Tuesday, 26 May 2009

Maisha Uingereza -2

26/05/2009
Utamaduni wa wenzetu ni tofauti na wa kwetu Afrika. Nyumbani tumezoea kusalimiana kila tunapokutana hata kama mtu hamfahamiani. Huku sio hivyo. Ukifika, kwa mfano, kituo cha basi au hospitali unakuta watu kimya kila mmoja na lake. Wengine wanacheza game na simu zao, wenye vitabu wako bize wanasoma au mtu na mwenzi wake wanabusiana hapo n.k. Hakuna cha jambo wala nini. Muda ukifika wa kupata kilichokupeleka hapo unafanya na kupotea!
Na ule utamaduni wetu wa kumwita mtu dada, shangazi, kaka, mzee n.k. haupo hapa. Ukimwita mtu kaka -atashangaa anaweza kukwambia mimi sio kaka yako au sio ndugu yako. Kama mtu unamfahamu unatakiwa kumwita jina lake la kwanza hata kama ana umri sawa na babu yako. Hakuna cha Mr. fulani, au Mrs. fulani. Hapo ndipo pagumu maana unaona kama utamdhalilisha kumwita kwa jina! Mtoto wa miaka 4 anamwita mtu wa miaka kama 50 kwa jina mfano Peter, Sarah n.k. Mtoto atamwita mama yake tu kama 'mama' lakini sio kwa watu wenye umri wa mama yake!
Ule utamaduni wetu wa kuwapenda na kuwajali watoto njiani huku ni mwiko! Usije jaribu kumsaidia kitu mtoto njiani hata kama anahitaji msaada. Hilo ni kosa kubwa mno kwa huku. Ukimshika mtoto tu ni kosa na tena unaweza kushitakiwa na kufungwa kwa kumdhalilisha mtoto. Kwa hiyo kaa mbali na watoto wa watu wengine. Kama ni mwanao sawa, lakini hakuna cha kusema huyu ni mtoto wa jirani.
Hakuna utamaduni wa kuazimana magazeti ndani ya basi, kama tufanyavyo nyumbani kwa kugawana kurasa za gazeti! Kama kitu si chako itabidi uangalie kijanja sio shingo feni!
Ila wana kautamaduni poa sana ka ustaarabu wa kupanga foleni kila panapotakiwa. Mfano kupanda basi au treni, au wakati wa kushuka watu hufuata utaratibu wa foleni tena kwa taratibu bila kusukumana. Wakati wa kulipia huduma dukani au huduma za benki n.k. wateja hujipanga foleni kwa kuzingatia aliyekuwa wa kwanza kufika eneo husika. Na kama wote mmefika kwa wakati mmoja haina tatizo watu hupeana nafasi ili kujipanga. Hapo ni raha sana na huu ustaarabu inabidi tujifunze na sisi huko nyumbani. Nadhani wanapokuja kutalii huko nyumbani huwa wanatushangaa tunavyombania kuingia ktk usafiri hasa wa daladala, mpaka wengine hupitia dirishani!

No comments: