Tuesday, 19 May 2009

Tumege uzoefu wa wazee wetu

19/05/20009
Ni rahisi kusikia mashirika yanaanzishwa kusaidia kina mama fulani -wajane kwa mfano, au walioachika au waliokatiza masomo yao n.k. Pia yapo ya kusaidiwa watoto ambao mara nyingi wanatokana na matatizo yaliyowapata kinamama hapo juu.

Nadhani wakati umefika kuwakumbuka watu wazima hasa wastaafu ambao wameamua kupumzika kwa sababu za kiafya au kisheria (umri wa kustaafu).

Wazee wetu hawa wanapoacha kazi, mara nyingi huwa wanabaki kuwa wapweke sana. Walizoea kutoka kila asubuhi na kurudi nyumbani jioni au usiku lakini inapotokea siku ya siku imefika na wakastaafu mabadiliko haya ya ghafla huwagharimu sana kifikra.

Ni vema ndugu zetu hawa nao wakakumbukwa hasa ktk namna ya kuwafanya waendane na hali halisi ya mabadiliko ya kimajukumu. Hapo nazungumzia afya ya akili.

Ushauri wangu ni kwamba serikali za mitaa zikisaidiana na asasi mbalimbali waanzishe vyombo (facilities) vya kusaidia kuwajumuisha watu wa kundi hili ili wajione wako ndani ya jamii. Wastaafu walio wengi kwa kweli hujiona kama ndio umuhimu wao ktk jamii umefikia ukingoni. Ni jukumu la kila mwanajamii kuhakikisha wakubwa zetu au wazazi wetu hawa wanaonekana kama wenzetu na kuwa mchango wao ktk jamii bado unahitajika, tena zaidi.

Ebu tuangalie namna ambayo tutachuma uzoefu wao kimaisha ili utusaidie ktk maendeleo yetu kwa ujumla. Tusiwaachie maarifa yao wakae nayo peke yao. Kundi hili ni muhimu sana ktk jamii na lina mengi ya kutusaidia. Kwa hiyo tusilale, tuwahusishe ktk mambo yote ili nasi tuupate uzoefu na utajiri wa fikra zao njema. Kwa kufanya hivi tutakuwa tunawasaidia kuwaweka 'fit' kiafya (mwili na akili) na bila shaka watafaidi maisha na kurefusha maisha yao pia.

Lakini yote haya tutayapataje ikiwa kila mstaafu yuko nyumbani kwake na familia yake? Mimi nasema, tunahitaji vituo vya kutukutanisha wote ili waweze kutoa mchango wao chanya. Serikali za mitaa na asasi za binafsi zina nafasi kufanya kitu cha maana hapa.

Hivyo ndivyo nionavyo mimi kwa ufupi tu.

No comments: