Tuesday, 3 March 2009

Waziri wa Fedha atembelea RG

Jana waziri wa fedha wa UK Bwana Alistair Darling alitembelea mji wa Reading. Madhumuni ya ziara yake ni kuangalia jinsi mji wa Reading ulivyoathirika kutokana na mtikisiko na kuyumba kwa hali ya uchumi nchini na duniani kote.

Nilimuona akipitishwa na wenyeji wake pale Market Place huku akionyeshwa majengo ambayo yamebaki wazi (matupu) baada ya shughuli za kibiashara kufa na hivyo kufungwa. Majengo hayo yako kati ya benki za Lloyds TSB na NatWest. Wakubwa wa Halmashauri ya Mji wa Reading walikuwa wakimjulisha ni nini kinafanyika ili majengo hayo yaendelee kutumika ili yasibaki kuwa mahame! Waziri alikuwa akitembea kwa miguu huku amezungukwa na utitiri wa waandishi habari na kamera zao.

Kusema kweli makali ya uchumi yameuma kweli kweli hapa UK na karibu kila mtu anapata maumivu yake! Viongozi nao wanahaha kutafuta dawa ya matatizo. Waziri mkuu Bwana Brown yuko Marekani tangu jana kuonana na Rais Obama na pia kama maandalizi ya mkutano mkubwa wa G20 utakaofanyika jijini London mwezi wa nne mwaka huu kujadili masuala ya kiuchumi duniani kwani hakuna nchi moja peke yake inayoweza kuyatatua au kuyamaliza bali ni juhudi za pamoja ndio zitakazopunguza makali na hatimaye kupata jawabu la matatizo haya.

No comments: