Friday 22 June 2007

Maoni: Waliooana*

Hi Anti Flora!!!!
Asante kwa kutoa nafasi kwa wasomaji wako kutoa au kuchangia mada ktk 'maisha ndivyo yalivyo'.
Napenda kuchangia hoja ya msomaji wako aishie Oxford, Uingereza.
Kwanza napenda kukupongeza wewe binafsi kwa mafundisho yako ktk jamii. Kila mara unasisitiza mambo muhimu katika kudumisha ndoa kwa mfano upendo, uaminifu, uvumilivu, kusameheana, kukosoana n.k. Naamini mada unazoandika kila wiki unazitumia kama mifano ktk kufikisha ujumbe kwa jamii.
Msomaji wako 'aliponda' moja kwa moja juhudi za mwanandoa uliyemzungumzia ktk kunusuru ndoa yake (rejea mada ya 17/09/2006). Kwa upande wangu na kwa mazingira ya kwetu Tanzania, juhudi hizo hazikuwa bure, kwa sabababu huyo mama alifanikiwa kulipatia jibu lile tatizo la mumewe! Kama kuna mambo ya virusi yameingilia ktk suala hili, basi, hilo ni suala lingine. Lile kubwa la msingi limepata jibu.
Hili suala la kudhibiti/kuzuia maambukizi (STDs & Infections) tukiliangalia kwa karibu kabisa kabisa linaweza kupata dawa/kinga kabla mtu hajapata magonjwa/maambukizi haya. Ktk ndoa kama kuna uaminifu wa kweli, upendo, uvumilivu n.k. mtu hawezi kwenda nje ya ndoa kimapenzi. Kila anapopata tamaa kimwili atamkumbuka mkewe kama vile anamwona kile anachofikiria au kutamani (ngono ya nje!!)
Yule mama uliyemsimlia 17.09.06, hana makosa na yeye alifanya kile kilicho ktk uwezo wake na akafaulu. Kuna msemo, mtu hujikuna pale anapofikia! Hapa tatizo liko kwa 'baba'aliyekuwa na kimada Morogoro.
Wanaume wengi tuna jeuri ya kufanya tutakavyo hasa kuhusu nyumba ndogo kwa vile wake zetu (wengi wao) ni kina mama wa nyumbani na wanatutegemea kwa kila kitu kimatunzo. Kwa mwanamke anayemtegemea mumewe kimaisha(kiuchumi) anakuwa ni mnyonge pale mumewe anapomkosea maana dume litasema ''leo nakurudisha kwenu'' sasa huyu mwanamke atasemaje, sanasana atanywea tu. Ninachotaka kusema ni kuwa ni wanawake wangapi Tanzania wanaweza kuwafumania waume zao na wakawa na jeuri ya kudai mume aende au wote waende kwa pamoja kupima maambukizi kabla ya kuendelea na mahusiano ya mwili?

Huyu msomaji wako wa Oxford amesahau kutofautisha mazingira aliyopo kwa sasa (Uingereza) na Tanzania, dunia ya tatu.

Mwanamke wa Uingereza ndie huyu hapa;

sheria inamlinda sana na watoto. (na kwa taarifa yako anti Flora, wanaume wengi kutoka Afrika wanaojifanya vijogoo kwa wake zao wanaipata joto ya jiwe Uingereza).

kama hana kazi, atalipwa 'job seeker's allowance', incapacity benefit.

kama hana mahali pa kuishi (hasa baada ya umri wa miaka 18 na kuendelea) atalipwa housing benefit au kutafutiwa nyumba ktk halmashauri ya serikali ya mtaa anayoishi(council house). Council zote zina nyomba kwa ajili ya 'wanyonge' kimapato, wenye kipato cha chini na wasio na makazi.

kama akiachika kwa mumewe na ana mtoto/watoto, atapata mafao kupitia Child Support Agency, child support scheme.

kuna kadi (credit) ya matibabu ya mama na mtoto ktk hospitali zote za serikali na binafsi ambapo watapata matibabu au kupima afya zao bure (hospitali zitaidai serikali gharama).

mtoto atapata nafasi ya kusoma chekechea, msingi, sekondari hadi A-level bure. Chuo kikuu kuna mikopo kwa kila mwanafunzi aliyepata nafasi chuo kikuu.

kama ana ulemavu atapata Disability and Carers service benefits.

kama ni mzima na ana uwezo wa kufanya kazi, atatafutiwa kazi kupitia vituo vya kutafuta kazi, Jobcentre Plus vilivyoko ktk miji yote Uingereza. Kazi zipo tele za wasomi na wasio wasomi.

Anti Flora ninajaribu kujenga hoja kwa hiyo naomba univumilie kwa porojo zangu hizi.

Ninataka nijenge mazingira ambayo mwanamke mtanzania kama yule wa tarehe 17.09.06 anaweza kusimama kidete na kumpeleka mumewe 'ANGAZA' wakapime.

Nimetoa mfano wa mama aishiye Uingereza na tumlinganishe na huyu wa Tanzania. Naamini utakubaliana nami kuwa huyu mama wa Uingerreza anaweza kumwambia mumewe wakapime ikiwa mume atafanya mambo nje ya ndoa. Na ikiwa mume wake atagoma au kubisha na mama akawa na msimamo kulinda afya yake asijeambukizwa
mama anaweza kusema watengane kwa kuhofia virusi. na wakitengana anaweza kuendelea na maisha bila wasiwasi kama nilivyoelezea hapo juu. Huyu mama wa Kiingereza hatapata tatizo lolote kimaisha.

Je yule mama wa kitanzania akimwambia mumewe wakapime na mume akagoma, mama ataamua nini; aondoke au akae na kuambukizwa?

Matatizo mengi kwa kina mama chanzo chake ni utegemezi kiuchumi kwa mume au ndugu.

* Barua yangu ya 28/9/2006 kwa Flora Wingia wa Magazeti ya Guardian na mwandishi wa makala ya 'Maisha Ndivyo Yalivyo' Nipashe Jumapili.

No comments: