Friday 2 November 2007

Prisons 1 Yanga 2

Yanga `yaikata ngebe` Prisons

2007-11-02 08:59:15
By Jacqueline Massano, Mbeya


Yanga jana iliweza kupunguza kasi ya Prisons ya Mbeya baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Kwa matokeo hayo sasa, Yanga imeweza kufikisha pointi 18 na kutofautiana pointi sita na Prisons.

Yanga iliweza kuondoka na ushindi baada ya kucheza soka ya kuvutia na ingeweza kuondoka na ushindi mkubwa kama washambuliaji wake wangekuwa makini.

Ni tofauti na Prisons, ambayo ilikosa uelewano katika mchezo huo, hasa upande wa beki.

Kuna uwezekano kunaweza kukawa kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na hofu ya kucheza na Yanga, ambayo katika siku za karibuni imeonekana kutulia na kuanza kukusanya pointi.

Yanga iliweza kujipatia bao la kwanza katika dakika ya 38 lililofungwa kwa `tik tak? na mshambuliaji mkongwe, Mkenya Maurice Sunguti.

Mrisho Ngassa, hata hivyo, aliyeingia katika kipindi cha pili, aliihakikishia Yanga ushindi baada ya kufunga bao maridadi katika dakika ya 73.

Alifunga bao hilo baada ya kumlamba chenga beki Sam Kamtande na Kipa Frank Mutego kabla ya kuzamisha mpira wavuni akiwa peke yake na goli.

Stephen Masika, hata hivyo, aliipatia Prisons bao la kufutia machozi katika dakika ya 85.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Jack Chamangwana alieleza kufurahishwa na ushindi wa timu yake.

Chamangwana alidai zilikuwa pointi tatu muhimu na pia alifurahishwa timu yake kuweza kupunguza kasi ya Prisons iliyoonekana kupaa kwenye msimamo wa ligi wakati ilipoanza.

Naye Kocha Juma Mwambusi wa Prisons alieleza masikitiko yake baada ya timu yake kupoteza mechi ya kwanza nyumbani.

Timu zilikuwa:
Prisons: Frank Mutego, Lusajo Mwakifamba, Stephano Masika, Aloyce Adam, Sylvester Kamtande, Godfrey Bonny, Said Mtupa, Misango Magai, Oswald Morris, Yonah Ndabila (Shabaan Mtupa dk.65) na Fred Chudu.

Yanga: Jackson Chove, Fred Mbuna, Abuu Mtiro, Wisdomu Ndlovu, Hamisi Yussuf, Credo Mwaipopo, Waziri Mahadhi (Mrisho Ngassa dk.46), Abuu Ramadhan, Gaudence Mwaikimba, Maurice Sunguti (Hamisi Suedi dk.76) na Abdi Kassim (Nadir Haroub `Cannavaro` dk.65).

Wakati huo huo, Victor Kwayu wa PST-Moshi anaripoti Toto African ya Mwanza ilipata pointi tatu za ugenini baada ya kuilaza Ashanti 2-0 kwenye mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Ushirika kwa mabao yaliyopachikwa na Castory Mubala na Joseph Lindo.

Naye Idda Mushi wa PST-Morogoro anaripoti kuwa mechi kati ya Polisi Morogoro na Kagera Sugar iliyokuwa ifanyike jana itachezwa leo badala ya jana kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro

From: Nipashe

No comments: