Saturday 19 April 2008

Andrew Chenge na kashfa yake!

Chenge ageuka `bubu` (SOURCE: Nipashe, 19 Apr 2008. By Dunstan Bahai)
Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, amegeuka bubu, hataki kuzungumza na waandishi, sasa anawakimbia.

Bw. Chenge maarufu kwa jina la `bilionea wa vijisenti`, alifanya kioja hicho jana jijini Dar es Salaam baada ya kufunga Mkutano wa Kimataifa wa masuala ya Usalama wa Vyombo vya Usafiri Baharini (IMO).

Bw. Chenge alipomaliza alitoka nje tofauti na kawaida yake kuzungumza na waandishi nje ya ukumbi, jana aliwaona waandishi hao kama adui zake.

Aprili 12, mwaka huu, gazeti la The Guardian la Uingereza, liliandika habari kuwa, Waziri Chenge amejilimbikizia dola zaidi ya milioni moja (zaidi ya Shilingi bilioni moja) kwenye benki moja iliyopo kisiwa cha Jersey, Uingereza.

Gazeti hilo lilieleza kuwa, inasadikiwa fedha hizo ni sehemu ya mgawo wa rushwa iliyotokana na ununuzi wa rada ya serikali ya Tanzania, wakati huo Bw. Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo, Mwenyekiti DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amemshauri Bw. Chenge, kujiuzulu.

Mchungaji Mtikila amesema ameanza kukusanya mikataba mibovu aliyodai ilisababisha hasara ya mabilioni ya fedha kwa serikali kwa nyakati tofauti.

Alisema pamoja na kumshauri Bw. Chenge ajiuzulu, ni vyema akarudisha fedha anazotuhumiwa kumiliki ili kulinda heshima ya taifa.

Akizungumzia mikataba inayokusanywa na kupitiwa kutoka kwenye taasisi na wizara, alisema ni pamoja na ile
-ya umeme ya Richmond, Dowans, IPTL, Songas, Aggreko na Net Group Solutions
-ya madini iliyosainiwa kati ya Benki Kuu (BoT) na Hazina
-ile ya Kampuni ya Simu Nchini (TTCL)
-ya ununuzi wa rada na ndege ya Rais,
-vyakula feki vyote vikigharimu mabilioni ya fedha.

Alisema mikataba hiyo itapitiwa kwa umakini na kamati maalumu pamoja na wanasheria alioafikiana nao ili kuiweka wazi kwa wananchi.

``Tunahitaji wanasheria wasiopungua 20 ili kukamilisha idadi ya 40 tunayohitaji ambao wako tayari kwa ukombozi,`` alisema.

No comments: