Saturday 27 October 2007

Kila mtu ana nafasi kujiendeleza kielimu!

Nimefurahishwa sana na habari kuwa mfungwa amesoma na kufaulu na hatimaye atatunukiwa shahada.
Hii ni changamoto kwa kila mtanzania ktk nafasi yake kuhakikisha anatumia muda wake vizuri, na kudunduliza kidogokidogo ili kujiendeleza! Hakuna kisingizio eti 'sikupata nafasi au sikuchaguliwa kwenda mlimani'. Chuo Hikuu Huria kipo kwa ajili yetu ambao hatukupata nafasi mlimani; hebu tuitumie fursa hii sasa!!
Na Mosonga

Mfungwa kutunukiwa shahada gerezani

27 Oct 2007
By Mwandishi Wetu

Mfungwa aliyehitimu masomo ya Shahada ya Sheria, atatunukiwa cheti chake gerezani na kufanyiwa sherehe yake huko huko.

Sherehe za kutunikiwa vyeti zinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam leo, ambapo wahitimu 1,145 watatunikiwa vyeti vyao.

Mfungwa huyo, Haroun Gombela ambaye ni wa kwanza kujisomea akiwa gerezani na kufanikiwa kuhitimu masomo yake, amepongezwa na Serikali kwa moyo wake wa kujiendeleza akiwa mfungwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Joseph Mungai, alitoa ufafanuzi huo juzi usiku katika kipindi cha Tuambie kinachorushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Bw. Mungai, alitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa iwapo mfungwa huyo ataruhusiwa kujumuika na wenzake katika sherehe hizo, Uwanja wa Taifa.

`Yeye atakabidhiwa digrii yake huko huko gerezani na atafanyiwa sherehe yake huko huko na magereza,` alisema.

Aidha, alisema mfungwa huyo, anaweza kuamua shahada yake ikatunzwa na magereza mpaka atakapomaliza kifungo chake, au akawakabidhi ndugu zake.

Alisema Shahada hiyo, ataitumia mara baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake.

Kadhalika Bw. Mungai, aliwataka wafungwa wengine kuiga mfano wa mfungwa Gombela, wa kujiendeleza wakati wakiwa gerezani.

`Hii inatufundisha kuwa ukiwa mfungwa, kuna nafasi ya kujiendeleza na ukatoka ukiwa na shahada yako,` alisema.

Akizungumzia suala la vitambulisho vya uraia, Bw. Mungai, alisema kuwa mwaka 2009, kila Mtanzania atakuwa anacho kitambulisho.

Alisema kuwa, mradi wa kutengeneza vitambulisho hivyo, utaanza katika mwaka huu wa fedha na utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu.

`Ifikapo mwaka 2009, kila mtanzania atakuwa na kitambulisho chake,` alisema Bw. Mungai.

Alisema, hivi sasa Serikali ipo katika mchakato wa kumpata wakala atakayetoka shirika la serikali na kupewa tenda ya kuchapisha vitambulisho hivyo.

Kuhusu wahamiaji haramu, Bw. Mungai alisema, serikali imepokea changamoto ya kuweka namba za mawasiliano zitakazowezesha raia wema kutoa taarifa moja kwa moja kwa Wizara husika wanapoona kuna watu wameingia nchini kinyume na sheria.

* SOURCE: Nipashe

No comments: