Saturday 28 July 2007

'Karibu JamboForums.Com'

Karibu JamboForums.Com- Tunapothubutu Kuongea kwa Uwazi!

Mpendwa mzalendo mwenzangu,
Ninayofuraha kubwa kwa niaba yangu na niaba ya wasimamizi wa Jukwaa la Maoni Huru la JamboForums, kutoa mwaliko kwako ili uweze kuungana nasi katika kushiriki katika mijadala mbalimbali inayohusu maisha na hali za watanzania na hatima ya taifa letu kwa ujumla.

Tovuti ya Jambo Forums ilianzishwa kama mwaka mmoja na nusu hivi uliyopita ili kuwa sehemu ambapo mijadala ya masuala mbalimbali yanayoihusu Tanzania kwa ujumla wake inaweza kufanyika kwa uhuru, uwazi, na kwa kuthubutu zaidi kuliko mtandao mwingine wowote ule ndani ya Tanzania. Dhamira ikiwa ni kuhakikisha uhuru wa kuongea unapewa upana zaidi na kwa usalama uwapo mtandaoni.
Utakapoamua kujiunga nasi kuna mambo kadhaa ambayo niyaweke wazi kwako ili kukusaidia kuelewa namna ya kujiunga nasi:-

Uanachama ni bure na kujiandikisha haichukui zaidi ya dakika tatu, ukiona hauwezi kuandika baada ya kujisajili vuta subira na jaribu muda mchache baadae huku ukiendelea kubarizi ndani ya tovuti na kusoma mijadala kadhaa iliyopita kuweza kujenga hoja.

Unaweza kujiandikisha kwa kutumia jina lako halisi, lakini wengi wa wanachama wetu hutumia majina bandia ili kulinda nafasi na hadhi zao. Muhimu ni kuweka barua pepe ambayo una hakika unaweza kuwasiliana na wanachama wa tovuti hii.

Una uhuru wa kuchangia jambo lolote katika forum hiyo katika lugha ya Kiingereza au Kiswahili; lakini bila kutukana ama kutaja majina ya kweli ya mmojawapo wa wanachama (hata kama ni Rafiki yako) kwani tulikubaliana tangu awali kuheshimu identity ya wanachama wetu.

Utambulisho wako wa kiintaneti (IP Address) uko salama, na hautatolewa kwa mtu yeyote au chombo chochote kile. Unakuwa kwenye mtandao salama na huna sababu ya kumwofia mtu bali kuwaheshimu waliomo kwenye mtandao huo.

Zipo faida nyingi za wewe kujiunga nasi zaidi ya kupata nafasi ya kutoa mawazo na maoni yako. Kubwa zaidi ni hizi zifuatazo.
Unakuwa kwenye mtandao ambapo habari za kushtukiza zinazoihusu Tanzania zinakufikia mara moja na kwa haraka kuliko mahali pengine popote hata zaidi ya radio! Habari zinakufikia papo kwa hapo na kesho yake utazisikia magazetini.

Habari nyeti zinazohusu taifa letu zinamwaga kwa kuthubutu na zile tetesi ambazo zinazungumzwa pembeni ni rahisi kuonesha makosa yake kabla hazijafikia vyombo vya habari vya nyumbani. Sisi tulio wanachama tunajisikia huru sana kuuanika ukweli wa mambo ili pumba ijulikane na itenganishwe na mchele.

Unaweza kutetea msimamo wako na hoja zako bila kujali itikadi au mfungamano wowote. Kinachopendwa na wengi kwenye Jambo Forums ni hoja na hoja peke yake. Msemo wa “hoja hujibiwa kwa hoja” utakuta unarudiwa mara nyingi. Wanachama wa tovuti hii ni wa dini tofauti, itikadi za kisiasa tofauti na hupingana kwa hoja. Jazba zipo lakini huwa tunavumiliana na kutulizana.

Hata hivyo mara nyingi kama mahali popote penye watu wanaojadiliana bila ya shaka utakutana na mambo mengine ambayo hayatakufurahisha kama watu kukejeliana, kurushiana madongo n.k yote hayo ndiyo yanaifanya Jambo Forums kuwa ni mahali ambapo utajisikia uko nyumbani na mahali ambapo panakupa burudani ambayo hutopenda kuikosa.

Mambo mengine mengi utayafahamu mwenye pindi ukijiunga nasi na wakati wowote ukihitaji msaada wa maelekezo au jambo lolote, tafadhali usisite kuwasiliana na http://us.f362.mail.yahoo.com/ym/Compose?To=invisible@jamboforums.com au http://us.f362.mail.yahoo.com/ym/Compose?To=webmaster@jamboforums.com kwani hawa wanaweza kukusaidia kwa ukaribu na bila kuchelewa.

Ni matumaini yangu wewe kama mzalendo, utaungana na wazalendo wenzio kwenye mjadala huru zaidi, wazi zaidi na wenye kuthubutu zaidi. Tafadhali ungana nasi kwa kutembelea http://www.jamboforums.com/ na ili kujisajili angalia upande wa juu kuna neno “Register” bonyeza pale kisha fuata maelekezo. Hutojutia kuitembelea tovuti hii na daima utakubali kuwa sasa watanzania wanaongea!

Baadhi ya vitu vilivyojadiliwa kwenye tovuti hii ni pamoja na hivi:
Maoni: Shirikisho la Afrika Mashariki (Watanzania, Wakenya, Waganda, Wanyarwanda na Warundi hujadiliana hapa juu ya mawazo yao kuelekea kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki [East African Federation]… Jaribu kupatembelea ujionee mabishano yanayoendelea)

Siasa (Hapa ndiko penye moto haswa! Siasa za Tanzania na Ulimwengu kwa ujumla wake hujadiliwa kwa mapana sana na kwa kujibizana kiheshima sana. Ni kwa kuangalia tulikotoka, tuliko na kuangalia tuendako)

Hoja nzito! (Kijiwe cha wachambuzi wa hoja zenye kuhitaji upembuzi yakinifu. Hapa kuna makala ndefu ambazo wachambuzi wa mambo huziweka na kutoa changamoto kwa jamii husika)

Vibweka vya 'wakubwa' (Hapa utakuta mikasa na udaku juu ya wale tunaowaita ‘wakubwa’ ikiwa ni pamoja na wanasiasa, matajiri na wote wenye majina makubwa ndani na nje ya Tanzania)

Kutoka Bungeni (Hoja zote zinazotokea Bungeni hujadiliwa hapa kwa kina na kuipitia miswada kadha wa kadha inayowakilishwa katika Bunge letu)

Habari kwa Ufupi (Hapa kuna habari toka vyanzo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti na television za ndani na nje ya Tanzania zinazowagusa watanzania kwa namna moja ama nyingine)

Kutoka Ughaibuni (Uko ughaibuni na kuna issue? Basi unaiweka hapa ili kuweza kuwaarifu wenzako ili nao watambue nini kinaendelea huko. Hakiachwi kitu, kuna wanaouvuruga ubalozi wetu uliko? Basi unawatumia ujumbe na unakuwa delivered!)

Nafasi za Kazi(Vacancies) (Hapa nafasi za kazi huwekwa kila kukicha na wale wanaotafuta ajira basi hujikuta wanafarijika pale wanapokuta kile walichokuwa wakikisaka siku nyingi)

Miscellaneous (Kwa hoja zinazokuwa hazina mahala pa kuwekwa katika tovuti hii huwekwa hapa na wahusika huzipeleka wanakoona panastahili)

NYEPESI (Hapa kuna zile nyepesinyepesi ambazo huenda ukizisoma ukabaki mdomo wazi!)

Uchumi na Biashara (Kwa wale wachumi hapa ndipo maskani pao)

Elimu (Matokeo ya mitihani, hoja zinazohusu ukuaji na uporomokaji wa elimu, scholarship za masomo n.k hujadiliwa hapa)

Michezo/Burudani (Mara nyingi utakuta hata mechi zinazochezwa nyumbani tunapata matokeo chapchap bila kusubiri magazeti ya kesho; wanamiziki wetu na wasanii kwa ujumla wanajadiliwa hapa na namna ya kuinua viwango vya michezo hiyo na ushauri kwa wasanii wetu)

Lugha (Wataalamu wa lugha hapa wanaghani na kujadiliana ukuaji wa lugha yetu ya Kiswahili)

Jokes/Vimbwenga/Udaku (Kuna mikasa ya hapa na pale na vikatuni vya kuvunja mbavu!)

Mahusiano na Mapenzi (Sina cha kukueleza kuhusu hapa, labda utembelee uone kilichopo)

Dini/Imani (Wachambuzi wa masuala ya kiimani hukutana hapa, uzuri wanaheshimiana na kujibizana kwa uelewa mpana, kama unapenda kujua juu ya suala lolote la kiimani jaribu kuwauliza uone mwitikio wao)

Kabrasha (Store) Letu (Hoja mbalimbali zilizojadiliwa zamani tukafikia muafaka huwekwa hapa kwa ajili ya kumbukumbu. Haina gharama kuzipitia kabla ya kujibu jambo flani ili kuweza kujua tuliwahi kuongelea nini na kivipi tulihitimisha)


Tutorials/Books + ICT Related issues + Online Technical Help

ICT & related Discussions (Hapa ni kwa wataalam wa mambo ya ICT na masuala ya makompyuta, angalia mijadala inayoendelea hapa)

Tutorials/Books/Notices (Kamata vitabu free of charge, omba notice usaidiwe namna ya kuzipata kirahisi n.k)

Downloads (All are Free of charge and safe!)

Tunakusubiri kwa hamu ndugu yangu!

UKISHAUSOMA UJUMBE HUU WAFAHAMISHE WENZAKO

Mosonga says: Huu mwaliko nimeupokea kupitia barua pepe yangu 27/7/2007. Ninapenda kutumia nafasi hii nami pia kuusambaza kwa wasomaji wangu popote walipo!

No comments: