Tuesday, 9 October 2007

Mishahara mipya sekta binafsi

Mishahara mipya hii hapa

09 Oct 2007
By MWANDISHI WETU, JIJINI

Kwa mtazamo wa juu juu, utasema Rais Jakaya Kikwete amerejea kutoka majuu na neema kwani ile kufika tu, Serikali yake ikatangaza viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.

Viwango hivyo vilitangazwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana , Bw. John Chiligati.

Mambo yako hivi:
350,000-Sekta binafsi za usafiri na mawasiliano (anga).

230,000- Huduma ya upakiaji na upakuaji wa mizigo.

300,000 –Makuli, wajenzi wa melini 300,000-Wafanyakazi wa mawasiliano ya simu kiwango kipya kitakuwa 200,000 Usafiri wa nchi kavu 250,000 Vyombo vya habari vya kibiashara 150,000 Vyombo vya kidini.

225,000 Meli za mizigo
196,000 Meli za uvuvi wa ndani
120,000-Wauza madawa maduka makubwa
90,000 Mahausigeli wa mabalozi
80,000 Mahausigeli wa vigogo
80,000 Watumishi wa bar, hoteli ndogo gesti
65,000 Mahausigeli, hausiboi wa walalahoi
65,000, Wafanyakazi wa kilimo mashambani

Kiwango hicho kwa watu wa daraja la chini ni neema kubwa kwani hadi sasa kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi kilichokuwa kinatumika ni Sh. 35,000 kwa wafanyakazi wa mashambani na kwa wale wa mjini Sh.48,000.

* SOURCE: Alasiri


Ifuatayo ni habari hiyohiyo kupitia gazeti Uhuru.

Kima cha chini sekta binafsi chatangazwa
Watumishi wa ndani, baa kulipwa 65,000/-
Vyombo vya habari vya biashara 250,000/-
NA MAGRETH KINABO
SERIKALI imetangaza kima cha chini cha mishahara kitachotumika katika sekta binafsi kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu, ambacho kitakuwa kati ya sh. 65,000 na sh. 350,000 kwa mwezi.
Kima hicho cha mshahara kitawahusu wafanyakazi wa baa, hoteli, majumbani, sekta ya madini, ulinzi binafsi, afya, biashara, viwanda, usafiri na mawasiliano.
Akitangaza mishahara hiyo kwa waandishi wa habari jana, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati alisema kiwango hicho pia kinawahusu wafanyakazi wa sekta ya kilimo.
Akitoa mchanganuo Chiligati alisema wafanyakazi walioajiriwa kwenye sekta ya kilimo wanatakiwa kulipwa kima cha chini sh. 65,000 kwa mwezi, mshahara ambao pia unawahusu wafanyakazi wa majumbani, ambao hawakai na waajiri wao.
Alisema wafanyakazi wa majumbani wanaofanya kazi kwa wafanyabiashara wakubwa na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini wanatakiwa kulipwa sh. 90,000 kwa mwezi.
Chiligati alisema wafanyakazi wa majumbani wanaofanya kazi kwa watu wanaolipiwa huduma hiyo, wanatakiwa kulipwa kima cha chini sh. 80,000 kwa mwezi.
Wanaofanya kazi kwa watu wa kawaida na hawalali kwa waajiri wanapaswa kulipwa sh. 65,000, wakati kwa wale wanaolala kwa mwajiri watalipwa mshahara wa kima cha chini sh. 25,000 kwa mwezi.
Alisema wafanyakazi wanaofanya kwenye hoteli za kitalii wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh.150,000; wakati wale wa hoteli za kiwango cha kati watalipwa sh.100,000; huku wale wa hoteli ndogo, baa, nyumba za wageni na migahawa watalipwa sh. 80,000 kwa mwezi.
Waziri Chiligati alisema kwa wale wanaofanya kazi kwenye sekta ya madini kima cha chini cha mshahara wanaotakiwa kulipwa ni sh. 350,000.
Wafanyakazi wa kampuni za ulinzi za kigeni na zile kubwa wanatakiwa kulipwa sh. 105,000 kwa mwezi, huku zingine zikitakiwa kulipa kima cha chini cha sh. 80,000.
Alisema wafanyakazi wa viwanda vikubwa na benki wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh. 150,000; wakati viwanda vidogo na biashara ndogo wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh. 80,000.
Chiligati alisema kwa sekta ya afya, wafanyakazi wa hospitali kubwa na maduka makubwa ya dawa wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh. 120,000; huku wale wa hospitali ndogo, zahanati, maduka madogo ya dawa na maabara wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh. 80,000.
Alisema kwa wafanyakazi wa sekta ya usafiri na mawasiliano wanaofanya kazi kwenye huduma ya anga wanatakiwa kulipwa kima cha chini cha sh.350,000.
Wakala wa forodha sh. 230,000, mawasiliano ya simu sh. 300,000, usafiri wa nchi kavu sh. 200,000, vyombo vya habari vinavyofanya biashara vinatakiwa kulipa kima cha chini cha sh. 250,000 na kwa vile vinavyotoa huduma za kidini wanatakiwa kulipa sh. 150,000.
Chiligati alisema katika sekta ya maji, bahari na maziwa, upande wa meli kubwa za kimataifa watalipwa kwa mujibu wa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) wa mwaka 2006. Meli za mizigo na abiria sh. 225,000, za uvuvi wa ndani sh. 196,000 na makuli na wajenzi wa meli sh. 300,000.
Alisema kila sekta binafsi itakuwa na kiwango chake cha kima cha chini cha mshahara, kwa kuzingatia uzalishaji wa faida, tija, uwezo wa mwajiri, na gharama za maisha.
“Kima cha chini kwa kila sekta kitatumika kwa wafanyakazi wote bila ya kujali ni wa mijini au vijijini, kwani tofauti za gharama za maisha kati ya mijini na vijijini sasa haipo,” alisema Chiligati.
Alisema vibarua wa siku kwenye kila sekta watalipwa kulingana na mishahara ya kima cha chini ya mwezi kwa sekta husika, na kwamba wafanyakazi wanaofanyakazi muda wa ziada wanastahili kulipwa.
Hata hivyo, aliwataka wafanyakazi kuongeza ufanisi kazini ili uzalishaji uongezeke.
Chiligati alisema mishahara hiyo inatokana na mapendekezo ya wajumbe walioteuliwa kufanya kazi hiyo waliotoka serikalini, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Alisema waligundua kuwa asilimia 15 ya wafanyakazi hawana mikataba ya ajira, hususan kwenye sekta ya usafiri na mawasiliano, majumbani, hotelini na ulinzi katika kampuni binafsi.
Mengine waliyoyagundua ni sehemu nyingi kutokuwa na mikataba ya huduma bora ya kazi, hawalipwi malipo ya ziada, waajiri hawajaandikisha wafanyakzi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na wanapoumia wakiwa kazini wanacheleweshewe malipo yao au kutolipwa.
Akizunguzia watumishi wa umma, Katibu Mkuu wa Chama cha Elimu ya Juu, Sayansi, Tekinolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), Adeligunda Mgaya alisema uamuzi uliofanywa na serikali kwa upande wa sekta binafsi umesaidia kutoa changamoto kwa serikali juu ya watumishi wa umma.
Alisema suala hilo bado liko kwenye majadiliano na kwamba baraza la pamoja la majadiliano litakutana Oktaba 23, mwaka huu.

source: Uhuru

No comments: