Tuesday 1 April 2008

Maazimio ya NEC (CCM) Butiama

Source: Majira, 01.04.2008 0146 EAT
Na George John, Musoma

MAZUNGUMZO ya Muafaka baina ya CCM na CUF kwa ajili ya kuleta hali ya utangamano wa kisiasa Zanzibar, sasa yatahusisha wananchi kwa kuyapigia kura za maoni.

Hatua hiyo ilifikiwa usiku wa kuamkia jana, baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bw. Pius Msekwa, kusoma mapendekezo ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM uliofanyika Machi 29 na 30 mwaka huu kijijini Butiama, Musoma.

Kimsingi, Bw. Msekwa alisema NEC ilikubaliana na yaliyofikiwa na kamati za mazungumzo hayo kutoka pande husika, lakini ikasema yapo marekebisho ambayo yanatakiwa kufanyika na hivyo kuwataka wajumbe wa kamati ya CCM kukutana na wenzao wa CUF kuyazungumza.

Lakini NEC iliazimia kuwa kutokana na ukweli kwamba mambo haya yakikubalika yataleta mabadiliko ya mfumo wa utawala wa Zanzibar, hapana budi wananchi wakahusishwa kwa kupiga kura za maoni.

Hata hivyo, NEC ilieleza kusikitishwa kwake na CUF kutangaza makubaliano kinyume na walivyokubaliana na CCM na kusema tabia kama hiyo inaweza kusababisha makubaliano kuwa magumu, ingawa kamati ya CCM ilipongezwa kwa kufanikisha mazungumzo hayo.

Kwa mujibu wa Bw. Msekwa, NEC inaamini kuwa njia hiyo ni muafaka katika kujenga utangamano, utulivu kisiasa na kiusalama katika visiwa vya Zanzibar.

Kuhusu kumuenzi Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Nyerere, NEC ilipokea taarifa ya dhamira ya Rais Jakaya Kikwete, ya kuweka hai kumbukumbu za Baba wa Taifa na kijiji cha Butiama, ambapo iliamuliwa kuwa katika ugawaji wa wilaya ya Musoma Vijijini kuwa wilaya mbili, basi Butiama iwe makao makuu ya mojawapo.

Iliamualiwa pia kuwa maadhimisho ya Siku ya Nyerere, Oktoba 14 mwakani, yafanyike kitaifa Butiama na mambo yote muhimu aliyoyafanya yakusanywe kwa mtiririko mzuri na yachapishwe, ili yatumiwe kama rejea muhimu kwa wananchi na vizazi vijavyo.

Kuhusu miiko ya uongozi, ilikubaliwa kuwa miiko iliyoko katika Katiba na kanuni za chama, itekelezwe kwa nguvu mpya kwa kuzingatia kuwa uongozi katika chama isiwe njia ya kujipatia riziki. Na watakaokiuka miiko wachukuliwe hatua zitakazokuwa wazi kwa umma.

NEC ilisisitiza umuhimu wa kutenganisha uongozi na biashara, ili kuondoa migongano ya kimaslahi na ukiukaji wa maadili na miiko ya uongozi ili CCM ibakiwe na taswira yake ya chama chenye viongozi waadilifu, wanaojali maslahi ya watu na jukumu lake kubwa la kutetea wanyonge.

Kutokana na hilo, NEC iliziagiza Serikali zote mbili kutunga sheria ili kuhakikisha kuwa vitu hivyoi viwili haviingiliani ili kuondoa migongano ya kimaslahi.

Kuhusu hoja ya kashfa ya Richmond bungeni, NEC ilibaini kuwa wananchi wanachukizwa sana na wizi, ubadhirifu na rushwa miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma.

"NEC imesisitiza viongozi wa CCM na Serikali wasiwe sehemu ya maovu kwani hali hiyo itajenga chuki ... zichukuliwe hatua thabiti kupambana na maovu yanapojitokeza na zionekane kwa umma," ilisema taarifa.

Akifafanua nje ya taarifa hiyo jana, Katibu Mwenezi wa CCM, Kapteni mstaafu John Chiligati, alikanusha madai ya kuwapo watu waliokaripiwa na kutishiwa kunyang'anywa kadi za CCM katika kikao hicho.

"Zaidi ya yale yaliyomo katika tamko la NEC hakuna suala la EPA lililojadiliwa kwa kina, kwani sisi tunaiachia Serikali ambayo imeunda Tume ili imalize kazi yake, hivyo hatukuwa na cha kujadili zaidi ha hapo," alisema.

Alisema ubadhirifu uliojadiliwa na hatua kuchukuliwa ni kuhusu Jumuiya ya Wazazi, ambapo viongozi watatu waliachishwa kazi kwa ubadhirifu na kutakiwa kurejesha fedha za Jumuiya.

"Walioachishwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya, Bw. Abihudi Malegesi ambaye alikutwa na ubadhirifu wa sh. milioni 43, Makamu wake, Bw. Ramadhan Nzori, sh. milioni 7.5 na Katibu Mkuu, Bw. Cosmas Hinju, sh. milioni 5," alisema Kapteni Chiligati.

NEC ililitaka Bunge kukemea maovu ya viongozi na watumishi wa umma na wabunge wa CCM waonekane dhahiri kushiriki kikamilifu katika hilo, huku Kamati ya Wabunge hao ikizungumza na kuelewana kuhusu masuala makubwa yanayowasilishwa bungeni ili kulinda maslahi ya chama.

NEC katika taarifa hiyo, ilieleza kubaini kuporomoka kwa maadili na nidhamu ya chama hicho na kutaka hatua zichukuliwe kurudisha nidhamu, maadili na mshikamano ndani ya chama.

Ili kufikia hilo, ilikubaliwa kuchukuliwa hatua za kuvunja makundi, kutokomeza rushwa katika uchaguzi, kuchuja kwa makini wagombea, kutoa mafunzo ya itikadi na kufufua moyo wa kujitolea.

Akizungumzia mapendekezo ya Butiama kuwa makao makuu ya wilaya, kiongozi wa Wazanaki, Chifu Japhet Wanzagi, akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, alisema Mwalimu Nyerere hakuwa tayari kuiona Butiama ikiwa makao makuu ya wilaya.

"Mwalimu yeye alitaka kuiona Butiama ikibaki kuwa kijiji cha mfano tu na hakuwa tayari kuiona ikibadilika kuwa kitu kingine, badala yake alitaka makao makuu yawe Kiabakari," alisema Chifu Wanzagi.

No comments: