Tuesday 16 October 2007

Baba Wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere

Kwa nini tunamkumbuka Baba wa Taifa?

14 Oct 2007
By Chris Joe

Leo ni siku ya Nyerere, au Nyerere Day kama wengi wanavyopenda kuiita. Ni siku tunayokumbuka kufariki dunia kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, miaka minane iliyopita.

Mwalimu Nyerere alifariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas, huko Uingereza ambako alikuwa anatibiwa.

Miaka minane ni midogo, lakini ni mingi pia, kutegemea unaitazama katika dira ipi. Kwa maisha ya mwanadamu, miaka minane ni midogo.

Kama ni mtoto ni ama anaanza darasa la kwanza au yupo darasa la pili, zaidi sana la tatu kutegemea sehemu anakoishi na jamii anamoishi, na hali ya wazazi au walezi kifedha.

Kwa hiyo tunaweza kusema kwa mtoto aliye katika madarasa hayo au kwa wale walio chini ya miaka minane, atakua anamfahamu Mwalimu katika historia na kumwona katika picha tu, yaani hawakubahatika kumwona.

Kama jinsi tunavyouona muda wa miaka minane kuwa ni mdogo kwa maana ya uchanga wake, vivyo hivyo tunavyouona muda wa miaka minane ya kufa kwake kuwa ni mdogo.

Kwa hiyo miaka minane ni muda mfupi mno kwetu sisi kusahau, au kuanza kusahau kuwa tulikuwa naye, na hasa ukizingatia kuwa tulimpenda mno Mwalimu kwa busara, hekima na maarifa alivyojaliwa navyo na Mwenyezi Mungu, na kwa jinsi alivyotupenda Watanzania.

Lakini tunapokumbuka kifo chake maana yake tunakumbuka mambo aliyotufanyia sisi Watanzania wakati wa uhai wake.

Kwa maana watu hukumbukwa ama kwa mabaya aliyoyafanya kwa watu wake na nchi yake kama Hitler wa Ujerumani, Ivan The Terrible wa Urusi wa enzi hizo au Iddi Amin Dada wa hapa jirani Uganda mwishoni mwa miaka ya sabini; au kwa mema yao, kama alivyokuwa Mahtma Ghandhi wa India na Mwalimu Julius Nyerere wa hapa kwetu Tanzania.

Isipokuwa watu kama Adolf Hitler hukumbukwa kihistoria tu na kutolewa mfano wa mambo asiyofaa kuigwa.

Hukumbukwa kwa kufurahi kwamba `bora amekufa`, ni kama kuuawa kwa simba mla watu. Lakini kumkumbuka mtu kama Nyerere ni kwa huzuni kwamba `mbona ametutoka mapema hivi kabla hatujafaidi mema aliyokuwa anatufanyia.`

Ni kama kumpoteza baba au mama au mtoto aliyekuwa kipenzi chako.

Na kwa jinsi hii tunamkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni nani asiyefahamu mema aliyotufanyia Mwalimu na aliyolifanyia taifa lake?

Pengine ni watoto hawa ambao wanaanza shule sasa, ingawa nafahamu pia kuwa wapo wachache ambao hata ungewafanyia wema wa kiasi gani, watakuona mbaya na hufanyi chochote chema.

Hao wapo na ndivyo walivyoumbwa. Hakuna kiasi chochote cha ushawishi kitakachowabadilisha tabia yao hiyo ya kutokuwa na fadhila. Ni hulka yao, na katika demokrasia ya kweli watu wa aina hii huvumiliwa tu.

Tukianza kuorodhesha mambo aliyofanya Mwalimu kwa nchi yake na watu wake tunaweza kujaza gazeti lote kwa wiki kadhaa mfululizo.

Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba asingekuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pengine uhuru wanchi hii usingepatikana mapema na kwa amani kiasi ulivyopatikana.

Ni kwa sababu ya busara za Mwalimu na ushawishi aliojaliwa kuwa nao katika uzito wa hoja zake, nchi hii ilipata uhuru mapema kuliko ilivyotarajiwa. Moja ya mambo yaloyowezesha kufanikiwa kwa jambo hili ni uelewa wake kuhusu nguvu ya umoja wa watu wake.

Ndiyo maana Mwalimu alisimamia kwa nguvu sana kwanza umoja wa kitaifa kwa kuwaunganisha Watanganyika (wakati huo) kwa lugha ya Kiswahili na la pili kubwa ni kuvunja uchifu na kwa maana hiyo kuvunja nguvu ya ukabila.

Ilifika wakati mtu akikuuliza kabila lako anaonekana wa ajabu, labda kwa lengo la utani.

Umoja wa kitaifa alioujenga Mwalimu na upendo aliopujenga kati yetu ndivyo vitu vilivyosaidia kuwepo na kushamiri kwa amani katika nchi yetu, jambo ambalo Watanzania tuna haki ya kujivunia kwa sababu watu wa mataifa mengine hapa Africa wangependa kuishi hapa kwetu kwa sababu kwao hawana uhakika wa kuiona siku ya pili salama.

Ni rahisi kubeza amani iliyoko nchini mwetu na baadhi ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi. Lakini siyo rahisi kujenga na kudumisha amani.

Ni rahisi kubeza upendano uliopo baina ya Watanzania na kuchochea chuki na uhasama kama wanavyofanya baadhi ya watu kwa manufaa yao, lakini wajue kuwa siyo rahisi kurudisha upendo na umoja baina ya watu walioanza kupigana na kuuana kama ilivyokuwa kwa majirani zetu huko Rwanda, Burundi, Kongo Somalia; na kama ilivyo sasa huko Darfur, Sudan.

Wanaopiga na kuuana katika nchi hizo ni binadamu kama sisi na mauaji kama hayo yanaweza kabisa kutokea hapa kwetu tusipokuwa waangalifu dhidi ya hao wanaochochea uhasama kati yeu kwa kutumia vyama vya siasa.

Tukumbuke kuwa pakitokea mapigano wao na familia zao watakuwa hewani na helikopta; watakuwa wanaongoza mapigano wakiwa familia zao mbali na nchi yetu.

Kwa kupenda kwetu amani na utulivu, watu hawa wanadiriki kutuita kondoo. Wanataka tuwe nyang`au tuuane sisi kwa sisi; wanataka tuwe mbogo tutiane mapembe ili wao wafurahi kwa sababu hawatakuwa hapa wakati huo.

Kwani hatuwezi kukosoa kwa hoja nzito bila kugeuka wanyama?

Mwalimu alipenda amani na alijenga misingi mizuri ya amani nchini mwetu; alipenda na kusisitiza umoja na alijenga umoja kwa nguvu zote; aliipenda na kuihubiri sana demokrasia, na pasingekuwa Mwalimu, si ajabu mpaka sasa tungekuwa tunazungumza utawala wa chama kimoja cha siasa.

Ni Mwalimu ndiye aliyeweza kuishawishi CCM wakubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi pamoja na kuwa asilimia 80 ya Watanzania walikataa mfumo huo.

Mwalimu alichukia sana rushwa na alisema kwa nguvu sana dhidi ya wanaoshiriki kutoa au kupokea rushwa.

Alisema `rushwa ni adui wa haki.` Alitufundisha kwa kina ubaya wa rushwa, na kwa vitendo alithibitisha kuwa anaichukia rushwa kwa kuidhinisha sheria kali dhidi ya watoa na wapokea rushwa, ambayo pamoja na kifungo ni kuchapwa viboko 24.

Katika sera yake ya Ujamaa na Kujitegemea Mwalimu alilenga kujenga taifa la watu walio sawa na wanaojitegemea, watu wanaopendana na kuheshimiana kwa ubinadamu wao.

Lakini kuna watu wameihujumu sera hii, watu hawa ni wale wanaopenda ubwana mkubwa bila kuwajibika.

Ni watu wanaopenda kuwanyanyasa wengine waonekane vikaragosi mbele yao.

Watu hawa ni wale wanaopenda rushwa kutoka hata kwa maskini abeche alolo, watu dhulumati wasiopenda wengine wapate, ni watu wanojiona bora zaidi kuliko wengine, wanaopenda kuabudiwa kama miungu watu duniani. Wamepata, lakini wanataka wapate zaidi wao tu.

Kwa hiyo kama tunamkumbuka Mwalimu kwa dhati, tuenzi aliyotufundisha na kutuachia, Umoja wa kitaifa, demokrasia ya kweli, amani iliyotukuka, mshikamano, uhuru, uadilifu, uwajibikaji na moyo wakujituma na kujitolea.

Hivi vyote vinaonekana kupungua siku hadi siku, na kwa namna hii hatuna sababu ya kujidai eti kunamkumbuka Baba wa Taifa.

Asante Mwalimu kwa yote uliyotuachia, na uzidi kupumzika kwa Amani, nasi tunakuahidi kufuata mafundisho yako.

* SOURCE: Nipashe

No comments: