Thursday, 29 January 2009

Barabara za zege Dar ni kiini-macho!!

Ule mradi wa mabasi ya abiria yaendeyo kwa kasi Dar tayari umeanza kunukia. Kuna barabara za zege zinatarajiwa kujengwa kwa ajili ya mabasi hayo.
Ninavyoelewa ujenzi wa kutumia zege hujumuisha pia nondo, kokoto ndogo na kubwa pamoja sementi na mchanga (na maji pia).

Wasiwasi wangu ni kuwa hilo zege likishamwagwa na kukauka kuna matatizo yakayofuata huko mbeleni. Kwa mfano vitu kama upitishaji wa miundombinu mbalimbali kama mabomba ya maji, simu, TV cables, umeme n.k. utasababisha nondo na zege kufumuliwa na hivyo kuathiri uimara na uzuri wa barabara hizo. Tumekuwa tukiona mara kwa mara pale ujenzi wa barabara unapokamilika na watu wengine wanaanza tene kuichimba na kupitisha mabomba au nyaya.

Kwa maoni yangu hakuna haja ya kujenga kwa zege kwani hata barabara za lami hudumu kwa muda mrefu tu. Nitatoa mfano wa kipande cha barabara kati ya Magomeni Mapipa na Faya (Fire) jijini Dar ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 20 sasa kwani ilifunguliwa mwaka 1986 na Waziri Mkuu wa wakati huo Dr. Salim Ahmed Salim. Barabara hii bado ni nzuri tu. Hawa jamaa wa mradi huu wanasema eti zege litadumu kwa muda wa miaka 20 kulinganisha na lami (miaka 5 hadi 9) -hii sio kweli. Hata barabara ya Port Access (sasa Nelson Mandela) imedumu kwa zaidi ya miaka 20!!. Ningependa kuona wahandisi wazawa wanatoa maoni yao juu ya hili, usije ukawa ni mwanya wa wachache kujipatia pesa zaidi na kutuacha Watanzania katika deni kubwa huko mbeleni.

Miradi ya magari ya abiria sio migeni duniani. Uingereza kila mji una mabasi ya abiria na barabara zinazotumika ni za lami kama kawaida tu. Na abiria wanapata huduma nzuri. Ni kwa nini Tanzania ionekane kama wavumbuzi wa mabasi ya abiria. Eti wanatumia lugha 'yaendayo kasi', kwani mji wa Dar una ukubwa gani wa kujitaji magari yaendayo kasi ya risasi?

Watanzania tuziuzwe au kudanganywa kirejareja namna hii. Hamna jipya hapo, wanatumia hayo maneno 'yaendayo kasi' kama kiini macho tu na kuongeza bili kwa taifa letu. Sisi tunahitaji mradi wa mabasi ya abiria (Full Stop). Mji wa Dar ni mdogo sana, na mabasi ya kawaida yanatosha sana ndugu zanguni! Subirini muone yatakuja mabasi ya kawaida kwa bei ya yaendayo kwa kasi!

Kalagabaho!

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Mradi wa magari yaendayo kasi kujenga barabara za zege Dar

Mradi wa Magari yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (DART) unatarajia kuanza kujenga barabara kwa kutumia zege badala ya lami, zitakazotumika kupitisha magari hayo ambapo dola za Marekani milioni 122.1, sawa na Sh. bilioni 150 zinatarajia kutumika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa DART, Cosmas Takule, alisema kutokana na uimara wa barabara hizo za zege, wana uhakika wa kudumu kati ya miaka 20 hadi 30 bila kufanyiwa matengenezo yoyote. Huduma za magari hayo zitaanza Novemba mwakani.

Alisema barabara za lami zinadumu kati ya miaka mitano hadi tisa kama hazikufanyiwa matengenezo.

Kadhalika, alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa maeneo ya maegesho ya magari jijini Dar es Salaam.

Alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kupunguza msongamano wa magari, tatizo ambalo limekuwa sugu hivi sasa jijini Daer es Salaam.

Alisema katika awamu ya kwanza ya mradi, watajenga barabara kuanzia Kimara hadi kivukoni jijini Dar es Salaam na kwamba hakuna gari yoyote itakayoruhusiwa kupita hapo zaidi ya magari yaendayo kasi.

Alifafanua kuwa barabara hiyo itakuwa na vituo vitano kutoka mwanzo hadi mwisho.

Takule alisema hawatatenga eneo jipya la kujenga barabara hizo bali zitakuwa sambamba na ile ya Morogoro inayotoka Kimara hadi kati kati ya jiji la Dar es Salaam.

Aidha, baadhi ya barabara zitaongezwa na kufanywa ziwe za kwenda bila magari kupishana (oneway).

Aidha, alisema wataweka barabara za juu katika makutano ya barabra za Mandela, Sam Nujoma na ile ya Nyerere.

Takule aliwataka wananchi kuamimini kwamba mradi huo upo na tayari serikali imetoa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaobomolewa nyumba zao zilizopo kando kando mwa zitakapopita barabara hizo.

Kwa upande mwingine alisema kutakuwa na magari ya mzunguko kuanzia eneo la Wazo, Kunduchi, Mwenge, Tabata, Uwanja wa Ndege, Mbagala na kuishia Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kuhusu mkandarasi alisema, DART ipo katika mchakato wa kumtafuta na kwamba mara baada ya kumpata, ujenzi utaanza muda wowote.

SOURCE: Nipashe, 2009-01-29 10:05:02 Na Richard Makore