Thursday 20 December 2007

'Boresheni makazi ya wananchi, sio kuyabomoa'

Kuwabomolea wenye makazi holela ni kosa - Magufuli

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. John Magufuli, amesema Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wanaobomoa nyumba za watu wanaoishi kwenye makazi holela wanapaswa kukamatwa na kuwekwa ndani.

Amesema hatabadili matumizi ya maeneo ya wazi, na ameahidi kuwashtaki kwa Rais Jakaya Kikwete, Wakurugenzi watakaojaribu kutwaa maeneo hayo.

Aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya kuwatunuku barua za toleo wamiliki 250 wa nyumba za mtaa wa Hananasif na Mkunguni Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Mradi wa kuboresha makazi kwenye maeneo hayo unaendeshwa na taasisi ya makazi ya WAT Advancement Trust.

Pia alisema waliojenga kwenye maeneo ya wazi wajiandae kubomolewa wakati wowote.

``Nawahakikishia maeneo ya wazi yataendelea kuwa ya wazi, kama eneo ni la michezo litabaki hivyo mpaka nife au niondoke wizara hii,`` alisema Bw. Magufuli.

Bw. Magufuli alisema kuwabomolea nyumba watu wanaoishi kwenye makazi holela ni kinyume na Sheria namba 4 na 5 ya mwaka 1990, ambayo alisema inawatambua wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Alisema badala ya kuwabomolea kinachotakiwa ni kuboresha makazi ya wananchi hao ili waishi kwenye maeneo bora kama watu wengine.

Bw. Magufuli aliziagiza halmashauri kuandaa hati miliki kwa wananchi ambao wametimiza masharti yanayotakiwa kwa ajili ya kupata hati hizo.

Alisema hati hizo zitawasaidia kupata mikopo katika taasisi za fedha nchini na kwamba tayari hati 96 zilizotolewa zimetumika kuwapatia mikopo wananchi.

Alisema baadhi ya wananchi waliopata hati hizo wamezitumia kuomba mikopo kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa watoto wao.

Waziri Magufuli alisifu jitihada zinazofanywa na WAT Advancement Trust, chini ya Mkurugenzi wake, Bi. Tabitha Siwale, katika kuboresha makazi jijini Dar es Salaam na aliahidi kuwa wizara yake itakuwa bega kwa bega na taasisi hiyo.

``Mama Siwale umefanya jitihada kubwa sana katika kuboresha makazi hapa Dar es Salaam. Katika umri wako ungetakiwa kupumzika lakini wewe umeamua kuwatumikia wananchi. Nakupongeza sana,`` alisema Bw. Magufuli.

Alisema serikali inaendelea na mradi wa kuyatambua makazi holela katika miji ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.

Alisema asilimia 75 ya wakazi wa jijini la Dar es Salaam wanaishi kwenye makazi holela na kwamba endapo watabomolewa watakaobaki ni asilimia 25 tu.

Aliwasisitiza wakazi wa Dar es Salaam kuunga mkono jitihada za WAT kuboresha makazi na kuwapatia wananchi hati kwani zinafaida kubwa.

``Ardhi ni mali lakini ile ambayo imepimwa na kupatiwa hatimiliki ina thamani kubwa zaidi ya ile ambayo haijapimwa, kwa hiyo ambao hamjalipa lipeni mpate hati,`` alisema.

* SOURCE: Nipashe, 20 Dec 2007
By Joseph Mwendapole

No comments: