Saturday 8 November 2008

EPA: watuhumiwa kutoka BoT mahakamani

Watuhumiwa zaidi kuhusu kashfa ya EPA wamesomewa mashtaka jana. Hawa ni wafanyakazi wa Benki Kuu ya TZ.

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Vigogo wanne wa BoT kortini kwa kusaidia EPA

2008-11-08 13:50:24
Na Hellen Mwango na Joseph Mwendapole


Maofisa wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu wakikabiliwa na jumla ya mashitaka matano ya kuhusu Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Walifikishwa mbele ya Mahakimu wawili tofauti, Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja na HakImu Mkazi Warialwande Lema kwa tuhuma za kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi na kujipatia ingizo isivyo halali na kuisabanishia serikali hasara ya jumla ya Sh bilioni 4.

Washtakiwa hao ni Mkuu wa Idara ya Madeni, Imani Mwakosya; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Madeni, Ester Komu; Kaimu Mwanasheria wa BoT, Bosco Kimela na Mwanasheria wa benki hiyo,Sofia Joseph.

Katika kesi ya kwanza, washtakiwa Mwaksyosa, Komu na Kimela kwa pamoja waliunganishwa na Rajabu Maranda, katika shtaka la kugushi, wizi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 207,284,391.44 Agosti 18 mwaka 2005.

Mshtakiwa Maranda juzi alisomewa mashitaka mengine ya kugushi, kuwasilisha na kujipatia kwa njia ya wizi Sh. 207,284,391.44 mali ya BoT kwa kupitia kampuni ya Rashhas ya Tanzania na General Marketing ya nje ya nchi.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa pili, watatu na wanne wakiwa waajiriwa wa BoT kwa kutumia nyadhifa zao walizembea kazini na kuidhinisha malipo yasiyo halali hivyo kuisababishia serikali upotevu wa kiasi hicho cha fedha. Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hauna pingamizi la dhamana endapo washtakiwa wataomba na kutimiza masharti yatakayotolewa na mahakama.

Baada ya madai hayo,Wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliomba mahakama itoe masharti mepesi kwa wateja wake.

Katika uamuzi wake, Mahakama iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 69 kila mmoja.

Pia, washtakiwa walitakiwa kutoa Sh. milioni 104 taslimu kama sehemu ya dhamana yao.

Aidha, walitakiwa wawasilishe hati za kusafiria na wasitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Hata hivyo, washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na walipelekwa rumande hadi Novemba 21 mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa maelezo ya awali.

Katika kesi nyingine, washtakiwa Rajabu Maranda, Farijala Hussein, Ester Komu, Imani Mwakyosa na Sofia Joseph ambaye ni Mwanasheria wa BoT, walIosomewa mashitaka ya kugushi na wizi wa Sh. 3,868,805,737.13.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mkazi, Warialwande Lema.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walighushi hati za kuhamisha mali kwa jina la kampuni ya Mwibare Farm ya Tanzania na Lakshmi Textile Mills Ltd ya Mumbai.

Katika shtaka la tatu, Wakili alidai kuwa washtakiwa hao waliiba Sh. 3,868,805,737.13, mali ya BoT.

Pia washtakiwa hao wanashtakiwa kwa kujipatia ingizo la fedha hizo baada ya kudanganya kwamba Kampuni ya Lakshmi imehamishia deni hilo kwenye akaunti ya kampuni ya Mwibare Farm.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Desemba 7 mwaka 2005 wakiwa waajiriwa wa BoT, kupitia nyadhifa zao walizembea kazini na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa walikana mashitaka hayo.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika na hauna pingamizi La dhamana.

Mahakama iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja. Pia walitakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria.

Masharti mengine ya dhamana ni kila mmoja kutoa Sh. milioni 450 taslim kama dhamana au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hizo na iambatane na taarifa ya mthamini wa serikali.

Kabla ya kupandishwa kizimbani, baadhi ya washtakiwa hao walikuwa wakibubujikwa na machozi wakati wakisindikizwa na askari kwenda kwenye mahabusu ya mahakama hiyo.

Mmoja wa washtakiwa alionekana akilia na kuonyesha ishara ya msalaba mara kwa mara huku wengine wakibubujikwa na machozi.
Kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Novemba 13 mwaka huu.

Washtakiwa hao wanafanya idadi ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo wakidaiwa kuchota fedha za BoT kupitia akaunti ya EPA kufikia 17.

Hali kadhalika, wakati maofisa hao wakisomewa mashitaka yao, washtakiwa 11 kati ya 13, akiwemo Jeetu Patel waliofikishwa mahakamani juzi wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana huku wawili wakitimiza masharti na kuwa nje kwa dhamana.

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...

...wawili wa EPA wajidhamini kwa 800m/-

2008-11-08 13:48:54
Na Waandishi Wetu


Wakati washtakiwa 15 wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakiendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, akiwemo Jeetu Patel, washtakiwa wawili kati yao wamejidhamini kwa Sh. milioni 400 taslim kila mmoja.

Pia washtakiwa hao wametimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika kama ilivyoagizwa na Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Saam.

Washtakiwa hao ni Davies Kamungu na Godfrey Mosha wanaokabiliwa na mashitaka 15 ya kugushi, kuwasilisha nyaraka bandia na kujipatia kwa njia ya wizi jumla ya Sh. 2,041,899,876.45.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Jumatano wiki hii na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Warialwande Lema.

Baada ya kusomewa mashitaka yao, upande wa mashitaka ulidai kuwa hauna pingamizi dhidi ya dhamana kwa washitakiwa.

Mahakama iliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 240.

Sharti lingine walilopewa na mahakama ni kutoa nusu ya fedha wanazodaiwa kuiba, ambapo ziligawanywa kwa washtakiwa watano.
Katika mgawanyo huo kila mshtakiwa alitakiwa kutoa Sh. milioni 400.

Pia washtakiwa hao walitakiwa watoe hati za kusafiria na wasitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila idhini ya mahakama.

Mahakama pia iliwataka washtakiwa hao kuripoti Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi.

Washtakiwa hao wawili waliweza kutimiza masharti ya kutoa Sh. milioni 400 taslim na wadhamini wa kuaminika kama mahakama ilivyotaka.

Mbali na Kamungu na Mosha washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Bahati Mahenge, Manase Mwakale na Eddah Nkoma Mwakale.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 2003 na Machi 2004 kwa ujanja ujanja walitumia nyaraka za kugushi kwa jina la Changanyikeni Residential Complex Ltd ya Tanzania kuwa imehamishiwa deni la Sh. 855,365,573.18 kutoka kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.

Washtakiwa hao wanadaiwa pia kati ya Agosti na Oktoba mwaka 2005, kwa ujanja ujanja walitumia nyaraka za bandia zikionyesha kuwa Marubeni Corporation ya Japan imeihamishia Changanyikeni Residential Complex deni la Sh.1,186,534,303.27, ambapo walifanikiwa kujipatia ingizo la fedha hizo kutoka BoT.

Washtakiwa wengine walioshindwa kutimiza masharti ya dhamana ni Jayantikumar a.k.a Jeetu Patel, Devendra Patel, Amit Nandy, Ketan Chohan na Jonson Lukaza, ambao wanadaiwa kuchota fedha kupitia kampuni ya Kernel Ltd ya Tanzania na Marubeni Corporation ya Japan, ambapo waliiba Sh. 6,300,402,224.64.

Kampuni nyingine ni Navy Cut Tobacco ya Tanzania Ltd na Matshushita Electrical Trading, ambapo washtakiwa waliiba Sh. 3,323,974,942.30.

Kampuni zingine ni Bencon International Ltd ya Tanzania iliyogushi nyaraka zilizoonyesha kuwa Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan, imeihamishia deni la Sh. 7,962,978,372.48, Bina Resorts Ltd ya Tanzania iliyogushi nyaraka zikionyesha kuwa imehamishiwa deni la Sh. 3,924,992,009.25 na C. Itoh & Company Ltd ya Japan.

Kampuni zingine ni Maltan Mining Company ya Tanzania ambayo iligushi nyaraka zilizoonyesha kuwa imehamishiwa deni la Sh. 4,924,494,477.03 na kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.

SOURCE: Nipashe