Tuesday 1 April 2008

Uwanja wa Taifa TZ (2)

Zawadi juu tukitumia uwanja mpya - Musonye
(SOURCE: Nipashe, 31 Mar 2008)
By Somoe Ng'itu

Shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limesema kuwa endapo serikali ya Tanzania itatoa kibali cha kuutumia uwanja mpya wa Kisasa katika mashindano yake ya Klabu Bingwa maarufu kama Kombe la Kagame, zawadi za washindi zitaongezeka.

Kwa zaidi ya miaka minne, zawadi ya mshindi wa kwanza katika mashindano hayo ni Dola za Marekani 30,000, wapili Dola za Marekani 20,000 na watatu Dola za Marekani 10,000 ambazo zote zinatolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Akizungumza na Nipashe, Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema kuwa makampuni mengi wanayozungumza nayo yanaonyesha kukubali kudhamini mashindano hayo kwa masharti kuwa yafanyike kwenye uwanja mpya.

Musonye alisema kuwa mbali na zawadi kuongezeka pia klabu zinazoshiriki pia zitapata fedha kwa ajili ya kujiandaa na mashindano yake ya ndani na kuhudumia wachezaji wake katika viwango vinavyotakiwa.

``Tukiruhusiwa kuutumia uwanja mpya, mashindano yatakuwa na hadhi zaidi na pia timu ambazo ndio walengwa watafaidika kwa kupata fedha nyingi kutoka kwa wadhamini,`` alisema Musonye.

Alisema kuwa hata mwaka jana wakati CECAFA ikiandaa mashindano ya Kombe la Chalenji walikosa wadhamini washiriki kutokana na kutokuwa na kibali cha kutumia uwanja mpya ambao uliwavutia wengi wakati timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilipocheza na Msumbiji na kuonyeshwa katika kituo cha televisheni cha Supersport.

Alisema kuwa mbali na Tanzania kukubali kuandaa mashindano haya kabla ya Sudan kutangaza kushindwa kuwa wenyeji, sababu kubwa ya wajumbe kuikubali Tanzania ni ubora wa uwanja mpya ambao ulionekana kuwavutia wote.

Alizitaja klabu ambazo zimethibitisha kushiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kufanyika Julai 12 hadi 26 ni pamoja na Simba, Yanga, Rayon na APR (Rwanda), Elman (Somalia), Ten Ten (Eritrea), Vital O (Burundi), Miembeni (Zanzibar), STI (Djibout) na URA ya Uganda.


..................................
Yafuatayo ni MAONI YANGU ya jana (31/3/2008) kuhusu Uwanja wetu wa Taifa.
Je, tutafika kwa mtaji huu?
...................................

Uwanja wa Taifa TZ unajiendeshaje?
Mara nyingi nimekuwa nikisoma habari ktk magazeti ya nchini kuwa wadau mbalimbali wa michezo wametuma maombi kwa Rais (serikali) kuhusu kuomba ruhusa ya kuutumia Uwanja wa Taifa ktk mechi mfano Yanga dhidi ya Simba au michuano mbalimbali mathalani klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Mara nyingi (au zote) huwa hakuna majibu au hakuna ruhusa kuutumia uwanja. Mfano dhahiri ni hizo habari kutoka gazeti la Nipashe la tarehe 31/3/2008 (Nakala ya habari hiyo iko hapo juu).

Mimi ninavyoelewa ni kuwa Uwanja huo ulijengwa kwa fedha zilizopatikana kama mkopo na hivyo zinatakiwa zirudishwe, na pia uwanja unatakiwa ujiendeshe kwa kujitegemea (kibiashara).

Gharama kama kulipia bili za huduma mbalimbali uwanjani (maji, umeme, simu, ulinzi n.k.) na mishahara ya wafanyakazi zinatakiwa zitoke katika mfuko wa uwanja.

Kwa sababu hii nilitegemea wamiliki wa uwanja wangehaha kutafuta matukio mbalimbali ya kitaifa au kimataifa ili kuutumia uwanja kuingiza hela kwa madhumuni hayo na vilevile kujitengenezea faida baada ya kulipa deni na bili.

Kinyume chake naona wamiliki wameshafunga mageti ya uwanja na kuufanya kama Makumbusho ya Taifa ambapo watu wanauangalia tu.

Cha ajabu eti ni wamiliki kusubiri wateja mbalimbali waje kuomba ruhusa kuutumia uwanja na tena wateja wanapeleka maombi yao kwa Mheshimiwa Rais (kama ninavyosoma ktk magazeti). Kwa maoni yangu mimi, nilitegemea wamiliki wa uwanja ndio wangekuwa mstari wa mbele katika kutangaza na kutafuta wateja wa kuutumia uwanja na sio kinyume chake!

Vipo viwanja katika sehemu mbalimbali duniani ambako vimefunguliwa karibu muda sawa na huo Uwanja wa Taifa. Lakini tayari viwanja hivyo vimeandaa matukio (events) mbalimbali, tena mfululizo, kwa mwaka mzima na ni mengi zaidi kuliko yale yaliyoandaliwa katika Uwanja wa Taifa.

Natoa mfano wa uwanja wa Taifa wa Wembley, London.

Wakati uwanja huo ulipokuwa unafunguliwa, tayari wamiliki walikuwa wameshatafakari mikakati ya namna ya kurudisha deni la kiasi cha Paundi milioni 798 (sawa na US$1.57bn.)** zilizotumika kuujengea. Tena hawa wa Wembley walikopa toka ndani ya nchi yao; lakini Uwanja wa Taifa walikopa nje ya nchi (China) na hivyo thamani na gharama deni la za fedha za kigeni ni kubwa zaidi.

Kwa hiyo wamiliki wa uwanja wa Wembley waliandaa mechi za kirafiki za timu yao ya taifa (Uingereza) dhidi ya Brazil na Ujerumani. Pia mechi za kimashindano kama fainali za FA Cup na mechi ya kufungua pazia la msimu wa Ligi Kuu 2007/08, maarufu kama Community Shield zote kati ya Chelsea na Manchester United zilihamishiwa Wembley kutoka uwanja wa Millenium, Cardiff.

Zaidi ya hapo kuna mechi za kuwania kufuzu fainali za Euro 2008 dhidi ya Russia, Israel, Estonia na Croatia zilifanyika Wembley mfululizo hadi Novemba maka jana.

Hawakuishia hapo hawa jamaa; bali waliandaa matamasha mawili makubwa mwaka jana mwezi Julai. Tamasha la kwanza lilikuwa la Mazingira na hali ya hewa duniani (Live Earth) chini ya usimamizi wa aliyekuwa makamu wa Rais Marekani kipindi cha urais wa Bwana Bill Clinton, Bwana Al Gore. Tamasha lililofuatia lilikuwa la kumuenzi Diana (Concert for Diana) miaka 10 tangu kifo chake. Katika matamasha yote watu walifurika uwanjani ambapo bendi mbalimbali za muziki zilitumbuiza kuanzia mchana saa 6 hadi saa 4 za usiku.

Matamasha mengine kufanyika Wembley mwaka jana ni ya mwanamziki George Michael, Muse na Mettalica.

Sio mpira wa miguu pekee uliopata nafasi Wembley bali hata rugbi (rugby league) lilifanyika pambano kati ya Catalans dhidi ya St helens ktk kuwania Challenge Cup ambapo St Helens ilishinda.

Mwezi Oktaba mechi ya ligi ya mpira wa 'miguu' (NFL) ilifanyika Wembley kati ya New York Giants na Miami Dolphins zote toka Marekani. Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa mechi ya ligi (NFL) kufanyika nje ya Marekani.

Halikadhalika, mwezi Desemba mwaka jana uwanja wa Wembley uliandaa mashindano ya mbio za magari kumtafuta bingwa wa mabingwa (Champion of champions) ambako Michael Schumacher, bingwa wa zamani wa Formula 1, alishiriki. Mazulia ya bandia yalitumika kuweka njia za magari kupita kuuzunguka uwanja mzima.

Hayo ni baadhi tu ya matukio ktk uwanja huo maarufu duniani.

Tayari mwaka huu tena uwanja umeshaandaa matukio kadhaa katika kalenda yake.

Fedha zinapatikana kupitia;
-viingilio au ukodishwaji wa uwanja,
-udhamini wa matukio hayo,
-utoaji huduma za vinywaji na vitafunwa uwanjani. Kuna baa na migahawa mingi sana ndani ya uwanja,
-uegeshaji magari ambapo huduma maegesho hulipiwa
-uwanja una duka la kuuza bidhaa za kimichezo hasa zenye nembo ya uwanja wa wembley, jezi za timu ya taifa ya mpira wa miguu na jezi za timu za mpira wa miguu; na pia
-Wembley wanao wadhamini rasmi(official partners).

Hizi zote ni juhudi za kukusanya fedha za kurejesha deni na kujiingizia kipato!

Mimi bado sielewi Uwanja wa Taifa Tanzania unavyojiendesha kimapato? Uwanja uko kimya kabisa (hautumiki). Maana sijawahi kusikia unatumika ktk shughuli yoyote zaidi ya mechi moja au mbili za mwaka uliopita. Na sasa hivi baraza la soka Afrika la Mashariki na kati (CECAFA) wanasubiri 'majibu' kama wataruhusiwa kuutumia uwanja katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (ikumbukwe mwaka uliopita walinyimwa kibali kuutumia uwanja (rejea habari katika gazeti; Nipashe 31/3/2008))!

(** takwimu hizi ni kwa mujibu tovuti ya wikipedia)

No comments: