Tuesday 4 November 2008

Mipango miji Lushoto: Vijiji kuwa vitongoji

Vijiji 14 vyafutwa Lushoto...

Serikali imevifuta vijiji 14 vilivyokuwa vinaunda Kata za Ubiri na Lushoto mjini na kuvipa hadhi ya kuwa vitongoji baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa kibali cha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji mdogo wa Lushoto.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, Gwatako Nyakoki, alisema amri ya kuvifuta vijiji hivyo na kupewa hadhi ya kuwa vitongoji, inatokana na sheria ya serikali za mitaa namba 7 ya mwaka 1982.

Alisema sheria hiyo inatoa mamlaka kwa vijiji kujifuta na kuwa vitongoji ambavyo vitawaruhusu wenyeviti wanaoviongoza kuwa wajumbe wa baraza la mamlaka hiyo.

Nyakoki aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Mamlaka hiyo uliofanyika mjini hapa mara baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na kukabidhiwa rasmi hati ya kuiongoza.

``Nimekabidhiwa rasmi mikoba ya kuiongoza mamlaka hii ambayo sasa inaanza kazi kwa mujibu wa sheria, ninachokiomba kwa sasa ni ushirikiano kati yangu na wananchi wa mji wa Lushoto…kwa kweli kazi ya kuongoza Mamlaka hii ni ngumu kwa sababu tunatakiwa kukazana ili tupewe hadhi nyingine ya kuwa Halmashauri ya Mji,`` alisema Ofisa huyo aliyeteuliwa akitokea Idara ya Maendeleo ya Jamii.

Awali akifungua rasmi shughuli za mamlaka hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Lucas Shemndolwa alisema Halmashauri yake inakusudia kutoa ushirikiano mkubwa kwa mamlaka hiyo ya mji ili kuisaidia iweze kujitegemea kama zilivyo mamlaka nyingine za miji ya Korogwe, Njombe na Kibaha.

Akizungumzia utendaji wa mamlaka hiyo, Shemndolwa aliitaka kutumia fursa zilizopo wilayani hapa zikiwemo rasilimali mbalimbali za asili kujiimarisha kiuchumi na kuufanya mji huo kuwa sehemu ya mfano nchini.

(SOURCE: Nipashe, 2008-11-04 12:06:21. Na Godfrey Mushi, Lushoto)

No comments: