Saturday, 22 November 2008

Hii ndio Roho mbaya, Uchu na Dhuluma!!

Unapopokonya mali ya mkeo usiyoitolea jasho

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niligusia barua pepe ya msomaji mwenzetu ambaye alilalamika kuhusu utapeli aliofanyiwa na mumewe kutaka kumpokonya nyumba yake aliyoijenga mwenyewe kabla ya ndoa yao.

Hata hivyo, nikampatia majibu ya mwanasheria kuhusu kilichomo ndani ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kwamba mali iliyochumwa na mke au mume kabla ya ndoa bado itabaki kwa mmliki isipokuwa ile au zile mali zilizopatikana ndani ya ndoa yao ndizo wanazopaswa kugawana.

Kufuatia makala ile, yupo jamaa mmoja aliwasiliana nami na kunielezea mtafaruku ulioikumba familia ya ndugu yake, ukifanana na mkasa tuliozungumzia wiki iliyopita. Siyo kisa kizuri ni cha kusikitisha kwa kuwa kilipelekea kifo.

Hiyo ikanithibitishia kuwa kumbe wapo ving`ang`anizi wa mali za wenzao ambazo hawakuzitolea jasho kuzitengeneza.

Katika simulizi ya tukio hilo lililotokea miezi kadhaa iliyopita katika mkoa mmoja nchini, akasema familia hiyo katika mwaka wa kwanza wa ndoa yao, kulikuwa hakuna matatizo.

Lakini kuanzia mwaka jana, mke na mume wakawa na mzozo wa mara kwa mara ambao marafiki wa karibu na pia majirani walidai kuwa huenda ulitokana na kutopata mtoto.

Hata hivyo, kwa mujibu wa jamaa huyu anayetoa simulizi kutokana na ukaribu na familia hiyo, akasema kuwa ugomvi wa wanandoa hao ulitokana na mali alizokuwa nazo mke kabla ya kuoana ambazo mume alizitaka.

Mwanamke huyo alikuwa na kazi nzuri, msomi na mchakarikaji katika kujiinua kimaendeleo.

Mumewe alikuwa mtu wa kawaida tu aliyeoana na mwanamama huyo, huku akiwa ameshajenga nyumba ambayo ndimo walikuwa wakiishi.

Inasemekana kuwa jamaa yule alihamanika kumpenda bibie kutokana na kazi nzuri aliyokuwa nayo na pia magari yake mawili ya kifahari.

Mzozo hasa ulikokea pale mume huyu alipoanza kumlazimisha bibie ampe gari moja alimiliki, lakini akawa anamkatalia.

Shinikizo kubwa la mume likiwa kwamba maadam amemuoa kihalali, basi mali zote za mke ni mali yake pia.

Hilo mke akalikataa na kumwambia kuwa kama anataka gari mojawapo itabidi amkopeshe kwani hata yeye magari hayo hakuyapata kirahisi bali kupitia mikopo katika benki na bado alikuwa hajamaliza deni.

Inavyosemekana mume huyu baada ya kuona mama ametia ngumu na magari yake, akaenda kupata ushauri kwa marafiki zake.

Unajua tena marafiki wengine siyo wazuri. Wapo watakaokushauri kuchukua maamuzi ya busara na wengine maamuzi ya maangamizi.

Siyo kila mtu anafurahia maisha au maendeleo ya mwenzake kwani wengine ni wabomoaji wakubwa na nyumba za wenzao.

Wanakupa ushauri mbovu, kisha wanakaa pembeni kusubiri matokeo, kisha wanakulaumu eti ingekuwa ni yeye au wao wasingechukua uamuzi ule. Ebo! Si ni wewe uliyemshauri?

Ufisadi wa kiroho huu, au siyo msomaji wangu?
Naam. Usiku mmoja ukazuka mzozo mkubwa kati ya wanandoa hao.

Majirani ilibidi wasikilizie kwenye paa na nyufa za madirisha ambako sauti zilisikika.

Inadaiwa kwamba baada ya muda sauti ilififia lakini mama yule akasikika akimsihi mumewe asimpige sindano.

Kisha ukimya ukatanda.
Ila kesho yake asubuhi, kumbe mama yule alikuwa tayari amefariki.

Bwana akamchukua haraka haraka na kumpeleka katika hospitali moja ambako baadaye aliwasiliana na jamaa zake, jamaa na marafiki kuwajulisha kuwa mwenzake(mkewe) amefariki dunia.

Jamaa zake hawakuamini ikabidi wakimbilie hospitali kujua kilichomuua. Wakataka mwili wa marehemu ufanyiwe uchunguzi lakini mume akazuia usiguswe na kwamba kinachotakiwa ni kuandaa mazishi, basi.

Hata wauguzi waliposhinikizwa na ndugu za marehemu uchunguzi ufanyike kujua chanzo cha kifo walikataa kufanya hivyo.

Ikahisiwa kuwa huenda ni njama za bwana yule kutaka kuficha ukweli wa kilichosababisha kifo kile.

Katika kikao cha maandalizi ya mazishi ulifumuka mvutano mkali, huku upande mmoja ukitaka uchunguzi ufanyike na mwingine ukitaka mazishi yafanywe bila kuchelewa.

Hatimaye, marehemu alizikwa lakini akiacha maswali lukuki. Kisa ung`ang`anizi wa mali usizozitolea jasho. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.

Mpenzi msomaji, hivi unapobaki na mali ambayo unajua fika kuwa siyo yako na mwenyewe aliyeitafuta kwa jasho ametangulia mbele za haki huku akiipigania mali hiyo bila mafanikio, utakuwa na raha gani?

Wiki ijayo nitakupa mfano mwingine pia wa kusikitisha ambapo mama alikufa kwa ugonjwa wa moyo baada ya kubaini kuwa gari lake, mume huligawa kwa hawara atambe nalo mjini kila anapokuwa safarini. Usikose, fuatilia kisa hicho uone walimwengu walivyo wabaya na vya wenzao.

Niishie hapa msomaji wangu kama una maoni nikandamizie kupitia barua pepe flora.wingia@guardian.co.tz
Wasalaam.
(source: Nipashe, 2008-11-16 13:22:35. Na Anti Flora Wingia)

No comments: