Thursday 19 June 2008

'Wakurya': awaonavyo Jenerali

Nimepitia haraka haraka makala ya 'Rai ya Jenerali Ulimwengu' ktk gazeti la Raia Mwema wiki hii Juni 18-24, nikaona habari kuhusiana na wakurya. Alichokisema Jenerali ni kweli.
Ila ni lazima niseme kuwa mara nyingi kusema ukweli kunatuacha ktk mazingira magumu ya kuchukiwa ktk jamii.
Wapo watu ktk jamii wenye kupenda sifa, kazi yao ni kurembaremba maneno kwa kuyafanya matamu (bila kuelezea hali halisi ilivyo) ili wasionekane wabaya.
Unapokuwa mpenda 'haki na ukweli' si ajabu kuona unachukiwa na wapenda njia za mkato; lakini ipo siku moja jamii itaelewa na kuthamini mchango wako, kwani penye ukweli uongo hujitenga!
............................
............................
(nukuu kutoka Raia Mwema 18-24 June, 2008)
'Ni muhimu, basi, kuwathamini wale wachache wanaodiriki kutoa maoni yao, wawe ndani ya utawala au nje, kwa sababu hawa ni watu adimu katika jamii yetu. Zamani kidogo niliwahi kuandika kwamba sote tunahitaji kuwa "Wakurya" kwa kiasi fulani, kwa maana ya kuambizana ukweli hata kama haupendezi. Hadi sasa "Wakurya" tulio nao bado hawatoshi. Tuwathamini hao wachache waliopo ...'

3 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Kilango: Siogopi 'NEC'
LICHA ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kuwataka wanachama wake kusubiri matokeo ya Tume ya Rais kuhusu uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za EPA, Mbunge wa Same Mashariki, Bibi Anne Kilango Malecela (CCM), amewasha moto bungeni na kuizungumzia akisema haogopi chochote.

Akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2008/9 bungeni jana, Bibi Kilango alisema:

- fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zisiporudishwa bungeni hapatatosha na hataogopa vitisho kwa suala hilo.

- aliitaka Serikali kueleza kuhusiana na waliokopa sh. bilioni 216 mwaka 1992 kama zilirudi kutokana na kuchukuliwa na alichokiita kikundi fulani cha watu wachache katika jamii.

- aliwataka wabunge wote kuungana na wasiogope vitisho, kwani wakisimama imara kutetea haki, Mungu naye atakuwa upande wao na watashinda.

Pia Mbunge wa Kishapu, Bw. Fred Mpendazoe (CCM), aliitaka Serikali ieleze ni nani wanaorudisha fedha za EPA na iwe wazi kuhusu ufisadi na ieleze mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe, kuhusiana na suala la kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Bibi Kilango alisema hakuna ulinzi katika fedha za umma na kwamba Serikali imeachia mwanya.

Kabla ya kuanza kushusha 'nondo' zake, Mbunge huyo, alitoa nukuu ya Mwanafalsafa wa Kigiriki aitwaye Socrates na kusema kama ilivyo falsafa hiyo naye atakuwa hivyo.

Alisema mwanafalsafa huyo alikwenda sokoni Ugiriki kwenye mkutano wa hadhara, akasema kitu ambacho alikuwa
akikiamini.

"Naomba ninukuu: Faithfulness to a cause is the most important thing in life, all great people have been considered great, because they died for a cause (Watu wengi maarufu duniani huwa tayari kufa kwa ajili ya kile wanachokiamini)," alisema Mbunge huyo na kusisitiza kuwa naye haogopi vitisho kwa kile anachokiamini na kusababisha ukumbi mzima kuwa makini kumsikiliza.

Mbunge huyo alisema kutokana na ulinzi wa fedha za umma kutokuwa mzuri, watu waliingia na kuchota fedha za EPA na kwamba kama umakini usipokuwapo, kila mwaka bajeti itakuwa sungura na haitatosha.

"Nazungumza bila kificho, fedha za EPA zisiporudishwa, hapa hapatatosha, Wabunge hawatakubali," alisema na kuzungumzia pia kuhusiana na sh. bilioni 216 alizosema zilitolewa kama mkopo na Serikali mwaka 1992 na hazijarudishwa zipo mikononi mwa wananchi wachache.

"Waziri atueleze fedha hizo zitarudi lini? Atuambie, zisiporudi hapatoshi, tabia ya kuacha kikundi kidogo kimiliki fedha ina athari," alisema na kuzitaja kuwa ni Taifa kukosa fedha za kutosha na pia amani ya Taifa kumong'onyolewa taratibu.

Pia alisema hakuna ulinzi mzuri kwenye madini na kwamba katika utalii pia hakuko sawa, ingawa kuna fedha zimelala, lakini watu wanaachwa wafanye wanavyotaka katika madini ya almasi na tanzanite.

"Wabunge tusiogope vitisho, tusimame imara, tutashinda Mungu atakuwa nasi ... tutapambana pesa zetu zirudi, tunataka tuthibitishiwe bungeni kuwa zimerudi si tuambiwe kwenye karatasi.

"Ukiona fedha za wananchi zinahodhiwa na kikundi kidogo, halafu wabunge mpo, ni bora msije," alisema Bibi Kilango na baada ya kumaliza kuchangia hoja yake, Spika wa Bunge Bw. Samuel Sitta, naye alichomekea kwa kusema: " Uzuri wa Spika mliyenaye haogopi vitisho," alisema na kusababisha kicheko kwa wabunge na baadhi ya watu waliokuwa wakifuatilia mjadala huo.

Naye Bw. Mpendazoe alisema suala la ufisadi lazima Serikali iliweke bayana, vinginevyo litaleta matatizo na kwamba ni vyema ikaelezwa hizo fedha za EPA nani wanarudisha, pia ieleze kuhusiana na mapendekezo ya Kamati ya Dkt. Mwakyembe kuhusu mambo ya Richmond.

"Unaweza kudanganya watu fulani kwa kipindi fulani, lakini huwezi kudanganya watu wote kwa muda wote," alisema Bw. Mpendazoe akinukuu baadhi ya falsafa za watu mbalimbali.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Stella Manyanya (CCM), alisema hawataacha kuuliza kama fedha za umma zitatumika vibaya.

Pia alisema kuna gazeti moja, lilijaribu kuandika kuhusiana na mambo ya Richmond na kusema kuwa asingependa kujibu kwa jana kwa kuwa Serikali bado inalifanyia kazi, lakini alisema majibu bado wanayo na wakati ukifika watajibu.

"Tuombe uhai tutajibu ... maana majibu bado tunayo," alisema Mbunge huyo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza suala la Richmond.

Kauli ya Bibi Kilango bungeni jana ilichukuliwa na baadhi ya wabunge wa CCM kuwa ni ukiukwaji wa msimamo wa chama hicho katika kikao chake mwishoni mwa wiki iliyopita Dodoma.

Katika kikao hicho, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, kulizuka makundi mawili moja likitaka watuhumiwa wa ufisadi wachukuliwe hatua za kichama huku lingine ambalo liliungwa mkono na wengi likitaka yasubiriwe matokeo ya uchunguzi wa Tume ya Uchunguzi ya Rais.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema hata Mwenyekiti aliridhia hatua ya kusubiri matokeo hayo na kuwataka wajumbe wa NEC kuhimiza masuala ya kukijenga chama na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.

Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Bibi Kilango ana haki ya kuzungumza chochote ambacho hakikiuki kanuni hizo, ili mradi anao ushahidi wa kutosha na si kusema uongo.

Mbunge huyo ambaye mwaka jana alikuwa mwiba mchngu katika suala hilo la ufisadi, anadaiwa kuwa katika mtafaruku na Mbunge wa Kigoma Mjini, Bw. Peter Serukamba (CCM), ambaye anadai alimtishia.

Bw. Serukamba amewasilisha malalamiko yake kwa Ofisi ya Spika kutokana na madai hayo.

(majira, 20.06.2008, 0054 EAT; Na Amir Mhando, Dodoma)

MOSONGA RAPHAEL said...

‘Wakurya’ wetu bado hawatoshi
NIMESHAURI katika makala ya wiki jana kwamba hatuna budi kuachana na utamaduni wa kumkubalia “mshindi” na “chama” chake kuchukua asilimia 100 ya madaraka ya utawala na kuwaacha wengine wote walioshindana naye nje kabisa.

Hapa, maneno “mshindi” na “chama” nimeyaweka katika mabano kwa sababu ambazo msomaji wa safu hii atakuwa amebaini. Kimsingi, mara nyingi huyo anayetangazwa kuwa “mshindi” si mshindi halisi, na pale anapokuwa kashinda kweli, ushindi wake ni mwembamba kiasi kwamba ni kwa mabavu tu ndiyo anaweza kuendelea kutawala. Aidha, kama ambavyo msomaji huyo atabaini pia kile kinachoitwa “chama” si chama bali mkusanyiko wa watu wenye malengo yanayosigana na kukinzana.

Barani Afrika mifano ni mingi. Hapa nyumbani imesemwa mara nyingi kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikushinda uchaguzi wa Zanzibar mwaka 1995, na kwamba Chama Cha Wananchi (CUF) kiliporwa ushindi wazi wazi. Bila hata kujadili kama madai hayo yana ukweli wo wote, tutajikumbusha kwamba kiongozi mmoja wa juu wa CCM Visiwani aliiandikia Tume ya Uchaguzi Zanzibar kusema kwamba CCM haiyakubali matokeo ya uchaguzi huo.

Swali ambalo wengi wamejiuliza ni hili : Iwapo CCM ilikataa matokeo ya uchaguzi lakini ikabaki madarakani, ni matokeo yapi iliyakataa na yapi yaliirejesha madarakani. Utata huu, naamini utakuwa nasi kwa muda mrefu sana, na labda hatutafanikiwa kupata jibu. Muhimu hapa, tukumbushane tena, ni kwamba Mwalimu Julius Nyerere, bila kusema kwamba uchaguzi ulikuwa umeporwa au la, alitamka kwamba kwa wembamba wa "ushindi" uliotangazwa, hakuna chama ambacho kingeweza kutawala peke yake.

Tunajua kwamba alipuuuzwa kabisa, CCM ikaendelea kutawala, na matokeo yake ni vifo vilivyotokea mwaka 2001 na kuzalisha wakimbizi wa kwanza wa Kitanzania tangu Uhuru. Leo bado wakuu wa CCM wanajikanyagakanyaga kuhusu "mwafaka" hata baada ya ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kulipa suala la mwafaka kipaumbele kwa ngazi ya juu kabisa.

Nako nchini Kenya mwishoni mwa mwaka jana tulishuhudia matendo ya aibu yaliyofanywa na Mwai Kibaki na washirika wake, matendo yaliyosababisha vifo vya mamia ya raia wa Kenya katika machafuko yasiyo na sababu yo yote bali uroho wa madaraka wa watawala wa nchi hiyo.

Kama vile kuna mashindano ya kumtafuta mwizi bora wa kura barani Afrika, Robert Mugabe naye akafanya mambo yake huko Zimbabwe kwa staili mpya : kukataa kutangaza matokeo ya uchaguzi "mpaka kieleweke" . Sasa, nchi hiyo iliyokuwa inazalisha chakula cha kutosha kulisha ukanda mzima wa kusini inakabiliwa na njaa ; theluthi ya raia wake wamekimbilia uhamishoni; mfumuko wa bei unatisha ; watu wanadundwa, wanauawa kwa sababu za kisiasa ; nchi imeingia katika hali ya utawala wa kijeshi bila kutangaza.. yote haya ili "Mzee Mkombozi" aendelee kukaa madarakani.

Mifano ni mingi katika bara hili linalosuasua bila maendeleo, bara linaloendelea kubaki nyuma wakati mabara mengine yote yanapiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi. Tunashindana kwa kuonyeshana ubabe, kila mtu kwa staili yake. Si vigumu kuanza kuamini kwamba Waafrika tumepata laana fulani ambayo inatufanya tuwe tofauti na binadamu wengine.

Ingeeleweka kama tungekuwa tunatawaliwa na wababe ambao, pamoja na ubabe wao, wanasimamia maendeleo ya kweli. Tunazijua nchi ambazo zimetawaliwa na wababe kwa miongo kadhaa, lakini zikapata maendeleo ya haraka, na ambazo baada ya miongo kadhaa ya kunyimwa uhuru wa mawazo sasa zinaonekana zina neema ya kiuchumi, na sasa zinaweza kuanza kujenga demokrasia inayoambatana na ustawi wa kuridhisha. Kwetu tumekosa yote : hatuna demokrasia, hatuna maendeleo.

Ni rai yangu kuwa ipo haja ya kujiangalia upya, kutafakari jinsi ambavyo tumekuwa tukijitawala na kutafuta sababu zinazotufanya tuendelee kuwa nyuma na kuziondoa sababu hizo. Yako mambo mengi ya kuyasaili, lakini mojawapo ni kwamba hatujakubali wala kuelewa kwamba sote tunatakiwa tuwe wadau katika uendeshaji wa nchi zetu, kwamba hakuna mtu wala kundi dogo la raia wanaoweza kudai ukiritimba wa akili, busara wala uwezo wa kutuamulia njia ya kufuata ili kuleta maendeleo. Maana yake ni kwamba hatuna budi kushiriki sote, kwa kiwango kinachowezekana na si kwa utashi wa watawala waliomo madarakani kwa wakati wo wote.

Tukubaliane kwamba watawala watatawala kwa ridhaa ya wananchi na si kwa sababu wamepata karama ya utawala kutoka mbinguni, na kwamba ni lazima wafanye kila linalowezekana kujua ni nini wananchi wao wanataka wafanyiwe, hasa kama sauti zao zimesikika zikisema, lakini hata kama hawajakisema wazi wazi. Mtawala wa haki, ambaye ni kiongozi, husikia hata zile sauti zilizo kimya, kwani ingawa maneno mengine huweza kuwa kelele zisizo maana, kimya kinaweza kuwa na mshindo mkubwa.

Zama zote za maisha ya binadamu zimetambua ukweli huu, lakini katika mazingira yetu, na kwa kuangalia viwango vyetu vya maendeleo, tunatakiwa tufanye tahadhari kubwa. Viwango vya uweledi wa watu wetu walio wengi si mkubwa sana, tukianzia kwenye elimu ya kawaida tu. Si raia wengi wamewezeshwa kuchanganua masuala magumu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa ufasaha mkubwa. Ukweli ni kwamba wengi wao wamekosa hata hiyo "elimu" tunayoikosoa kwamba ni duni.

Aidha, kutokana na miaka mingi ya kutopewa mwanya wa kusema wanalolihisi moyoni, wengi wamepoteza ujasiri wa kueleza wanachotaka, mara nyingi si bure kwani katika maeneo mengi ya nchi bado wanaadhibiwa kwa kusema ukweli wao. Ni mara ngapi tumepata taarifa za watu kupigwa au kusumbuliwa kwa njia mbali mbali kwa sababu tu wameuliza maswali yasiyowafurahisha wakubwa ?

Katika hali kama hiyo tunatakiwa tujue kwamba tunayo nakisi kubwa katika medani hizi mbili : Moja, tunayo nakisi ya wananchi wenye elimu na weledi wa kutosha wa kuchanganua masuala magumu yanayohusu maendeleo yao ; pili, tunayo nakisi ya wananchi (hata wenye weledi) wenye ujasiri wa kusema kwa sauti kile wanachoamini.

Hili linajidhihirisha katika ngazi zote, toka chini hadi juu kabisa, katika jamii yetu. Tunajua kwamba hata wale waliopata nafasi za utawala si wote wanao weledi wa kutosha kuhusu masuala mengi yanayohusu hali halisi ya dunia. Wengi mno wameingia katika nafasi walizo nazo kwa hila ambazo tunazijua, hila ambazo zinawafanya raia wengi wanaojiheshimu wasite kuingia katika "mchezo" wa siasa kwa kuhofia kuchafuka.

Wengi wa hao wanaodiriki kuingia katika mchezo huo, wawe na uwezo au la, hawathubutu kusema wanachokiamini kwa kuchelea kupoteza nafasi zao, hata kama wanaona kabisa kwamba mambo hayaendi yanavyotakiwa. Bima yao ya ya kuhakikisha wanabakia katika nafasi zao ni ukimya, na kufuata msitari uliochorwa na wale wanaoonekana kwamba ndio wakubwa kabisa.

Kwa jinsi hii tumetengeneza kabila zima la watu walio katika nafasi za utawala ambao "hawana" rai kuhusu lo lote linaloendelea kwa muda wote wanapokuwa katika nafasi za "neema". Mara nyingi watakushangaza pale wanapopoteza nafasi zao, kwani utawasikia wakiongea, tena kwa uchungu, kuhusu mambo yanavyokwenda hovyo katika asasi ambamo walikuwa wakitumika hadi majuzi tu.

Kisichotumika huvia. Wale waliobaki katika nafasi za utawala kwa muda mrefu bila kuzisumbua akili zao kufikiri na kutafiti njia mbadala za kuendesha nchi hujikuta, baada ya muda, wamevia kimawazo, na mchango wao unakuwa si kingine bali manung’uniko na malalamiko yasiyosaidia lo lote.

Ni muhimu, basi, kuwathamini wale wachache wanaodiriki kutoa maoni yao, wawe ndani ya utawala au nje, kwa sababu hawa ni watu adimu katika jamii yetu. Zamani kidogo niliwahi kuandika kwamba sote tunahitaji kuwa "Wakurya" kwa kiasi fulani, kwa maana ya kuambizana ukweli hata kama haupendezi. Hadi sasa "Wakurya" tulio nao bado hawatoshi. Tuwathamini hao wachache waliopo
...............................
...............................
(Jenerali Ulimwengu Juni 18, 2008; hii ni sehemu ya kwanza ya Rai ya Jenerali Ulimwengu. habari zaidi: Raia Mwema)
...............................

MOSONGA RAPHAEL said...

MAJIRA WAMWOMBA RADHI MBUNGE:
Sitaidharau NEC kamwe-Kilango
MBUNGE wa Same Mashariki, Bibi Anne Kilango-Malecela (CCM), amesema kamwe hataidharau Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kwani ni chombo kinachoheshimika.

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya kutafsiriwa juzi kuwa kauli yake juu ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu Tanzania (BoT), inakiuka msimamo wa NEC na hivyo haiogopi, Bibi Kilango alisema hakuwa na maana hiyo.

"Mimi ni mwanachama wa CCM, NEC mnayoisema ni ya CCM siwezi hata siku moja nikasema siiogopi, kwa sababu ndiyo yenye uamuzi wa mwisho katika mambo mbalimbali ya chama hata mustakabali wa uanachama wangu," alisema Mbunge huyo machachari.

Alisisitiza kuendelea kukipenda na kukiheshimu chama chake na NEC pia, sambamba na kutetea haki ya Watanzania wakiwamo wapiga kura wake wa Jimbo la Same Mashariki.

Juzi bungeni akichangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2008/9, Bibi Kilango alisema hataogopa vitisho vyovyote katika kuzungumzia maslahi ya Taifa, ambapo alisisitiza fedha za EPA zirejeshwe na waliozichukua BoT.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa alikuwa anakwenda kinyume na kilichokubaliwa na NEC iliyokutana mwishoni mwa wiki iliyopita Dodoma, ambapo lilisisitizwa suala la EPA lisijadiliwe tena hadi Tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza suala hilo imalize kazi yake.

Gazeti hili kwa kuzingatia tafsiri hiyo ndiyo sababu likaandika kichwa kilichosema 'Kilango: Siogopi 'NEC'' na kumsababishia usumbufu Mbunge Kilango. Tunasikitika kwa hali hiyo ambayo haikulenga kumchafua kwa msingi wowote.

Tunachukua fursa hii kumwomba radhi Bibi Kilango na wengine ambao kwa namna moja au nyingine walisumbuliwa na kichwa hicho cha habari.

(source: Majira, 21/06/2008 01:53 EAT)