Friday, 13 March 2009

Uchumi unapochoma!

Jamani dunia iko ktk kipindi kigumu kiuchumi na kimaisha kwa ujumla. Serikali mbalimbali duniani hata za mataifa makubwa kiuchumi kama Marekani na Uingereza zimetikiswa na hali hii ya uchumi.

Kwa wananchi wa kawaida hali ni ngumu zaidi. Maisha ktk ngazi ya familia yamezidi kupanda kila kukicha huku vipato vyao vikizidi kuwa duni au vinaporomoka chini. Kila mmoja wetu anahisi joto la ukali wa maisha kwa sasa.

Kwa kuzingatia hii shida tuliyoko, nimeona nitoe maoni au mchango wangu juu ya ni nini tufanye ili kukabiliana na ugumu wa maisha. Ni matumaini yangu kuwa kwa njia hii ya kubadilishana mawazo, tunaweza kupunguza makali ya maisha kwa kutumia uzoefu wa kila mmoja wetu.

Ni vema pia tuwaelemishe wadogo zetu, watoto wetu au wana familia kwa ujumla ili waelewe kinachoendelea. Hali ya usiri ndani ya familia huleta kutoaminiana. Lakini kukiwa na uwazi na ukweli kuhusiana hali ya uchumi ndani ya familia, misuguano ya kifamilia itapungua ama kutoweka kabisa na badala yake furaha, amani na mshikamano vitatanda ndani ya nyumba.

Sasa tufanye nini basi ili kukabiliana na hili balaa la kiuchumi?

Mimi ushauri wangu na maoni yangu ni mafupi na rahisi. Tujaribu kujijengea utamaduni wa kujitosheleza ktk mahitaji ya kimsingi kwa njia ya kujitegemea. Yaani tupunguze matumizi ya hela ktk kununua vitu au huduma ambazo sio za lazima au zile ambazo tunaweza kuzifaidi bure. Nitatoa mifano michache hapa chini:

1. kujilimia bustani ya mboga na matunda (kama eneo linapatikana).
Nina imani ktk nchi yetu maeneo yapo kwa ajili ya kilimo cha bustani na upatikanaji wa maji sio mbaya sana na hivyo inawezekana kujitosheleza mboga za majani na matunda kwa ajili ya afya zetu.

2. kuanzisha ufugaji mdogo-mdogo.
Mfano, kuku wa kienyeji au wa kisasa, mifugo kama mbuzi, kondoo na ng'ombe kwa ajili ya nyama na maziwa. Mbolea inayotokana na vinyesi vya mifugo hii itatumika ktk kilimo cha bustani.
Mazao ya ziada ya mifugo hii (maziwa, nyama, ngozi, mbolea n.k.) tunaweza kuuza na kujipatia fedha zaidi.

3. kujipikia vyakula nyumbani badala ya kununua gengeni au hotelini.
a) vitafunio. unaweza kujipikia mwenyewe vitu kama keki, maandazi, chapati na vitumbua kwa matumizi yako na familia nzima badala ya kununua vitafunio ambavyo vitagharimu fedha nyingi ili kutosheleza familia. Unachotakiwa kufanya ni kununua unga wangano, mafuta ya kupikia, sukari, chumvi n.k. kwa ajili ya kupika vitafunio. Vitu hivyo pia (mafuta ya kupikia, chumvi n.k.) vitatumika kupikia chakula cha mchana na usiku!
b)kujipikia na kula nyumbani badala ya kununua chakula magengeni au hotelini.
mapishi nyumbani ni nafuu kwa vile chakula kitakuwa kwa ajili ya familia nzima na kwa mara moja. Unapokula gengeni utashiba peke yako kwa gharama ambayo ingelisha familia nzima ktk mlo mmoja. Unaweza pia kwenda na chakula/vitafunio kazini, hivyo kuokoa gharama za kununua.
Kumbuka wanaofanya biashara hii hutaka kurudisha gharama ya vitu walivyotumia kupika na pia kupata faida, kwa hiyo wanakutoza hela zaidi wewe ambazo unaweza kuziokoa kwa kujipikia.

4. kujifunza ususi au unyoaji nywele.
a) kwa kina mama; unapoajifunza kazi za ususi unakuwa unapunguza gharama za kwenda saluni kusuka nywele au kuweka rasta. Ukisuka mwanao nae atakusuka au ndugu yako atakusuka. Hela utakayookoa kwa mwezi ukiizidisha kwa mwaka mzima utakuwa umeokoa kiasi kikubwa cha hela.
b) kwa kina baba; jinunulie mkasi, nyembe au mashine ya kunyolea. Ukishapata hii mashine au mkasi huwezi tena kutumia hela zaidi, kazi yako itakuwa ni kunyoa tu kila unapohitaji bila kwenda saluni. Nawe pia utaokoa hela za kwenda saluni kila mwezi.

5. punguza bili za umeme kwa kununua taa (balbu) za kutumia umeme kidogo. Siku hizi zipo balbu za umeme kidogo na hutoa mwanga wa kutosha. Ondoa taa zote za zamani. Pia washa taa ile unayotaka kutumia. Kama chumba au mahali fulani hapatumiki ni vema uzime taa zake. Washa tu pale unapohitaji mwanga.
Kwa vyombo vya umeme (tv, video na dvd players n.k.) navyo unatakiwa kuvizima kama havitumiki. Kama unataka kuwa na friji, tumia friji yenye 'kihisi' jotoridi ambacho huzima friji pale ubaridi wa kwenye friji unapofikia kiwango kinachotakiwa na kuwasha tena friji ubaridi unapopungua.

6. Zungusha matumizi ya maji.
Maji ukishayatumia kwa shughuli moja unaweza kuyatumia tena kwa matumizi mengine ya nyumbani mfano kudekia, kumwagilia bustani au maua n.k.

7. tembea kwa miguu au tumia baiskeli.
Unaweza kuokoa maelfu ya hela kwa mwaka endapo utaamua kutumia usafiri wa baiskeli au kutembea kwa miguu ktk umbali wa kawaida. Kwa kutembea kwa miguu mara kwa mara utaweza pia kupata faida ya kuupa mwili mazoezi bure kabisa!

8. vaa nguo zako ulizo nazo kwa sasa.
Hizo nguo ulizonazo ni nzuri na zinakufaa, kwa nini uende dukani tena kutafuta nyingine?
Hata viatu vyako bado ni vizima na vinapendeza kwa nini unavitelekeza na kununua jozi zaidi?
Jiepushe na kasumba ya kwenda na fasheni. Hii ni pamoja na vitu kama simu za mikononi, vito vya thamani n.k. Endelea kutumia vitu hivyo ulivyo navyo tayari na okoa fedha kwa kuachana na kasumba ya kwenda na fasheni -maana fasheni haziishi kila msimu zinaibuka mpya, ukishindana nazo wewe ndio utakuwa mshindwa!

9. punguza sherehe zisizokuwa za lazima.
Sherehe za mara kwa mara hugharimu fedha nyingi, kwa hiyo ni vema suala la matanuzi, tafrija au sherehe litazamwe kwa umakini (hili linategemea mtazamo wa mtu binafsi).

10. kama unavuta sigara na kulewa pombe, utakuwa unaelewa mzigo ulionao kulipia vileo hivyo na ninadhani mwenyewe unaamini ipo haja ya kuachana na vitu hivyo.

Mwisho, penda kile ulichobarikiwa kuwa nacho. Jiepushe tamaa - kutamani usichoweza kuwa nacho. Zaidi ya yote mshukuru Mungu kwa alichokubarikia.

No comments: