Saturday 6 June 2009

Jicho la 3: "Kimbelembele"

Na tuwe wakweli: Hakuna jambo kubwa lililofanyika katika historia ya dunia bila kusimamiwa na watu ambao wangeweza kusemwa kwamba wana ‘kimbelembele’.

Hatari ya kujitokeza na kuchukua nafasi ya mbele katika jambo lo lote ina zahma zake, kama ambavyo historia inatufunza.

Yesu Kristo asingewambwa msalabani kama angetulia Nazareti akatengeneza vitanda vya samadari akawauzia wakoloni wa Kirumi.

Patrice Lumumba asingechinjwa na kuyeyushwa katika mapipa ya tindikali kama angekubali ubeberu ufanye unavyotaka nchini Kongo, wala Nelson Mandela asingefungwa kwa miongo mitatu kama angekubali kwamba ni ada ya mtu mweusi kumtumikia mtu mweupe.

Wote hawa walikuwa ni watu wa ‘kimbelembele’ cha aina fulani, ‘kimbelembele’ kilichowasukuma na kuwaweka mbele ya wenzao, wakati mwingine bila hata kujua kwamba walikuwa wamesimama mbele, wanaonekana, na kwa hiyo ni mabango ya shabaha.

Issa Shivji angeweza akabakia katika taaluma ya uwakili na akatengeneza ‘vijisenti’ vya kutosha na akaendesha gari linalofanana na la profesa wa kisasa (achana na magari ya akina Calculus). Lakini amejitokeza, akasimama mbele katika masuala kadhaa. Ana kimbelembele.

Masoud Kipanya angeweza akachora picha za ndege wanafurahi angani, au jua linakuchwa magharibi mwa Kigoma na zikampa utajiri mkubwa kutoka kwa watalii na Wazungu waliopotea njia. Asingekuwa kiongozi bali angekuwa mchoraji tajiri, kwa sababu angekuwa amekosa kimbelembele.

Lakini Kipanya ni kiongozi kwa sababu amesukumwa na kimbelembele kitakatifu kutumia sanaa yake kujenga demokrasia na jamii iliyo bora nchini mwake. Ni kiongozi.

Filbert Bayi (Christchurch, 1974) angeweza akabaki ndani ya kundi kubwa la wakimbiaji, asichukue ‘risk’ ya kujitanguliza na kujifanya shabaha, na akamwachia John Walker ashinde mbio zile, rekodi ya dunia isingevunjwa siku hiyo.

Alichofanya Bayi ni kwamba mara aliposikia mlio wa bunduki, aliruka na kwenda mbele ya kila mtu, na akabakia mbele hadi mwisho wa mbio hizo. Kimbelembele chake kikaleta sifa ambayo haijawahi kuletwa na mtu mwingine nchini Tanzania.

Naam, kiongozi hana budi kuwa na kimbelembele!



source: raia mwema (rai ya jenerali)

No comments: