Thursday, 2 April 2009

Rais Kikwete na mgao wa umeme Dar

Thu. April 02, 2009

Hali ya Upatikanaji wa Umeme Nchini
Ndugu Wananchi,Kwa takriban miezi mwili sasa umeme umekuwa gumzo kubwa hapa nchini. Mjadala umekuwa wa namna mbili.

Kwanza umehusu nia ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kununua mitambo ya Kampuni ya Dowans pale Ubungo.

Na, pili, umehusu mgao wa umeme unaoendelea tangu tarehe 26 Machi, 2009 mpaka sasa hasa hapa Dar es Salaam na wilaya jirani.

Mgao wa Umeme
Ndugu Wananchi,Kiini cha kuwepo kwa mgao wa umeme ni kuharibika kwa mitambo miwili ya kuzalisha MW 53 za umeme katika kituo cha kuzalisha umeme cha SONGAS. Jumamosi tarehe 28 Machi, 2009 mtambo mmoja wenye uwezo wa kuzalisha MW 20 ulitengemaa hivyo upungufu umebaki MW 33 kutoka kwenye mashine ya pili.

Taarifa niliyopewa leo ni kuwa hitilafu yake ni kubwa hivyo huenda ikachukua mpaka wiki mbili au tatu au zaidi kutengemaa. Maana yake ni kwamba mgao utaendelea kuwepo kwa kipindi hicho.

Hivyo, Ndugu zangu, mgao huu hauna uhusiano na ile hadhari aliyoitoa Dkt. Idris Rashid, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alipokuwa akizungumzia suala la Dowans kuwa nchi inaweza kuingia kwenye giza siku za usoni.

Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa wataalamu wa TANESCO, mfumo wetu wa umeme nchini, kwa sasa, hauna ziada ya umeme unaosubiri kutumika kama akiba. Kutokana na hali hiyo, kunapotokea upungufu wowote wa uzalishaji wa umeme kwa sababu yoyote ile, kama huu uliotokea tarehe 26 Machi, 2009, husababisha kuwepo kwa mgao wa umeme kwa watumiaji.

Umeme wote unaozalishwa hapa nchini hutumika na wala mahitaji halisi hayajatoshelezwa. Kimsingi umeme unaopatikana na kutumika ni chini ya mahitaji (supressed demand). Ni asilimia 14 tu ya Watanzania ndiyo wanaopata na kutumia umeme wakati watu wengi sana wanaohitaji umeme bado hawajapata.

Ndugu Wananchi;
Wakati wote Serikali kwa kushirikiana na TANESCO imekuwa na mipango ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini. Kwa upande wa uzalishaji kumekuwepo hata na ratiba ya lini, kituo kipi na cha ukubwa gani kinaratajiwa kuwepo. Utekelezaji wa mipango hiyo ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo sasa.

Mwaka 2007, kufuatia matatizo makubwa ya umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji, mpango huo ukaboreshwa na kuongezwa ujenzi wa vituo vya kutumia gesi asilia na makaa ya mawe. Utekelezaji wa mpango wa uzalishaji wa umeme kwa mujibu wa uboreshaji uliofanywa mwaka 2007 uko nyuma ya wakati. Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe Kiwira umechelewa kwa sababu ya ugumu wa kupata mikopo kutoka kwenye vyombo vya fedha. Kiini cha tatizo ni hofu inayotokana na taarifa hasi kuhusu mradi huo. Mradi wa kuzalisha megawati 300 kutokana na gesi asilimia ya Mnazi Bay unacheleweshwa na matatizo ya sasa ya kudorora kwa uchumi wa dunia ambapo nimeambiwa kwamba wabia muhimu wamejitoa kwa sasa.

Ndugu Wananchi,
Kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo ni dalili kuwa baada ya muda si mrefu hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa mbaya hata kama mitambo yote ya sasa itakuwa inafanya kazi kwa ukamilifu. Kwa sasa mahitaji yanaongezeka kwa asilimia 10 – 15 kwa mwaka. Hili ni ongezeko kubwa sana ambalo linahitaji kusiwepo kukwama kokote. Kwa nia ya kutaka kupunguza makali ya tatizo hilo, ndipo uongozi wa TANESCO ukaona waombe kununua mitambo ya Dowans ambayo wakati huo ilikuwa inatangazwa kuuzwa. Uamuzi huo ukazua mtafaruku mkubwa ambao sina haja ya kuelezea kwa kirefu kwani wengi wetu tunaufahamu vizuri. Baada ya kuona ugumu wa kuendelea na nia hiyo, uongozi wa TANESCO umechukua uamuzi wa kuachana na nia yao hiyo.

Ndugu Wananchi;
Katika taarifa yake ya kutamka uamuzi wa kuachana na nia ya kununua mitambo ya Dowans, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alielezea hofu yake kwamba uamuzi huo unaweza kusababisha nchi kuwa gizani hapo baadaye. Taarifa hiyo imeleta hofu kubwa katika jamii. Nataka kuwatoa hofu na kuwahakikishia Watanzania wenzangu wote kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa nchi yetu haifikii hatua hiyo. Tutahakikisha kuwa nchi haiwi gizani na kwamba umeme wa ziada unaotakiwa utapatikana na shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma zitaendelea kama kawaida.

Ndugu Wananchi;
Tayari Wizara ya Nishati na Madini imeshaanza kuchukua hatua ambazo zinaonesha kuwa na mwelekeo wa kutia matumaini. Naamini tutafanikiwa. Tukiwa tayari, taarifa itatolewa. Penye nia pana njia.

Napenda kutumia nafasi hii kusema mambo mawili.

Kwanza, kwamba, nawapongeza viongozi wa TANESCO kwa uamuzi wao wa busara wa kuachana na nia yao ya kununua mitambo ya Dowans. Wameyasoma vizuri mazingira na nyakati na kufanya uamuzi muafaka.

Pili, niwaombe wanasiasa wenzangu kuwa, maadam waliokuwa na nia ya kununua mitambo hiyo hawanayo tena, suala hili limemalizika.

Sioni sababu ya kuendelea kulumbana, kutiana vidole machoni na kutoleana maneno makali na mengine hata hayastahili kusemwa. Tumekuwa tunawatia hofu wananchi kwa jambo lisilokuwepo tena. Nawaomba muzihifadhi nguvu zenu na bongo zenu ili muwafanyie wananchi mambo yenye tija kwao. Wanalo jukumu kubwa la kujiletea maendeleo kwa lengo la kujiondoa kwenye umaskini na kuwa na hali bora ya maisha yao.
Uongozi wetu wanasiasa unahitajika sana katika juhudi zao hizo. Tuelekeze nguvu zetu na maarifa yetu huko. Wapeni pumzi wananchi kutokana na malumbano haya.


(hotuba ya Rais, 31/march/2009)

No comments: