Tuesday 10 July 2007

Dar: Bei ya vyakula Juu

Bei ya vyakula yapaa

Wakati nauli za mabasi ya kwenda bara zikiwa zimepanda maradufu, bei za vyakula katika masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam imepanda kwa asilimia 80.
Uchunguzi wa Nipashe katika masoko mbalimbali yanayouza vyakula vya nafaka na matunda, umegundua kuwa baadhi ya vyakula vilivyopanda bei ni mchele, maharage, unga wa ngano, karanga, mihogo, viazi mviringo, ndizi, mtama na ulezi.
Baadhi ya masoko yaliyotembelewa ni Buguruni, Ilala na Kariakoo.
Mfanyabiashara wa mchele katika soko la Buguruni, Bw. Rashid Hussen alisema kabla ya kupanda kwa gharama za mafuta walikuwa wakisafirisha gunia moja la mchele la kilo 70 hadi 120 kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kwa Sh. 3,000 hadi 3,500. Alisema kwa sasa wanalazimika kusafirisha kiasi kama hicho kwa Sh. 6,000 hadi 6,500. Alisema kutokana na gharama hizo wanalazimika kuuza mchele (super) kutoka Mbeya kilo moja kwa Sh 1,000 hadi Sh.1,200. Aliongeza kuwa katika kipindi hiki cha mavuno, kabla ya kupanda kwa ushuru wa mafuta, bei ilikuwa kati ya Sh. 400 hadi Sh. 500 kwa kilo. ``Kipindi kama hiki cha mavuno ambacho kinaanzia Mei hadi Julai, mchele ulipaswa kuuzwa bei ya chini kabisa lakini usafiri unatumaliza kabisa katika kipindi kama hiki mwaka jana mchele ulikuwa bei ya chini kabisa,`` alisema Bw. Hussen.
Naye Bw. Ally Juma ambaye anauza maharage katika soko hilo, alisema kupanda kwa gharama za usafirishaji kumewalazimisha wapandisha bei ya bidhaa hiyo. Alisema maharage aina ya soya kwa sasa yanauzwa kati ya Sh. 900 hadi Sh. 950 ambapo zamani walikuwa wakiuza kati ya Sh. 600 hadi Sh.700 kwa kilo moja.
Naye Bi. Fau Fadi ambaye anauza matunda, alisema machungwa yanauzwa kati ya Sh. 50 hadi 200 wakati awali yaliuzwa kati ya Sh. 20 hadi Sh.100 kwa chungwa moja. Tunda moja aina ya fenesi kutoka Mramba, Kisarawe lenye ukubwa wa kati linauzwa Sh. 2,000 hadi Sh. 2,500 ambapo zamani lilikuwa likiuzwa kati ya Sh.1,200 hadi Sh.1,500. Aidha bei ya parachichi moja kutoka mkoani Kilimanjaro linauzwa kati ya Sh. 300 hadi Sh. 500 wakati awali likiuzwa Sh. 200 hadi Sh. 300. Pia, ubuyu ambao zamani uliuzwa kwa kisadolini kimoja Sh. 500 hadi Sh. 550 sasa unauzwa Sh.1,500 hadi Sh.1,550.
Na katika maduka ya nyama bidhaa hiyo imepanda pia. Kilo moja inauzwa kati ya Sh. 2,700 hadi Sh. 2,900 wakati awali iliuzwa Sh. 2,400 hadi Sh. 2,600. Nyama wanayoita steki (isiyo na mifupa), kilo moja inauzwa Sh. 3,400 hadi Sh. 3,500. Pia bei za samaki aina ya dagaa, karoti, nazi na pilipili bei kwa sasa ipo juu kulinganisha na mwezi uliopita ambapo fungu moja la pilipili linauzwa Sh.100 hadi Sh.150 wakati awali ilikuwa Sh. 50 kwa Sh. 70.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wafanyabishara katika masoko hayo walilalamikia kupanda kwa gharama za kusafirishia bidhaa zao kutoka mashambani kwenda sokoni.

SOURCE: Nipashe, Na Godfrey Monyo, 10/7/2007

No comments: