Saturday, 8 November 2008

Mikopo Elimu ya Juu

Serikali imesema haitakopesha wanavyuo kwa asilimia 100 kama wanavyoomba iwe. Kwa hiyo wanafunzi wataendelea kuchangia gharama kama ilivyo sasa.

4 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Pinda: Hakuna mikopo asilimia 100

2008-11-08 13:47:05
Na Abdallah Bawazir, Dodoma na Godfrey Monyo, Dar


Serikali imesema haitatoa mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100 kama wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wanavyoshinikiza.

Akizungumza wakati akifunga mkutano wa 13 wa Bunge mjini hapa jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, pamoja na mambo mengine, alisema wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wataendelea kuchangia gharama za elimu, ili wanafunzi wengi zaidi waweze kupata elimu hiyo nchini.

``Sera ya uchangiaji elimu inalenga kutumia rasilimali na fedha kidogo za serikali ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata elimu ya juu, kwa hiyo, siyo busara serikali kuwalipia asilimia 100 hata wale wanaotoka kwenye familia zenye uwezo, hili ni jambo lisilowezekana,`` alisisitiza Pinda.

Alifafanua kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2008/2009 serikali imetenga Sh. bilioni 119 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kwamba endapo ingetoa mikopo kwa asilimia 100 ni wanafunzi 42,000 tu ndiyo wangeweza kukopeshwa badala ya 60,000 wanaopata hivi sasa.

``Kwa upande mwingine kuwapatia wanafunzi wote 60,000 mkopo kwa asilimia 100, kiasi cha Sh. bilioni 163.7 zingehitajika, utaratibu huu umewasaidia sana wazazi wasio na uwezo, mimi najiuliza ni kwa nini mtoto wa waziri mkuu, au spika au mbunge au mfanyabiashara maarufu afaidike na utaratibu huu badala ya kusaidia wasio na uwezo,`` alihoji.

Alieleza kuwa utoaji wa mikopo unaoongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo namba 9 ya mwaka 2004 pamoja na kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali na kwamba sheria hiyo inaweka bayana masharti ya kutoa mikopo hiyo.

``Utaratibu wa kuwabaini wasio na uwezo na wale wenye uwezo unatokana na sheria, utaratibu wa kung`amua uwezo wa kiuchumi ndiyo pekee uliyopo kwa sasa kuwatambua wanafunzi wenye uwezo kulingana na hali zao za kiuchumi.

Alisema Tanzania ndiyo nchi yenye sera nzuri zaidi ya kuchangia elimu kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki, akitolea mfano kuwa nchini Kenya wastani wa wanafunzi 120,000 wameandikishwa kwenye vyuo vikuu nchini humo, lakini wanaopata mikopo ni 10,000 tu ambapo kwa upande wa Uganda kati ya wastani wanafunzi 30,000 wanaodahiliwa kwa mwaka ni 4,000 tu ndiyo wanaopata mikopo kutoka serikalini, wakati kwa upande wa Tanzania, wanafunzi 60,000 wanapata mikopo hiyo hivi sasa.

``Tuelewe kwamba sera ya uchangiaji gharama za elimu ya juu si jambo geni, lipo kwa nchi nyingi duniani, hapa kwetu utaratibu huu hauko katika elimu ya juu peke yake, bali uko katika elimu ya sekondari, vyuo, pia katika huduma nyingine za jamii kama afya, maji na nishati.

Kwa ujumla gharama wanazolipa wanafunzi wa elimu ya juu ni za chini sana ukilinganisha na gharama halisi,`` alisisitiza Waziri Mkuu.

Katika hotuba hiyo, Pinda pia alizungumzia kashfa ya kuvuja kwa mitihani ya kudato cha nne mapema Oktoba mwaka huu.

``Taarifa za kuvuja kwa mitihani ni jambo la aibu na lilipokelewa kwa mshtuko mkubwa siyo tu kwa watahiniwa, bali pia kwa wazazi na wananchi wote kwa jumla, hali hii inatokana na ukweli kwamba kama taifa tukijenga dhana ya uvujaji wa mitihani ni dhahiri inaathiri aina ya wanataalam watakaopatikana katika nchi yetu kwa miaka ijayo`` alisema.

Alisema kuwa pamoja na kuchunguza tukio hilo, serikali itatumia matokeo ya uchunguzi huo kuimarisha Baraza la Mitihani la Taifa ili kukomesha vitendo hivyo.

Pia aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wote kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu elimu ya msingi, wanapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, bila ya kutoa vizingizio.

``Wakati tunakaribia kufika mwisho wa mwaka 2008, tunatarajia kwamba vijana wetu waliofanya mtihani wa darasa la saba watapata majibu yao wakati wowote, jumla ya wanafunzi 1,017,865 walifanya mtihani huo ambapo tunatarajia wanafunzi 631,076 sawa na asilimia 62 watafaulu na tunatarajia takribani 504,860 sawa na asilimia 80 ya waliofaulu watachaguliwa kuingia sekondari,`` alisema.

Wakati huo huo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamejiunga na vyuo vingine vya umma vilivyoanza mgomo wao Jumanne kwa lengo la kuishikiza serikali kuwapatia mikopo kwa asilimia 100.

Wakati Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Dar es Salaam (Daruso) wanatangaza kugoma, vyuo ambavyo vilikuwa tayari vimeanza vimesitisha mgomo wao kwa muda hadi keshokutwa.

Mgomo huo ulianza Jumanne wiki hii na kushirikisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Chan`gombe (DUCE),Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha Afya, Sayansi na Tiba cha Muhimbili (MUHAS).

Vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo cha Ardhi (ARU) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa.

Rais wa Daruso, Athony Machibya, aliiambia Nipashe kuwa kutokana na vurugu zilizofanyika juzi wameamua kuitisha Bunge ili kutaka ridhaa yao ya mgomo.

Alisema kikao hicho kilifanyika saa saba mchana na idadi kubwa ya wabunge walipitisha mgomo ufanyike kushikiza serikali kubadilisha sera ya utoaji wa mikopo.

Machibya alisema kuwa sera hiyo ni kandamizi na haiwapi nafasi watoto wa masikini kupata elimu na kama haitoshi sera hiyo ndiyo iliyozaa bodi ya mikopo.

Rais huyo alisema kuwa mgomo huo utaanza rasmi Jumatatu ambapo wataungana na wenzao ambao tayari wameshaanza siku chache zilizopita.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma (UVEJUTA), Godbless Charles, alisema kuwa wamesitisha kwa muda mgomo huo.

Alisema kuwa sababu ya kusitisha ni kufuata sheria ya vyuo vikuu kuwa kama mgomo ukidumu mfululizo kwa siku tatu chuo kitafungiwa na hivyo ili kujiepusha na hali hiyo wameingia madarasani kama kawaida.

Charles alisema kuwa wanashangazwa na ukimya wa serikali kuhusu mgomo wao
``Sisi tumeanza mgomo, lakini serikali imeendelea kuwa kimya maana yake nini ... na kama ni kwa sababu wanadai hawautambui umoja wetu mbona matatizo yetu yanajulikana?`` alihoji kiongozi huyo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa keshokutwa kutakuwa na mgomo mkubwa zaidi na mara hii watabuni mambo mengine ya kuishinikiza serikali kutoa kauli yenye kueleweka.

Rais wa DIT, Jerome Maharangata, alithibitisha kusitishwa kwa mgomo huo na kuahidi kuendelea nao keshokutwa.

Waziri wa Mikopo DUCE, Fransis Robat, alithibitisha kusitishwa kwa mgomo huo na kusema utaendelea wiki ijayo.

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...


'Mikopo elimu ya juu kwa 100% ni ndoto'

Habari Zinazoshabihiana
• Bodi Elimu ya Juu yazindua kampeni kukusanya mikopo 10.08.2007 [Soma]
• ...Wasomi wataka kuzungumza naye 15.08.2006 [Soma]
• Wasomi vyuo vikuu waunda tume'kuivaa' Bodi ya Mikopo 29.10.2007 [Soma]

Na Grace Michael, Dodoma

SERIKALI imesema haiko tayari kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa asilimia 100 kama wanavyodai, bali itaendelea na utaratibu wa kuchangia gharama za elimu ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata mikopo hiyo.

Mbali na hilo, pia Serikali haitakuwa tayari kuvumilia wanaochochea migomo isiyo ya lazima na isiyofuata sheria, taratibu na kanuni, kwani ina athari kubwa kiuchumi na inahatarisha amani na usalama wa nchi.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, wakati akiahirisha Mkutano wa 13 wa Bunge ambao ulichukua wiki mbili.

“Hatuna uchaguzi mwingine zaidi ya kuchangia elimu ili wanafunzi wengi wapate elimu ya juu...napenda nirudie kusema kuwa haitawezekana kutoa mikopo kwa asilimia 100, kwani kwa kufanya hivyo, ni kuwanyima wanafunzi wengine haki ya kupata elimu ya juu kama ilivyokusudiwa,” alisema Bw. Pinda.

Kuhusu mikopo alisema kwa utaratibu wa kawaida, gharama za elimu zinatakiwa kuchangiwa kati ya Serikali na mzazi na kwa kufanya hivyo, inawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata mikopo.

Alisema kwa sasa jumla ya wanafunzi 60,000 wanapata mikopo kati ya wanafunzi 80,000 waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali ambapo kama ingetolewa kwa asilimia 100, wanafunzi wachache zaidi wangeweza kupata mikopo hiyo.

“Tanzania tunatoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi tofauti na nchi ya Kenya, inayotoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 kati ya 120,000 ambapo Uganda inatoa mikopo kwa wanfunzi 4,000 tu kati ya wanafunzi 30,000 waliodahiliwa, hivyo kwa kiwango hiki utaratibu huu hauwezi kubadilika,” alisema Bw. Pinda.

Alisema pamoja na wanafunzi kutolipa ada halisi mikopo wanayolipa kwa kipindi cha miaka 10 huwa haina riba, ambapo kwa hali ya kawaida mikopo hiyo ilitakiwa kulipwa kwa riba hivyo kwa hali hiyo Serikali hubeba mzigo wa riba hiyo.

Kuhusu migomo inayojitokeza mara kwa mara, alisema migomo na maandamano yanayofanywa na vikundi mbalimbali yakiwamo maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu, migomo ya wafanyakazi wa Reli, madaktari na wauguzi, walimu na maandamano ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki si njia sahihi ya kupata haki zao.

Alisema pamoja na Serikali kuruhusu migomo katika mazingira fulani kisheria ni lazima maslahi ya nchi yazingatiwe na kuyalinda.

“Serikali inatoa mwito kwa makundi yote nchini kuacha kutumia migomo kama njia pekee ya kupata haki, kwani migomo ina athari nyingi hivyo kwa mazingira hayo, Serikali haitawavumilia wanaochochea migomo isiyo ya lazima na isiyofuata sheria, hatua kali dhidi yao zitachukuliwa,” alionya Bw. Pinda.

Aidha alisema Serikali haitavumilia watendaji wake wanaosababisha au kushindwa kutatua kero za wananchi mpaka wananchi hao wafikie hatua ya kugoma wakati uwezo wa kutatua kero hizo upo.

Kuhusiana walimu, Bw. Pinda aliwataka kujenga utamaduni wa kuwasilisha madai ya kweli ya stahili zao, ili kuharakisha uhakiki wa madeni yao na kupunguza kero ya kucheleweshwa malipo.

Alisema Serikali imeongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya pembejeo kutokana na fedha za EPA, hivyo mabadiliko katika upatikanaji wa pembejeo yatakuwapo kama ilivyokusudiwa ili kuboresha kilimo.

(source: majira 08/11/2008)

MOSONGA RAPHAEL said...

Chuo Kikuu Dar chafungwa

2008-11-13 10:19:09
Na Richard Makore


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani kimewasimamisha masomo kwa muda usiojulikana wanafunzi wote wanaochukua shahada ya kwanza kutokana na kugoma kuingia madarasani kwa wiki moja.

Taarifa iliyotolewa jana asubuhi chuoni hapo na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala ilisema wanafunzi wengine wanaochukua shahada ya uzamili, udaktari (PhD), kozi fupi na wageni kutoka nje ya nchi wataendelea na masomo kama kawaida.

Agizo la kuwasimamisha wasomi hao liliwataka wawe wameondoka mara moja eneo la chuo na hosteli zao za Mabibo zilizopo jijini Dar es Salaam.

Aidha, taarifa hiyo ilifafanua kuwa sababu ya kufunga chuo hicho ni kutokana na wanafunzi hao kugoma kuingia madarasani pamoja na kuendelea kufanya vurugu ambazo zilikuwa zinahatarisha amani katika eneo la chuo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi ya kumwaga maji ya kuwasha na askari wenye bunduki wakiwa wametanda maeneo mbalimbali ya chuo.

Baada ya kutolewa tangazo hilo na kubandikwa katika mbao za matangazo chuoni hapo, wanafunzi walionekana wakiwa kwenye harakati ya kuondoa mizigo yao ili waondoke.

Kutokana na agizo hilo kuwataka kuondoka mara moja polisi walionekana wakifuatilia kwa karibu wanafunzi hao ili kuhakikisha wanabeba mizigo yao na kuondoka.

Katika hosteli za Mabibo, Nipashe ilishuhudia baadhi ya wanafunzi hao wakiwa na majonzi wakati wakihamisha mizigo yao.

Hata hivyo, wengine walionekana wakiingia hapo wakiwa wamejazana kwenye magari huku wakiimba EPA, EPA, EPA wakiimanisha Akauti ya Madeni ya Nje.

Aidha, walisikika wakisema kuwa kama mafisadi wasingeiba fedha za EPA zingetosha kuwasomesha, lakini hivi sasa wanafukuzwa kama wakimbizi wakati wakidai mkopo wa asilimia 100.

Baadhi ya wanafunzi hao walionekana wakipita katika maeneo ya chuo na hosteli za Mabibo huku wakiongea wenyewe kama watu waliorukwa na akili.

Akizungumza na Nipashe, Naibu Mkuu wa Makamu wa Chuo ambaye anashughulikia utawala, Profesa Yunus Mgaya alisema, chuo hicho kimewatimua wanafunzi hao kwa maagizo ya Baraza la chuo hicho.

Alisema mwanafunzi yoyote atakayekaidi agizo la kuondoka hapo atakumbana na polisi ambao muda wote walikuwa wakirandaranda eneo la chuo na magari yao.

Aidha, Profesa Mgaya alisema, wanafunzi wa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (IJMC) ambayo ipo chini ya chuo hicho hawakuguswa na adhabu.

Alisema wanafunzi hao wa IJMC waliandika barua mapema kwa uongozi wa chuo kuwataarifu kwamba hawashiriki katika mgomo.

Kwa upande wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha jijini Dar es Salaam, (Duce) alisema, adhabu hiyo pia haitakihusu.

Hata hivyo, alikiri kwamba Duce jana asubuhi kulikuwa na mgomo na kwamba kama wataendelea hatua zaidi kama zilizochukuliwa na chuo kikuu sehemu ya mlimani zitachukuliwa pia kwao.

``Duce kipo chini ya chuo hiki, lakini kinatawaliwa na bodi ya magavana hivyo siwezi kukitolea maelezo zaidi ila taarifa nilizonazo jana walikuwa na mgomo,`` alisema.

Akizungumzia Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa nacho alisema kulikuwa na mgomo, lakini hatua za kuwatimua wanafunzi wake bado hazijachukuliwa.

Akizungumza na Nipashe jana asubuhi Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Antony Machibya, alisema kuwatimua wanafunzi sio suluhisho la madai yao.

Alisema ukweli unabakia pale pale kwamba Serikali ina jukumu la kuwapatia mkopo kwa asilimia 100 bila kujali madaraja wala familia wanazotoka.

Alisikitishwa na kitendo cha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe kuwapa ahadi hewa kwamba atamtuma mtu ili akazungumze nao, lakini juzi jioni wakashangaa kuona akitangaza kwenye televisheni na kuwataka waingie madarasani.

Alisema Daruso ilionana na Profesa Maghembe juzi na kumueleza madai yao ambapo aliahidi kumtuma mtu ili akutane nao, lakini akawadanganya.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ya Profesa Maghembe kuwakacha, Daruso itamtafuta Rais Jakaya Kikwete ili kumpa malalamiko yao baada ya kubaini kuwa wengine wote ni wababaishaji na hawawezi kutatua matatizo yao.

Akizungumza juzi, Profesa Maghembe, alisema sera ya uchangiaji wa elimu ya juu haiwezi kubadilika kwa haraka kama wanavyotaka wanafunzi hao.

Alisema sera hiyo ilipitishwa na Bunge na kwamba ili iweze kubadilishwa lazima ipitie huko.

Akizungumza wakati akiahirisha Bunge wiki iliyopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa asilimia 100 ni kitu kisichowezekana.

Utaratibu wa sasa baadhi ya wanafunzi wanapata mkopo kwa asilimia 60, 80 na wengine wasikuwa na uwezo wanapata kwa asilimia 100.

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...

Wanafunzi Chuo Kikuu Moshi `wapagawa`
2008-11-18 14:10:16
Na Jackson Kimambo na Salome Kitomary, PST, Moshi

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Stadi za Biashara (MUCCoBs) wamegoma kuingia madarasani na kufanya uharibifu wa mali pamoja na kuwashambuliwa kwa mawe na mchanga wahadhiri wa chuo hicho, kwa lengo la kushinikiza chuo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutatua matatizo yao matatu ya msingi.

Kutokana na mgomo na vurugu hizo, jana Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) pamoja na askari kanzu wakiwa na silaha za aina mbalimbali walikizingira chuo hicho ili kuhakikisha hali ya amani na utulivu inarejea.

Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Paul Saria, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa kuwa mgomo huo una lengo la kuishinikiza HESLB kuwapatia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa wakati kwani hadi sasa hawajapata mikopo hiyo.

Alisema tangu waingie chuoni humo kati ya wanafunzi zaidi ya 595 ni 123 pekee ndio wamepata mikopo hali inayowalazimu wengine kuishi maisha ya tabu chuoni humo na hivyo kushindwa kuzingatia masomo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana chuoni humo, pia wanafunzi hao wanaungana wa wanafunzi wengine wa vyuo vikuu vya umma nchini waliogoma kuishinikiza serikali kuwapatia mkopo kwa asilimia 100 tofauti na ilivyo kwa sasa, wanataka sera ya uchangiaji wa elimu ya juu nchini ibadilishwe.

Mgomo huo ulioanzishwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza uliungwa mkono na wa mwaka wa pili na tatu, baada ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuwashambulia wenzao waliokuwemo madarasani wakiendelea na masomo yao.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Suleiman Chambo, alisema kutokana na mgomo huo ambao umaenzishwa na kushinikizwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza, kamati ya taaluma ilikutana kwa dharuara.

Alisema katika kikao hicho iliamuliwa kuwasimamisha masomo wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa muda usiojulikana hadi hapo itakavyotangazwa vinginevyo na uongozi wa chuo hicho.

``Wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wanapita darasa hadi darasa wakishinikiza wenzao kutoka madarasani na kufukuza walimu waliokuwa wakiwafundisha kwa kupiga kelele, kurusha mawe na kuwamwagia mchanga hali iliyowalazimu walimu kukimbia na wanafunzi kutoka na kuungana na wenzao,`` alisema Prof. Chambo.

Prof. Chambo aliongeza kuwa mara watakapotangaziwa kurudi wanafunzi watalazimika kufuata mashariti matatu, ikiwemo ya kuandika barua ya uthibitisho wa kulipa asilimia 100 ya ada, kuomba kurudi chuoni na kufuata mashariti ya chuo pamoja na kuleta vyeti halisi vinavyothibitisha sifa zao.

Alisema pia watakaobainika kuwa vinara wa mgomo huo watachukuliwa hatua za kinidhamu kama kusimamishwa masomo na kwamba wanafunzi hao wanatakiwa kuwa wawe wameondoka chuoni hapo ifikapo jana saa 10 jioni.

Alisema katika mgomo huo wahadhiri wanne waliokuwa madarasani wakifundisha walishambuliwa hali iliyowalazimu wengine kujificha chini ya meza na wengine kukimbia ili kujiokoa.

Tangu wiki iliyopita vyuo vikuu vya umma vimekumbwa na wimbi la migomo, wakiishinikiza serikali kutoa mkopo kwa asilimia 100 kwa ajili ya kugharimia elimu ya juu.

Wanaitaka serikali kubadili sera ya mikopo kwani inabagua wanafunzi kwa misingi ya kipato.

Mgomo huo ulianza katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani na baadaye vyuo vingine kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce). Vyuo vyote hivyo vimesimamisha wanafunzi kutokana na migomo hiyo.

Ardhi waanza mgomo
Naye Simon Mhina anaripoti kuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (Ardhi University) jana walianza mgomo baridi, ambao unatarajiwa kuwa mkubwa leo, wakidai kukatwa fedha za kujikumu kwa chakula, kupata mikopo asilimia 100, pamoja na kushinikiza wenzao waliofukuzwa Septemba mwaka huu warejeshwe.

Wanafunzi hao walikusanyika kwenye viwanja vya chuo hicho mapema asubuhi huku wakihamasishana kutoingia darasani, hadi madai yao yatekelezwe.

Hata hivyo, majira ya saa 4.30 wanafunzi hao walionekana kugawanyika huku wengine wakidai taarifa za mgomo huo zimekuwa za kushtukiza.

Wanafunzi hao walioonekana kuwa na jazba, kila upande ulionekana kutetea hoja yake, hali iloyosababisha mvutano mkubwa.

Baadaye baadhi ya wanafunzi waliingia madarasani huku wengine wakishikilia msimamo wao wa kutoingia darasani.

Mmoja wa `vinara` wa mgomo huo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema `wamewaruhusu` wenzao wanaodai taarifa za mgomo zimechelewa kuwafikia waingie darasani, lakini leo wataungana wote kugoma.

Kinara huyo ambaye ni mmoja wa serikali ya wanafunzi alisema wameamua kuitisha mgomo huo kwa vile wanayo madai makubwa kuliko hata yale yaliyotolewa na vyuo vikuu vingine nchini, ambavyo tayari vimefungwa.

Alisema hakuna sababu yoyote ya kuendelea kusoma, wakati wenzo waliotimuliwa wanaendelea kusota mitaani.

Kuhusu kukatwa pesa za kujikimu, kinara huyo alisema wao ni watoto wa masikini, wazazi wao wameshindwa kuwalipia ada inayotakiwa, lakini chuo kimeamua kuwakata fedha hizo ili kufidia.

DIT nako kwachemka
Naye Mashaka Mgeta anaripoti kuwa wanafunzi wa shahada ya kwanza katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wamegoma kuingia darasani, ili kuishinikiza serikali ibadili sera ya kuchangia elimu ya juu, na kuwarejesha wanafunzi waliofukuzwa vyuo vikuu bila masharti.

Rais wa serikali ya wanafunzi (DITSO), Cleophace Maharangata, alisema jana kuwa mgomo huo ni utekelezaji wa azimio la Baraza la wanafunzi, lililofanyika Novemba, 5 mwaka huu.

``Suala la kuwepo mgomo huu lilipitishwa na Baraza la wanafunzi, lakini tuliusitisha ili kusubiri tamko la serikali,`` alisema.

Maharangata, alisema wakati wakiwa katika subira hiyo, kauli iliyotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, kuhusu ugumu wa kubadilishwa sera hiyo, imewafanya watekeleze azimio la kugoma.

Mapema jana asubuhi, wanafunzi waliokadiriwa kufikia 600 waligoma kuingia madarasani, badala yake waliandamana kwenye maeneo tofuati yaliyopo ndani ya DIT.

Wanafunzi hao walikuwa wanaimba nyimbo na wengine walibeba mabango yaliyohimiza umuhimu wa kuifanyia marekebisho sera hiyo.

Mkuu wa DIT, Profesa John Kondoro, alisema uongozi wa chuo hicho hauna taarifa zilizowasilishwa rasmi, kuhusu mgomo huo.

``Wameamua kugoma, lakini uongozi haujui sababu yake, kwa maana hatujapata taarifa rasmi kutoka kwa wanafunzi,`` alisema.

-Alisema wanafunzi hao, waliokutana nyakati za usiku, walikubaliana kuhusu kada inayostahili kugoma, kutokana na chuo hicho kuwa na wanafunzi wa shahada, stashada na wanaochukua masomo ya jioni.

``Tumeambiwa kwamba waliogoma ni wale wa shahada ya kwanza tu, sasa hii inaonekana kwamba mgomo huu haukukubaliwa na wanafunzi wote,`` alisema.

Aidha, Profesa Kondoro alisema wanafunzi wachache wa shahada ya kwanza, waliendelea na masomo wakati wenzao wakigoma, hali iliyowafanya idadi kubwa ya walioshiriki mgomo huo, kuwatoa kwa nguvu kutoka darasani.

Kwa mujibu wa Profesa Kondoro, uongozi wa DIT uliwaagiza wakuu wa idara, kuwaita wanafunzi wahusika, ili kuzungumza nao kupata suluhu ya mgomo huo.

SOURCE: Nipashe