Friday 5 June 2009

Mwelekeo wa Bajeti ya 2009/10 TZ

Bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha wa 2009/10 inatarajia kupanda kutoka Sh. trilioni 7.2 za mwaka huu hadi Sh. trilioni 9.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 32, ambayo imeainisha maeneo sita ya kipaumbele.

Akifafanua vipaumbele vya bajeti hiyo ambayo inatarajiwa kusomwa Alhamisi ijayo mjini Dodoma, Mkulo alisema:

-kipaumbele cha kwanza ni elimu ambayo imeongezewa fedha kwa asilimia 22 kutoka Sh. trilioni 1.4 ya mwaka 2008/09 hadi Sh. trilioni 1.7 mwaka ujao wa fedha. Lengo la kutenga kiasi hicho cha fedha ni kuimarisha ukaguzi wa elimu kwa ngazi zote nchi nzima.

-kipaumbele cha pili ni miundombinu ambayo bajeti yake imeongezeka kwa asilimia 12.7 ikilinganishwa na mwaka 2008/09. Katika mwaka wa fedha wa 2009/10, Wizara ya Miundombinu imetengewa Sh. trilioni 1.0 ikilinganishwa na bajeti inayomalizika ya Sh. bilioni 973.3. Serikali inatarajia kuboresha barabara, madaraja, bandari, viwanja vya ndege, kuimarisha mashirika ya reli (TAZARA na TRL) na Shirika la Ndege (ATCL).

-kipaumbele cha tatu ni afya ambayo imetengewa Sh. bilioni 963.0 kutoka Sh.bilioni 910.8 mwaka 2008/09. Kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, bajeti itajikita katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za uzazi na mtoto na kuimarisha rasilimali watu katika ngazi zote.

-kipaumbele cha nne ni kilimo ambacho kimeongezewa bajeti kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo bajeti ya wizara hiyo imepanda kutoka Sh. bilioni 513 mwaka unaomalizika hadi Sh. bilioni 666.9 mwaka ujao. Fungu kubwa katika sekta hii linaenda katika kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo za kutosha kwa wakulima na wafugaji. Waziri Mkulo alisema katika kutekeleza kaulimbiu ya 'Kilimo Kwanza', serikali itaweka msukumo katika uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo, viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

-kipaumbele cha tano ni Wizara ya Maji ambayo imetengewa Sh. bilioni 347.3 mwaka huu kutoka Sh. bilioni 231.6 mwaka 2008/09. Hii ndiyo Wizara iliyoongezewa bajeti inayokaribia kufikia asilimia 50. Kipaumbele katika sekta ya maji ni kuboresha upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida na umwagiliaji.

-kipaumbele cha sita ni Wizara ya Nishati na Madini ambayo hata hivyo, bajeti yake imeporomoka kwa asilimia 24.6 kutoka Sh. bilioni 378.8 mwaka huu hadi Sh. bilioni 285.5 mwaka ujao. Akifafanua sababu za bajeti ya Wizara hiyo kushuka, Waziri Mkulo alisema ni kutokana na kumalizika kwa mikataba ya kuzalisha umeme kwa makampuni matatu ya kukodi ambayo ni Dowans, Alstom Power Rental (APR) na Aggreko. Alisema kipaumbele cha Wizara kwa mwaka 2009/10 ni kuhakikisha upatikanaji wa umeme mijini na vijijini. Hata hivyo, alisema theluthi moja ya bajeti hiyo inatarajiwa kutoka kwa wafadhili.


CHANZO: NIPASHE 05-june-2009

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Akiwasilisha mfumo wa mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2009/2010 kwa kamati ya Uchumi na Fedha ya Bunge jana, Mkulo alisema serikali imepanga kukusanya Sh. trilioni 5.1 kutokana na vyanzo vya ndani, Sh trilioni 3.2 ni misaada na mikopo kutoka kwa wahisani na Sh trilioni 1.2 ni mapato mengine ambayo yatatoka katika halmashauri, mauzo ya hisa na mikopo ya ndani.

Katika bajeti hiyo matumizi ya kawaida ni Sh trilioni 6.68 na ya maendeleo ni Sh trilioni 2.82. Kutokana takwimu hizo, bajeti ya maendeleo katika sekta mbalimbali itategemea ahadi za wahisani na mikopo ya taasisi za nje.

Alisema mapato ya halmashauri ambayo sasa yamehamishiwa mfuko mkuu Hazina ni Sh. bilioni 138, mapato kutokana na mauzo ya hisa Sh. bilioni 15 na mikopo ya ndani Sh. trilioni 1.08.

Kwa mujibu wa Mkulo, makadirio ya makusanyo ya serikali kwa mwaka huu ni Sh trilioni 5.1 sawa na asilimia 16.4 ya pato la taifa ikilinganishwa na makadirio ya asilimia 15.9 ya mwaka huu.

Hata hivyo, makadirio ya mwaka jana yamefanikiwa kwa asilimia 90 ambapo serikali ilipanga kukusanya Sh. trilioni 4.7, lakini ilifanikiwa kukusanya Sh. trilioni 4.2 hadi Machi mwaka huu.

Mkulo alisema ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato ya mwaka ujao, Serikali inakusudia kuanzisha vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha na kudhibiti makusanyo na kupunguza misamaha ya kodi. Vilevile, kwa mara ya kwanza, Serikali itajumuisha mapato ya serikali za mitaa kwenye Bajeti Kuu.

Katika mikopo ya ndani, Serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 1.08 ambazo Sh. bilioni 576.4 zitagharimia dhamana zilizoiva wakati Sh bilioni 506.1 zitatumika katika matumizi ya kawaida.

Alisema bajeti ijayo pia inalenga kuendelea kupeleka madaraka kwa wananchi, maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao na maandalizi ya sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2012.

Mkulo aliongeza kwamba ili kufanikisha azma hiyo, serikali itatafuta mikopo zaidi kutoka kwa mashirika ya kimataifa yakiwemo mashirika ya nchi za Saudi Arabia na Kuwait ambazo zimeonyesha nia ya kuisaidia serikali.

Alisema kuwa katika mwaka ujao wa fedha, serikali itafanikisha uanzishwaji wa benki ya kilimo, kuongeza kima cha chini cha pensheni, kuongeza na kuboresha mitaji ya benki za umma, kugharimia maandalizi ya kurejesha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kupunguza madeni ya mashirika ya umma.

Kwa mara ya kwanza, serikali itasoma bajeti yenye kaulimbiu ambapo mwaka huu, kaulimbiu ya bajeti inasema 'Kilimo Kwanza'.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliochangia mfumo huo wa bajeti walisema haijazingatia usawa hasa kwa kupanga kutumia fedha nyingi kuliko mapato.


chanzo: gazeti Nipashe 05/jun/2009

MOSONGA RAPHAEL said...

Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), alisema miaka yote serikali imekuwa ikipandisha bajeti bila kufanya tathmini ya maisha ya wananchi.

Naye Mbunge wa Busega (CCM), Dk. Rafael Chegeni, alisema Bunge haliwezi kupitisha bajeti hiyo kwa sababu kuna upendeleo mkubwa katika kupanga fedha za kujenga barabara.

Alionya kwamba iwapo serikali itaiwasilisha ilivyo Bunge linaweza kuvunjika.

Mbunge wa Ilemela (CCM) Antony Diallo, alisema Bunge halitaweza kupitisha bajeti hiyo kwa maelezo kuwa inampendelea Rais, Waziri wa Fedha, Waziri wa Miundombinu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Dk. Abdallah Kigoda kwani barabara za kwao ndizo zimetengewa fedha.



Mtazamo wa bajeti ya mwaka jana

Katika bajeti ya mwaka 2008/09 serikali ilikusudia kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua Sh. trilioni 4.7 sawa na asilimia 18.5 ya Pato la Taifa, lakini kwa kipindi cha Julai, 2008 hadi Machi 2009 serikali imekusanya Sh. trilioni 3.2 hivyo kumekuwa na upungufu wa Sh. bilioni 330 ikilinganishwa na lengo.



Mikopo ya ndani

Serikali iliuza dhamana na hatifungani zake zenye thamani ya Sh. bilioni 559 ambazo zililipia dhamana zilizokuwa zimeiva na kusaidia ujazi wa fedha.

Vilevile, Serikali pia imeongeza akiba yake Benki Kuu (BoT) hadi Sh. bilioni 186.8



Misaada na Mikopo

Misaada na mikopo kutoka kwa wahisani kwa mwaka 2008/09 ilikuwa Sh. bilioni 940.6 ambazo ni asilimia 116 ikilinganishwa na makadirio ya awali ya Sh. bilioni 812.1. Misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Julai 2008 hadi Machi 2009 ilikuwa Sh. bilioni 926.6.



Matumizi ya serikali

Matumizi kwa kipindi cha Julai 2008 hadi Machi 2009 ni Sh. trilioni 4.7 sawa na asilimia 88 ya makadirio ya Sh. trilioni 5.4. Katika kiasi hicho, trilioni 3.1 zimetumika katika matumizi ya kawaida wakati Sh. trilioni 1.6 ni matumizi ya maendeleo.

Mishahara ya watumishi wa serikali kuanzia Julai 2008 hadi Machi 2009 ni Sh. trilioni 1.24 sawa na asilimia 102 ya makadirio ya trilioni 1.21.



Malipo ya riba

Malipo ya riba kwa madeni ya ndani ni Sh. bilioni 144 sawa na asilimia 106 ya lengo la kulipa Sh bilioni 153.5.

Riba kwa madeni ya nje ni Sh. bilioni 24.3 sawa na asilimia 106 ya makadirio.

Madeni mengine Sh biloni 284 sawa na asilimia 106 ya lengo.


chanzo:
gazeti - NIPASHE, 05/juni/2009