Tuesday 10 July 2007

Makala: Malezi ya mtoto

Kitovu cha malezi ni mzazi...mwalimu asilaumiwe asilani!

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita nilidodosa kuhusu mabadiliko ya tabia kwa watoto wetu hasa wawapo mashuleni. Nikauliza ni nani hasa wa kulaumiwa? Niliruhusu uwanja wa majadiliano, maoni na ushauri.
Nilipofungua email ya safu hii, nilipata maoni ya msomaji wetu mahiri anayeishi Geneva, Switzerland. Ametoa uchambuzi mzuri wa suala lile ambapo kwa ujumla yeye ametupa lawama kwa wazazi. Hebu tulia usikie uchambuzi wake:-
``Poleni na kazi ya kuandaa makala nzuri kila jumapili. Nimeguswa na makala ya leo (Jumapili iliyopita) na ile iliyotangulia kabla ya hiyo kuhusu malezi ya watoto. Napenda kuchangia kama ifuatavyo. Kuhusu hoja ya mtoa hoja kutoka Dodoma kuwa kuna watoto wengine huzaliwa na tabia nzuri na hawabadiliki hata wakidanganywa, ni kwamba lazima tufahamu kuwa watoto wote (sio baadhi), huzaliwa wakiwa wema na mazingira ndio huwabadilisha. Isitoshe, uwezo wa kutobadilika tabia unatokana na namna jinsi wazazi wanavyomfundisha na jinsi mtoto anavyopokea mafundisho. Hapa napenda kusisitiza nafasi muhimu ya mzazi na kwa namna yeyote wazazi wasikwepe wajibu katika hili.
Kuhusu nafasi ya mwalimu na mabadiliko ya tabia ya mtoto, napenda kuweka wazi kuwa mwalimu wa Tanzania ya leo anafanya kazi kwenye mazingira magumu mno ambayo kwa mtu aliye nje ya kazi hiyo, kamwe hawezi kuyajua na hata akisikia inakuwa kama hadithi tu. Ukweli mazingira magumu ya taaluma hiyo hayampi mwalimu morali ya kutimiza wajibu wake kikamilifu. Mwalimu asiyepata mshahara kwa miezi kadhaa, hajalipwa malimbikizo yake, anaishi kwenye nyumba kama banda la kuku, hajaenda likizo kwa miaka kadhaa na lundo la matatizo mengine, ni wazi hana muda wa kuangalia maendeleo ya tabia ya mwanafunzi. Mwalimu huyu leo amepoteza uhuru wake wa kumwadhibu mtoto. Ni mara ngapi tunaona wazazi wakimfungia kibwebwe mwalimu eti kisa amempa adhabu mtoto wao! Hivi mwalimu kama huyu atathubutu tena kumgusa mtoto wa mtu? Ni hivi karibuni nimesikia tena tamko la wizara kupitia Naibu Waziri wake akisisitiza kuhusu kuondoa adhabu ya viboko mashuleni. Sisemi kwamba watoto wachapwe kila wakikosa, ila kwa mwalimu kiboko ni adhabu nyepesi kuliko adhabu nyingine ambazo zinahitaji usimamizi wa muda mrefu kama kazi za nje. Shinikizo la wazazi na mamlaka za elimu zimempunguzia mwalimu uwezo wa kudhibiti nidhamu ya mwanafunzi.
Suala lingine ni kwamba familia zetu leo hii hazina muda wa kuangalia mienendo ya watoto, baba na mama wote wako busy na harakati za maisha, hivyo jukumu la malezi wanaachiwa walimu, eti kwa sababu wanalipwa mishahara kwa kazi hiyo! Naijua shule moja ya sekondari huko Morogoro, kuna kipindi karibu asilimia 70 ya wanafunzi wake ni watoto wa watu wenye uwezo kifedha ila hawana muda wa kulea watoto wao na wanawasukumia kwenye shule hiyo. Watoto hao wana tabia mbovu na hata mwalimu afanyeje kamwe hawezi kurekebisha tabia zao. Baadhi ya wazazi wao wanaomba eti wakati wa likizo wabaki huko huko shuleni. Yaani mzazi hataki hata kumwona mtoto wake, sasa unataka mwalimu ndio afanye nini!
Kingine ni kuiga maisha ya kizungu na kuwalea watoto kama Marekani na Ulaya (narejea makala ya juma lililopita). Hapa nakubaliana na mchangiaji kutoka Marekani kuhusu umuhimu wa malezi ya mtoto kuwa ya pande mbili. Ila sikubaliani naye anapotaka kutushawishi kuwa mtoto asiguswe kabisa. Napenda kumwambia kimaadili Watanzania tuko mbali zaidi ya wazungu na ukiongea na wazee wa kizungu wanakiri hilo na wanajuta kupotea kwa maadili ya watoto wao. Ukiingia kwenye madarasa ya shule za kizungu hali ni kusikitisha mno, wanafanya utumbo wote bila ya mwalimu kufanya kitu. Kwa mfano, wasichana wanajiremba darasani, wanapiga simu, wanabusiana kimahaba na mwalimu anawaangalia tu na hana uwezo wa kufanya chochote. Mara ngapi vitoto vya kimarekani vinakuja na bunduki shuleni na kuua wenzao kama kuku? Hivi na sisi tufikie hapa siku moja?
Namalizia kwa kutoa ushauri kuwa malezi ya mtoto ni ya jamii nzima na kumtupia mpira mwalimu ni kumwonea tu, kila mmoja wetu atimize wajibu wake na watoto watakuwa na maadili mema.
Constantin Njalambaya, Geneva, Switzerland.

Mpenzi msomaji, hayo ndiyo maoni na ushauri wa ndugu yetu huyo. Bila shaka uchambuzi wake umeuelewa. Bado anaamini kuwa jamii kwa ujumla wake ndiyo yenye jukumu la kudhibiti na kusimamia malezi bora ndani ya familia zetu, tukianzia pale majumbani mwetu(wazazi). Mtoto ukimkosea kimalezi wakati wa makuzi yake, basi umempotezea mwelekeo. Tuangalie wahenga walifanya nini katika kulinda maadili mema ambayo wengi wetu tumekulia hata kuwa viongozi bora wa sasa. Pamoja na kisingizio cha kwenda na wakati au wengine wanaita utandawazi, lakini bado jamii inapaswa kuwa makini na mabadiliko ya maisha duniani huku tuking`ang`ania tamaduni zetu ambazo hadi sasa zinafaa kuenziwa. Wazazi wengine wamefikia hatua wanadekeza watoto wao eti wanawalea kizungu. Kwanini kizungu na si kiafrika? Huu uzungu umesaidia? (rejea email ya ndugu yetu wa Geneva).
Bado tunaweza kuokoa kizazi hiki ikiwa kila mmoja wetu, serikali na asasi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya kijamii zitaelimisha misingi bora ya malezi bora katika taifa letu. Hakuna kisichowezekana tukiweka nia na dhamira ya kweli.
Wasalaam.


SOURCE: Nipashe, 08/7/2007, Na (Anti) Flora Wingia, fwingia@yahoo.com

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Mimi ni mpenzi na msomaji mkubwa wa makala za 'Maisha Ndivyo Yalivyo' zinazoandaliwa na Anti Flora. Pia nimeshawahi kuwasiliana nae kwa e-mail, na sehemu ya maoni yangu kwake yako ktk blog hii.

Namkumbuka Anti Flora tangu enzi zile akiandikia Uhuru/Mzalendo.
Hongera sana Anti Flora!