipo kazini (pay slip), n.k. Sijui ni kwa nini watu wengine hupenda kufungua barua ama nyaraka za siri za mambo yasiyowahusu! Ubongo na uafrika wetu haupotei hata kama mtu anaishi Ulaya!! Kwa hili inabidi tubadilike kifikra na kiupeo, maana wengi wa wanaoishi hapa toka nje ya Ulaya (mfano Afrika) ni wasomi tena wa kiwango cha elimu ya juu.

Wazawa wa UK wanapenda sana michezo na utamaduni. Michezo ipo mingi sana. Na michezo yenye ushabiki wa kiwango kikubwa ni kama mpira wa miguu, mpira wa ragbi, tennis, mchezo wa kriketi, mbio za magari, pikipiki, farasi na mbwa. Ktk michezo hii watu hupenda kucheza kamari za kubashiri matokeo ktk michezo mbalimbali.

Ktk uwanja wa habari ndugu zetu hawa hawako nyuma. Kuna vituo vingi sana vya televisheni na redio. Ktk tv kuna stesheni za bure na za kulipia (za kulipia ni nyingi zaidi na hurushwa kwa kupitia satellite na cable). TV za bure huruhwa kwa njia ya kawaida (terrestrial). Mtu yeyote mwenye tv anaweza kupokea matangazo ya bure ya tv ktk mtindo wa 'analogy' au pia mtu anaweza kuyapata kupitia box (freeview box) ambalo hupokea matangazo ya tv na redio ktk hali ya 'digital'. Free view box in stesheni (channels) zaidi ya 50. Stesheni za bure ktk tv ni kama ifuatavyo: BBC One, BBC Two, ITV, Channel 4 na Channel 5. Hata hivyo hakuna cha bure ktk kuangalia tv. Mtu yeyote anayetumia TV ya rangi au 'black and white', DVD player/recorder, Video player/recorder n.k. ni lazima alipe leseni ya TV (TV Licence) kwa BBC ambayo ni Paundi za Uingereza 145 (GBP 145) kwa mwaka, pia inaweza kulipwa kwa awamu kulingna na uwezo wa mtumiaji. Hii hela ndiyo inayotumiwa na BBC kuendesha shughuli zake pamoja na mishahara ya wafanyakazi wake. Na ndio maana Stesheni zote za BBC (radio na TV) huwa hazina matangazo ya biashara. Mapato ya BBC ni kupitia karo (fee) ya leseni ya TV ambayo hulipwa na kila familia UK.

No comments: