Friday 30 January 2009

Hii ni kashfa?

Sakata la kuhusu kuingiliwa kwa mchakato wa kumpata mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa linabidi lishughulikiwe mapema ili kuepusha hasara kwa Taifa (au kuupata ukweli).

Serikali au vyombo husika visipende kusubiri makosa yatendeke ndipo tuwashughulikie wahusika. Detection rate inatakiwa kuongezeka, na ndio maana kuna watu wa TAKUKURU na Usalama wa Taifa ktk vyombo mbalimbali. Ndio maana mimi natoa wito kuwa tuwatumie ipasavyo hawa watu (Takukuru na usalama) ili kuepusha hasara zinazoweza kuepukika.

Kumbuka: kinga ni bora kuliko tiba.

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

...Maswali 10 kwa Masha
1.Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, majibu ya wazabuni walioingia hatua ya pili ya mchakato wa kupata kazi ya kutengeneza vitambulisho vya taifa hayajatolewa kwa wahusika Je, kampuni ya Sagem Securite ilijua vipi imeenguliwa hadi kulalamika kwa Waziri Masha?

2.Hadi sasa taarifa zinasema si Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wala Bodi ya Zabuni, waliopewa nakala ya barua ya malalamiko ya Sagem Securite, kwa hali hii ni Waziri pekee mwenye barua hiyo, Je, ni halali kukalia barua na kulalamika tu bila kuonyesha vyombo husika?

3.Kwa nini Sagem Securite walilalamika kwa Waziri tu na si kwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani na nakala ya malalamiko kupelekwa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) kama maelekezo ya zabuni yalivyoonyesha?

4. Kwa nini hata pale Waziri Masha ambaye ni mwanasheria mahiri alipopata malalamiko ya Sagem Securite hakuwaelekeza pa kwenda kwa mujibu wa sheria ya PPRA, badala yake aliamua kuchukua jukumu hilo kwa niaba ya mzabuni?

5.Sheria ya PPRA haitoi fursa ya kulalamika kuhusu zabuni kama vyombo vyote vinavyohusika katika kupitia mchakato wa zabuni ya umma vitakubaliana kwa mujibu wa sheria je, ni kwa nini Waziri Masha alijitokeza na kumtaka Katibu Mkuu wake aombe maelekezo PPRA wakati bodi ya zabuni hakutofautina?

6.Uchunguzi wetu umeonyesha wazi kwamba vyombo kadhaa vya usalama wa nchi vilishiriki katika mchakato wa zabuni hiyo ambavyo ni Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) tangu hatua ya awali, je, malalamiko ya Masha ya kutokukubalina na maamuzi ya bodi ni kielelezo cha kukosa imani na vyombo hivyo na kwamba yeye peke yake ndiye anayeona hitilafu katika mchakato huu?

7.Waziri Masha anadai kulalamikiwa na Sergen Securite, inakuwaje anataka hata makampuni ambayo hayajalalamika rasmi kwake yarejeshwe kwenye mchakato wa zabuni?

8. Kwa nini Waziri Masha hakumweleza Waziri Mkuu ukweli wote kuhusu kampuni ya Sagem Securite hata baada ya kuelezwa na bodi ya zabuni, ni kwa nini pia hakuwa na ujasiri wa kumwona Katibu Mkuu Kiongozi kujua sababu za kumwagiza Katibu Mkuu wake aendelee na mchakato wa zabuni, ni nguvu gani inamsukuma kushindwa kuona yote haya?

9. Kwa nini Waziri Masha ameamua kumpuuza Katibu Mkuu wake, kwa nini hataki afanye kazi kama mtendaji na anamshinikiza kisiasa, je, anataka kuwa msimamizi wa sera na mtendaji kwa wakati mmoja?

10.Waziri Masha anataka kuwaambia Watanzania kwamba mchakato mzima wa zabuni ya vitambulisho vya taifa una utapeli, rushwa na kwa maana hiyo ufutwe kwa sababu tu kampuni ya Sagem Securite imeenguliwa kwenye zabuni?

Watanzania wangependa kusikia majibu ya Masha ingawa amekwisha kusema kwamba hawezi kuzungumzia barua aliyomwandikia Waziri Mkuu wala uingiliaji wake mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa kwa sababu anatekeleza kazi za Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

SOURCE: Nipashe, 2009-01-30 10:46:38
Na Boniface Luhanga, Dodoma

MOSONGA RAPHAEL said...

Kampuni anayoibeba Masha ni balaa tupu

Kampuni ya Sagem Securite ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha anadaiwa kuibeba katika mchakato wa kupata mzabuni wa kutekeleza Mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambao utaigharimu serikali kiasi cha Sh. bilioni 200, kama ni sawa na iliyoomba kazi ya aina hiyo nchini Nigeria mwaka 2003 ni ya hatari.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, kampuni hiyo, ikijiita Sagem Securite iliwatia matatani mawaziri watatu wa serikali ya Nigeria wakati huo ikiongozwa na Rais Olusegun Obasanjo, kutokana na kudaiwa kuwahonga mawaziri hao kiasi cha Dola za Marekani milioni 2.

Hongo hiyo ilidaiwa kutolewa kama kishawishi kwa viongozi hao ili waibebe katika zabuni ya kutengeneza vitambulisho vya kitaifa vilivyokuwa viliigharimu nchi hiyo kiasi cha Dola za Marekani milioni 214.

Mradi huo unafanana na ambao serikali ya Tanzania inataka kuanzisha wa kutengeneza vitambulisho vya taifa ambao utagharimu taifa Sh. bilioni 200 (sawa na Dola za Marekani milioni 150).

Rais Obasanjo kwa kukasirishwa na uroho wa wasaidizi wake, alimfuta kazi Waziri wa Kazi na Uzalishaji wa nchi hiyo, Hussaini Akwanga.

Akwanga alidaiwa kutenda kosa hilo akishikilia wadhifa wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Nchi ya Nigeria.

Chanzo hicho kilisema kuwa Rais Obasanjo alichukua hatua hiyo wakati uchunguzi wa kashfa hiyo ukiendelea, lengo likiwa ni kupiga vita rushwa kwa watumishi wa umma.
Wakati akimfukuza kazi Akwanga, Rais Obasanjo alisema Waziri huyo, alilidhalilisha taifa.

Waziri huyo na wenzake watano walifunguliwa mashtaka mahakamani kwa makosa 16 yanayohusiana na sakata hilo, linalokadiriwa kusababisha hasara ya Dola za Marekani milioni 214 sawa na Sh. 300 bilioni. Waliofikishwa kortini walidaiwa kula rushwa ya Dola za Marekani milioni mbili.

Walioshtakiwa pamoja na Akwanga, na nyadhifa walizokuwa nazo kwenye mabano ni Turi Akerele (Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani), Dk. Okwesilieze Nwodo (Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha Peoples Democratic Party), Dk. Mohammed Shatta (Waziri wa Nchi wa Mambo ya Ndani) na Sunday Afolabi aliyweahi kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo.

Afolab alishtakiwa kwa kupokea Dola za Marekani 330,000, Akwanga alimuwezesha binti yake kupokea Dola za Marekani 30,000 kwa niaba yake.

Mwakilishi wa kampuni hiyo nchini Nigeria ndiye aliyedaiwa kutoa rushwa hiyo akishirikiana na Nwodo na Akerele alipokea Dola za Marekani 500,000.

Kampuni hiyo ikielezwa kuhusika na kashfa hiyo kuhusu vitambulisho vya taifa nchini Nigeria, jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alithibitishia Bunge kwamba Waziri Masha alimwandikia barua pamoja na mambo mengine akimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi kuingilia wizara yake bila kumuhusisha katika mchakato wa zabuni ya vitambulisho hivyo.

Akijibu mwaswali ya papo kwa papo bungeni, Pinda alisema taarifa hizo ni kweli kwa kuwa kuna nyaraka zimenyofolewa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.

``Hilo ni kweli kabisa, maana kuna watu wamenyofoa folio pale Wizara ya Mambo ya Ndani,`` alisema Pinda alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, aliyetaka kujua sababu za Waziri Masha kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa kinyume cha sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watu wavute subira ili mchakato huo ukamilike kwanza ndipo mwenye kutaka kuhoji afanye hivyo.

``Mheshimiwa Slaa umetuwahi, lakini jambo hili linafanyiwa kazi. Ingekuwa ni vizuri ukasubiri mpaka mchakato umalize ulete madai kama haya ingesaidia sana,`` alisema Pinda, na kuongeza:

``Mchakato huu haujafika mwisho. Tusubiri halafu tutamhukumu Waziri ukikamilika.``

Hata hivyo, ilibidi Spika, Samuel Sitta, alilazimika kuingilia kati kwa kuyakataa baadhi ya maswali yaliyoelekezwa kwa Waziri Mkuu na Dk Slaa kutokana na kuonekana kwamba baadhi ya wabunge walionekana kuleta malumbano na Pinda.

``Nadhani tukitumia kipindi hiki kulumbana na Waziri Mkuu, si sahihi Ukipata `facts` na we uliza ufafanuliwe `facts` na siyo kuleta malumbano na kung`ang`ani kile unachodhani wewe ni sahihi,`` alisema Spika Sitta.

Alimshauri Dk. Slaa kutumia njia nyingine ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi kama hakuridhika na majibu aliyopewa na Waziri Mkuu ili kutoa fursa ya kujadiliwa na wabunge wengi zaidi.

Naye Joseph Mwendapole anaripoti kuwa Dk Slaa, amesema anaandaa hoja binafsi kwa ajili ya kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, awajibishwe kwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kutengeneza vitambulisho vya taifa.

Akizungumza na Nipashe jana, Dk. Slaa alisema anashangaa kuona Waziri Masha akiingilia shughuli ambayo anajua fika kuwa hana mamlaka nayo kisheria.

Alisema anashangazwa na hatua ya Waziri Masha kuandika barua ya malalamiko kwa Waziri Mkuu kutetea kampuni ya Sagem Securite iliyoomba zabuni ya kutengeneza vitambulisho hivyo.

Waziri Masha anadaiwa kuitetea kampuni hiyo baada ya Bodi ya Zabuni ya Wizara hiyo kuiengua katika mchakato wa kuwania zabuni hiyo.

Dk. Slaa alisema Masha kama angeona kuna taratibu zimekiukwa alipaswa kumwelekeza mlalamikaji (Sagem Securite), hatua za kuchukua kuwasilisha malalamiko badala ya yeye (Masha) kulalamika kwa niaba ya kampuni hiyo.

``Mchakato wa zabuni hii una usiri na mashaka sana...na mashaka haya yanadhihirishwa na waziri ndani ya serikali kulalamika kwa niaba ya kampuni iliyoomba zabuni,`` alisema na kuongeza kuwa Waziri hana mamlaka ya kuingilia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya zabuni.

Aidha, alisema kama Waziri alikuwa na mashaka na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya zabuni, alipaswa kuielekeza kampuni ya Sagem kwenda kulalamika kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Zabuni (PPRA) na si yeye kulalamika.

``Kama kulikuwa na malalamiko, PPRA ndiyo ilipaswa kuchunguza na kutoa jibu kama kuna sheria au taratibu imekiukwa au la, sasa yeye anakimbilia kwa Waziri Mkuu kufanya nini na ana maslahi gani na kampuni hiyo?`` alihoji Dk. Slaa na kuongeza kuwa Masha ni mwanasheria na alijua fika kuwa anachokifanya ni kinyume cha sheria.

Alisema atakapokamilisha hoja yake hiyo ataiwasilisha kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge ambayo ndiyo ina mamlaka ya kupanga siku ya kusikilizwa kwa hoja hiyo.

Alisema inashangaza kuona mabilioni ya fedha za umma zikizidi kuyeyuka katika mchakato usio na mwisho, lakini hakuna anayewajibishwa.

Dk. Slaa alipinga kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa jana bungeni kuwa mchakato wa zabuni hiyo unaendelea kwa kuwa sasa umesimama.

``Nitaomba kama haya yanayosemwa juu ya Masha ni kweli basi awajibishwe kwa kuwa kila anayekiuka Sheria lazima achukuliwe hatua za kisheria,`` alisema.

Masha anadaiwa kufanya hivyo akidai kutoridhishwa na hali halisi ya mchakato huo kabla hata matokeo ya kupatikana mzabuni hayajatangazwa.

Kampuni hiyo, ni kati ya makampuni 54 yaliyoomba kupewa zabuni hiyo. Ilienguliwa katika mchujo wa tatu, baada ya mchujo wa kwanza kuyaengua makampuni 33 na kubaki 21 na mchujo wa pili, kuyaengua makampuni 13 na kubaki manane.

Wajumbe wanaounda bodi hiyo, ni wanatoka Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Zimamoto na Uokoaji, Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

SOURCE: Nipashe, 2009-01-30 10:49:51
Na Waandishi Wetu