Monday, 30 June 2008

Ripoti ya EPA

(Na Mwandishi Wetu, 29.06.2008 0033 EAT. (Majira))
Ripoti ya ufisadi EPA yavuja
*Yadai Utawala wa Mkapa ulishindwa kuuzuia
*Kampuni zenye fedha zao zatinga mahakamani

SERIKALI ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa, ilishtukia harufu ya ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), iliyokuwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tangu mwaka 1997 lakini ikashindwa kuizuia.
Makosa hayo ya utawala wa Mkapa ndiyo yaliyoendelea kuruhusu mwanya wa ufisadi kwenye akaunti hiyo hadi Januari, mwaka juzi ulipoingia utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Hayo yamo kwenye ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na kampuni ya Ernst & Young ambayo gazeti hili limenasa nakala yake.
Katika kipindi cha wiki kadhaa, ripoti hiyo iliyokuwa siri kubwa, imekuwa ikisambazwa kwa kasi miongoni mwa watu mbalimbali baada ya kuvuja kutoka serikalini. Ripoti hiyo ndiyo iliyosababisha Rais Kikwete kumfuta kazi aliyekuwa Gavana wa Benki hiyo, marehemu Dkt. Daud Balali na kuingia Profesa Benno Ndulu.
Utata wa malipo ya EPA Ripoti hiyo inaanika kuwa tangu mwaka 1997 Serikali ya Mkapa ilianza kubaini utata katika uendeshaji wa akaunti ya EPA na kuanza kuihoji BoT ikitaka maelezo ya kina kuhusu akaunti hiyo.
"Tume ya Ukaguzi imebaini kuwa kupitia barua ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina (Raphael Mollel) ya Oktoba 17, 1997, Wizara ya Fedha ilianza kuwa na shaka kuhusu uendeshaji wa akaunti ya EPA," inasema ripoti ya Ernst & Young na kukariri sehemu ya barua hiyo ya Mollel kwenda BoT iliyoandikwa:
"Hazina ingefurahi kama ingeweza kupata hesabu halisi ya fedha zilizoko kwenye akaunti ya EPA, ili iweze kuweka sera nzuri zaidi katika matumizi ya fedha hizo."Kama unavyojua Hazina imekuwa ikipata tetesi zinazotofautiana kuhusu hali halisi ya akaunti hiyo. Wakati fulani iliashiriwa kwamba hakuna pesa yoyote kwenye akaunti hiyo na kuwa madeni yangepaswa kulipwa kupitia raslimali za nchi."Uchunguzi huo hata hivyo umebaini kuwa pamoja na barua hiyo, uongozi wa BoT haukuwa tayari kutoa ushirikiano huo, jambo ambalo sasa linazidi kuiongezea nguvu dhana, kwamba ufisadi kwenye akaunti hiyo ulianza kufanyika siku nyingi.
Baada ya miaka mingi ya ukimya, hatimaye katika barua yake ya Julai 2005, kwenda kwa Katibu Mkuu wa Hazina, Bw. Gray Mgonja, Gavana wa Benki Kuu wakati huo, Dkt. Ballali, aliashiria kuwa isingekuwa rahisi wao kutoa hesabu halisi ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya EPA. Akataja tatizo la mfumo wa kompyuta."Ifahamike kuwa ni vigumu kwa sasa kutoa hesabu halisi za akaunti ya EPA, kwa sababu malipo yote yanafanyika kadri maombi (ya wadai) yanavyokuja na hakuna muda maalumu. Hata hivyo pindi matatizo ya kiufundi katika mfumo wetu wa kompyuta yatakapokuwa tayari, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa mchanganuo," ilisema barua hiyo. Tofauti na maelezo hayo ya Dkt. Ballali, hesabu za wadai zilizo sahihi na zilizokuwa na utata zilikwishawekwa bayana kupitia ripoti ya Lazard iliyokamilika mwaka 2004 na zaidi, wakati BoT wakisingizia mtandao wa kompyuta kuwa mbovu, mtandao huo huo ndio mwezi mmoja uliofuata, uliotumiwa na watendaji wa Benki hiyo kuidhinisha malipo kwa kampuni 22.
Uchunguzi unaonesha kuwa wakati Dkt. Ballali akiieleza Serikali kuwa kulikuwa na tatizo la kompyuta, lakini malipo yakaendelea kupitia orodha zilizokuwa kwenye mtandao huo, hadi mauti yanamfika jijini Washington, Marekani, hivi karibuni. Hakuwahi pia kuipa Serikali taarifa rasmi kuhusu EPA kama alivyoahidi na kama ilivyoombwa tangu mwaka 1997 na Serikali nayo ilionekana ghafla kuondoa wasiwasi wake juu ya akaunti hiyo."Timu ya ukaguzi haikupata ushahidi wowote kuwa mchanganuo huo uliwahi kuwasilishwa kwenye Wizara ya Fedha," inakariri Ernst & Young katika ukurasa wa 19 wa ripoti yake. Mchanganuo mgumu?Wakati viongozi BoT wakishindwa tangu mwaka 1997 kuonesha mchanganuo wa fedha za EPA, uchunguzi wa kikaguzi umedhihirisha kuwa katika akaunti ya fedha hizo namba 9991 509 101 ambayo awali ilikuwa NBC kabla ya kuhamishiwa kwenye akaunti namba 9924 191 011 iliyokuwa BoT, ushahidi kadhaa uliopatikana umehitimisha kuwa mfumo wa kompyuta ya akaunti hiyo haukuwa na hitilafu yoyote na ulikuwa ukiendelea kutumika. Kwa mfano, hadi mwaka 2004 takwimu halisi kuhusu akaunti ya EPA zilikuwa hivi:
Madeni yaliyohakikiwa na kulipwa dola milioni 228,
madeni ambayo wadai waliruhusu yafutwe (ikiwa sehemu ya msaada) dola milioni 216. Jumla ndogo dola milioni 444.
Hesabu zaidi za akaunti hiyo zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya deni hilo iliyosalia ilikuwa haijalipwa kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:
Madeni yaliyokuwa na utata/kesi dola milioni 25, wadeni waliokataa masharti (ya mkusanya madeni) dola milioni 14,
deni lisilokidhi viwango (cha mkusanya madeni) dola milioni tatu, wadai ambao hawakujitokeza kabisa dola milioni 48, deni ambalo ilishindikana kuhakikiwa, dola milioni 143, jumla ndogo dola milioni 233 na jumla ya deni lote (lililolipwa na lililobaki na utata) dola milioni 677. Kwa mujibu wa mapendekezo ya Mkaguzi wa Kimataifa M/S Lazard aliyefadhiliwa na Benki ya Dunia, BoT ilishauriwa kutolipa deni lililosalia lenye utata la dola milioni 233, kutokana na utata ulioanishwa hapo juu na ushauri huo ulikuja kutiliwa nguvu baadaye na ripoti nyingine ya wakaguzi wa PriceWaterhouseCoopers ya Ufaransa. Lakini mwaka mmoja baadaye, BoT hiyo hiyo ikaibuka, katika mazingira tata na kuanza kuwalipa waliojiita mawakala wa kampuni hizo za nje. Kipindi chote hicho Serikali iliyokuwa imekwishaona utata na iliyokuwa ikinyimwa ripoti za akaunti hiyo, haikuonekana kuwa na wasiwasi tena."Ripoti (ya wakaguzi kutoka M/S Lazard) ilihitimisha kuwa sehemu kubwa ya madeni yalishapitwa na wakati na ikaishauri Wizara ya Fedha kutoyalipa," inasema ripoti ya Ernst&Young, Wizi wa kisomi Huku zikitumia mihuri ya mawakili wenye majina na maelezo hewa, nyingi kati ya kampuni 22 zilizopitishiwa malipo kutoka akaunti ya EPA, sasa imebainika kuwa zilighushi nyaraka mbalimbali. Ernst & Young wanaonesha kuwa kati ya sh. 133,015,186,220 zilizochotwa kutoka EPA, nyaraka zilizowasilishwa na zile kampuni 22 zinazotuhumiwa kuchota sh. 90,359,078,804, 13 zilibainika kuwa za kughushi. Ripoti ikaeleza zaidi kuwa kiasi kilichosalia cha sh. 42,656,107,416.61 haikuweza kubainika mara moja usahihi au ubatili wake, kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana nyaraka zozote au sehemu ya fedha hizo kuwa na kesi mahakamani. Serikali kizimbani Hivi sasa pamoja na kuwapo kesi za awali, imebainika kuwa baadhi ya kampuni ambazo majina yao yalitumika katika ulaghai wa fedha za EPA ikidaiwa kuwa yalitoa ruhusa madeni yalipwe kwa niaba yao, yamekana kufanya hivyo na baadhi pamoja na mambo mengine, yakilalamikia uzembe wa Serikali ya Tanzania kupitia BoT kwa kuwalipa watu ambao wao kamwe hawakuwa na mikataba nao. Majira Jumapili ilijaribu kuwasiliana na baadhi ya kampuni zilizoingizwa katika utapeli wa EPA kwa fedha zao kulipwa mawakala hewa, karibu zote ziliamua kutolizungumzia suala hilo, huenda zikisubiri hatua za kisheria.Watendaji wa kampuni za Mirrlees Blackstone ambayo kuanzia mwaka 2002/03 ilibadili jina na kuitwa Man B & W Diesel Limited, Metsopaper na Iveco ambazo ni miongoni mwa wahanga wa majina na mihuri yao kughushiwa, hawakupenda kulizungumzia sana suala hilo kwenye vyombo vya habari walipotakiwa na gazeti hili kulizungumzia. Sakata la EPA kwa kifupi Kati ya mwaka 1970 na 1980, Serikali ya Tanzania ilipokea huduma mbalimbali kutoka kampuni na taasisi za nje, lakini kushuka kwa thamani ya shilingi kulikochangiwa na vita ya Kagera kunaifanya Serikali ishindwe kulipa madeni hayo kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.Kati ya mwaka 1985 na 1995, Benki ya Dunia iliona haja ya kuisaidia Tanzania kulipa madeni hayo kupitia mikakati mbalimbali ukiwamo wa kuyanunua (Debt Buy Back).
Mwaka 1985 Akaunti ya EPA ilihamishwa kutoka NBC kwenda BoT.Mwaka 1994, ili kuhakiki wadai halisi, Tanzania ilitangaza kwenye vyombo vya habari vya kimataifa wenye madai wajitokeze. Kampuni chache sana zikaitikia mwito huo.

No comments: