Thursday, 13 November 2008

Mbunge Richard Nyaulawa afariki dunia

JK aongoza mamia kumuaga Nyaulawa

RAIS Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Bw. Richard Nyaulawa (57) aliyefariki alfajiri ya Jumapili iliyopita akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam.

Rais Kikwete aliyeambatana na mkewe Mama Salma Kikwete, akionekana mwenye huzuni aliwaongoza mawaziri, wabunge na ndugu na marafiki wengine wa marehemu kuuaga mwili wa marehemu Nyaulawa katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Martha, Mikocheni, Dar es Salaam.

Nyaulawa aliyefariki kwa ugonjwa wa saratani ya ini pamoja na kuwa Mbunge na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, pia alikuwa mmiliki na Mkurugenzi mwanzilishi wa kampuni ya magazeti ya Business Times inayochapisha magazeti ya Majira, Spoti Starehe, Dar Leo na Business Times.

Ibada ya kuaga mwili wa marehemu Nyaulawa ilianza saa saba mchana katika kanisa hilo ambapo Rais Kikwete aliwasili kwa kustukiza katika eneo hilo mara tu baada ya ibada ya kumwombea marehemu kumalizika ambao awali Naibu Spika wa Bunge, Bibi Anne Makinda ndiye aliyekuwa akiongoza msafara wa viongozi wa Bunge.

Mara baada ya kutoa heshima zake za mwisho Rais Kikwete alikaa pamoja na mjane na watoto wa marehemu kanisani hapo kwa muda akionekana kuguswa na msiba huo.

Mwili wa marehemu ilifikishwa katika kanisa hilo ukitokea nyumbani ambapo mamia ya waombolezaji walifika kuaga.

Bada ya mwili kufika kanisani hapo Padri Paulo Haule, aliendesha ibada maalumu kwa ajili ya kumuombea marehemu Nyaulawa kabla ya mwili wake kusafirishwa leo kwa maziko yatakayofanyika kijijini kwa marehemu, Ingala, Mbeya Vijijini.

Muumini mzuri

Akitoa mahubiri mbele ya waombolezaji, Padre Haule alisema marehemu alikuwa muumini na mtu aliyekuwa akimpenda sana Mungu kwani alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo aliyeyatumia madaraka yake vizuri kwa kuhamasisha waumini wenzake kuchangia ujenzi wa kanisa hilo huku na yeye binafsi akitoa misaada ya hali na mali.

Alisisitiza kuwa marehemu Nyaulawa alishirikiana na waumini wenzake katika ibada za jumuiya kwa kukaa kwenye mikeka na kusali pamoja bila kuonesha kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kifedha wala madaraka makubwa ya ubunge.

Mchango wake ni thabiti

Wakiendelea kumuomboleza marehemu, baadhi ya wanasiasa mashuhuri nchini wamesema Bw. Nyaulawa atakumbukwa kwa mengi.

Kwa upande wake Bibi Anne Makinda alisema mchango wa marehemu Nyaulawa bungeni hautafutika kwa sababu alikuwa mbunge makini aliyechangia hoja zake kwa mpangilio, usahihi na hakudakia hoja.

Alimueleza marehemu kuwa mmoja wa watu wachache wa aina yake kwa sababu aliwapenda wabunge wenzake, wananchi wa jimbo lake na mikoa ya kusini inayozalisha chakula kwa wingi ya Ruvuma, Iringa, Mbeya na Rukwa.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Bw. Reginald Mengi alisema marehemu alikuwa Katinu wake siku za awali katika chama hicho na siku zote alikuwa mtulivu tofauti na wengi wanaobahatika kuwa na fedha kuringa sana.

Mbunge wa Kasulu (CCM), Bw. Daniel Nsanzugwanko alisema marehemu Nyaulawa alimpokea aliporudi kutoka masomoni mwaka 1995 na kumpa kazi katika kampuni ya Business Care na katika kipindi hicho alikuwa mshauri mkubwa na kumpa mbinu za kubuni taasisi za kusaidia wananchi.

Aliongeza kuwa hivi karibuni marehemu alimdokeza kuwa baada ya kustaafu ubunge alikuwa na mkakati wa kuanzisha kituo cha kuwaendeleza waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe aliyejumuika na waombolezaji wengine kanisani hapo alisema msiba huo umewagusa sana wafanyabiashana na wanasiasa kama yeye ambaye naye ni mmiliki wa gazeti la Tanzania Daima.

Mbunge wa Igunga (CCM), Bw. Rostam Aziz alisema sifa kubwa ya marehemu ni kuwa alikuwa mpole, mwema na mahiri katika kuwasilisha na kutetea hoja zake bungeni.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Bw. Christopher Ole Sendeka alisema marehemu Nyaulawa alikuwa mtu mwenye msimamo katika mambo ya msingi na yenye maslahi kwa nchi na wananchi wa jimbo lake kwa sababu hakuyumba wala kutetereka.

Mbunge wa Kawe (CCM), Bibi Ritha Mlaki alisema atamkumbuka marehemu kwani alikuwa akisali naye katika Kanisa hilo ambako anakumbuka kuwa alitoa michango mkubwa ya ujenzi wa kanisa hilo na bungeni alikuwa akishauriana naye katika masuala mbalimbali ya kibiashara na kiuchumi.

Mbunge wa Kinondoni, Bw. Idd Azzan alisema marehemu hakuwa na dharau, alimheshimu kila mmoja wa rika tofauti bila kujali madaraka yake na kabla ya kifo chake alimfuata na kupewa ushauri katika mambo mbalimbali ya kiuchumi.

Mbunge wa Muleba Kusini, Bw, William Masilingi alisema wakati fulani aliwahi kusafiri na rais kwenda India ambapo alikwenda kumjulia hali marehemu Nyaulawa alipokuwa huko kwa matibabu ambapo alimwambia kuwa akipata nafuu ataendelea kukomboa wananchi wake kwa kilimo bora cha kutumia pembejeo kutoka mkoa wa Mbeya.

Naye mbunge wa kuteuliwa wa Mjini Magharibi anayewakilisha walemavu, Bibi Zulekha Haji alisema marehemu alikuwa mchangamfu na uwezo wake mkubwa ndiyo uliwafanya wabunge wamchague kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). (source: majira, habari Na Peter Mwenda)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Richard Nyaulawa Pumziko la milele

MAISHA siku na nyakati katika dunia hii ya aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Bw. Richard Nyaulawa vimefikia kikomo rasmi baada ya kuzikwa kijijini kwake Inyala, Mbeya Vijijini, umbali wa kilometa 20 kutoka Mbeya Mjini.

Maziko hayo yaliyofanyika jana alasiri, pia yalihitimisha siku takribani tano za marehemu Nyaulawa kuliliwa na wengi, kuhuzunisha wengi na kuwaachia wengi simanzi na kutoamini kilichotokea tangu alipofariki dunia alfajiri ya Jumapili iliyopita kwa ugonjwa wa saratani ya ini.

Ni maziko yaliyowaachiwa wanafamilia yake, ndugu zake, wafanyakazi wake katika kampuni ya magazeti ya Business Times aliyoiasisi na kuiongoza vyema, tafakuri nzito, tafakuri ya maisha mapya na ukurasa mpya bila yeye.

Maziko hayo ambayo yaliongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma, Naibu Spika wa Bunge, Bibi Anne Makinda, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile, wabunge wenzake na viongozi waandamizi wa vyama mbalimbali vya siasa na wananchi, yalivuta hisia za wengi na kutoa tafsiri pana juu ya Nyaulawa kuwa mwanadamu wa aina gani katika Dunia hii wakati wa uhai wake.

Huzuni aliyokuwa nayo Rais Kikwete inaweza isieleweke kirahisi kwa wengi-si kwa sababu alimfahamu Nyaulawa kama mmoja wa wabunge makini kiasi cha kumpa nyadhifa za kumsaidia ukiwamo ujumbe wa Bodi ya Mamlaka za Bandari na uenyekiti wa Bodi ya Pareto, bali pia tafsiri moja ya huzuni ya Rais inarudi miaka ya 1970 walipokuwa katika siku ngumu za uanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo wakati Rais Kikwete akiwa mbele kwa darasa moja katika darasa la Uchumi, Bw. Nyaulawa alikuwa nyuma yake na waliokuwa nao nyakati hizo, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro aliyekuwa darasa moja na marehemu, wanamkumbuka jinsi alivyokuwa mmoja wa wanafunzi waliokuwa wakisifika kwa umahiri darasani, kiasi cha kufahamika hata kwa wanafunzi wa madarasa ya juu.

Maziko ya marehemu Nyaulawa, huzuni ya Rais Kikwete na historia hii adhimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inalikumbusha Taifa kuwa Rais Kikwete binafsi aliwahi kukumbwa na mshituko mwingine kutokana na kifo cha kiongozi mwingine mwandamizi wa nyakati hizo za UDSM-marehemu Juma Akukweti ambaye alisoma mwaka mmoja na Rais.

Mwili wa marehemu Nyaulawa ulisafirishwa jana alfajiri kwa ndege ya Zan Air iliyoongozwa na rubani Kanali Hamisi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere na kuwasili uwanja wa Ndege wa Mbeya saa 4.15 asubuhi na kusafirishwa kwenda kijijini Inyala kwa gari.

Kukusanyika kwa wananchi wengi barabarani kila mwili huo ulikokuwa ukipitishwa, kulizidi kuonesha jinsi hayati Nyaulawa alivyoishi katika Dunia hii kwa miaka yake 57 aliyojaaliwa na Mola wake.

Si wananchi wote kati ya wengi waliokuwa wakilipungia jeneza hilo, waliweza kupata fursa ya kuwasilisha uchungu uliokuwa nyoyoni mwao, lakini hotuba ya Padri Tresfoni Tweve wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bakita, Inyala, ilionekana kuwakilisha huzuni ya wengi.

Katika hotuba yake hiyo katika misa ya wafu kwa marehemu Nyaulawa, kiongozi huyo wa dini alimsifu marehemu kwa mambo matatu ambayo ni adhimu na adimu-aliipenda jamii yake; aliipenda nchi yake na alimpenda Mungu wake.

Akifafanua mtazamo wa marehemu ulioakisi mapenzi yake hayo matatu, Padri huyo alisema akiwa hai, marehemu Nyaulawa alimweleza kuwa aliingia katika siasa si kutafuta chochote kingine, bali kuitumikia nchi yake huku pia mkewe, Bibi Getrude Nyaulawa naye akistaafu kazi, ili akaishi kijijini Inyala akasaidie kuinua vikundi vya akina mama.

Pamoja na kuwa jana ilikuwa siku ngumu kwa wengi, hasa wanafamilia lakini mtu mmoja maalumu, mwenye sababu maalumu na zenye umaalumu wa pekee, Bw. Rashid Mbuguni, kipenzi cha siku nyingi na mtu ambaye walishibana na marehemu na kushirikiana sana katika biashara zao, baada ya siku tano za kuamua kutosema chochote, akihuzunika tu moyoni, jana aliamua kusema, akimuaga kwa uchungu mshirika wake.

Unapozungumzia kampuni ya Business Times inayochapisha pamoja na gazeti hili magazeti ya Business Times, Dar Leo na Spoti, kituo cha Radio Times FM 100.5, Kiwanda cha Uchapishaji cha Business Printers na kampuni ya ushauri wa biashara na uwekezaji ya Business Care Group, unazungumzia pacha wawili-Nyaulawa na Mbuguni.

Ni mawazo yao ya muda mrefu ya kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kwa kuwa na sekta ya habari iliyo huru yaliyokuwa kweli, rasmi Novemba 5 mwaka 1988 walipoanza kuchapisha nakala ya kwanza ya gazeti huru na la kwanza binafsi nchini la Business Times lililofuatiwa na Majira miaka kadhaa baadaye.

Katika miaka yote 20 ya kuwapo kampuni hiyo, Nyaulawa na Mbuguni ndivyo 'vichwa' viwili adhimu vilivyokuwa nyuma ya mafanikio ambayo kampuni hizo zimeyafikia kwa sasa.

Akimuaga mpendwa wake, mwenza wake na mshirika wake, Bw. Mbuguni alitoa ahadi iliyoonekana kuwa si ya wanafamilia na wafanyakazi wa Business Times pekee, bali ahadi yake kwa Watanzania wote, kuwa wale ambao marehemu amewaainisha kuendeleza biashara zake, atafanya nao kazi na kuwachukulia kuwa ni familia moja.

Maisha ya hayati Nyaulawa kwa miaka 57 duniani pamoja na kuhitimika kwa sifa zote zilizowaachia wengi huzuni, kwa upande mwingine yanaipa furaha familia, wafanyakazi na wabunge wenzake na wote waliomjua au kufaidika na kazi za mikono yake-kwa sababu ni mmoja wa wanadamu wachache ambao katika kipindi chote cha maisha yao, alitenda wema na hakutazama nyuma, amekwenda zake, kwa Mola wake, ni pumziko la milele.

(source: majira, Na Masoud Sanani, Mbeya)