Tuesday 25 November 2008

Ajali za barabarani zaua Dom na Singida

Ajali zaua 25 papo hapo
*Zahusisha mabasi ya Zuberi, Sai Baba na Fuso
*Abiria 84 wajeruhiwa, 50 walazwa Dom, Singida
*Basi la Zuberi labiringika korongoni Sekenke

Hillary Shoo, Singida na Flora Amon, Dodoma
ZAIDI ya watu 25 wamekufa na wengine 84 kujeruhiwa ambapo 50 wamelazwa katika hospitali za Singida na Dodoma baada ya mabasi mawili kupata ajali tofauti katika mikoa hiyo.

Katika ajali ya Singida, watu zaidi ya 20 walipoteza maisha na 35 kulazwa katika hospitali ya Iramba, huku ajali ya Dodoma walikufa watu watano na 15 kulazwa katika hospitali ya Mkoa ya Dodoma.

Wakati ajali ya Singida ilitokea juzi saa 2.30 asubuhi katika Mlima Sekenke ilihusisha basi la Zuberi lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, ya Dodoma ilihusisha basi la Sai Baba lililokuwa likitoka Dodoma kwqenda Dar es Sakaam na kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso.

Basi la Zuberi ni aina ya Scania lenye namba T 677 AGJ wakati la Sai Baba ni namba T 700 ADK na lori la Fuso ni namba T 870 ASK.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Bibi Celina Kaluba alisema chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa basi hilo na mwendo wa kasi.

Kamanda Kaluba alisema hadi jana idadi kamili ya watu waliofunikwa na basi hilo ilikuwa haijajulikana vizuri kutokana na ugumu wa kazi ya uopoaji ambapo basi hilo lilipinduka na kuporomoka kwenye korongo na kulala chali.

Hata hivyo, Kamanda Kaluba alisema hadi juzi saa 10 jioni idadi ya abiria waliokuwa wamekufa ilifikia 17 na kazi kubwa ilikuwa ni namna ya kuligeuza basi hilo ambalo limepinduka chali huku zana zinazotumika zikiwa duni, hali iliyofanya kazi ya uopoaji kuwa ngumu.

Akisimulia chanzo halisi cha ajali hiyo Kamanda Kaluba alisema imetokea kutokana na ubovu wa basi hilo na ubishi wa abiria wakimlazimisha dereva kuendelea na safari huku wakijua kuwa basi hilo lilikuwa likihitaji matengenezo.

Alisema baada ya mabishano makali dereva wa basi hilo, ambaye alinusurika katika ajali na kukimbia, aliamua kulipeleka gari hilo kituo cha Polisi kwa ajili ya ukaguzi.

"Baada ya ukaguzi tuliwaamuru walipeleke gereji iliyopo eneo la Namfua mjini hapa lakini baadae tukasikia kuwa abiria walimlazimisha dereva kuendelea na safari," alisema Kamanda Kaluba na kuongeza kuwa basi hilo lilikuwa na matatizo kwenye 'kompresa' na breki.

Alisema majina kamili ya waliokufa bado hayajajulikana lakini kazi inaendelea kwenye eneo hilo na majina kamili ya marehemu na majeruhi yalitarajiwa kupatikana jana baada ya kazi hiyo kumalizika.

Mmoja wa majeruhi aliyenusurika kwenye ajali hiyo, Bw. Ahmad Seleman mfanyabiashara wa Mwanza, alidai kuwa mara baada ya kufika kwenye mlima huo mkali, aliona basi likiwa katika mwendo mkali.

"Baadaye lilipanda kwenye kilima kikali kwa kasi na kujikuta likitumbukia kwenye korongo kubwa la mlima huu, kwa kusema kweli dereva pale hakuwa na ujanja, kwani mwendo ulikuwa mkali mno, we fikiria kupanda kwenye kile kilima si mchezo," alisema.

Akizungumza kwenye eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Parseko Kone, alisema alisikia kuwapo kwa ajali hiyo akiwa kwenye ziara ikabidi kuahirisha na kwenda eneo la tukio hilo saa 3 asubuhi jana.

Hata hivyo, Bw. Kone alisema tayari ameagiza tingatinga kutoka kampuni ya kichina ya CGC iliyoko Isuna kwenda Sekenke kusaidia kuligeuza basi hilo ili kuopoa miili zaidi iliyokandamizwa kwenye korongo hilo.

Bw. Kone alisema vifaa vinavyotumika ni duni, hivyo kazi ya kuopoa miili ni ngumu, lakini aliwapongeza vijana wa Shelui kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha miili hiyo inaopolewa yote ili kupata idadi kamili.

"Kwa kweli hii ni ajali mbaya sana kutokea katika mkoa wangu, huwezi kuamini kama kuna watu wamepona kwenye ajali hii, inanisikitisha sana," alisema kwa masikitiko Mkuu huyo wa Mkoa, huku machozi yakimlengalenga.

Nako Dodoma, Flora Amon anaripoti, kwamba watu hao watano walikufa papo hapo na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea Manchali.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Godfrey Mtey, aliwaambia waandishi wa habari hospitalini hapo jana kuwa walianza kupokea maiti na majeruhi jana saa 7.30 mchana.

Dkt. Mtey alisema kati ya watu watano waliokufa ni mmoja tu ndiye aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Seleman Hassan, mkazi wa Tanga ambapo wengine wanne majina yao bado hayajafahamika.

Aliwataja walijeruhiwa kuwa ni Bw. Miraji Omar (17) mkazi wa Kiteto, Bw. Michael Kibisa mkazi wa Chinangali, Bibi Scholastica Zakaria, Bw. Jonas Jefunila wa Maili mbili, Dodoma, Bw. Zacharia Mgalo (30), mkazi wa Dar es Salaam, mtoto Erasto Peter miezi 9, wa Mpalanga na Bw. Baraka Mlumba wa Ihumwa.

Wengine ni Bw. Maneno Ngomai (29), Bw. Mahomanyika, Bibi Mariam Senyo (23) mkazi wa Chadulu, Dodoma, Bw. Shaaban Mustapha (14) wa Vingunguti Dar es Salaam, Bw. Yohana Seterina (26) wa Dar es Salaam, Bw. Shaaban Bakari (10) wa Kiteto na Bw. Haruna Saimon wa Majengo, Dodoma, Bibi Feli Nemsudi (28) wa Arusha na Bw. Alikadi Emmanuel (32) wa Singida.

Alisema jumla ya majeruhi 49 walifikishwa hospitalini hapo na kati yao 34 walitibiwa na kuruhusiwa na aliongeza kuwa waliolazwa wamevunjika mbavu, miguu na mikono.
(source: majira, 25/11/2008)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

20 wafa, 88 hoi ajali ya mabasi

2008-11-25 14:09:37
Na Waandishi Wetu, Singida na Dar


Watu 20 wamekufa na wengine 88 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti za magari moja ikihusisha basi kupinduka na lingine kugongana uso kwa uso na lori, katika mikoa ya Singida na Dodoma.

Katika ajali iliyotokea mkoani Singida, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Celina Kaluba alisema watu 15 walikufa na wengine 35 kujeruhiwa.

Kamanda Kaluba alisema ajali hiyo ambayo ilitokea jana saa 2:00 asubuhi baada ya basi la Zuberi kuacha njia na kuangukia kwenye korongo katika mteremko wa mlima Sekenke, wilayani Iramba.

Alisema basi hilo lenye namba za usajili T 677 AGT, lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Dk. Anthony Mboru alithibitisha kupokea majeruhi 35 wa ajali hiyo ambao wamelazwa hospitalini hapo.

Kamanda Kaluba alisema polisi wanaendelea na upelelezi kujua chanzo halisi cha ajali hiyo.

Alisema juhudi za kuwaokoa majeruhi na mali zao, zilikuwa zikiendelea baada ya kuagiza greda la kulivuta basi hilo.

Kamanda Kaluba alielezea wasiwasi wake kuwa huenda idadi zaidi ya waliokufa na majeruhi ikaongezeka iwapo kutakuwa na watu walionaswa ndani ya basi hilo.

Habari kutoka mkoani Dodoma, zinasema watu watano wamekufa papo hapo na wengine 53 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Saibaba lililokuwa linatoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Waliokufa katika ajali hiyo ni madereva wa magari hayo, utingo wa Fuso na abiria wa basi, pamoja na mtu mmoja anayedaiwa kuwa na matatizo ya akili.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 6:00 mchana kwenye kijiji cha Manchari, kilomita 40 toka Dodoma mjini na chanzo inadaiwa ni mtu mmoja mwenye ugonjwa wa akili ambaye alikuwa akivuka barabara.

Wakisimulia tukio hilo, baadhi ya majeruhi waliozungumza na Nipashe katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, walisema basi hilo lenye namba za usajili T 700 ADK liliondoka Dodoma jana saa 5:00 asubuhi.

Walisema, lilipofika katika kijiji hicho, huku likiwa kwenye mwendo wa kasi lilimkwepa kichaa aliyekuwa anavuka barabara na kwenda upande wa pili ambako kichaa huyo alikutana na Fuso lenye namba za usajili T 870 ASK na alirudi tena barabarani, na wakati huo tayari dereva wa Fuso na Saibaba walikuwa wameshapoteza mwelekeo na kugongana.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfrey Mtei, hospitali hiyo imepokea majeruhi 53 kati yao 15 wamelazwa na wengine 34 walitibiwa na kuruhusiwa.

Alisema, majeruhi hao ambao wamelazwa wodi namba 1, 8, 11, na 15, wameumia sehemu mbalimbali za mwili na wengine kuvunjika mikono na miguu.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Miraji Omary (17), mkazi wa Kiteto, Michael Kibisa, mkazi wa Chinangali Dodoma, Scholastica Zakaria, Jonas Luana, mkazi wa Maili Mbili, Zacharia Mgalo (30), mkazi wa Dar es Salaam, Erasto Peter (8) mkazi wa Mpalanga.

Wengine ni Barlea Mlumba (28) wa Ihumwa, Maneno Ngoma (29) wa Mahomanyika, Mariam Senyo (23) wa Chadulu, Shabani Mustapher (10) Vingunguti Dar es Salaam, Haruna Simon (14) wa Majengo, Yohana Setelina (26) wa Dar es Salaam, Shabani Baker, wa Kiteto, Fany Nemsuli (28) wa Arusha na Arkard Emmanuel (32) wa Singida.

Maiti hao wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakisubiri kutambuliwa na ndugu zao.

Habari hii imeandikwa na Jumbe Ismaily, Singida na Mary Edward, PST Dodoma

SOURCE: Nipashe 25/11/2008.