Friday 29 June 2007

Kifo cha Amina Chifupa (MB -Vijana CCM)

KIFO CHA AMINA CHIFUPA…
Bunge laahirisha shughuli zake
Na Mwadini Hassan, Dodoma
BUNGE la Jamhuri ya Muungano, jana liliahirisha shughuli zake zote kwa heshima ya Mbunge wa Viti Maalum, Amina Chifupa, aliyefariki dunia juzi.Ukumbi mzima wa Bunge mjini hapa, ulilizima simanzi baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuwatangazia wabunge kifo cha mbunge huyo aliyekuwa akiwakilisha vijana. Ujumbe wa wabunge wasiopungua 32 ukiongozwa na Spika Sitta, uliondoka hapa jana saa nane mchana kwa ndege maalum ya kukodi, kwenda Dar es Salaam, kuliwakilisha Bunge na serikali katika msiba huo.“Kwa masikitiko makubwa nawatangazia kifo cha mbunge mwenzetu, Amina Chifupa, kilichotokea jana (juzi) saa 2.43 usiku katika hospitali ya jeshi Lugalo, Dar es Salaam. “Katika dakika zake za mwisho baba yake mzazi, mama yake mzazi na mumewe walikuwa naye,” alieleza Spika mara baada ya kusomwa dua za kuiiombea nchi na Bunge, wakati bunge lilipoanza shughuli zake saa tatu kamili asubuhi.Wakati tangazo hilo likiendelea, baadhi ya wabunge akiwemo Spika mwenyewe, walionekana wakifuta machozi, na baada ya tangazo hilo bunge liliahirishwa kwa saa moja hadi saa nne asubuhi, kutoa nafasi za kufanya maandalizi ya Bunge kwa msiba huo.Baada ya kuahirishwa bila kuwepo kipindi cha maswali na majibu, baadhi ya wabunge walishindwa kujizuia na kulia kwa sauti ndani ya ukumbi, na hasa wabunge wanawake, ambao baadaye walikutana kwa kikao cha dharura.Kamati ya Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge, zilikutana mara moja baada ya Bunge kuahirishwa kupanga taratibu zitakazofuata kufuatia msiba huo.Bunge liliporejea katika kikao chake saa nne asubuhi, Spika alitangaza kwamba kikao cha Kamati ya Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge kimeamua: “Baadhi yetu twende Dar es Salaam leo (jana) saa nane mchana, tukaungane mkono na familia ya marehemu kuwafariji kwa msiba huu."Tumeamua tuwe na uwakilishi wa vyama vya siasa, uwakilishi wa maeneo ya nchi, kwa maana ya Tanzania Bara na Zanzibar na maeneo ya kijinsia," alitangaza Spika huku ukumbi ukiwa katika ukimya mkubwa na majonzi yakionekana nyusoni mwa wabunge ambao baadhi yao walikuwa wakifuta machozi."Wabunge wanawake wamepitisha azimio waende wote (kwenye msiba), nasikitika hilo halitawezekana," alisema na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutaweka utaratibu ambayo baadaye inaweza kukwamisha shughuli za bunge siku zijazo.Akifafanua uwakilishi uliopangwa kwenda Dar es Salaam kuwakilisha Bunge na serikali kwenye msiba wa Amina, Spika Sitta alisema utakuwa na wabunge wote Iringa, ambao ndiyo mkoa wake kwa kuzaliwa na wabunge wote wa Dar es Salaam.Serikali itawakilishwa na Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.Alisema watakuwemo wabunge wanne wa vyama vya upinzani watakaoongozwa na kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed.Spika alisema baada ya ujumbe huo ambao pia utajumuisha Katibu wa Bunge na makatibu wasaidizi wawili na wabunge wengine kadhaa, alisema leo ujumbe mdogo utakaoongozwa na Mbunge wa Singida Kaskazini, Mohammed Missanga, utakwenda Njombe kuhudhuria mazishi.Marehemu Amina aliyezaliwa Mei 20, 1981 na kuapishwa kuwa mbunge Desemba 29, 2005, atazikwa leo katika kijiji cha Lupembe, wilayani Njombe, Iringa.

…Vilio na simanzi vyatawala bungeni
Na Mwadini Hassan, Dodoma
VILIO, simanzi na majonzi vilisikika na kuonekana waziwazi bungeni jana, baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kutangaza habari za kifo cha mbunge Amina Chifupa.Karibu kila mbunge alionekana kuguswa na habari hizo, akiwemo Spika mwenyewe ambaye wakati akitangaza taarifa za kifo hicho, alishindwa kujizuia na kuonekana akifuta machozi akiwa amesimama mezani pake ndani ya ukumbi wa Bunge.Hali ilikuwa tete zaidi kwa wabunge wanawake, ambao walionekana wakimwaga machozi huku wakiwa na vitambaa mikononi wakifuta machozi mara kwa mara wakati Spika akiendelea kutoa tangazo la kifo hicho, kilichotokea juzi saa 2.43 usiku.Amina Chifupa aliyekuwa mbunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Vijana wa CCM, alifariki dunia katika hospitali ya jeshi Lugalo, jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa matibabu.Hali ya majonzi ilizizima zaidi baada ya Bunge kuahirishwa moja kwa moja kwa siku ya jana karibu saa 4.25 asubuhi, ambapo baadhi ya wabunge wanawake walisikika wakilia kwa sauti huku wakifarijiana kwa kukumbatiana.Habari za uhakika kutoka ndani ya Bunge zilithibitisha jana kwamba, hii ni mara ya kwanza kwa historia ya karibuni ya Bunge, kuahirisha shughuli zake kutwa nzima kwa sababu ya kifo cha mbunge.Hali ya simanzi kutokana na kifo cha mbunge huyo machachari aliyejipatia jina kutokana na michango, hoja na maswali yake bungeni, ilianza kuonekana mapema wakati wabunge walipokuwa wakiingia maeneo ya viwanja vya bunge, kutokana na habari hizo kuanza kufahamika kwa baadhi yao mapema.Kama ilipangwa, baadhi ya wabunge waliingia ndani ya Bunge wakiwa wamevaa nguo nyeupe, ambazo siku hizi zimekuwa maarufu kuvaliwa na wanawake wakati wa misiba.

JK amlilia Amina Chifupa
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete, ameeleza kupokea kwa mshituko mkubwa taarifa ya kifo mbunge wa CCM Viti Maalum, Amina Chifupa.Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema kifo hicho kimetokea wakati usiotarajiwa, huku akihitajika, lakini vivyo hivyo alikuwa ameanza kuvuma kisiasa."Wengi tutamkubuka marehemu Amina Chifupa kwa mchango wake muhimu alioutoa bungeni na katika jamii hasa mongoni mwa vijana."Alikuwa hodari katika kujkenga hoja na kutetea maslahi ya vijana wenzake na taifa kwa ujumla. Alikuwa kijana msema kweli na jasiri katika kutoa maoni yake kwa jambo analoliona," alisema Rais Kikwete.Huku akinukuu misemo mbalimbali ya kijamii, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa kwake na kifo cha mbunge huyo katika umri wa ujana wake."Kwa hakika kifo chake kinawagusa na kuwasikitisha watu wengi nchini. Wabunge wamempoteza mbunge mwenzao kipenzi, CCM wamempoteza nyota yao."Familia yake imempoteza nyota yao. Familia yake imempoteza mtoto na ndugu wa karibu. Mwanawe amempoteza mama. "Mzazi mwenzake amempoteza mzazi mwenziwe wa kusaidiana naye kulea mtoto wao mdogo. Jamii imempoteza mwana jamii mwema, mkarimu na mwenye moyo wa huruma," alisema Rais Kikwete. Aliwahakikishia jamaa za karibu wa marehemu, huzuni hiyo haikuwa peke yao, bali ni ya wote wanaoguswa na kifo hicho, huku akisisitiza ni "Mapenzi ya Mungu."Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umetoa rambirambi kutokana na kifo hicho cha Amina.Rambirambi za UVCCM zilizotolewa katika taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Taifa, John Nchimbi, zilisema hawataweza kumsahau kutokana na uwakilishi wake hasa wa kutetea maslahi ya vijana nchini wakati wote."Amina alikuwa ni mchapakazi hodari, mkweli na ambaye siku zote alitetea masuala ya vijana, sifa ambayo ilimfanya apendwe na wengi," ilisema taarifa hiyo.Nchimbi katika taarifa yake, alibainisha kwamba wakati wote wataendelea kukumbuka kwa utashi aliokuwa nao katika utumishi wa uwakilishi wa jamii katika chombo hicho cha kutunga sheria."Tunaungana na wabunge, familia, ndugu na jamaa za Amina Chifupa, kuomboleza kifo chake na tunamwomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu, nguvu na afya katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo," ilihitimisha taarifa hiyo.Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema chama hicho na yeye binafsi wameshitushwa na kifo cha Amina.Walimsifu marehemu kama mtetezi wa jamii ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo Watanzania wamempoteza kiongozi shupavu."CUF - tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, Spika Samuel Sitta, wabunge, ndugu na jamaa wa marehemu na tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” ilisema taarifa ya CUF, iliyotiwa saini na msemaji Mbaralah Maharagande.

Naye Mwadini Hassan, anaripoti kutoka Dodoma kuwa, Chama cha Mapinduzi kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Mbunge wa Viti Maalum, Amina Chifupa, na kusema namna ya kumuenzi ni kutetea na kuyasimamia yote aliyokuwa akiyatetea.Kauli hiyo ya CCM ilitolewa hapa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, makao makuu ya chama.Alisema, marehemu Amina alikuwa kiongozi imara katika kutetea hoja, na hasa kupambana na dawa za kulevya, ambapo alidiriki kueleza hadharani kuwa "hata kama ni mumewe au yeye mwenyewe anajihusisha na biashara ya dawa hizo, watajwe ili wafikishwe katika vyombo vya sheria."Makamba alisema, Amina alichukia biashara ya dawa za kulevya, ambayo imekuwa chanzo cha kuwaharibu vijana wengi nchini, ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.Makamba alitaja eneo jingine ambalo marehemu alilisimamia imara kulitetea, ni la watoto wa mitaani na wanaoishi katika maisha magumu, ambapo licha ya yeye kujitolea kwa hali na mali kupambana na tatizo hilo, alikuwa mara kwa mara akiitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kuwasaidia kwa kuwapatia makazi ili waondokane na hali zao.Marehemu Amina alisema Makamba, aliwahi kulia alipowatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hali ambayo ilionyesha alikuwa akiumizwa na hali hiyo na aliahidi kujitahidi kuwasaidia. "Namna nzuri ya kumuezi, ni kuyaendeleza aliyokuwa akiyasimamia na kuyatetea, na hasa kwa Umoja wa Vijana ambao alikuwa akiuwakilisha bungeni," alisema.

(source: uhuru, 28/6/2007)

No comments: