Tuesday, 9 June 2009

'Bunge lafupishwa': Ni kama nilivyoshauri!

Naipongeza serikali na vyombo husika kwa kujali maslahi ya Taifa kwa uamuzi wao wa kufupisha kikao cha Bunge la Bajeti.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, kikao kimeanza leo tarehe 09 hadi mwezi wa Julai mwishoni. Bajeti ya serikali itasomwa Bungeni tarehe 11.Juni.2009.

Itakumbukwa hivi karibuni nilitoa wito kuhusu kufupishwa kwa kikao hiki. Kwa hiyo uamuzi huu wa kulifupisha Bunge umenifurahisha mimi binafsi hasa kwa kuona kuwa serikali inasikiliza na kujali maoni ya wananchi! (ujiko!)

Ufuatao ni wito wangu nilioutoa tarehe 09/Mei/2009 kuhusu kikao cha Bunge la Bajeti 2009/10:

Saturday, 9 May 2009
Hali ngumu ya Uchumi: Bunge lifupishwe
Bunge la Jamhuri ya Muungano liko mbioni kukutana ktk marathoni ya vikao vya kujadili na kupitisha bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2009/10.

Kama wote tujuavyo, hiki ni kipindi kigumu sana kiuchumi duniani kote. Ni vizuri viongozi wetu na wawakilishi wetu wakazingatia hali tuliyonayo na kuchukua hatua za kusaidia kupunguza makali ya uchumi.

Mojawapo ya hatua za kuchukua ambazo ziko ndani ya uwezo wetu ni kufupisha urefu wa vikao vya Bunge. Kwa kawaida vikao vya bajeti huchukua miezi miwili (Juni hadi Agosti kila mwaka).

Napendekeza kwa waandaaji wa ratiba za
1. hotuba za mawaziri kuwasilisha bajeti na
2. muda wa waheshimiwa wabunge kujadili bajeti hizo,
zifupishwe kwa asilimia 10 au zaidi.

Hotuba kuu ya waziri wa fedha na wa mipango kuhusu hali ya uchumi wa nchi ndizo zipewe muda wa kawaida, lakini hotuba zote za wizara zinazofuata zifupishwe kama nilivyopendekeza kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.

Haitakuwa uamuzi wa busara kutumia gharama kubwa kuendesha vikao wakati huduma muhimu kwa wananchi zinayumba kwa kukosa fedha za kuziendesha. Kama wananchi wanaambiwa wafunge mikanda kila siku, inakuwaje wakubwa waendelee kulegeza ya kwao?

Kila mtanzania ana wajibu wa kubana matumizi ktk nafasi yake aliyoko, na nyie wawakilishi wetu fanyeni vivyo hivyo!


(source: mosonga blog; Saturday, 9 May 2009)

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

16th Session of Parliament to start in Dodoma

Dodoma , 4 June 2009

The legislators will meet in Dodoma from 9th June 2009 for the Budget session.

The 16th Session of Parliament is expected to continue up to the end of July.

The Finance Minister, Hon. Mustafa Mkullo,MP is expected to deliver a budget speech on the 11th June 2009 and thereafter Members of Parliament will debate on the budget of the next fiscal year.

Each Ministry will in due course present their budget for 2009/10 to the legislators for discussions in House.


source: www.parliament.go.tz

MOSONGA RAPHAEL said...

Uamuzi huu wa Serikali wastahili pongezi


KIKAO cha bajeti cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kilianza jana Jumanne, mjini Dodoma. Kwamba safari hii kikao hicho kitachukua mwezi mmoja na wiki tatu tu kumalizika badala ya miezi mitatu, ni kitu cha kufurahisha.

Ni kwa msingi huo tunapenda kuipongeza Serikali yetu na Bunge letu, kwa kuchukua hatua hiyo ya kupunguza siku za kikao cha bajeti; hatua ambayo wananchi wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.

Tunatambua kwamba hatua hiyo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kupunguza matumizi katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia umeporomoka. Ni matarajio yetu, hata hivyo, kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua nyingine za kubana matumizi katika sekta nyingine.

Ni matarajio yetu vilevile kwamba kupunguzwa kwa siku za kikao hicho cha bajeti, hakutapunguza umakini wa Bunge letu; na kwamba wabunge wetu hawatatumia hatua hiyo kama kisingizio cha kutojadili vyema bajeti za wizara wakianzia na bajeti yenyewe ya Serikali.

Keshokutwa (Ijumaa) Serikali itawasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2009/2010. Ni jukumu la wabunge kuhakikisha bajeti hiyo inaendana na hali ya sasa ya anguko la uchumi wa dunia; kwa maana kwamba kila senti inakwenda tu katika matumizi ambayo ni ya lazima.

Ni wajibu wa wabunge wetu kuisoma kwa makini bajeti hiyo ya Serikali na kuichambua ili wajiridhishe kama kweli inaweza kutuvusha katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia. Na kama hawaridhiki nayo, basi, ni wajibu wao kuionyesha Serikali mapengo yanayostahili kuzibwa katika bajeti hiyo.

Kwa ufupi, wananchi wanatarajia, safari hii, kuuona umakini wa wabunge wao katika kuijadili bajeti ya Serikali yao kuliko ilivyopata kuwa tangu waingie bungeni miaka minne iliyopita.

Tunatarajia kwamba, kwa mara ya kwanza, wabunge wetu wataweka siasa za vyama pembeni na kujadili kwa umakini bajeti hiyo ambayo, kwa kiasi kikubwa, inaamua mustakabali wa Taifa letu katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia.

Hatutarajii kuwaona baadhi yao wakisinzia bungeni wakati wa kuwasilishwa bajeti hiyo na wakati wa kujadiliwa. Tunatarajia kuona Bunge lililo hai kweli kweli lililosheheni wabunge wenye hoja nzito za kuisaidia Serikali namna ya kuwavusha Watanzania masikini katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa dunia. Kila la heri.chanzo: Raia Mwema. Juni 10, 2009
Na John Bwire