Saturday 1 December 2007

Siku ya Ukimwi duniani

Rais Jakaya Kikwete, leo atatumia maadhimisho ya Ukimwi Duniani kuhutubia wananchi katika utaratibu wake aliojiwekea wa kuzungumza na Watanzania kila mwisho wa mwezi.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa, maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Mkoani Tabora ambako atakuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele na mfano bora kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kwa kuongoza katika upimaji Ukimwi na mkewe, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupima kwa hiari hapa nchini iliyofanyika Julai 14, 2007.

`Kampeni ambayo imeendelea na kuongeza ujasiri kwa wananchi wa Tanzania ambapo siku ya kesho (leo) pia itatumika kuonyesha tathmini na mafanikio ya kampeni aliyozindua Rais,` ilieleza taarifa hiyo.

Kaulimbiu ya masuala ya Ukimwi mwaka huu inasema, `zuia Ukimwi, timiza ahadi yako, ongoza mapambano`, kauli inayotoa msisitizo kwa viongozi katika ngazi mbalimbali kuwa mfano kwa kuongoza mapambano dhidi ya Ukimwi.

Maadhimisho ya siku hii hutoa fursa kwa nchi na watu kutathmini hali halisi ya mwelekeo wa udhibiti na pia kubaini changamoto, mafanikio na kuweka mikakati ya baadaye ya kudhibiti janga la Ukimwi.

Wakati huo huo, naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile atawaongoza zaidi ya watu 1,000 katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Maadhimisho hayo yanafanyika katika ukanda wa machimbo ya dhahabu wilayani Chunya.

Kwa mujibu wa Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la Students Partnership Worldwide-Tanzania (SPW TZ), Bw. Kenneth Simbaya, maadhimisho hayo katika ngazi ya kimkoa yatafanyika katika kijiji cha Makongorosi na zaidi ya watu 1,000 wanatarajiwa kuhudhuria.

Alisema kutokana na kuwepo kwa machimbo ya wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu na mwingiliano wa watu na wafanyabiashara wilayani humo, eneo hilo limekuwa katika hatari kubwa ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi.

Alisema sababu hizo ndizo zilizofanya maadhimisho hayo katika ngazi ya kimkoa yafanyike wilayani Chunya ili kutoa elimu zaidi kwa jamii.

Hivi karibuni Waziri Mkuu Edward Lowassa, akiwa katika ziara mkoani hapa, aliwahimiza viongozi na wananchi wa Wilaya ya Chunya kulivalia njuga suala la vita dhidi ya Ukimwi katika eneo hilo la machimbo ya dhahabu ili kuwanusuru wakazi wake.

Alisema maadhimisho hayo yameandaliwa kwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya na SPW TZ ili kuunga mkono vita dhidi ya Ukimwi.

Akizungumzia ujumbe wa mwaka huu, Bw. Simbaya alisema yapo mafanikio makubwa ambayo yamekwishapatikana tangu kuanza kwa ugonjwa huo.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kuwepo kwa uongozi imara ambao umekuwa ukizungumzia tatizo la Ukimwi mara kwa mara.

* SOURCE: Nipashe, 01 Dec 2007

No comments: