Monday, 2 March 2009

Maisha ni kujaribu, kujaribu na kujaribu!

Kama umeona film au documentary ya maisha ya kisiasa ya Mama Margareth Thatcher utaamini kuwa maisha ni kujaribu mara nyingi kadri uwezavyo.

Huyu mama ambaye ni Baroness kwa sasa na waziri mkuu wa zamani, hakuingia ktk ulingo wa siasa kirahisi. Alipata vipingamizi vingi enzi zile za miaka ya 1950 ktk kupata nafasi ya uwakilishi bungeni.

Vipingamizi alivyokumbana navyo vilitokea ndani ya chama chake (wanachama na viongozi) na pia kutoka kwa wabunge wa chama chake. Wengi walimkataa au kumwekea mizengwe kwa sababu ni mwanamke na pili alikuwa na watoto wadogo mapacha.

Kuna majimbo kama matano (au zaidi) ambayo yalimkataa Mama asiwe mgombea kupitia chama chake, hadi yeye mwenyewe akata tamaa kabisa.

Bahati mbaya zaidi kuna mbunge mmoja ambaye alisaidiwa sana na Mama Thatcher ktk kampeni za uchaguzi hadi kushinda jimbo lake. Siku moja Mama alienda kumsalimia na kumwomba ushauri na msaada ktk mambo ya kisiasa. Mbunge huyo akamkatalia kabisa na akamwonya Mama asirudie kumfuatafuata!

Siku moja mume wake akamwambia Mama ajaribu tena kugombea ktk jimbo moja liloko London (Finchley) kwa vile mbunge wake alikuwa ametangaza kustaafu.

Baada ya kutafakari sana, Mama akamkubalia mumewe (Denis). Mama akapeleka jina lake jimboni ili lijadiliwe na kupigiwa kura. Cha ajabu hata mbunge huyo anayeng'atuka alitaka kumzibia Mama Thatcher asipate kuteuliwa na chama chake ili agombee ubunge!!!

Ktk mchujo wa kwanza Mama alipita, wakabaki watatu. Lakini yule mzee 'mstaafu' akaendelea kutia mizengwe na kumkatisha tamaa Mama! Ndipo Mama Thatcher akamwendea huyo mbunge pembeni na kumpasha kuwa yeye ameamua na atagombea na atawatumikia wapiga kura wake kikamilifu.

Mungu si Athumani, Mama akawabwaga wagombea wenzake na kupitishwa kuwa mgombea wa Conservative ktk jimbo. Uchaguzi ulipofika Mama alishinda na kwenda Bungeni.

Mama alipofika bungeni alimwona yule mbunge (aliyemsaidia ktk kampeni zake na aliposhinda akamruka Mama). Yule mbunge kwa wivu au aibu akawa anajifanya hamwoni Mama na akawa anampita Mama bila hata kumsalimia kwa vile enzi zile Mama alikuwa bado mdogo lakini mwenye uwezo mkubwa kisiasa.

Kwa hiyo Mama aliendelea kuwa mbunge wa jimbo lake kwa miaka 31, ambapo aliweza pia kuwa waziri mkuu wa nchi kwa miaka zaidi ya 10 (1979 -1990).

Kutokana na film hii ya Mama Thatcher, nimejifunza kuwa ktk maisha hapa duniani kuna vikwazo vingi. Na mbaya zaidi kuna watu ambao hawapendi kuona ndoto za wenzao zikitimia. Na wengine hata husimama njiani ili kukinga au kuziba njia za wenzao kuelekea ktk mafanikio.

Lakini ipo siku moja pale kweli itakapojidhihirisha na mafanikio kupatikana. Ndio maana nasema: endelea kujaribu bila kukata tamaa, huenda tundu la mafanikio lipo jirani kabisa na hapo unapoonekana kupoteza nguvu za mapambano zaidi kimaisha, kama tulivyoona huyu kwa Mama!

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Maisha ya Baroness Thatcher.

-Watoto wake wawili mapacha (wa kiume na kike) wanaitwa Mark na Carrol

-Alianza siasa kwa kugombea jimbo la Dartford mwaka 1949 bila mafanikio.

-Alikuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1959.

-Jimbo alilowakilisha bungeni (house of commons) lilijulikana tangu 1950 kama Finchley.

-Mwaka 1997 jimbo la Finchley lilibadilishwa mipaka na kujulikana kama Finchley & Golders Green.

-Film/documentary inayoonyesha maisha yake inaitwa
'The Long Walk to Finchley:
How Margareth Thatcher might have done'.
Kwa mara ya kwanza ilionyeshwa Juni 2008 BBC2 na imerudiwa tarehe 01/03/2009 BBC Two -saa 3 hadi 4 usiku za Uingereza.