Friday 12 October 2007

Utabiri wa Nyerere kuhusu Afrika na Ulaya

Mwalimu Nyere alifariki tarehe 14/10/1999 ktk Hospitali ya Mt. Thomas, London kutokana na saratani ya damu.
Mwalimu ni miongoni mwa watu mashuhuri ninaowaheshimu duniani. Nilipokuwa darasa la tano au la sita nilisoma kitabu cha somo la Kiswahili (Tujifunze Lugha Yetu kitabu cha 7 au 8?). Ndio mwanzo wa kumjua Mwalimu enzi za udogo wangu. Sura mojawapo ktk kitabu hicho ilianza na huu msitari, 'Watendamema ni wengi ila mashujaa ni wachache ...). Ktk sura hiyo walimwongelea mwalimu JK Nyerere.
Mwalimu atabaki ktk kumbukumbu zangu daima na ni mfano wa kuigwa!
Makala ifuatayo imeandikwa na ndugu Nimi Mweta, inazidi kunikumbusha ushujaa wa Mwalimu!! (Unaposoma makala hii kumbuka pia kuwa Mwalimu aliwahi kuwa mwenyekiti wa South-South Commission. Linganisha hoja ya Mwalimu kuhusu 'location' ya bara la Afrika na 'location' ya nchi ya Mexico ambayo iko ktk eneo la South-South Commission ingawa kijografia iko kaskazini. Oanisha maoni ya Mwalimu juu ya Mexico na haya anayoongelea mwandishi Nimi Mweta).
Na Mosonga


Hatma ya utabiri wa Nyerere kuhusu Afrika na Ulaya, 1997 hadi 2007
12 Oct 2007
By Nimi Mweta

Mwishoni mwa 1997, Mwalimu Julius Nyerere alihudhuria kongamano la `Uongozi katika Bara la Afrika,` katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa muda wa siku tatu mfululizo, ambako alichangia mada katika maeneo tofauti, akatoa mada ya ufunguzi.

Ilihusu nafasi ya Afrika katika dunia ambayo katika muongo huu (tangu mwaka 2000) inajulikana kwa nguvu zaidi kama `dunia ya utandawazi.`

Mwalimu hakuwa na utabiri mzuri kwa Afrika, na vinginevyo labda alikuwa akisoma `hitma` ya fikra yake kuhusu `ukoloni mamboleo` hadi 1997.

Ni hali ambayo imekuwa wazi zaidi, kupambanua yaliyofikiriwa wakati ule.

Mwalimu alikuwa na fikra ambayo kwa mbali ilikaribiana na ile ya Mwalimu Ali Mazrui wa Kenya, mshindani wa Mwalimu kifikra alipokuwa mkuu wa kitivo cha taaluma za jamii huko Makerere miaka ya mwisho ya 60 na mapema miaka ya 70.

Profesa Mazrui anaiona Afrika kama bara lililovurugwa katika utamaduni wake na wageni kutoka nje, huku ikiwa haina uwezo wa kutumia fursa mpya za teknolojia, tofauti na Asia ambayo haijavurugwa katika utamaduni wake, na imetimua fasaha na vya kutosha teknolojia kutoka magharibi hivyo kubadili viwango vya maisha vya watu wake.

Mwalimu aliiona Afrika inadidimia tu.

Katika mada yake hiyo iliyosikilizwa kwa makini sana katika ukumbi wa Nkrumah mbele ya waalimu wa Chuo Kikuu, wanafunzi, mabalozi kutoka sehemu tofauti duniani na watu wengine, Mwalimu alisema tofauti na nchi nyingine zinazoendelea, Afrika haina uwezo wa kuilazimisha Ulaya (na Amerika) kuisaidia ipasavyo kimaendeleo.

Akiwa amechukulia ule mfumo wa misaada uitwao Marshall Plan, uliotungwa na Marekani kujenga upya Ulaya kwa mfumo wa soko baada ya Vita Kuu ya Pili, Mwalimu alitoa rai kuwa umbali wa nchi nyingi za Afrika kwa Ulaya au Marekani, au Japani, ndiyo kikwazo kikubwa katika hali hiyo.

Wengine wako karibu, wanahamia huko, kuzifanya nchi zilizoendelea zitoe jawabu.

Alieleza kuwa nchi za Marekani Kusini zina nguvu ya kuathiri sera za uchumi au kuhusu maendeleo yao kwa nchi kubwa ya Marekani kwani wananchi wake wanahamia huko kwa maelfu kila kukicha, na kuwazuia si rahisi.

Kwa maana hiyo Marekani ilibuni mpango wa kujenga soko la pamoja (au eneo la biashara huria) la Marekani na nchi za kaskazini ya Bara la Amerika, yaani NAFTA inayoundwa na Marekani, Canada na Mexico.

Ulaya ilikuwa inaendelea kupanua uanachama kwa nchi zilizokuwa sehemu ya fungamano la nchi za kisoshalisti ambazo ziliacha kambi ya Urusi na kuingia mfumo wa soko.

Hata nchi za Afrika Kaskazini (za Kiarabu) zipo katika harakati ya ushirikiano maalum na Umoja wa Ulaya, kwani watu wake wanakwenda huko kwa wingi, kuhama mafarakano, vita, udini.

Alisema Afrika iko mbali na Marekani, na Ulaya na hasa na Japani, kwa hiyo watu wake hawana uwezo wa kutoa shinikizo kwa kuhamia katika nchi kubwa zinazofanya maamuzi ya uchumi duniani - mtazamo unaoonyesha kuwa ndiyo njia pekee iliyobaki.

Suala ni kama uchambuzi au taswira hiyo bado ina `nguvu ya hoja` katika hali halisi kama jinsi ilivyoonekana wakati huo, au hali ya dunia imebadilika kiasi cha kuona hali ya dunia kwa njia nyingine.

Bado Afrika haina nguvu kuathiri sera za wakubwa kutokana na umbali, au yako maeneo ambako mpangilio huu wa picha (taswira) sasa umebadilika?

Mtazamo wa Mwalimu unaweza kuitwa ni kielelezo cha mfikiriaji wa Brazil wa miaka ya 1960 aitwaye Andre Gunder-Frank, aliyetoa mfumo wa ubepari wa dunia au utandawizi kama kitovu na pembezoni .

Alisema ziko nchi za kati na za pembezoni katika mfumo huo, na ndani ya pande hizo mbili, kuna kati ya kati na kati ya pembezoni, kama ilivyo pia pembezoni ya kati na pembezoni ya pembezoni,` ambayo kimsingi ndiyo Bara la Afrika.

Ni mtazamo ambao unatoa taswira ya kuogopesha ya uduni wetu.

Mtazamo huo wa Mwalimu ni kielelezo cha kukua au kukamilika kwa kukata tamaa kimsingi kuhusu uwezo wa kuzitaka nchi zilizoendelea kujitolea ili Afrika iweze kupiga hatua kwa uhalisi fulani.

Baada ya kusisitiza jambo hilo kwa miaka mingi tangu baada ya uhuru, Mwalimu na viongozi wakuu kadhaa wa nchi `tangulizi` kati ya nchi zinazoendelea (ikiwemo Ugiriki, India, Mexico) zilikutana na Marekani wakati huo Ronald Reagan akiwa rais, kwenye mji wa kitalii wa Cancun nchini Mexico ambako Rais Reagan alisema `no` au kwa Kirusi `nyet` kuhusu kile kilichoitwa `new international economic order` aliyoitaka Mwalimu na wanaharakati wa pande zote za dunia.

Mwalimu ni `mzimu` wa harakati dhidi ya IMF na Benki ya Dunia tangu mwaka 1981, aliposema IMF ni `mfuko` wa kusaidia nchi zenye matatizo (ya urari wa malipo) si `International Ministry of Finance,` yaani taasisi (wizara ya fedha) ya kuzipangia nchi hizi sera zao....

Kwa mtazamo wa Mwalimu, hapawezi kuwa na matumaini` yoyote kwa Afrika nje ya kufikiwa kwa `new international economic order,` na hata kama hiyo haifikiwi kwa nchi zote kwa pamoja au kwa mpangilio mmoja wa nyenzo au sera, basi Afrika ipate mradi maalum wa `Marshall Plan` wa kujinasua, kwa mfano kwa ujenzi wa miundombinu thabiti, vifaa vya kisasa vya kilimo, n.k. Profesa Jeffrey Sachs, mshauri wa Dk Kofi Annan kwa `malengo ya maendeleo ya milenia` na mchumi bingwa na mwanaharakati wa Marekani, amebakia na fikra kama ile ya Mwalimu takriban kwa kila alilonena.

Siyo mawazo `yaliyochoka,` bado.

Ina maana kwamba fikra za Mwalimu Nyerere ziko pale pale kwa uhalisi wake kuhusu kile kinachoendelea katika uchumi wa dunia?

Jibu ni ndiyo na hapana, kuwa kama suala ni kubadilisha nchi hizi (hasa za Afrika, lakini pia `mabaki` ya Asia ya Kusini, Marekani ya Kati, Kusini na visiwa vya Kiafrika vya Mashariki ya Mbali) basi mpangilio unaoendana na hali ilivyo ni hiyo `Marshall Plan.`

Ila tu kuna tatizo kuwa nchi nyingi zimepata fedha nyingi kama Nigeria kuhusiana na mafuta, au Congo kwa utajiri wa madini, bila kuweza kupiga hatua zozote.

Tanzania imepata takriban dola bilioni 50 za misaada tangu uhuru, na leo hivi watu wanadai kuwa tuna umaskini wa kutisha kutokana na mikataba ya kodi za madini, ambayo serikali imeingia na makampuni makubwa tangu 1998.

Ni kweli eti vianzio vya umaskini vimewekwa, au kujengwa upya wakati Mwalimu anakaribia kufariki?

Ni wazi kuwa yako matatizo katika mfumo mzima wa fikra ambayo Mwalimu anaitetea, ambayo hakuwahi kupata ufumbuzi wake kutokana na `kuuganda` mfumo wa ki-Keynes na `dili mpya` nchini Marekani na Uingereza baada ya Vita Kuu ya Pili, ya kuwaboresha wafanyakazi kwa serikali kutoa fedha katika mabenki kufanya kinachohitajika.

Mwalimu alitaka hilo lifanyike kwa nchi zote changa, na sera zake za Ujamaa zilikuwa ni kufanya hivyo kwa upande wa Tanzania, yaani wa ndani, na aliweka misingi ya viwanda, elimu na taasisi za afya - vyote vikaporomoka kutokana na msingi wake wa kutegemea mauzo ya mazao nchi za nje.

Thamani ya fedha ikashuka, mazao mbadala na yale ya kilimo bora cha mashine kilichopunguza bei ya mazao na bado kinapunguza bei hizo ikawa vikwazo kwa kufanikisha lengo la kutumia fedha za ndani kufikia viwanda na kilimo bora, hivyo sharti fedha hizo zitoke nje.

Mwalimu aliona, hadi kufikia mwisho wa mwaka 1997, kuwa haiwezekani, kwani Afrika iko pembezoni mwa dunia, na hata watu wake wakifa, wengine hawatashtuka. Je, kuanza kwa `malengo ya milenia,` AGOA, EPA, TICAD, China ni jawabu?

* SOURCE: Nipashe

No comments: