Tuesday, 31 March 2009

Nani kasema machinga wanataka ghorofa?

Tuesday, March 31, 2009
Nimekuwa nikisoma magazeti ya kwetu (TZ) na kuona jinsi viongozi wa manispaa za Dar wanavyopanga mipango kuhusiana na wafanyabiashara ndogo-ndogo maarufu kwa jina la machinga.

Pia nimeona picha ya jengo jipya la ghorofa mbili au tatu, pale uwanja wa Karume ambalo ni kwa ajili ya machinga.

Sielewi kama upembuzi yakinifu ulifanyika kisawasawa kabla ya kutekeleza mpango huu wa kuwajengea machinga au kama machinga walihusishwa ktk kutoa mawazo yao maana huu ni mradi unaowagusa kimaslahi.

Kwa maoni yangu siamini kuwa machinga walihitaji au bado wanahitaji ghorofa ili kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Tukumbuke kuwa msingi mkuu wa hawa machinga ni kutafuta soko la watu mbalimbali hasa wa kipato cha chini au kawaida. Mara nyingi wateja wa machinga ni wale ambao hawamudu bei za bidhaa ktk maduka ya rejareja mitaani. Ndio maana machinga hutembea kwa mguu siku nzima kupita huku na huko wakitafuta wateja tena kwa bei zisizo na uhakika, na wakati mwingine huuza kwa bei za kutupa!

Unapoamua kumjengea huyu machinga jengo la 'kisasa' (kwa maana ya wana-manispaa) unakuwa unamwondoa machinga ktk mlinganyo (equation) wa biashara.

Kwanza itabidi wajisajili kwa mamlaka inayoendesha jengo (manispaa). Halafu watatakiwa wachangie gharama za uendeshaji jengo kama vile umeme, huduma ya maji safi na maji taka, usafi na ukarabati wa jengo, pango la jengo (maana hawa ni wapangaji -jengo sio mali yao) n.k.

Ukishamtwisha machinga gharama hizi zote, atajikuta anaelemewa na mzigo wa malipo na hivyo kulazimika kuongeza bei za bidhaa zake (nyongeza bei ni ktk jitihada za kukidhi gharama mbalimbali za uendeshaji jengo, na vile vile itabidi nae apate faida). Hali ikifikia hapo, hiyo biashara inakuwa si ya machinga tena - hilo ni daraja la juu ya machinga. Machinga hana mtaji wa kuhimili gharama hizi, na kama machinga atauza bei kama za maduka ya Kariakoo au Zanaki, kuna haja gani mteja anasafiri hadi uwanja wa Karume halafu apande ghorofa kununua bidhaa ambazo anaweza kuzipata kwa bei nzuri zaidi Kariakoo au Kinondoni?

Hayo majengo ya ghorofa yaliyobatizwa kuwa ni ya machinga yatageuka kuwa maeneo ya watu wengine (wafanya biashara wakubwa) ambao sio walengwa. Au labda hii ni janja ya kutafuka wafadhili wa kujenga jengo kwa jina la machinga huku wahusika wakijua fika kuwa watakaonufaika na mradi ni wateule wachache (ambao sio machinga)?

Kwa maoni yangu, machinga walihitaji eneo zuri/tambarare la wazi linalofikika kirahisi kwa miguu na usafiri wa gari au basi. Pili walihitaji majengo (structures) ya kawaida kabisa ktk usawa wa ardhi (ground level - achana na mambo ya ghorofa, kwa sababu ukishajenga ghorofa mpangaji wako hawezi kuwa machinga tena! Utakuwa umemjengea Patel, Masawe au Mpemba fulani vile!)

Napendekeza mabanda yajengwe kama ifuatavyo (construction method/materials):
- sakafu ya sementi,
-kuta za tofali au mbao ama bati, na
-paa la canvas (tent materials) - yaani turubai ngumu isiyopenyesha maji au bati za kawaida
.

Yaani ni mjengo rahisi (simple), na ujenzi wake ni wa bei nafuu kabisa! Uendeshaji wa majengo haya wangeachiwa machinga wenyewe waratibu. Utaratibu wa kodi za serikali za mtaa ufanywe na mamlaka husika.

Suala la machinga linahitaji suluhisho la haraka, rahisi kutekelezeka na kwa gharama nafuu kwa mamlaka husika na kwa machinga pia.

Uzoefu Zaidi
Ktk mji wa Reading, Uingereza kuna mitaa miwili napenda kuitolea mfano maana inao wafanyabiashara wadogo (wajasiriamali) wanaofanana na machinga. Hosier Street nyuma ya Broad Mall na Broad Street (katikati ya mji.

Pale Broad Street kuna wafanyabiashara ndogondogo wengi sana. Biashara zao ni za kuhamahama siku hadi siku. Wanakuja na vibanda ambavyo vinavutwa na gari dogo na viwekwa katikati ya mtaa na vinabaki hapo hadi jioni vinaondolewa jioni hadi kesho yake tena wanakuja kufanya biashara. Wengine huwa wanasukuma vibanda au vifremu vyao kutoka upande mmoja hadi mwingine kila baada ya dakika chache - kwa hiyo havikai sehemu moja. Nilishawahi kuwauliza baadhi ya wafanyabiashara hao ni jinsi gani wamepata ruhusa kufanya biashara hapo. Waliniambia kupata leseni ya kufanya biashara ya kutembeza vitu ni rahisi sana. Kinachofanyika ni mhusika kwenda kituo cha polisi na kuomba kibali cha kuzungusha biashara yake mtaani hapo au kibali cha kuweka biashara bila kuzungusha. Polisi ndio hutoa kibali cha mfanyabiashara (kuweka kibanda au cha kuzungusha mtaani). Kibali hutolewa kwa muda fulani na muda huo ukiisha mhusika anatakiwa aende kuongeza muda.

Na kuhusu Hosier Street, hapo naweza kupafananisha na 'soko mjinga'. Wafanyabiashara hujenga vibanda vyao kwa vyuma au mbao kisha huvifunika kwa canvass (turubai). Siku zinazoruhusiwa kufanya biashara hapo ni kila Jumatano hadi Jumamos jioni. Siku ya jumamos jioni mabanda yote hubomolewa na kuondolewa na wahusika. Siku ya Jumanne jioni wafanyabiashara hurudi kujenga tena 'mahema' ya vibanda vyao tayari kwa biashara J'5 hadi J'mos. Biashara inayofanyika ni ya mboga za majani, matunda, vifaa vya umeme na elektroniki (mfano simu za mkononi, cd, redio, betri n.k.), mabegi, n.k. Yaani hapo Hosier Street shughuli zake zinafanana kabisa na za machinga wa Tanzania. Hapana majengo ya biashara - pako wazi. Wenye biashara ndio huweka mahema yao popote watakapo kwa muda ulioruhusiwa. Na kuna wakati eneo hilo lilitakiwa kujengwa ofisi za halmashauri ya mji. Somo tunalojifunza hapa ni kuwa watu wa halmashauri waliwaomba wafanyabiashara watoe maoni au ushauri wao kuhusu maeneo ambayo wangependa kuhamishia shughuli zao. Kwa hiyo watu wa serikali za mitaa waliwahusisha wafanyabiashara juu ya mstakabali wao, sio wakubwa kuamua wenyewe maofisini ni wapi pa kuwapeleka au ni nini cha kuwafanyia wafanyabiashara!

Muda wa viongozi kuwapangia wajibu wananchi ulishapitwa na wakati, siku hizi ni enzi za kusikiliza wananchi wanataka kufanya nini na serikali au mamlaka husika wanachofanya ni kuwawezesha wananchi kutimiza azma yao.

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Ghorofa jingine la Wamachinga kujengwa Manispaa ya Temeke

2008-09-10 17:22:29
Na Sharon Sauwa, Temeke


Halamashauri ya Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es Salaam imetoa notisi ya kutoendelezwa kwa maeneo waliyopewa katika soko la TAZARA Vetenary ili kupisha ujenzi wa Jengo la kisasa la wamachinga.

Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Jerome Bwanausi, ameliambia Alasiri kuwa wafanyabiashara hao kuwa hivi sasa, tayari Manispaa hiyo imeshaanza kuandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.

Hata hivyo, akasema bado haijafahamika jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara wangapi na gharama za ujenzi wake zikoje.

Akasema wawekezaji kutoka China wameonyesha nia ya kuingia ubia katika ujenzi wa jengo hilo.

"Tayari Halmashauri ya Temeke imeshatoa notisi kwa wafanyabiashara kutoendeleza maeneo hayo kwa ajili ya kujenga jengo hilo,"akasema Bw. Bwanausi na kuongeza kuwa wawekezaji hao kutoka China wamefika katika eneo hilo na kuliangalia.

Akasema wafanyabiashara ambao watatoka katika eneo hilo watapata nafasi katika jengo la wamachinga linalojengwa Kariakoo na kwamba wale watakaokosa nafasi watapewa kipaumbele katika jengo hilo la Tazara litakapokamilika.

Akasema utaratibu unaandaliwa kwa ajili ya kuwapatia nafasi katika jengo la Kariakoo, ili waweze kuachia nafasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo hilo.

Hivi karibuni kundi la wafanyabiashara 68 kutoka katika soko hilo walielezea kuhusiana na kusimamishiwa kwa ujenzi wa vibanda vya biashara Tazara Vetenary.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Bw. Musa Kitenga, alisema waliiomba manispaa iyo iwapatie nafasi katika soko hilo kwa kipindi kirefu bila kujibiwa na hivyo kulazimika kumuona Diwani wa kata ya Chang'ombe, Bw. Noel Kipangule, ambaye aliuamuru uongozi wa soko kuwapatia nafasi.

Hata hivyo, akasema wakiwa katika ujenzi uongozi wa manispaa ulifika na kuwakataza kuendelea na ujenzi kwasababu diwani hakuwashirikisha katika maamuzi.

Akaiomba Serikali kuwapatia nafasi ya kufanyia biashara ili waweze kufanya shughuli zao na kuweza kujikimu kimaisha.

SOURCE: Alasiri