Wednesday 11 July 2007

Habari za nyumbani

JK afanya mabadiliko Benki Kuu
Ateua naibu gavana watatu
NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa naibu magavana watatu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), na kila mmoja kuainishiwa kazi zake.Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ikiwa na saini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, ilieleza kuwa, walioteuliwa ni aliyekuwa Mshauri Mwandamizi wa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Profesa Benno Ndulu.Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Shughuli za benki katika BOT, Lila Mkila na aliyekuwa Naibu Gavana pekee, Juma Reli.Taarifa hiyo ambayo ilieleza kuwa uteuzi huo unaanza Juni 26, mwaka huu, ilifafanua kuwa, majukumu ya Profesa Ndulu katika BOT ni sera za fedha na uchumi, Mkila atashughulikia usimamizi wa shughuli za mabenki, na Reli anakuwa Naibu Gavana anayeshughulikia utumishi na utawala.Gavana wa Benki Kuu anaendelea kuwa Daudi Balali.

Kandoro amtetea Kombe
Ni sakata la ‘breakdown’ kuvuta magari mazima
NA ESTHER KATUA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro ametetea uamuzi wa kuzuia ‘breakdown’ kubeba magari mazima, akisema umeamuliwa kwa mujibu wa sheria mama, ambayo haiwezi kumezwa na sheria ndogo.Kandoro alitoa ufafanua huo jana jijini Dar es Salaam, baada ya Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Mohamed Yakub kupinga amri iliyotolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, James Kombe ya kupiga marufuku ‘breakdown’ kuvuta magari mazima kwa madai ya kuegeshwa ovyo.“Alichokizungumza Kombe ni utekelezaji wa sheria kuu za nchi ambazo ni sheria mama. Na alichokizungumza Naibu Meya sijui alitumia sheria ipi?, lakini kama ni sheria ndogo haiwezi kuimeza sheria kuu,” alisema Kandoro.Kandoro alisema ni busara kwa viongozi hao kukutana waweze kutekeleza sheria kuu inayotawala nchi, ili kuweza kuwatumikia wananchi.Kwa upande wake, Kamanda Kombe alisema anafanya kazi kwa mujibu wa sheria na alichokiagiza ndiyo sheria ya nchi inavyosema.Juzi Naibu Meya Yakub aliipinga kauli ya Kombe wakati akitoa nasaha kwa baraza la madiwani, baada ya kumchagua tena kushika wadhifa huo.Yakub alisema kisheria Kombe hana mamlaka yoyote kupinga sheria zilizopitishwa na Manispaa ya Ilala, ambayo inao uwezo wa kufanya hivyo.Wakati huo huo, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA), Mujengi Gwao, amesema wamiliki wa daladala wanaopandisha nauli kiholela wanavunja sheria.Gwao alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa kufafanua kuhusu baadhi ya mabasi kutoza nauli ya sh. 400 kwa safari kati ya Ubungo na Kariakoo.Alisema kwa sasa wao na vyama vingine vya wamiliki wa mabasi na vyombo vya usafiri majini, wako katika mchakato wa kujadili gharama za nauli na kwa maana hiyo wanaopandisha watakuwa wanavunja sheria.Gwao alisema wadau mbalimbali wa usafirishaji jijini wakiwemo Chama cha Wenye Mabasi ya Abiria (TABOA) na DARCOBOA jana waliwasilisha mapendekezo yao kuhusu upandaji wa nauli na kwamba watatoa majibu baada ya kujadili kwa pamoja.Alisema suala la kupanda kwa nauli ni la lazima, lakini kitendo cha mtu kuchapisha tiketi mpya hivi sasa, kabla ya wao kutoa tamko, ni kinyume cha sheria na muhusika anastahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba baadhi ya mabasi yanatoza nauli hiyo mpya.Juzi, gazeti moja lilimkariri Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Anastas Selemani, akisema mamlaka yake baada ya kupata taarifa ya kupanda kwa nauli imeamua kuitisha kikao hicho.Sakata la kupanda kwa nauli limeanza baada ya serikali kutangaza ongezeko la bei ya petroli na dizeli katika bajeti ya mwaka huu.Naye mwandishi wetu MAGRETH KINABO anaripoti kuwa nauli za mabasi yaendayo mikoani kutoka Dar es Salaam zinaendelea kupanda, licha ya SUMATRA kuwaonya wamiliki wa mabasi hayo.Gazeti hili jana lilishuhudia nauli hizo zikiwa bado zimepanda katika viwango tofauti kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo.Kwa mabasi yanayokwenda katika mkoa wa Kilimanjaro nauli ni kati ya sh. 22,000 hadi sh. 30,000; Morogoro sh. 5000, Mwanza sh. 45,000 kwa njia ya kati na sh. 52,000 hadi sh. 55,000 kwa kupitia Nairobi, Kenya.Wakati mabasi ya kampuni ya Zuberi nauli ya kwenda Mwanza ni sh. 32,000.Kwa upande wa mikoa mingine kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi ni kati ya sh. 25,000 hadi 30,000; Tanga sh. 15,000, Dodoma sh. 12,000 na Kagera ni kati ya sh. 60,000 mpaka sh.70,000. Katika hatua nyingine mwandishi wetu NJUMAI NGOTA anaripoti kuwa mabasi saba yaendayo mikoani yameshachukuliwa hatua na SUMATRA.Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mawasiliano kwa umma wa SUMATRA, David Mziray alisema tayari mabasi hayo yamechukuliwa hatua kwa kosa la kupandisha nauli kiholela.Hata hivyo, Mziray hakutaka kuweka wazi ni hatua gani zilizochukuliwa na majina ya mabasi hayo.Alisema mabasi hayo yamepandisha nauli kabla ya SUMATRA kutangaza rasmi nauli ya usafiri nchini.Mziray alisema jana walipokea mapendekezo ya nauli kutoka TABOA na DARCOBOA, ingawa hakueleza ni kiasi gani kilichopendekezwa.“Tumepokea mapendekezo ya nauli kutoka TABOA na DARCOBOA tutazifanyia kazi na tutatoa majibu ikiwa ni pamoja na nauli itakayopendekezwa baada ya kikao kitakachoshirikisha wadau," alisema.Alisema kikao hicho kinatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

WAKATI KAMPENI YA KUPIMA UKIMWI IKIWADIA
Wengi wameathirika bila wenyewe kujijua
Na Mwandishi Wetu
KAMPENI ya kitaifa ya kupima virusi vya ukimwi kwa hiari itazinduliwa rasmi Jumamosi ijayo, na kuendelea kwa utaratibu wa kanda hadi Desemba Mosi, mwaka huu.Wakati uzinduzi huo ukifanyika, ni fursa ya watu kujua hali ya afya zao.Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu ya Ukimwi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk. Bennett Fimbo alisema juzi kuwa kampeni hiyo itazinduliwa kwa Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo vituo zaidi ya 200 vimetayarishwa kwa ajili ya mkoa huo."Maandalizi yote yamekamilika na kila kitu kipo tayari kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni hiyo," alisema.
source: uhuru 11/7/2007

Kilio cha nauli sasa kila mahali
2007-07-11 10:38:11
Na Godfrey Mushi, PST Tanga
Abiria wa mabasi yaendayo mikoani jijini hapa, wametishia kuandamana hadi kwenye ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupinga kupanda kwa nauli.? Walisema kama SUMATRA haitaingilia kati suala la kupanda kwa nauli na kutoa suluhisho, wataandamana. Baadhi ya wasafiri waliozungumza na PST jana katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, walisema wanasikitishwa na kitendo hicho cha kupanda maradufu kwa nauli, hasa katika stendi ya Ubungo jijini Dar es Salaam, ambapo baadhi ya abiria walishindwa kusafiri.? Walidai iwapo wamiliki wa mabasi?hayo, pamoja na?mawakala wao, hawatapunguza nauli hizo, wananchi wa jiji wataandamana kuomba serikali iwachukulie hatua. Abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kuja Tanga walikuwa wakitozwa hadi Sh. 10,000 kwa kila abiria ukilinganisha na nauli ya kawaida ya Sh. 6,500 na kusababisha malalamiko kwa wananchi wakiitaka serikali kuhakikisha mabasi yote ya mikoani yanashusha nauli.? Mmoja wa abiria hao, Bi. Sikudhani Abdallah, mkazi wa Kange jijini hapa, alisema kupanda huko kwa nauli za mabasi kumesababisha baadhi ya abiria kushindwa kurejea katika vituo vyao vya kazi baada ya kumaliza Sikukuu ya Sabasaba na mapumziko ya mwisho wa juma.? ``Kama ilivyokuwa kwa wenzetu wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, nauli zimepanda maradufu, pale Ubungo jana mimi nilitozwa Sh. 10,000 kwa tiketi moja na nilikuwa na familia yangu ya watu watatu, sasa hamuoni jamani tunavyopata shida ? Tunaiomba serikali izuie kupanda kwa nauli maana Waziri alikwishatoa tamko Bungeni,`` alisema Bi Sikudhani. PST ilipotembelea kituo cha stendi kuu jijini hapa ilibaini wasafiri wengi waliokumbwa na adha hiyo ni wale waliokuwa wakitokea Dar es Salaam kuja Tanga. Abiria wanaotoka Tanga kwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wanalipa Sh. 8,000 mpaka 10,000 kulingana na utaratibu wa kampuni. ? Mmoja wa mawakala wa mabasi yaendayo Kilimanjaro na Arusha, Bw. Alli Pengo, alipohojiwa kuhusiana na kupanda kwa nauli hizo alidai kuwa inatokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji ikiwamo mafuta na vipuri.? ``Kama unavyojua ndugu yangu, sisi hatufanyi kusudi bali tunatoza kulingana na hali ilivyo. Hivi sasa mafuta hapa Tanga kwa lita moja ni Sh. 1,500 na vipuri navyo vimepanda bei, hamuoni kwamba hata sisi tunapata hasara?`` Alihoji Bw. Pengo.? Mwanzoni mwa mwezi huu, Waziri wa Fedha Bi. Zakhia Meghi aliwataka wananchi wasiwe na wasiwasi kwa maelezo kuwa SUMATRA pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini (EWURA) watahakikisha nauli za mabasi na bei ya mafuta ya petroli na dizeli havipandi holela kuliko kiwango muafaka. Wakati huo huo, Aisha Hamza na Catherine Alais wa PST wanaandika kutoka Arusha kwamba Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Bw. Matei Basilio, amewaagiza askari polisi wa jijini hapa kuwakamata mara moja wamiliki wa magari ya abiria ya masafa marefu ambao wamepandisha nauli kiholela. Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kamanda Basilo alisema amepokea malalamiko toka kwa wananchi wakidai kupandishiwa nauli kiholela toka kwa wamiliki wa mabasi hayo. ``Naagiza kukamatwa mara moja wamiliki ambao mabasi yao yamepandisha nauli,`` aliagiza Kamanda Basilio. Aliongeza kuwa kupandishwa kwa nauli hizo kiholela kumewaletea abiria usumbufu hivyo. Alisema wamiliki hao, hasa wa mabasi ya masafa marefu, wamekuwa wakipandisha nauli kiholela ambapo wamejiamulia wenyewe, na sio kuidhinishwa na SUMATRA ambapo ni kosa. Alisema kuwa mbali na kuagiza polisi wawakamate wamiliki hao, amewataka askari wa usalama barabarani kuwasaidia wananchi pindi wanapoona kuwa hawatendewi haki. ``Nimepokea barua toka SUMATRA wakikemea kitendo hicho na kusema kuwa wamiliki hao wasipandishe nauli bila kufanya nao mawasiliano, hivyo wakitaka kufanya hivyo kuna utaratibu wa kufuata,`` alisema. Aliongeza kuwa katika taarifa ya SUMATRA ilieleza kuwa kama wamiliki hao wanataka kupandisha nauli, wanatakiwa wafuate sheria na kanuni ambapo kwanza wawasilishe mapendekezo yao. Alisema kuwa katika mapendekezo hayo ni lazima utaratibu maalumu ufuatwe kwa mhusika ambapo katika barua hiyo anatakiwa aandike jina kamili la kampuni yake na anuani, namba ya usajili, leseni, njia na umbali. Pia aeleze kiwango cha nauli cha mwanzo na sababu za kutaka kupandisha nauli na kiwango chake, ambapo kama watakubaliana na hoja hizo watamkubalia mhusika. Kwa sasa wanafunzi hulazimishwa kulipa Sh. 200, wakati abiria wengine hulipa 350, mpaka 400, badala ya Sh. 200 hadi 250 kwa baadhi ya maeneo kutokana na umbali.
SOURCE: Nipashe 11/7/2007

No comments: