Saturday 25 October 2008

Zanzibar ni nchi, lakini sio taifa!

Zanzibar ni nchi isiyokuwa na utaifa katika mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo Tanzania bara, lakini nje ya Tanzania, Zanzibar na Tanzania Bara zinatambuliwa kuwa ni taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mfumo huo, masuala yote yanayohusu utaifa, kama vile ushiriki katika Umoja wa Mataifa, Jumuiya za kikanda, na mahusiano ya kibalozi, yanaratibiwa na Serikali ya Muungano wa Tanzania. (gazeti Nipashe 25/10/2008)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Kitendawili cha hadhi ya Z`bar chateguliwa!

Wanasheria Wakuu wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wamesema Zanzibar ni nchi isiyokuwa na utaifa katika mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kauli hiyo sasa imeondoa utata wa hadhi ya Zanzibar katika Muungano.

Tamko hilo la Wanasheria hao, limetolewa na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha alipokuwa akifunga kikao cha Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.

Waziri Kiongozi alisema Wanasheria Wakuu walikutana Oktoba 11, mwaka huu kwa lengo la kutafuta tafsiri sahihi juu ya hadhi ya Zanzibar kama ni nchi ama la, ikiwa ni agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilolitoa bungeni wakati wa kikao cha bajeti.

Nahodha alisema Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo Tanzania bara, lakini nje ya Tanzania, Zanzibar na Tanzania Bara zinatambuliwa kuwa ni taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema katika mfumo huo, masuala yote yanayohusu utaifa, kama vile ushiriki katika Umoja wa Mataifa, Jumuiya za kikanda, na mahusiano ya kibalozi, yanaratibiwa na Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kwa msingi huo, tamko lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Zanzibar ni nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano, ni sahihi kwa vile utaifa wa Zanzibar ulikufa kama wa Tanganyika baada ya kufikiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 1964.

Hata hivyo, alisema yapo mambo ambayo Zanzibar imekuwa ikinufaika nayo ambayo hayahitaji utaifa na kupokea misaada na mikopo ya moja kwa moja kutoka kwa washirika way maendeleo na mashirika ya misaada ya kimataifa.

Alisema kwa kuzingatia jiografia, Zanzibar ni nchi yenye mipaka kwa vile ina Serikali na watu wanaoishi ndani ya mipaka hiyo na hivyo ni sahihi kusema Zanzibar ni nchi isiyokuwa na utaifa kwa vile ni sehemu ya taifa la Jamhuri ya Muungano.

Kuhusu suala la vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, Waziri Kiongozi alisema vitambulisho hivyo vitasaidia vyombo vya Serikali kuwapatia haki za kisiasa na kikatiba wananchi wake kama vile kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

Alisema kutokana na kuwepo kwa malalamiko kuwa kuna fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi zimekuwa zikichukuliwa na wageni kutoka nje ya Tanzania, ndio maana Serikali inaweka vitambulisho hivyo.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kiliahiriswa hadi Januari 21, mwakani.

(SOURCE: Nipashe, 2008-10-25 13:15:55
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar)