Tuesday, 14 October 2008

TRM wasema NO! kwa 'sisiemu'

................................
"Kamanda Tossi, unapima maji ya Kirumi kwa kidole?``
-Kutoka Nipashe 14/10/2008
................................

Stori na Mosonga Raphael
Wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wameshinda ktk uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge na udiwani ktk jimbo la uchaguzi Tarime na kata ya Tarime mjini.

Kwa ushindi huo, wananchi wa jimbo la Tarime ni kama wamepeleka salaam kwa wenzao nchi nzima 'wajifunze kusema NO' kwa CCM!

Kwa mtaji huu wa CCM kutojali uwajibikaji kwa wananchi na upotevu au utumiaji mbaya wa fedha za umma uliozagaa serikalini, si ajabu ktk uchaguzi mkuu ujao 2010 tukashuhudia maajabu zaidi na wapinzani kuongeza nguvu zaidi bungeni na hata ktk urais, hakuna ajuaye ...!!!

Leo ni kumbukumbu ya mwaka wa 9 tangu kifo cha Baba wa Taifa ambapo Tarime wamemkumbuka Mwalimu kwa onyo kali kwa CCM. Nadhani hata Mwalimu angefurahi kuona matokeo haya. Wananchi hawawezi kuibeba CCM hata kama haibebeki, ni lazima wapewe onyo (wake up call) na wasipojirekebisha vya kutosha ni nani atashangaa mwaka 2010 kuona Rais mteule Mbowe au Rais mteule Lipumba akiapishwa?

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Chadema yaipiga bao CCM

2008-10-14 10:30:46
Na Mashaka Mgeta, Tarime


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanikiwa kutetea kiti chake cha ubunge jimbo la Tarime kilichokuwa wazi baada ya kifo cha Chacha Wangwe.

Chadema pia kimetwaa kiti cha udiwani kata ya Tarime Mjini, ushindiambao umekiacha mbali Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kimetoa upinzani mkali katika kinyang`anyiro hicho.

Akitangaza matokeo hayo jana, Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Tarime, Trasias Kagenzi, alisema jumla ya wapiga kura 146,919 walijiandikisha, lakini 67,733 pekee ndio waliojitokeza kupiga kura.

Alisema mgombea kupitia Chadema, Charles Mwera, alipata kura 34,545 (asilimia 51), wakati Christopher Kangoye wa CCM alipata kura 28,996 (asilimia 42).

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Mbunge mteule huyo kupitia Chadema, alimzidi Kangoye kwa kura 5,549 Wagombea wengine ni Enock Marwa wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 949 (asilimia 1.4) na Denson Makanya wa DP aliambulia kura 305 (asilimia 0.45).

Kagenzi alisema kura halali zilikuwa 64,795, na kwamba kura 2,938 zilikataliwa kutokana sababu mbalimbali, zisizokidhi kanuni na sheria za uchaguzi.

Hata hivyo, wakati matokeo hayo yakitangazwa, wagombea kupitia CCM, Kangoye na NCCR-Mageuzi, Marwa, hawakuwepo.

Kangoye alifika muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, ambayo hata hivyo alisema hayatambui.

Ninashangaa kuniambia kwamba matokeo yametoka, mimi ndio ninakuja kuwasilisha matokeo tuliyoyapata kwa mawakala wetu, haya yalitolewa siyatambui, alisema.

Kauli ya Kangoye, inatofautiana na ile ya Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alipozungumza hivi karibuni na waandishi wa habari, na kusema chama hicho kitayakubali matokeo yatakayotangazwa.

Kabla ya kusoma matokeo hayo, Kagenzi alisema wagombea wa vyama vyote walisaini na kuyakubali matokeo hayo.

Matokeo yamekubaliwa na kusainiwa na wote, ni matokeo halali na kila mgombea atapewa nakala yake, Kagenzi alisema.

Hii ni mara ya tatu kwa CCM kushindwa katika uchaguzi mdogo, tokea mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992.

Mara ya kwanza ilikuwa Mwaka 1996, baada ya mgombea wa NCCR -Mageuzi, Augustine Mrema kushinda uchaguzi mdogo wa jimbo la Temeke.

Mara ya pili, CCM ilishindwa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Magu, ambapo Mwenyekiti wa UDP, John Momose Cheyo, aliibuka mshindi.

Matokeo hayo yalitangazwa katika ukumbi wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Mbunge Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto na Mkuu wa kikosi cha operesheni maalum cha Polisi, Venance Tossi.

Pia walikuwepo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, waangalizi wa kimataifa na waandishi wa habari.

Kwa upande wa udiwani, mgombea wa Chadema, John Heche, alishindwa kwa kura 4,820 dhidi ya kura 3,239 alizopata mgombea kupitia CCM, mfanyabiashara maarufu Peter Zakaria.

Wagombea wengine wa udiwani na vyama vyao kwenye mabano walikuwa ni David Wangwe `Osama` (NCCR-Mageuzi) aliyepata kura161, John Lutente (CUF) aliyepata kura 79 na Joness Sando wa DP aliyeambulia kura 24.

Hali ilikuwa ya utulivu katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Tarime, ambapo polisi wenye silaha na mabomu ya machozi na risasi za moto, walitanda kuzunguka eneo hilo.

Kamata-kamata Muda mfupi kabla ya kutangazwa matokeo hayo, polisi waliendesha msako na kuwakamata watu kadhaa, wengi wakiwa ni vijana, kutokana na kile kilichoaminika kuwa ni kufanya vurugu.

Nipashe ilishuhudia watu hao wakifikishwa katika kituo cha polisi wilayani Tarime, wakiwa ndani ya magari ya Shirika la Umeme (TANESCO) lenye namba SU 36270 na lile la halmashauri ya wilaya lenye namba SM 4249.

Magari mengine yalikuwa ya polisi, ambapo watu zaidi ya 20 wanakisiwa kukamatwa.

Sina hakika kama watatosha katika chumba hicho kidogo cha mahabusu, ama wengine wanahamishiwa kwenye vituo vya nje, alihoji mmoja wa waangalizi wa kimatifa, ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina lake.

Shangwe mjini Tarime Maelfu ya wakazi wa Tarime walianza kusherehekea ushindi wa Chadema tangu saa 11 alfajiri, ambapo gari lenye spika kubwa lilitumbuiza watu, nje ya nyumba ya wageni iitwayo Makoma, mahali walipofikia baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Nyimbo za kuisifu Chadema na `kuiponda` CCM, zilisikika kiasi cha kuwahamasisha watu walionekana katika makundi, wakiandamana kwenda kwenye eneo hilo.

Hata baada ya matokeo hayo kutangazwa, maelfu ya watu walimiminika barabarani, wakiwa wameshika matawi ya miti, mabango na wanawake wakipeperusha khanga na vitenge, huku madereva wa magari na pilikipiki wakipiga honi na kuendesha vyombo hivyo vya usafiri kwa madaha.

Miongoni mwa mabango yaliyoonekana, yalisomeka ``Makamba wahuni wa Tarime ni soo, Makamba jimbo limechukuliwa na wahuni, CCM habari ndio hiyo.``

Maandishi hayo yalidaiwa kuwa majibu ya kauli iliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, alipowaita wafuasi wa Chadema kuwa ni wahuni.

Pia kulikuwa na mabango yaliyosomeka, ``Kamanda Tossi, unapima maji ya Kirumi kwa kidole.`` Kirumi ni jina la asili la mto Mara.

Kuzuia kufika Bomani Askari polisi walitanda maeneo yote ya kuzunguka ofisi za halmashauri ya wilaya ya Tarime maarufu kama Bomani, mahali palipotumika kutangaza matokeo hayo.

Hivyo watu walizuiwa kuingia katika eneo hilo, hali ambayo ni tofauti na ilivyokuwa katika utangazaji wa matokeo katika chaguzi nyingine zilizopita
kutoweka kwa viongozi wa CCM Viongozi na makada wa CCM walioshiriki kampeni za uchaguzi huo, wamedaiwa kuondoka mjini hapa tangu juzi Jumamosi.

Miongoni mwao ni Makamba, ambaye hadi matangazo hayo yanatolewa, hakuonekana ama kupatikana kwa simu yake ya mkononi.

Baadaye Nipashe ilimpata akiwa uwanja wa ndege Mwanza.

Mbali na Makamba, makada walioshiriki kampeni za jukwaani na zile za nyumba kwa nyuma na ambao hawaonekani mjini hapa, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha propaganda, Hiza Tambwe na Shaibu Akwilombe.

Charles Mwera (Chadema) Mwera akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa mshindi, alisema ushindi alioupata ni matokeo ya kukubalika kwa sera, mipango na usimamizi wa shughuli za maendeleo ya jamii ambazo zimekuwa zikifanywa na Chadema katika halmashauri hiyo.

Wilaya ya Tarime ni miongioni mwa halmashauri chache zinazoundwa na madiwani wa upinzani. Mwera pia ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Ninaenda kuwa mwakilishi wa wananchi wa Tarime bila kujali itikadi zao, alisema.

Mwera akizungumzia hatua ya polisi kuwapiga wafuasi wa Chadema kwa mabomu ya machozi na kufyatua risasi kabla ya kutangazwa matokeo hayo alisema:``Si kitendo kizuri kwa sababu kila mpiga kura na raia wengine wana haki ya kujua mshindi baada ya kutimiza wajibu wao wa kidemokrasia.

Christopher Kangoye (CCM) Aliingia ukumbini, ikiwa ni takribani dakika 15 baada ya matokeo kutangazwa.

Kwanza alionekana kushtuka, kisha akakutana na mmoja wa walinzi wa halmashauri aliyekuwa mlangoni, na ambaye hakumtambua, hivyo kumzua asiingie.

Baada ya kutambulishwa kwamba ni Kangoye, mlinzi huyo alimruhusu, lakini wakati huo, Kagenzi na maofisa wa polisi walikuwa wameshatoka. Alipohojiwa, alieleza kushtushwa na matokeo hayo, na kutamka bayana kwamba hakubaliani nayo.

Siyatambui matokeo hayo, kwa maana kulikuwa na mapungufu mengi sana ambayo tumekuja kuyaleta kwa Msimamizi, ninashangaa kusikia ameshatangaza, alisema huku akielekea ofisi ya Kagenzi.

Denson Makanya (DP) Mgombea huyo ambaye ni mchungaji, kama alivyo Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila, alisema uchaguzi uliendeshwa vizuri na kwamba anakubaliana na matokeo.

Watu wamepiga kura, zimeonyesha kuwa Mwera ndiye aliyewafaa, hatuna cha ziada, zaidi ya kukubailiana na maamuzi yao, alisema.

Hakuna sherehe za ushindi Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto, anasema hapatakuwa na sherehe zozote za kushangilia ushindi huo.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema kazi inayowakabili wabunge wa upinzani hususan Chadema, ni kufanya kazi ya kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.

Hatukumnadi Mwera ili ashinde na kufanya sherehe, sisi hatuna sherehe, tunachotaka ni aje kuungana nasi kuifanya kazi tuliyotumwa na wananchi bungeni, alisema Zitto.

Kauli ya polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, alisema shughuli ya kusimamia ulinzi na usalama wakati wa kampeni hadi uchaguzi mdogo ilikuwa changamoto kubwa.

Ulikuwa wakati mgumu, ninashukuru tumekuwa na ushirikiano mzuri hasa na waandishi wa habari, lakini tumefika mwisho salama,Ӡalisema.

Barlow alisema kuna wakati polisi ililazimika kutumia nguvu kudhibiti vurugu na fujo ambazo zingeathiri amani na mwenendo wa kampeni na uchaguzi kama hatua hizo zisingechukuliwa.

Alisema ilipofikia hatua ya amani na utulivu kutoweka, polisi ilitumia nguvu kubwa, lengo likiwa ni kuwawezesha wakazi wa Tarime kutumia haki yao ya kidemokrasia kushiriki uchaguzi huo.

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...

Imetolewa mara ya mwisho: 14.10.2008 0104 EAT

Tarime ni ya CHADEMA

*Mwera awatimulia vumbi Kangoye, Makanya na Haruni
*Makamba akubali yaishe asema 'walibanwa nusu uwanja'
*Alonga kama mgombea wao hajaridhika aende mahakamani

WAKATI CHADEMA ikiibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani Tarime, CCM imepinga matokeo hayo kupitia mgombea wake, Bw. Christopher Kangoye katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, mgombea wa CHADEMA, Bw. Charles Mwera, alipata kura 34,545 dhidi ya kura 28,996 alizopata Bw. Kangoye.

Akitangaza matokeo jana, Msimamizi wa Uchaguzi, Bw. Trasias Kagenzi, alisema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 67,733, halali zikiwa 64,795 na 2,938 zikiharibika.

Katika pingamizi lake, Bw. Kangoye alisema hakubaliani na matokeo yaliyompa ushindi mgombea Bw. Mwera.

Bw. Kangoye alitangaza msimamo huo muda mfupi baada ya kufika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kukuta tayari matokeo hayo yameshatangazwa na Msimamizi.

Alidai kuna baadhi ya mambo, ambayo hata hivyo hakuyataja, hakubaliani nayo hivyo alitarajia kuwasilisha rasmi malalamiko yake kwa Msimamizi bila kusema kama anaweza kwenda mahakamani kupinga kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

“Mimi nimekuja kusikiliza matokeo, nikidhani nimeshinda nafika, naambiwa eti tayari matokeo yameshatangazwa...mimi siamini, lazima nikalalamike kwa Msimamizi wa Uchaguzi, kuhusu mambo fulani fulani yaliyojitokeza katika uchaguzi huu,” alisema Bw. Kangoye akiwa amefuatana na mtu aliyetajwa kuwa ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Tarime.

Wakati Bw. Kangoye alilalamikia matokeo hayo, vyama vingine vimekubaliana na matokeo hayo huku kauli ya Bw. Kangoye ikipingana na ya Katibu wa Uenezi wa CCM, Kapteni mstaafu John Chiligati aliyoitoa juzi mbele ya waandishi wa habari mjini hapa, kuwa watakubaliana ma matokeo yoyote yatakayotangazwa.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, shangwe, nyimbo na vigelele vilitawala hasa kuitokana na wagombea wote wawilib wa CHADEMA akiwamo diwani mteule wa Tarime Mjini Bw. John Heche naye kushinda dhidi ya mfanyabiashara Peter Zacharia wa CCM.

Bw. Trasias ambaye alitangaza matokeohayo chini ya ulinzi mkali wa Polisi ukiongozwa na Mkuu wa Operesheni Maalumu Polisi, Bw. Venance Tossi, alisema wapiga kura 146,919 ndio waliotarajiwa kupiga kura juzi.

Mbali na CHADEMA na CCM, vyama vingine vilishoshirikini DP ambacho mgombea wake, Mchungaji Benson Makanya alipata kura 305 na NCCR-Mageuzi ambayo mgombea wake, Bw. Marwa Haruni alipata kura 949.

Akizunguza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Zitto Kabwe, alisema ushindi huo ulitarajiwa, kutokana na chama hicho kuwa makini katika kushughulikia mambo ya kitaifa hasa yanayogusa uchumi wa nchi.

Hata hivyo, alisema alisikitishwa na vitisho vya Jeshi la Polisi, kuwapiga wananchi kwa mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha, huku wakiwanyanyasa wagombea wa chama chake, hali ambayo pia ilichangia idadi kubwa ya watu kushindwa kujitokeza kupiga kura.

“Polisi walitumia nguvu kubwa kuisaidia CCM, lakini nguvu ya umma ilikataa na wao wakajua hilo, ndiyo maana wamekubaliana na umma wa wana Tarime, sasa kazi kubwa ni kapambana na ufisadi kwa kasi na nguvu kubwa tena kwa vitendo,” alisema Bw. Kabwe.

Naye Bw. Mwera alisema ushindi aliopata ni matokeo ya kazi nzuri aliyoifanya akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi za CHADEMA hata kufikia kutoa elimu bure ya sekondari kwa watoto wote wanaojiunga na sekondari.

Alisema kazi kubwa sasa katika kurejesha imani aliyopewa na wananchi wa Tarime, ni kuvaa viatu vya marehemu Chacha Wangwe kwa kutetea maslahi ya wananchi wa Tarime, yakiwamo madini na ardhi, ili raslimali hizo zitumike kikamilifu kuwakomboa wana Tarime.

“Nilijua lazima niwe mbunge, kwani tayari nilianza kazi ya kutumikia wananchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na huduma zingine za kijamii, nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri hii,” alisema Bw. Mwera.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Tarime Mjini, Bw. Renatus Mahimbali, alimtangaza Bw. John Heche kuwa diwani wa kata hiyo kwa kupata kura 4,820, akiwashinda Bw. Zacharia wa CCM aliyepata 3,239 huku NCCR ikipata kura 161, CUF 79 na DP kura 24.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, barabara zote za Tarime zilifungwa baada ya wananchi wa rika mbalimbali kujitokeza na kufanya maandamano makubwa kwa kuimba nyimbo za furaha na kejeli kwa CCM na za kupongeza ushindi.

“Makamba habari ndiyo hiyo, hapa ni Tarime si Kiteto... uliotuita wahusi sasa soo mzee, umeambulia ulichopanda,” walisikika wananchi hao wakiimba na mabango yakionesha maandishi hayo.

Naye Reuben Kagaruki anaripoti, kwamba Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amesema anakusudia kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Bw. Mwera, kwa kile anachodai haukuwa huru na wa haki.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mchungaji Mtikila, alidai uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu kutoka kwa baadhi ya watu.

"Huwezi kusema uchaguzi ulikuwa halali wakati watu tumepigwa mawe na kuumizwa ni lazima tufungue kesi ya kupinga matokeo," alisisitiza Mchungaji Mtikila.

Alipoulizwa anajisikiaje kwa chama cha upinzani kushinda jimbo hilo, Mchungaji Mtikila alisema kwa Tarime CHADEMA ndicho chama tawala na vyama vingine ndivyo vilikuwa vya upinzani.

"Kwa Tarime CHADEMA ndicho chama tawala kwa sababu ndicho kinaongoza halmashauri na sisi tuliobaki (Ikiwa ni pamoja na CCM) tulikuwa wapinzani, hivyo si kweli kusema kuwa chama cha upinzani kimeshinda," alisisitiza Mchungaji huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema, alisema wananchi wa Tarime wameonesha ushujaa na wamedhihirisha kuwa hawahongeki kwa kofia na fulana.

Alisema kuna umuhimu kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wowote, kwenda Tarime kujifunza kwani wameonesha ukomavu wa kisiasa. Alisema kushindwa kwa CCM hizo ni dalili za mvua ya rasharasha, kwani kazi ndiyo kwanza inaanza.


nao Jovin Mihambi na George Boniphace, wanaripoti kutoka Mwanza kwamba CCM imekiri kuwa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani Tarime ulikuwa mgumu kuliko viongozi wake walivyokuwa wakitarajia.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Alisema yeye na CCM wameupokea ushindi huo na kuongeza kuwa CHADEMA ilikuwa inajibu mapigo ya uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa dhidi ya CHADEMA ambayo ilipata kura 30,000 za Freeman Mbowe huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 50,000.

Alisema mchakato mzima wa uchaguzi katika jimbo la Tarime kwa upande wa chama chake ulikuwa haumpi usingizi kwani CCM ilikuwa imebanwa 'nusu uwanja'.

Alisema kushindwa kwa CCM katika udiwani na ubunge
si kwamba chama hicho hakina uwezo wa kunyakua kiti hicho katika uchaguzi wa mwaka 2010 na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inaangalia wapi imeteleza na kujikwaa na
kuangalia upya kwa kusahihisha makosa ambayo yalijitokeza katika uchaguzi ambao umepita na kuipa CHADEMA ushindi.

Alisema kutokana na ushindi wa CHADEMA, CCM inakubali matokeo ingawa hadi sasa mgombea wake katika ngazi ya ubunge amekataa kusaini karatasi ya kukubali matokeo.

Alisema kuwa mgombea huyo, ana haki ya kutafuta haki mbele ya sheria, lakini atafanya hivyo kwa gharama yake na wala si ya CCM.

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge na udiwani umefanyika, kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Tarime na Diwani wa Tarime Mjini, Bw. Chacha Wangwe kilichotokea kwa ajali ya gari eneo la Pandambili mkoani Dodoma Julai 28 mwaka huu.

Kutoka Iringa Francis Godwin, anaripoti kwamba
CCM mkoani humo imejikuta chali baada ya mgombea wa udiwani wa TLP kata ya Lupingu, Ludewa, Bw. John Kiowi kuibuka kidedea.

Bw. Kiowi alipata kura 633 dhidi ya kura 578 alizopata mpinzani wake, Bw. Alfred Kona wa CCM.

Akitangaza matokeo kwa mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jana, Kaimu Katibu wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Bw. Fridolin Mwapinga, alisema CCM imekubali matokeo.

Na George John, Tarime (Gazeti la Majira)