Monday 3 December 2007

Mbagala Town

Kuna watu wanaosema kuwa Mbagala na Temeke kwa ujumla ni maeneo ya uswahilini. Kwa namna fulani watu hao wanamaanisha kuwa maeneo hayo (Mbagala/Temeke) na wakazi wake ni watu wa daraja la chini kimaisha au kijamii!

Kwa maoni yangu ni kwamba Mbagala ni mji mdogo ambao una wakaaji wengi. Uko njiani kupanuka/kukua kiuchumi na maendeleo ktk kipindi cha miaka 10 ijayo.
Tayari kuna benki moja ya biashara imefunguliwa na barabara ya Kilwa inaendelea kupanuliwa kwa sasa.
Kiabiashara ni eneo ambalo lina matumaini makubwa.
Nina imani kuwa watu wengi sasa watavutiwa kuja kuishi na/au kuwekeza Mbagala hasa kutokana na kuwepo soko kubwa (walaji).

Nakumbuka Rais Museveni wa Uganda ktk miaka ya 1990, aliwahi kusema kuwa,
'endapo kila mwananchi wa China atanunua kopo moja dogo la kahawa (450g) toka Uganda, na kufanya kahawa hiyo kuwa kinywaji chake basi Uganda itakuwa tajiri'.
Nadhani Mheshimiwa Rais Museven alimaanisha ukubwa wa soka nchini China; na soko ni watu!

Mbagala pia yaweza kuwa na soko kubwa sana. Karibu kila biashara ndogo tu yenye kuuza vitu au huduma za bei nafuu inayoanzishwa Mbagala, wateja wa uhakika wapo. Na hivyo ndivyo maendeleo yanaanza taratibu.

Wenzetu wazungu wametutangulia kwa sababu wanajali kila senti inayotoka kwa mteja bila kujali ni tajiri au hana uwezo mkubwa kiuchumi; kwao mteja ni mteja! Na mteja anathaminiwa.

Hata Ndugu yetu Reginald Mengi alianzia biashara za kujaza wino ktk kalamu za wino aina ya Epika. Hata mimi nilipokuwa nasoma shule ya msingi nilizitumia hizi kalamu miaka ya 1980. Hivyo ndivyo alivyoanza Ndugu Mengi pale barabara ya Pugu (sasa inaitwa Nyerere) - alianza kwa shida sana. Yeye mwenyewe Ndugu Mengi alisimulia mwanzo wake wa kuhangaikia maisha kibiashara wakati wa ufunguzi wa vikundi vya Skuvi mwaka 1995. Lakini kama kuna mtu aliyekuwa anamcheka Ndugu Mengi enzi hizo, leo hii mtu huyo ajitokeze mbele na amcheke tena Ndugu Mengi!

Tukianza mambo ya kuwasema wa uswahilini na kujisifia wa uzunguni, tutabaki kuabudu vya wenzetu. Harakati za kijamii ktk kujikwamua kiuchumi zinaanzia popote. Ndio maana nasema kuwa Mbagala itajengwa na wana Mbagala wenye moyo!

Chako ni chako, na cha kuazima hakistili matako!

No comments: