Thursday 10 April 2008

Tusioneane aibu! Reli wawajibike.

Shirika la Reli wana wajibu wa kuwapatia abiria wake usafiri mbadala (kama vile kukodi mabasi) pale inapotokea treni zimesimamisha au kukatiza huduma bila tahadhali kwa abiria/wasafiri. Kutokana na hali hiyo, Shirika linatakiwa liwajibike kulipia gharama za ukodishwaji hayo mabasi ili abiria wafike waendako.
Kwa kweli hakuna sababu abiria waachwe wakihangaika njiani (kituoni) pasi kujua hatima ya usafiri wao.
Kimsingi abiria hao hawakufikishwa pale walipokata tiketi na kulipa nauli ili wapelekwe. Kwa hiyo Shirika la Reli wanatakiwa kutimiza mkataba wake na abiria kwa kuwasafirisha abiria bila matatizo au kuchelewesha ratiba zao hadi kituo chao cha mwisho kwa kutumia usafiri wa kukodi kwa gharama za Shirika.
Naona hapa kuna tundu ktk sheria ambapo inawapa Shirika la Reli nguvu za kuwatelekeza abiria kiasi hiki na kuwasababishia usumbufu na mahangaiko makubwa kimaisha, bila Shirika kuwajibika ipasavyo.
Naomba wizara husika na vyombo vya kutetea haki za raia vilitazame hili suala kwa umakini ili lisiwe kawaida katika maisha ya kila siku ya wasafiri au wananchi kwa ujumla.

Tafadhalini wahusika; Watanzania wanastahili huduma bora, na sio huu ubabe wanaotendewa na kutelekezwa katika mahangaiko! Ni lazima muonyeshe kuwa mnawajali. Huu ni wakati wa vitendo. Muda wa ahadi-nadharia (longolongo) ulikwishapita zamani sana!
(mosonga2002@yahoo.com)
.............................

Abiria wa treni waliokwama sasa wageuka vibarua Moro
(* SOURCE: Nipashe, 10 Apr 2008. By Devota Minja, Morogoro)
Abiria waliokwama katika stesheni ya Morogoro, wamelazimika kulima vibarua ili kupata fedha za kujikimu. Wakizungumza na PST, abiria hao ambao walikwama katika stesheni hiyo kwa zaidi ya wiki moja, wamelalamikia kushindwa kusafiri kwa wakati japo wameambiwa kuwa mgomo umemalizika.

Walisema kuwa baadhi yao wamelazimika kulima mashamba na wengine kupalilia mahindi kwa miraba huku wakilipwa ujira wa kati ya Sh. 1,000 na Sh. 3,000 kulingana na makubalianao kati ya mwenye shamba na kibarua. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa wazee waliokwama kituoni hapo kwani walikuwa hawana uwezo wa kufanya vibarua kutokana na kutokuwa na nguvu za kulima.

Mmoja wa abiria Bw. Izack Musa, aliyekuwa akitokea Mbeya kwenda Kigoma, alisema baada ya kukwama walilazimika kurudishiwa nauli zao. Alisema kwa mujibu wa maelekezo waliopatiwa stesheni hapo, lazima wafuate utaratibu wa kukata tiketi upya.

``Tunashangazwa, wanakuja abiria wengine wanapata tiketi sisi tuliorudishiwa tunaambiwa tusubiri hadi wiki ijayo,`` alisema Bw. Izack.

Mkuu wa Stesheni ya Morogoro, Bw. Flavian Nyawale, akijibu malalamiko hayo alisema kuwa, kwa mujibu wa taratibu, abiria ambao walikwama na kulazimika kurudishiwa nauli zao walitakiwa kufuata utaratibu mpya wa kukata tiketi. Bw. Nyawale aliwahakikishia abiria hao kuwa taratibu zitafanyika ili waweze kusafiri.

No comments: